Chama cha muungano nchini Afrika Kusini kimefungua kesi mahakamani kupinga sheria iliyomkasirisha Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Chama cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini, ambacho ni chama cha pili kwa ukubwa katika muungano unaounda serikali, kilifungua kesi mahakamani siku ya Jumatatu kupinga sheria ya kutaifisha ardhi; sheria ambayo Rais wa Marekani Donald Trump aliirejelea alipositisha misaada kwa nchi hiyo mwaka jana.
Kesi hiyo imezua mvutano na chama kikubwa zaidi, African National Congress, wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba.
Sheria ya Kutaifisha Ardhi (Expropriation Act) inaruhusu serikali kuchukua ardhi kwa ajili ya maslahi ya umma—katika baadhi ya matukio bila kumlipa mmiliki fidia—ikiwa ni sehemu ya juhudi za kushughulikia athari za mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid).
Imekuwa mada ya mjadala mrefu na mara nyingi wenye mvutano mkali kwa miaka mingi, na ikapitishwa kuwa sheria na Rais Cyril Ramaphosa mnamo Januari 2025. Hakuna ardhi iliyochukuliwa hadi sasa.





