Kwa nini dhahabu ya Afrika haifanyi Afrika kuwa tajiri?

p

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Afrika ina akiba kubwa ya dhahabu duniani. Nchi kama Afrika Kusini, Ghana, Mali, Sudan, Tanzania, na Burkina Faso huchimba mamia ya tani za madini hayo ya thamani kila mwaka, na hivyo kuongeza nguvu katika akiba ya benki kuu duniani, huuzwa masoko ya vito vya kifahari, na kutumika katika vifaa vya elektroniki vya kisasa.

Hata hivyo, unapotembea katika miji na vijiji vilivyo karibu na migodi hii mikubwa, hakuna miji iliyostawi, wala shule nzuri, wala vituo vya afya vya kisasa. Badala yake, utakutana na umaskini, uharibifu wa mazingira, na miundombinu chakavu.

Hali hii huu inatajwa na wachumi kama "Laana ya Rasilimali.” Ambapo mataifa yenye wingi wa maliasili na rasilimali hazina ukuaji mzuri wa uchumi, kuna tawala za kifisadi, na maendeleo mabovu katika maisha ya binadamu, kuliko nchi zisizo na utajiri kama huo.

Kwa nini dhahabu inashindwa kuleta utajiri barani Afrika?

Athari za Ukoloni

Ili kuelewa rasilimali ya dhahabu barani Afrika, mtu lazima aangalie historia. Wakati wa enzi ya ukoloni, uchimbaji wa madini katika bara la Afrika ulibuniwa kwa ajili ya usafirishaji wa nje tu.

Miundombinu kama vile njia za reli, barabara, na bandari iliundwa sio kuunganisha masoko ya ndani au kukuza biashara ya kikanda, bali ili tu kuhamisha madini hayo kutoka migodi ya ndani moja kwa moja hadi bandarini na kuziingiza katika meli zinazoelekea miji mikuu ya Ulaya.

Kufuatia uhuru katikati ya karne ya 20, mataifa mengi huru ya Afrika yalirithi mifumo hii ya uchimbaji bila kuwa na mtaji, ufundi, miundombinu, au mamlaka ya kisheria ya kutaifisha au kuichakata.

Kwa hivyo, makampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini yalijiingia kama mbadala wa ukoloni na kudhibiti uchimbaji, na kuhifadhi mtiririko wa kiuchumi ambapo mtaji na faida huhamia nje huku madeni ya kijamii, kiuchumi, na kimazingira yakibaki ya ndani.

Afrika kushindwa

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Kushindwa kwa sekta ya dhahabu barani Afrika kumetokana na ukosefu wa nyongeza ya thamani ya ndani. Mataifa mengi yanayozalisha dhahabu barani Afrika husafirisha dhahabu nje katika kama mali ghafi au nusu iliyosafishwa.

Faida za kiuchumi, uzalishaji wa ajira, na mkusanyiko wa utajiri katika dhahabu hutokea chini ya mnyororo huu:

Kuibadilisha dhahabu kuwa kipande safi kwa ajili ya uwekezaji. Kubadilisha dhahabu kuwa vito vya kifahari, vipuri vya viwandani, na sarafu zilizotengenezwa kwa dhahabu.

Vituo vya usafishaji duniani kote viko nchini Uswisi, Falme za Kiarabu (Dubai), India, na Uingereza kusafisha dhahabu ghafi kutoka Afrika, na nchi hizo ndio hupata faida kubwa, na kuuza nje bidhaa zinazotokana na dhahabu kwa faida kubwa.

Kwa kusafirisha nje dhahabu ghafi, mataifa ya Afrika kimsingi husafirisha nje kazi za usafishaji dhahabu na mapato ya kodi, na kubaki chini kabisa katika kiwango cha faida ya Biashara hiyo kimataifa.

Magendo na ulaghai

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Sehemu kubwa ya dhahabu ya Afrika haijawahi kuingizwa katika takwimu za biashara za kitaifa au rejista za kodi za serikali. Makundi ya ufuatiliaji wa kimataifa yanakadiria kwamba dhahabu yenye thamani ya mabilioni ya dola husafirishwa kinyume cha sheria kutoka barani humo kila mwaka.

Mamilioni ya wachimbaji madini wa Afrika hufanya kazi katika shughuli zisizo rasmi. Ingawa hupata mapato muhimu kwa kaya zao vijijini, dhahabu isiyo rasmi hununuliwa mara kwa mara na wanunuzi haramu, husafirishwa kwa njia ya magendo kuvuka mipaka, na kusafirishwa hadi vituo vya biashara vya kimataifa bila uthibitisho.

Na baadhi ya mashirika na makampuni ya biashara yanatoa ripoti mbovu kuhusu kiasi, uzito, ubora au usafi wa dhahabu inayosafirishwa nje ili kupunguza ushuru wa mauzo ya nje na majukumu ya kodi ya kampuni, na hivyo kunyima hazina za serikali mapato muhimu.

Dhahabu hiyo inapofika katika vituo vya kimataifa vya kusafisha, mara nyingi huyeyushwa, huthibitishwa tena, na kuunganishwa katika mnyororo wa ugavi wa kifedha wa kimataifa, na kuacha mataifa itokako bila faida yoyote ya kiuchumi.

Uwekezaji wa kinyonyaji

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Wakati wa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, chini ya shinikizo la kuvutia Uwekezaji, serikali nyingi za Kiafrika zilisaini Mikataba ya Uwekezaji wa Madini ya muda mrefu ambayo ilipendelea sana makampuni ya madini ya kigeni.

Ili kupunguza hatari za kisiasa na kifedha, serikali mwenyeji mara nyingi hupewa, viwango vya chini vya mrahaba. Mara nyingi huwa ni kati ya 3% na 5% ya thamani jumla na misamaha ya mshuru kwa makampuni hayo.

Mikataba ya kisheria inayozuia kodi kwa miaka 20 hadi 30 kuongezwa, ikizuia serikali kuongeza kodi au kurekebisha mirabaha hata wakati bei za dhahabu duniani zilifikia viwango vya juu.

Kwa hivyo, bei za dhahabu zinapopanda duniani kote, makampuni ya madini ya kimataifa yanaripoti faida kubwa kwa wanahisa wa kimataifa, lakini hazina za serikali za Afrika zinapokea malipo ya mrabaha ya wastani tu.

Uharibifu wa mazingira na jamii

l

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

Wakati faida ya umma kutokana na uchimbaji wa dhahabu bado ni ndogo, gharama za ndani ni kubwa. Uchimbaji mkubwa unahitaji kuondoa watu katika maeneo makubwa ya ardhi, kuharibu mifumo ikolojia, na huharibu vyanzo vya maji.

Zaidi ya hayo, uchimbaji madini usio rasmi na usiodhibitiwa huingiza kemikali hatari kama vile zebaki na sianidi katika mifumo ya mito na udongo.

Wakazi wa vijijini wanaozunguka maeneo haya wanakabiliwa na sumu ya metali, ardhi ya kilimo iliyoharibiwa, na vyanzo vya maji vilivyochafuliwa.

Badala ya kuwaondoa jamii za wenyeji katika umaskini, uchimbaji wa dhahabu mara nyingi huwafanya kaya za kilimo kuwa maskini kwa kuharibu msingi wa mazingira wa riziki zao.

Kitendawili cha dhahabu barani Afrika si jambo lisiloepukika, bali ni matokeo ya miundo ya kihistoria, ukosefu wa usawa wa kibiashara, na uchaguzi wa sera. Ili dhahabu iwe injini ya utajiri halisi wa ndani, mageuzi muhimu kote barani.