Klabu, pombe na elimu, ndani ya 'Drunken Lectures' jijini Nairobi

- Author, Beldeen Waliaula
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Tafakari hali hii, umefika katika eneo la burudani na mbali na kuifurahisha nafsi yako kwa kupata burudani na muziki, unapokea pia masomo mbali mbali kama ilivyokuwa shuleni, ila tu mazingira ndiyo yaliyobadilika.
Hii ndio taswira tuliyokumbana nayo tulipozuru eneo moja la burudani Jijini Nairobi ambapo wateja waliofika wanasema kwamba wanapata mafunzo muhimu kuhusu masuala mbali mbali katika jamii, na bado wakifurahia vinywaji vyao.
Kikao hiki 'maalumu' kinafahamika kama Drunken Lectures, ambapo watu wanaopenda kubugia vileo hujumuika kubadilishana maarifa na kujifunza.
Vikao vya 'Drunken lectures' vilianza kuhudhuriwa mwaka wa 2024 baada ya maandamano makubwa ya Gen Z nchini Kenya.
Kila baada ya wiki mbili watu kutoka tabaka mbali mbali hufika katika eneo hilo la burudani, kujiburudisha baada ya siku ndefu, wengine wakisuburi foleni ndefu ya magari kupungua barabarani na kujipatia fursa ya kuhudhuria masomo katika darasa hilo maalum.

'Darasa' ndani ya klabu
Hili ni 'darasa' tofauti lisilo na ubao, madawati wala mitihani.
'Wanafunzi' wanaohudhuria vikao hivyo wanaelezea kwamba kujadili mada muhimu nje ya mazingira ya kawaida inasisimua ikilinganishwa na kuhudhuria mihadhara rasmi.
"Leo nimekuja kuwasaidia marafiki zangu ambao ndiyo wanaongoza na kufunza mada ya leo. Ila nimehudhuria vikao kama hivi awali,nimekuja pia kuskiza maoni ya watu kuhusu mada ya leo, ila mara ya kwanza nilipokuja nilipenda mazingira haya, ndiyo maana nimerudi tena," anasema Elkana Mudi ambaye ni mwanasayansi.
Joy Wangeci ambaye ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi, anasema mara ya kwanza alihudhuria kupitia mwaliko wa rafiki yake, ila sasa imekuwa kama desturi kwa yeye kuhudhuria vikao hivyo kila siku ya Jumatatu.
"Kuna jamii nzuri hapa, na mada wanazo jadili ni za muhimu na za kipekee kwa hivyo nimejipata nikirudi mara mara, pia ni sehemu nzuri ya kukutana na marafiki" Anaeleleza Joy.
Kwa Lynn Ndinda ambaye ni mwanahabari, hii ni sehemu nzuri kwake ya kutoa maoni yake, kuzungumza, kujifunza na kutangamana na marafiki.
"Nilipokuja mara ya kwanza nilihisi mwamko fulani wa akili, na mtazamo wangu wa vitu umebadilika, mada hubadilika kila wakati, kwa hivyo unajifunza mengi yanayoendelea duniani, nimetengeneza marafiki wengi, nimepata mawazo ya kufanya biashara,ukija hapa ni wewe kuamua unywe pombe na upate maarifa, au unywe tu au upate mafunzo pekee"

Mada zinazohusu jamii
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu kuanzishwa kwake, wanao andaa wanasema wamekuwa wakikutana mara mbili kwa mwezi, huku mada zikichaguliwa kwa kuzingatia masuala yanayowavutia watu na yale wanayoyaona yana umuhimu kwa jamii.
Mada hizo zinaweza kugusa historia, siasa,elimu, utamaduni na masuala mengine ya kijamii.
Tulipozuru eneo hilo, mada ya siku ilikuwa Mikrobiolojia na kuelewa virusi, bakteria na fungi ambazo huleta magonjwa.
Mhadhiri wa siku alikuwa Aboka Ely mwanamikrobiolojia, ambaye alikuwa anawahamasisha watu kutotumia dawa aina ya antibiotiki mara kwa mara, kwani bakteria zimeanza kuwa sugu, na magonjwa mengi hayaponi kwa haraka.
"kwa sasa antibiotiki nyingi hazifanyi kazi,kwa hivyo tunajaribu kufunza wanasayansi wanaotufuata kujua jinsi ya kukabiliana na tatizo hili sugu" anasema Ely
Mazingira ya klabu yanasemekana kuwa rahisi kwa watu kuelewa masuala muhimu katika jamii ambayo yanawahusu au kuwagusa moja kwa moja.
"Mtu atakumbuka nilisoma kuhusu antibiotiki nikiwa kwenye klabu, na niliambiwa sifai kujinunulia mwenyewe bila ushauri wa daktari. Hii ni tofauti kama ningekuwa na kikao rasmi kwenye ukumbi ni rahisi sana kusahau, ila katika mazingira haya ya watu kunywa pombe, ni rahisi kukumbuka kwani mtu anajua akienda kujiburudisha anapata mafunzo."
Wanaoshiriki pia hupata fursa ya kuuliza maswali na kuchangia mada ya siku na pia kutoa maoni yao
"Walevi wana mawaidha mazuri"

Mutinda Kilonzo kijana mwenye umri wa miaka 23,anasema wazo la kuanzisha 'Drunken Lectures' lilitokana na kuwa na pengo la watu kutaka kujadili masuala muhimu huku wakiburudika bila shinikizo lolote.
"Tulikuwa tunakutana kwa maktaba ila mwitikio haukuwa mkubwa. Kuna marafiki wetu wanaopenda sherehe, Nairobi watu wanapenda kubugia kikombe kimoja au viwili, na mtu akiwa kwenye klabu wao huwa na maarifa na mawaidha mengi. Tuliangalia wanachopenda wakazi wa Nairobi ambapo nikuenda klabu na kujiburudisha, kwa hivyo tukaumua tuunganishe burudani na masomo."
Drunken Lectures kulingana na Mutinda ni kikao cha watu wenye umri wote kutoka kwa wadogo hadi wakubwa

Drunken Lectures kama biashara
Licha ya kuwa sehemu ya kuwapatanisha watu, ni biashara kwa Mutinda na marafiki zake ambao wanaandaa ghafla hizi.
"Ingawa kuna kiingilio cha kulipa, mara nyingi sisi hutegemea wasamaria wema, wanaojitolea kufadhili vikao vyetu, huku wengine wakitupa biashara ili kuendeleza mihadhara hii," Anaelezea Mutinda














