Nchi 10 zinazoongoza kwa uaminifu duniani na 10 zinazofanya vibaya zaidi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

'Waitaliano wana shauku kubwa. Waswideni ni warembo. Waingereza wanapenda kupanga foleni.' Wengi wetu tuna mazoea kutoa kauli za jumla kama hizi kuhusu watu kutoka nchi mbalimbali.

Mara nyingi, mtazamo huu wa jumla hutokana na dhana potofu, chuki au uzoefu tuliopata wakati wa likizo – na siyo ukweli wa kisayansi.

Hata hivyo, wakati mwingine, wanasayansi huwa na mawazo kama hayo: je, inawezekana kulinganisha kwa kina mwenendo wa taifa zima?

Katika tafiti moja ya aina hiyo, watafiti walijaribu kuandaa ramani ya dunia inayoonyesha nchi zenye watu waaminifu zaidi na zile zenye watu wasio waaminifu.

Hili halikutegemea uchunguzi wa tabia za watu viwanja vya ndege, bali majaribio yaliyohusisha pochi zilizopotea.

Watafiti walikabidhi jumla ya pochi 17,003 zilizodaiwa 'kupotea' kwa watu wanaosimamia biashara na taasisi mbalimbali, katika miji 355 na mataifa 40.

Kisha, wakanakili idadi ya pochi zilizorudishwa kwa wenyewe.

Haya ndiyo waliyoyabaini.

Watafiti walipopeana vipochi 'vilivyopotea', si vyote vilivyorejeshwa kwa wenyewe - na kiasi cha pesa kilichokuwemo kilikuwa na umuhimu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Matokeo ya utafiti wa uaminifu

Baada ya utafiti huo wa pochi, raia wa Uswizi, Norway na Uholanzi walitajwa kuwa 'waaminifu zaidi'.

Nchi zilizochukuliwa kutokuwa 'waaminifu' ni Peru, Morocco na China, huku China ikirudisha kama asilimia 7 ya pochi tupu na Peru asilimia 13 tu ya pochi zenye pesa.

Marekani na Uingereza walikuwa takriban katikati ya orodha, nafasi ya 21 na 22 mataifa yenye uaminifu zaidi, na asilimia 52 na asilimia 50 viwango vya pochi kurejeshwa mtawalia.

Kwa ujumla, kilele cha orodha ya uaminifu kilitawaliwa na nchi tajiri sana, ambapo nchi masikini zilielekea kuonekana mwisho wa orodha, zikipendekeza kuwa watu maskini zaidi wanaweza, kwa nadharia, kuwa na motisha kubwa za kiuchumi za kuiba.

Nchi 10 zinazoongoza kwa 'uaminifu

  • Switzerland
  • Norway
  • Uholanzi
  • Denmark
  • Uswidi
  • Poland
  • Czechia
  • New Zealand
  • Ujerumani
  • Ufaransa

Nchi 10 zinazoongoza kwa 'kutokuwa na waaminifu':

  • Uturuki
  • China
  • Morocco
  • Peru
  • Kazakhstan
  • Kenya
  • Malaysia
  • United Arab Emirates
  • Indonesia
  • Ghana
Wakazi wa Uswisi walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuzirejesha pochi kwa wamiliki wake, na hivyo kutajwa kuwa nchi yenye uaminifu zaidi kati ya zile zilizohusishwa katika utafiti huo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Sio rahisi hivyo

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Naam," huenda unawaza. "Tayari tuna orodha za viwango, kwa hivyo tumepata jibu la swali hilo. Sasa tunajua ni nchi zipi zilizo na watu waaminifu zaidi."

Hata hivyo, usikimbilie kufanya uamuzi. Ingawa orodha hizo zinaweza kuonekana kuwa za mwisho na zenye uhakika, bado hakuna makubaliano ya wazi kuhusu sababu za matokeo hayo.

"Huenda bado hatuna jibu la uhakika," anasema Dkt. Jareef Martuza, ambaye hufanya utafiti kuhusu uaminifu na profesa msaidizi katika Idara ya Mikakati na Usimamizi ya Chuo cha Uchumi cha Norway.

"Utafiti huo wa pochi unaonyesha kuwa baadhi ya nchi zilikuwa na viwango vya juu vya watu kurejesha vitu vilivyopotea kuliko nyingine; hali inayoweza kuchangiwa na mambo kadhaa, kama vile maslahi binafsi ya mtu anayefanya uamuzi, kanuni za jamii kuhusu kurejesha vitu vilivyopotea, na pengine tofauti nyingine za kimazingira au kiutamaduni."

Aidha, katika tafiti za awali kuhusu mada hiyo hiyo, watafiti walifikia uamuazi tofauti. Kwa mfano, Dkt. David Hugh-Jones kutoka Chuo Kikuu cha East Anglia (UEA) aligundua tofauti kubwa katika viwango vya uaminifu miongoni mwa mataifa mengi, kulingana na jinsi uaminifu huo ulivyopimwa.

Kwa mfano, washiriki walipoulizwa kurusha sarafu na kutoa taarifa ya matokeo—huku upande wa 'kichwa' ukizawadiwa pesa—kiwango cha uaminifu kilianzia asilimia 3.4 nchini Uingereza hadi asilimia 70 nchini China.

Lakini walipoulizwa kufanya jaribio la mtandaoni—ambapo ilikuwa rahisi kudanganya na majibu sahihi yalizawadiwa pesa—washiriki kutoka Japan walionyesha uaminifu mkubwa zaidi, wakifuatiwa na wale wa Uingereza, huku wale wa Uturuki wakiwa na kiwango cha chini kabisa cha uaminifu.

Inaonekana kuwa wanasayansi hupata majibu tofauti kulingana na swali mahususi wanalouliza kuhusu 'uaminifu'.

Kuelewa mienendo ya binadamu

Kwa hivyo, utafiti huo wa pochi zilizodondoshwa hauwezi kutuambia kikamilifu ni nchi zipi zilizo na watu waaminifu zaidi kuliko nyingine.

Hata hivyo, licha ya mapungufu yake, unaweza kutupatia maarifa kuhusu tabia za watu. Jambo moja la kushangaza lililoonekana ni kwamba, katika nchi 38, pochi zilizokuwa na kiasi kikubwa cha pesa ($94.25) zilirudishwa mara nyingi zaidi kuliko zile zilizokuwa na kiasi kidogo ($13.46).

Kwa ujumla, asilimia 51 ya watu waliokabidhiwa pochi zenye kiasi kidogo cha pesa waliripoti kupatikana kwake, ikilinganishwa na asilimia 72 kwa zile zenye kiasi kikubwa.

Katika nchi zote isipokuwa Mexico na Peru, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kurudishwa kwa pochi zenye kiasi kidogo cha pesa kuliko zile tupu.

Pochi zilizodondoshwa ni njia mojawapo ya kupima uaminifu, lakini si njia pekee – na kila jaribio linaonekana kutoa matokeo tofauti.

Chanzo cha picha, Getty Images

Haijabainikai wazi kama hilo lilitokana na watu kuwahurumia wenye pochi hizo au kusita kutenda kosa kubwa zaidi. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa pochi hizo zilikabidhiwa mahali ambapo wapokeaji walikuwa wakifanya kazi.

"Kwa kuzingatia kuwa watu katika taasisi moja wanaweza kufahamiana na kuanza kutuhumiana, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kugunduliwa iwapo pochi hiyo isingekabidhiwa," anasema Profesa Nigel Holt, mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Aberystwyth.

"Hali hii huenda ikawa tofauti na pale unapookota pochi mwenyewe kwenye usafiri wa umma, ambapo jambo pekee unalokabiliana nalo ni dhamiri yako mwenyewe."

Utafiti wa awali unaonyesha kuwa pesa haikuwa kitu pekee cha kuzingatiwa. Katika utafiti uliofanyika mwaka wa 2009, mtafiti Profesa Richard Wiseman aliacha pochi kimakusudi katika maeneo mbalimbali jijini Edinburgh, na asilimia 42 ya pochi hizo zilirudishwa kwake.

Aligundua kuwa kuna uwezekano mkubwa zaidi wa pochi kurudishwa ikiwa zilikuwa na picha ya mtu binafsi – kwa mfano, picha ya mtoto mchanga wa kuvutia, mtoto wa mbwa, au wanandoa wazee. Inabainika kuwa binadamu wana hisia na kuguswa na mambo zaidi kuliko tunavyodhani.

Tunapenda kuwa waaminifu

Unaweza pia kushangazwa na kiwango cha uaminifu walicho nacho binadamu wengi. Katika makala ya kisayansi, watafiti waliandika kuwa matokeo yao yalifichua "kiwango cha juu cha uaminifu wa kijamii katika mataifa mbalimbali".

Bila shaka, utafiti wa awali uliofanywa na Martuza ulionyesha kuwa jamii huwa na tabia ya kupuuza au kutothamini vya maadili ya raia wenzao.

Katika utafiti uliohusisha washiriki 8,000, timu ya Martuza ilichunguza jinsi watu walivyojiendesha ikilinganishwa na matarajio ya washiriki wengine. Waligundua kuwa takriban theluthi mbili ya washiriki hao walikadiria vibaya kiwango cha ukosefu wa uaminifu wa washiriki wengine, wakidhani ni kikubwa zaidi kuliko kilivyokuwa.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hata hivyo, uaminifu huo hutoweka tunapokabiliwa na vivutio au motisha—iwe ni kwa ajili ya jamii zetu au sisi wenyewe.

Katika utafiti wa hivi karibuni—ambao bado haujapitiwa na wataalamu wengine katika fani hiyo—uliohusisha zaidi ya watu wazima 5,000 nchini Marekani, Martuza aligundua kuwa wafuasi wa vyama vya Democratic na Republican walikuwa na uwezekano mkubwa wa kusema uongo ikiwa walihisi kuwa kufanya hivyo kungeinufaisha kundi lao la kisiasa.

"Katika mradi wetu unaochunguza mwenendo wa watu kutokuwa waaminifu miongoni mwa jamii mbalimbali, tunagundua kuwa watu husema uongo zaidi ili kunufaisha kundi lao la kisiasa kuliko mtu wa kundi jingine, licha ya kutopata faida au hasara yoyote binafsi kutokana na uongo huo," alisema.

Lakini uaminifu huo wa kikundi una mipaka yake. Utafiti huo pia ulionyesha kuwa, wakati mapato ya mtu binafsi yalipokuwa hatarini, watu walikuwa tayari kusema uongo ili kujilinda—bila kujali kama Mwanademokrasia au Mrepublican angepoteza kitu.

Hatimaye, maslahi binafsi husalia kuwa sababu muhimu inayoathiri kiwango cha uaminifu wa watu.

Martuza anapanga kuendeleza utafiti huu, kwa kufanya tafiti zaidi kuhusu sababu—na watu tunaoshirikiana nao—zinazotufanya tuwe tayari zaidi kusema uongo na kudanganya.

"Hili bado ni jambo ambalo hatuna taarifa za kutosha kulihusu," anasema. "Baadhi ya tafiti kutoka kwa kundi letu la watafiti zinaonyesha kuwa, mbali na maslahi binafsi, [utambulisho wa] mtu anayeathirika au anayenufaika unaweza kuwa sababu muhimu.

"Kwa kuwa maisha yetu yanazidi kuhusisha mwingiliano na watu tusiowajua katika masuala ya kifedha—ambapo tunapata tu taarifa chache kuhusu mtu mwingine—kuchunguza maadili katika mazingira mbalimbali kunaweza kuwa na manufaa makubwa kisayansi na kijamii."