Enzi ya droni za kuzuia mashambulizi inafikia kikomo: Kwa nini hali hii imetokea na nini kitachukua nafasi yake?

Chanzo cha picha, УНІАН
- Author, Олег Черниш
- Nafasi, ВВС News Україна, Київ
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 12
Ubunifu wa Ukraine katika miaka ya hivi karibuni - droni za kuzuia mashambulizi zenye propela nyingi - unaanza kupoteza umuhimu wake taratibu. Ingawa mara kwa mara bado zinafanikiwa kuangusha droni za Urusi zinazoendeshwa kwa injini za ndege, lakini kwa sasa tayari kunaonekana kuwa na kikomo cha teknolojia hii na kuilazimu Kyiv kutafuta suluhisho jipya.
Droni za kuzuia mashambulizi kama vile P1SUN, Sting, Octopus, General Chereshnya na Litavr zimekuwa alama ya kujivunia ya sekta ya ulinzi ya Ukraine. Katika majira ya kuchipua ya mwaka 2026, baada ya kuanza kwa vita nchini Iran, droni hizo pia zilikuwa bidhaa zilizotafutwa sana na falme za Mashariki ya Kati zilizokuwa zikikabiliwa na mashambulizi ya droni za Iran zinazojulikana kama Shahed.
Nchini Ukraine, vifaa hivi vimekaribia kuondoa tishio la droni za Urusi za aina ya Shahed, zinazojulikana kama Geran-2. Hata hivyo, mafanikio hayo yanahusu toleo la kawaida la droni hizo, ambalo hutumia injini ya mwako wa ndani inayotumia petroli. Urusi imekuwa ikizitumia tangu majira ya kupukutika kwa majani ya mwaka 2022.
Droni hizo zilikuwa na kasi ya kilomita 150–200 kwa saa, hivyo kuwa shabaha rahisi kwa droni za Ukraine za kuzuia mashambulizi, ambazo zinaweza kuongeza kasi hadi kilomita 250–300 kwa saa.
Lakini Urusi ilipoanza kurusha kwa wingi droni za Geran zinazoendeshwa kwa injini za ndege katika majira ya kiangazi ya mwaka 2026, droni za Ukraine za kuzuia mashambulizi zilishindwa kwa kiasi kikubwa kukabiliana nazo. Kwa hakika, huenda tayari zilikuwa zimefikia karibu kikomo cha uwezo wake.
Kwa nini hali hii imetokea, na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa?
Tishio la Kujibu Mapigo
Urusi haijaachana kabisa na droni zinazotumia petroli, na inaendelea kurusha makumi ya droni hizo kila siku sambamba na zile mpya zinazoendeshwa kwa injini za ndege.
Hata hivyo, droni hizo hushambulia zaidi maeneo yenye ulinzi hafifu, hasa karibu na mstari wa mbele wa mapigano, kama vile miji ya Zaporizhzhia na Sumy.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Licha ya droni hizo za Shahed kuwa nafuu zaidi kuliko matoleo mapya, idadi kubwa zaidi inahitajika ili kuhakikisha shabaha inapigwa au, zaidi ya hapo, kuharibiwa. Hii ni kwa sababu ni rahisi zaidi kwa mifumo ya ulinzi wa anga kuziangusha.
Kwa mfano, vyanzo katika Jeshi la Ukraine vimeiambia BBC kwamba ili kuharibu kituo kimoja cha mafuta, adui anaweza kutumia hadi droni 10 za kawaida za Shahed badala ya droni moja inayoendeshwa kwa injini ya ndege.
Kwa hiyo, haishangazi kwamba Urusi inajaribu kutumia droni zenye injini za ndege kushambulia shabaha zilizo hatarini zaidi katika eneo la mji mkuu wa Ukraine au magharibi mwa nchi hiyo.
Urusi hutumia zaidi droni za Geran-4, zilizoundwa kwa msingi wa Shahed-238, na Geran-5, ambazo zinafanana na droni ya Iran ya Karrar. Kasi yake ni mara mbili hadi tatu zaidi ya ile ya Shahed za kawaida, ikiwa kati ya kilomita 350 na 450 kwa saa. Katika baadhi ya hali, kasi hiyo inaweza kufikia kilomita 500–600 kwa saa.

Chanzo cha picha, Reuters
Mbali na kasi, urefu ambao droni hizo zinazoendeshwa kwa injini za ndege hurukia nao umeongezeka. Hapo awali ziliruka katika urefu wa kilomita 3–4, lakini sasa zinaweza kufikia kilomita 5–8.
Njia yenye ufanisi mkubwa zaidi ya kukabiliana na droni za Geran ni kutumia ndege za kivita. Ukraine hutumia ndege zake za F-16 kwa kazi hiyo, na zinafanikiwa kuangusha droni hizo kwa kutumia makombora ya angani-kwa-angani au mizinga ya milimita 20.
Droni za Urusi zikifanikiwa kupenya safu hiyo ya ulinzi, mifumo ya makombora ya kupambana na ndege, droni za kuzuia mashambulizi au makombora ya kubebwa na mtu mmoja (MANPADS) inaweza kutumika kukabiliana nazo. Minara ya kiotomatiki yenye bunduki za kupambana na ndege inaweza kulinda moja kwa moja maeneo yanayolengwa dhidi ya mashambulizi ya angani, ikiwa kama safu ya mwisho ya ulinzi.
Ni wazi kwamba njia yenye ufanisi na usalama zaidi ni kuziangusha droni hizo kabla hazijafika katika maeneo ya makazi, na ikiwezekana mbali zaidi na maeneo yanayoweza kuwa shabaha ya mashambulizi.
Katika wiki za hivi karibuni, takwimu zilizochapishwa na Jeshi la Anga la Ukraine zinaonyesha ongezeko la idadi ya droni za Urusi zinazoendeshwa kwa injini za ndege, lakini pia ongezeko la ufanisi wa kuziangusha. Kwa kawaida, kiwango cha mafanikio ni asilimia 50–60, ingawa katika baadhi ya siku kimefikia asilimia 70–85.
Inaonekana Ukraine inaweza kukabiliana na tatizo hili na kuongeza kiwango cha kuziangusha hadi asilimia 90–95 katika siku za usoni.
Lakini kuna changamoto nyingine.
Ongezeko kubwa la kasi
Kwa mujibu wa mamlaka za Ukraine, Urusi tayari inajiandaa kutengeneza toleo jipya la droni zake zinazoendeshwa kwa injini za ndege.
Kasi yake inatarajiwa kufikia kilomita 700–800 kwa saa.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Yevheniy Khmara, aliwaambia waandishi wa habari kuhusu jambo hilo tarehe 11 Oktoba.
"Tunafanya kazi kutafuta njia za kukabiliana na kizazi kijacho cha vitisho. Watengenezaji na sekta ya ulinzi wamepewa jukumu la kuwasilisha mapendekezo na mifano ya majaribio," alisema.
Droni za Geran zikifikia kasi ya chini ya sauti, takribani kilomita 800–900 kwa saa, zitakuwa karibu zaidi na kundi la makombora ya kusafiri (cruise missiles), na hivyo kuwa shabaha ngumu zaidi kwa droni za kuzuia mashambulizi.
Kama ilivyotajwa awali, droni nyingi za Ukraine za kuzuia mashambulizi zimejengwa kwa kutumia muundo mmoja wa kimuundo na aerodinamiki, unaotambuliwa kuwa bora kwa kuangusha droni za Urusi zinazolipuka zinapogonga shabaha.
Hizi ni droni zenye propela nyingi zinazotumia muundo wa Tailsitter, zikiwa na sehemu ya mbele yenye umbo la kombora na propela nne pamoja na injini za umeme. Muundo huo huziruhusu kuruka na kutua wima, jambo linalozifanya ziwe rahisi kutumia katika maeneo ya mapigano. Pia, muundo huo husaidia kudhibiti droni na kuongeza kasi kabla ya kushambulia shabaha.
Miundo ya hivi karibuni ya droni hizo za kuzuia mashambulizi ina kasi ya kilomita 300–400 kwa saa na inaweza kufanya kazi katika urefu wa hadi kilomita 3–5.
Hii inamaanisha kwamba katika hali fulani zinaweza kuangusha droni za Geran zinazoendeshwa kwa injini za ndege. Kwa hakika, tayari kuna matukio kadhaa yaliyorekodiwa ya droni hizo za Urusi kuangushwa kwa njia hiyo. Lakini si jambo linalotokea kwa utaratibu wa kawaida; badala yake, ni matukio machache yanayotokea katika mazingira maalumu.

Chanzo cha picha, Прес-служба Кремля
Tatizo ni kwamba mafanikio hayo yalipatikana tu pale droni ya Urusi ilipopunguza kasi, kwa mfano wakati wa kugeuka au kufanya maneva nyingine. Hata katika hali hizo, ni droni moja tu kati ya saba au nane za Ukraine zilizofanikiwa kuangusha shabaha.
Kadiri kasi inavyoongezeka na kuzidi kilomita 400 kwa saa, muundo wa kopta yenye propela nyingi unaacha kuwa faida na badala yake unakuwa kikwazo. Muundo huo hupunguza kasi badala ya kuiongeza.
Kwa kuzingatia kwamba mara nyingi droni ya kuzuia mashambulizi hulazimika kuikimbiza droni ya Urusi ili kuifikia, inahitaji kuwa na kasi kubwa zaidi.
"Droni ya kuzuia mashambulizi lazima iwe na kasi inayozidi kwa kiasi kikubwa kasi ya shabaha, ikiwezekana kwa asilimia 20–30, na iwe na mifumo ya kiotomatiki ya kutambua na kuelekeza shabaha," Alexiy Komlichenko, mkurugenzi wa maendeleo wa kampuni ya NOCTIS, ameiambia BBC. Kampuni hiyo hutengeneza droni ya kuzuia mashambulizi ya ZIRKA, yenye kasi ya kilomita 410 kwa saa.
Hata hivyo, katika kasi hizo, inakuwa vigumu kwa mwendeshaji kutambua shabaha, kuielekezea droni na kuendelea kuifuata kwa wakati. Hivyo, mchakato huo unahitaji kuendeshwa kwa njia ya kiotomatiki kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo.
Tatizo la kasi lisingekuwa kubwa kiasi hicho kama droni za Ukraine zingeweza kushambulia droni za Geran zinazoendeshwa kwa injini za ndege zikiwa zinakutana nazo uso kwa uso. Lakini jambo hilo ni gumu sana, hasa kwa sababu linahitaji mfumo mpya kabisa wa kuelekeza droni kwenye shabaha.
Kampuni ya NOCTIS inasema kukutana na shabaha uso kwa uso ili kuizuia hakuwezekani bila mambo matatu: kugundua shabaha mapema, kuelekeza droni ya kuzuia mashambulizi kiotomatiki kwenye sehemu ambayo itakutana na shabaha, na mfumo wa kujiongoza kuelekea shabaha katika hatua ya mwisho ya safari.
"Kama suluhisho linalofanya kazi la kuzuia shabaha kwa kuzikabili uso kwa uso litapatikana, litabadilisha kwa kiasi kikubwa uwiano wa uwezo wa mifumo inayotumika katika ulinzi wa anga," kampuni ya Wild Hornets, inayotengeneza mojawapo ya droni zenye ufanisi zaidi za kuzuia mashambulizi iitwayo Sting, imeiambia BBC. Toleo lake lililoundwa kukabiliana na droni zinazoendeshwa kwa injini za ndege linaitwa Sting S.
Kampuni hiyo imesema tayari inafanyia kazi suluhisho hilo.
Hata hivyo, baadhi ya watengenezaji wa Ukraine wanakiri wazi kwamba huenda droni za kawaida zenye propela nyingi tayari zimefikia kikomo cha uwezo wake.
"Kikomo chake ni karibu kilomita 400 kwa saa. Droni za kuzuia mashambulizi zenye propela nyingi haziwezi kuruka kwa kasi zaidi, bila kujali unachofanya kuziboresha," Rudolf Hakobyan, mkuu wa kampuni ya General Chereshnya, ameiambia BBC News Ukraine.
Licha ya droni ya General Chereshnya Bullet yenye propela nyingi kufanikiwa kuangusha droni kadhaa za Urusi za Geran-4 katika majira haya ya kupukutika kwa majani, mkuu huyo wa kampuni anakiri kwamba tayari wanafanyia kazi matoleo mapya yanayopaswa kuwa na ufanisi zaidi.
Droni mpya za kuzuia mashambulizi
Kwanza, droni hizo zitakuwa na muundo mpya wa mwili. Hazitakuwa tena na muundo wa kopta, bali zitafanana na ndege.
"Kasi inayozidi kilomita 400 kwa saa inahitaji ndege ndogo zinazotumia injini za ndege. Kila mtu anafanyia kazi teknolojia hii, nasi pia," Hakobyan alisema.
Kwa upande mwingine, Alexiy Komlichenko wa NOCTIS anaamini kwamba droni za kuzuia mashambulizi zinazoendeshwa kwa propela zinaweza kuendelea kuwa na umuhimu ikiwa zitawekewa mfumo wa mseto wa uzalishaji wa nguvu. Mfumo huo unaweza kujumuisha injini ya ndege (turbojet) au kifaa cha kuongeza msukumo kwa kutumia roketi, sambamba na propela na injini zake, kwa ajili ya hatua ya mwisho ya safari.
Chaguo jingine ni kuzipa droni hizo uwezo wa kujiongoza zinapokabiliana na shabaha zinazokuja upande wa pili. Hii inahusisha kukokotoa kwa usahihi njia ya kukutana na shabaha na muda wa kulipuka kwa kifaa cha kulipua kilichowekwa kwenye droni.
Tukirejea droni zenye muundo wa ndege, teknolojia hiyo si mpya kwa Jeshi la Ukraine, lakini kwa muda mrefu imekuwa kivulini mwa droni ndogo na za bei nafuu zaidi zenye propela nyingi.
Hata hivyo, kwa sasa, kwa mujibu wa wawakilishi wa mamlaka za Ukraine, ni droni zenye muundo wa ndege zinazoonyesha ufanisi mkubwa zaidi dhidi ya droni zinazoendeshwa kwa injini za ndege.

Chanzo cha picha, СБУ
Kwa mfano, Waziri wa Ulinzi Yevheniy Khmara na Rais Volodymyr Zelenskyy wameisifu hadharani droni ya Bars, ambayo ina muundo huo wa ndege.
Droni hiyo, inayojulikana kama droni ya kombora, ilitengenezwa mwaka 2025. Hata hivyo, kwa muda mrefu kazi yake kuu ilikuwa kufanya safari za masafa marefu kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya maeneo ya nyuma ya safu za ulinzi wa Urusi. Inakadiriwa kuwa na uwezo wa kusafiri hadi kilomita 1,000 na kasi ya kilomita 700 kwa saa.
Inaonekana kwamba mwaka huu mtengenezaji wake aliweza kuibadilisha ili itumike katika shughuli za kujilinda.
Droni ya Bars imeonyesha ufanisi katika jukumu hilo.
"Moja ya vikosi vyetu, wakati wa operesheni ya kivita, kilitumia droni tano za kuzuia mashambulizi za Bars na kuangusha shabaha tano za angani. Hii inamaanisha ufanisi wa asilimia 100. Kwa sasa, uzoefu huu unafanyiwa utafiti na kupanuliwa, huku wataalamu na vikosi vingine vikihusishwa katika kazi hiyo," Waziri Khmara alisema.

Chanzo cha picha, NV.ua
Hata hivyo, Rais Zelenskyy alisema kwamba droni hizo zinatengenezwa kwa ushirikiano na Ujerumani, na kwamba Ukraine itapokea droni 2,000 katika siku za usoni.
Kwa mujibu wa naibu kamanda wa Jeshi la Anga, Yuriy Cherevashenka, kufikia mwanzoni mwa Oktoba, kampuni 20 za Ukraine zilikuwa zikifanya kazi ya kutengeneza droni za kuzuia mashambulizi zinazoendeshwa kwa injini za ndege.
Kati ya kampuni hizo, 14 tayari zina bidhaa zilizokamilika na zinafanya majaribio. Droni sita kati ya hizo zinaonekana kuwa na matarajio makubwa.
Hadi sasa, serikali imeidhinisha rasmi aina mbili tu za droni hizo kwa matumizi ya kijeshi. Kasi yake ni kati ya kilomita 460 na 560 kwa saa, na kwa sasa hakuna mipango ya kuzizalisha kwa kiwango kikubwa.
"Huu si uzalishaji wa wingi kwa sababu droni hizi zina gharama kubwa kiasi. Kwa hiyo, kwa sasa tunazungumzia makumi ya droni tu, si zaidi," Kanali Cherevashenka alisema.
Kikwazo kikubwa
Changamoto kubwa zaidi ni upatikanaji wa injini ndogo za ndege zinazohitajika kwa ajili ya droni hizo.
Urusi imeweza kutatua tatizo hilo kutokana na usambazaji mkubwa wa injini kutoka China, na pia tayari imeanzisha uzalishaji wake wa ndani. Inakadiriwa kwamba uzalishaji huo huenda tayari unakidhi asilimia 40 ya mahitaji yake.
Kwa sasa, Ukraine inalazimika kutegemea watengenezaji wa Ulaya, ambao wanashindwa kufikia kasi inayohitajika ya uzalishaji.
"Injini za ndege ndiyo changamoto kubwa zaidi tuliyonayo kwa sasa. Inachukua muda mrefu, miezi kadhaa, kuwasilisha injini kutoka nchi inakotengenezwa. Na injini hizo hazifiki kila wakati kwa sababu kuna vikwazo vya usafirishaji kutoka nchi zinazozalisha au urasimu unaohusiana na nyaraka zinazohitajika ili kuvipitisha vifaa hivyo mpakani," naibu kamanda wa Jeshi la Anga alisema.
Waziri Khmara anasema nchi hiyo inajaribu kuanzisha uzalishaji wake wa injini hizo.
"Nchini Ukraine tayari kuna miradi kadhaa ya maendeleo na watengenezaji ambao serikali inawaunga mkono na kuwasaidia. Kwa jumla, kuna takribani watengenezaji 20 wa Ukraine katika makundi matatu makuu. Kwa aina moja ya injini, mahitaji yanayolengwa kufikia mwaka 2027 yanaweza kufikia takribani injini 10,000 kwa mwezi," alisema.
Haijulikani ni nani hasa ambaye amefanikiwa kuanzisha uzalishaji wa ndani wa vipengele hivi muhimu nchini Ukraine. Hata hivyo, mwanzoni mwa Septemba, mtengenezaji wa droni za Bars alisema katika mahojiano kwamba injini yake mwenyewe ilikuwa katika hatua za mwisho za majaribio.
Njia nyingine za kukabiliana na tishio
Baada ya kufikia kikomo katika maendeleo ya droni za kuzuia mashambulizi, baadhi ya watengenezaji wa Ukraine wameelekeza nguvu zao katika eneo jingine: utengenezaji wa makombora madogo na ya bei nafuu.
Tangu mwanzoni mwa vita, Urusi imekuwa ikilenga teknolojia hii, hasa kwa kutumia makombora ya kuongozwa ya kupambana na ndege ya mfumo wa Pantsir ili kuzuia mashambulizi ya droni za Ukraine.
Jeshi la Anga la Ukraine lina taarifa kutoka kwa vyanzo vyake kuhusu angalau kampuni moja kubwa ya kutengeneza droni ambayo tayari imeanza mchakato wa kubuni na kuzalisha silaha za aina hii badala ya kuendelea kutegemea droni za kawaida za kuzuia mashambulizi.
Watengenezaji wengine pia wanaangalia mwelekeo huo, wakiona uwezekano wa teknolojia hiyo.
"Tunafanyia kazi eneo hili. Lakini kwa sasa, jukumu letu la kwanza ni kutengeneza njia yenye ufanisi ya kuangusha droni za Geran zinazoendeshwa kwa injini za ndege, kwa kutumia teknolojia ambazo tuna utaalamu mkubwa zaidi nazo. Katika siku zijazo, maarifa haya yatatusaidia kutengeneza suluhisho za kuangusha shabaha ngumu zaidi, kama vile makombora madogo ya kusafiri," kampuni ya Wild Hornets iliiambia BBC.
Kuna mantiki katika hatua hiyo.
Kadiri droni zinazoendeshwa kwa injini za ndege zinavyofanana zaidi na makombora ya kusafiri katika sifa zake, ndivyo inavyozidi kuwa wazi kwamba zinahitaji kukabiliwa kwa kutumia mbinu za kawaida za kijeshi, yaani makombora ya kupambana na ndege.
Kanali Cherevashenka anasema kwamba hakuna njia nyingine ya kuepuka mwelekeo huo.
"Lazima tuelewe kwamba, mapema au baadaye, tutalazimika kutumia makombora kwa sababu itakuwa vigumu kuangusha shabaha zinazosafiri kwa kasi ya chini ya sauti kwa kutumia droni."
Kwa mujibu wake, Ukraine tayari inatumia makombora madogo, yakiwemo yanayotengenezwa na kampuni ya usanifu wa silaha ya Luch Design Bureau, kuangusha droni zinazoendeshwa kwa injini za ndege. Makombora hayo yanaonyesha ufanisi wa juu kiasi, unaokadiriwa kufikia asilimia 50.

Chanzo cha picha, Міністерство оборони України
Rais Zelenskyy, alipokuwa akizungumzia suala hili, alitaja maendeleo ya kombora la Nika, ambalo kwa sasa liko katika hatua ya majaribio.
Maelezo kuhusu mradi huo hayajatangazwa hadharani.
Kwa mujibu wa utabiri wa rais huyo, matokeo ya programu hiyo yataonyeshwa katika siku za usoni. Ikiwa itafanikiwa, uzalishaji wake utaweza kuongezwa.
"Programu ya makombora madogo — sitataja majina kwa sasa, kuna aina kadhaa — lakini bila shaka tutaona matokeo yake katika nusu ya pili ya mwezi huu. Ikiwa kutakuwa na matokeo mazuri, tutaweza mara moja kuongeza uzalishaji hadi kiwango kinachofaa," alisema.
Kutafuta njia za kukabiliana na droni za Shahed zinazoendeshwa kwa injini za ndege za Urusi hakuhusu tu ufanisi wa silaha hizo. Kwa Ukraine, suala la gharama linaweza kuwa muhimu zaidi.
Ikiwa kombora moja dogo la kupambana na ndege au droni ya kuzuia mashambulizi itagharimu karibu sawa na droni ya Geran inayolengwa, Kyiv haitaweza kushindana na Moscow katika mbio hizi za kiteknolojia. Hii ni kwa sababu daima kunahitajika droni nyingi za kuzuia mashambulizi kuliko idadi ya shabaha zinazolengwa.
Gharama ndogo ya droni za kawaida za Ukraine za kuzuia mashambulizi — ambazo hugharimu takribani mara 10 chini ya Shahed inayotumia petroli — ilikuwa mojawapo ya sababu zilizozifanya zipendwe na kutumiwa sana.
Sasa Ukraine inahitaji kutafuta suluhisho litakalokuwa na gharama nafuu kwa kiwango hicho hicho.
Chaguo jingine ni kwa watengenezaji kuachana na dhana ya droni ya kuzuia mashambulizi inayotumika mara moja tu.
Katika siku zijazo, droni hiyo inaweza kubadilishwa na kuwa jukwaa la angani linaloweza kutumiwa tena. Jukwaa hilo lingeweza kupandisha silaha ndogo za kushambulia zenye gharama nafuu hadi kwenye urefu mkubwa, ili ziweze kushambulia droni zinazoendeshwa kwa injini za ndege zikiwa katika umbali mfupi.



































