Wanasayansi wabainisha mbinu 5 zakukufanya uwe na Mvuto zaidi

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Imebainika kuwa watu wenye mvuto mkubwa wanatabia kadhaa zinazofanana

Ikiwa unataka kuwa na mvuto kama Tom Cruise au Taylor Swift, badala ya kutumia muda na pesa nyingi kubadilisha mwonekano wako, zingatia zaidi tabia zako. Mashabiki na watu waliohojiwa na wawili hao wamewahi kuelezea haiba yao ya kipekee.

Wenye mazungumzo, tabasamu na uwezo wa kuitikia wengine vizuri, Cruise na Swift huonekana kana kwamba wanavutiwa kweli na mtu wanayezungumza naye na wanazingatia kikamilifu mazingira ya kijamii wanayokuwamo.

Hili linaendana na tafiti za saikolojia. Bila shaka, mwonekano wa mtu unaweza kuvutia mwanzoni, lakini kadiri unavyoingiliana na mtu na kumfahamu zaidi, ndivyo utu wake na namna mnavyoelewana vinavyokuwa muhimu zaidi.

Kwa kuzingatia hilo, hizi hapa njia tano za kisaikolojia za kuongeza mvuto wako.

1. Jifunze kuchangamana na wengine

.

Kwa mujibu wa tafiti, watu wenye hulka ya kupenda kuchangamana na wengine huwa wanachukuliwa kuwa na mvuto zaidi wanapokutana na watu kwa mara ya kwanza.

Hii ni kwa sababu huonyesha hisia chanya zaidi, kama vile kuwa na uchangamfu, kutabasamu mara kwa mara na kuzungumza kwa sauti inayoashiria uchangamfu na kujiamini.

Hiyo ni kwa sababu, kwa kawaida, watu hao hupenda kushirikiana na wengine.

.

Hata kama kawaida yako wewe si kuchangamana na watu wengi, unaweza kuanza kuonyesha tabia hizi kwa juhudi kidogo.

Ikiwa una hulka ya kujitenga na kupendelea kuwa peke yako, unaweza kutiwa moyo na utafiti unaoonyesha kuwa watu wenye hulka hiyo hufurahia kujitahidi kuwa wachangamfu na kuchangamana na wengine zaidi ya wanavyodhani watafurahia.

2. Sikiliza kwa makini na onyesha kuvutiwa na wengine

.

Mashabiki wanaovutiwa na Tom Cruise wanasema ana uwezo wa kukufanya uhisi kana kwamba kuzungumza nawe ndilo jambo pekee lililo akilini mwake.

Mchekeshaji na mtangazaji wa zamani wa vipindi vya usiku, Stephen Colbert, aliwahi kusifu jinsi Taylor Swift alivyomsikiliza kwa makini binti yake, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 14, walipokutana.

Haya yote yanaendana na tafiti zinazoonyesha kuwa watu huonekana kupendeza zaidi wanapoonyesha ushiriki wa dhati katika mazungumzo na kuuliza maswali ya kufuatilia majibu ya wenzao.

Kwa hiyo, njia nyingine rahisi ya kuongeza mvuto wako ni kuonyesha nia ya kweli ya kuwafahamu wengine na kuuliza maswali yanayoonyesha udadisi wa dhati.

3. Kuwa mkarimu

Matokeo ya tafiti mbalimbali yanaonyesha kuwa watu wanaotenda kwa wema na kusaidia wengine bila kutarajia malipo huwa wanachukuliwa kuwa na mvuto zaidi.

Kwa mfano, utafiti kuhusu sifa ambazo watu huzitafuta kwa wenzi wa kimapenzi unaonyesha kuwa wema ni mojawapo ya sifa zinazotamaniwa zaidi, na katika baadhi ya tafiti umeonekana kuwa sifa muhimu zaidi.

Pia, kuna tafiti zinazoonyesha kuwa sura za watu zinaweza kuonekana kuwa na mvuto zaidi pale zinapohusishwa na mtu anayeelezwa kuwa mwenye wema.

Matokeo haya yanaashiria kuwa kuwa mkarimu, kuwasaidia wengine na kuwa tayari kuzingatia mahitaji yao kunaweza kuongeza mvuto wako.

4. Usijichukulie kwa uzito kupita kiasi

.

Imekuwa jambo la kawaida kusikia kwamba watu hutafuta wenzi wa kimapenzi wenye ucheshi. Hata matangazo ya watu wanaotafuta wenzi yamekuwa yakitaja mara kwa mara kuwa na uwezo wa kuchekesha kama sifa muhimu.

Tafiti zinaunga mkono wazo hilo. Katika majaribio ya kukutana kwa muda mfupi kwa lengo la kutafuta mwenzi wa kimapenzi (speed dating), pamoja na majaribio mengine yanayofanana, watu wenye ucheshi na uwezo wa kutoa kauli za kuchekesha kwa ustadi huwa wanachukuliwa kuwa na mvuto zaidi.

Hata hivyo, kujitahidi kupita kiasi ili kuchekesha kunaweza kuwa na matokeo tofauti na yaliyokusudiwa.

Kwa hiyo, funzo muhimu zaidi kutoka katika tafiti hizi ni kujifunza kuchukulia mambo kwa wepesi, kuona upande wa kuchekesha wa hali mbalimbali na kuepuka kujichukulia kwa uzito kupita kiasi.

5. Kuwa mbunifu

g

Nadharia moja inaeleza kuwa ucheshi huvutia kwa sababu inaweza kuwa ishara ya ubunifu na akili. Kwa upande mwingine, ubunifu wenyewe huonekana kuwa na mvuto kwa sababu unaashiria kuwa mtu anaweza kuwa na mchango wenye manufaa kwa wengine.

Wazo hili linaendana na utafiti unaoonyesha kuwa washairi na wasanii huwa na idadi kubwa zaidi ya wenzi wa kimapenzi katika maisha yao ikilinganishwa na wastani wa watu wengine. Hii ni dalili inayoweza kuashiria kuwa watu wengine huwavutia zaidi, ingawa ushahidi huo bado si wa mwisho.

.

Ushahidi mwingine unaoweza kushawishi zaidi unatokana na utafiti ulioonyesha kuwa sura zilezile zilionekana kuwa na mvuto zaidi zilipowasilishwa pamoja na simulizi la ubunifu lililoelezwa kuwa limeandikwa na mtu anayehusika na sura hiyo.

Kwa kuzingatia matokeo hayo, kuonyesha ubunifu wako kunaweza kuwa njia nyingine ya kuongeza mvuto wako. Unaweza, kwa mfano, kushiriki mashairi uliyoandika au kuonyesha vipaji vyako vya kisanii.