Waridi wa BBC: "Mazishi yangu tayari yalikuwa yameandaliwa" asimulia mwanamke anayeishi na Virusi vya HIV

- Author, Beldeen Waliaula
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Margaret Lavonga,mwenye umri wa miaka 55 na mama wa watoto wawili, ameishi na virusi vya HIV kwa zaidi ya miaka 30.
"Nilijua niko na virusi nikiwa mjamzito baada ya kufanya vipimo na nikaambiwa matokeo yangu si mazuri"
Kipindi hicho kuugua au kupatikana na virusi vya HIV ilikuwa jambo baya kutokea kutokana na unyanyapaa uliokuja na ugonjwa huo.
"Ni wakati ambao walikuwa wameeka mabango kila mahali yakiwa na magofu ya watu ya kionyesha kichwa na mifupa.
Nilipoambiwa kwamba niko na virusi, niliona kwamba mimi nakufa kesho yake."
Kipindi hicho Margret anapatikana na virusi vya HIV, madawa ya kupunguza makali ya ugonjwa wa ukimwi yalikuwa bado hayajafika nchini Kenya, ilimlazimu kuficha hali yake ya Afya hadi alipojifungua mwaka wa 1999, ila bahati mbaya mwanawe alifariki miezi miwili baadaye.
"Hospitalini kujifungua hali ilikuwa ngumu, kila mtu aliogopa kunikaribia wakihofia kuambukizwa ukimwi"

Baada ya hapo Margaret akaanza kuugua, kwa muda wa miaka miwili, hangeweza kutoka kitandani, akihudumiwa na dadake ambaye alikuwa anaelewa hali yake wakati huo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alilazwa hospitalini mara kadhaa, bahati nzuri alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupata madawa ya kupunguza makali ya ukimwi nchini Kenya.
Kisa cha kwanza cha HIV kiliripotiwa nchini Kenya mwaka wa 1984, na kwa wale walioapatikana na ugonjwa huo wakati huo, siku zao za kuishi zilikuwa zinahesabiwa.
Wengi walikumbana na unyanyapaa, kutengwa na familia na marafiki, huku watoto wengi wakisalia mayatima.
Ila kuna wale kama Margaret waliopata virusi vya HIV miaka mwaka wa 1999, wameishi nao kwa zaidi ya miaka 30 na sasa wanazeeka wakiwa na virusi hivyo.
Kwake safari ya kumeza dawa za kupunguza makali ya ukimwi ARV's haijakuwa rahisi.
"Mwanzoni tulikuwa tunapewa dawa tatu tofauti,hizo dawa zilikuwa kubwa, zilikuwa na madhara mengi, wakati mwingine ungemeza dawa hizo ungepata ndoto au njozi haujihisi ukiwa wewe, wakati mwingine unaendesha.
Naweza sema wale wanapata virusi kwa sasa wanabahati kwasababu dawa wanazomeza hazina madhara kubwa."
Margaret anatuelezea kuwa kabla ya kuanza kumeza madawa alikuwa tayari kwa kifo kwani tayari alikuwa amepunguza uzani wa mwili wake hadi kufikia kilo 34, na wazazi wake waliposikia kuhusu hali yake wakaanza kuandaa mazishi yake.

Kuna kipindi aliacha kumeza dawa kwa madai kuwa ameokoka na kutegemea maombi, ila hali yake ya afya ikadorora tena mara moja, ikabidi akue mtiifu kwa kumeza dawa hadi sasa.
Virusi vya HIV hulenga seli nyeupe za damu, na kudhoofisha kinga ya mwili. Hii huifanya rahisi kwa mtu kuambukizwa magonjwa kama vile kifua kikuu Pamoja na magonjwa mengine.
Ila kuishi na kuzeeka ukiwa na virusi vya HIV inakuja na changamoto zake.
"Ingawa sasa nina ujasiri wa kuzunguma kuhusu ugonjwa huu, wakati mwingine mimi hujifungia chumbani na kulia. Wakati mwingine nahisi kama singekuwa na virusi hivi labda ningekuwa nimepiga hatua fulani maishani."
Changamoto anayoyapitia sasa ni maradhi ya uzee ambayo yanashinikizwa na yeye kuwa na virusi vya HIV.
"Kwa sasa nina Athritis, jongu, shinikizo la damu,matatizo ya macho. Kwa kawaida watu wakizeeka hupata magonjwa ya uzee, lakini kwetu magonjwa ya uzee huja na makali zaidi ikilinganishwa na watu wengine."
Kumeza dawa kila siku anatuelezea si jambo rahisi. "Wakati mwingine mimi hutamani kuchukua likizo ya kutomeza dawa, lakini nina watu wanaoniunga mkono na kunihimia kila siku niendelee na safari hii"
Ingawa matibabu ya virusi hivyo yameimarishwa na kuboreshwa kila kuchao, changamoto bado ipo kwa vijana ambao hawazingatii kumeza dawa za kupunguza makali ya HIV kila siku.
"Ningependa kuwahimiza kizazi cha sasa wanaopatikana na virusi vya HIV au waliozalia nayo, safari ya kuishi na virusi vya HIV siyo rahisi lakini haiuwi,kitu ambacho kinauwa ni magonjwa tegemezi, kwa hivyo ukipatikana na ugonjwa huu meza dawa na utaishi Maisha marefu, kama bado huna ni bora kuendelea kujikinga"
Kenya kwa sasa ina idadi kubwa ya watu wanaoishi na virusi vya HIV ambao wanazaidi ya umri wa miaka 50.
Kati ya wagonjwa million 1.4 wanaoishi na virusi vya HIV nchini Kenya, 27% wanazaidi ya miaka 50.
Ndoto ya Maragaret ni kuishi hadi kufikia miaka 120 licha ya kuwa na virusi vya HIV.
"Kwa wazee wenzangu nawasishi wasikate tamaa, wasiache kumeza dawa, wacha tufe na uzee lakini tusife kwasababu tumeacha kumeza dawa magonjwa tegemezi yakatumaliza," anasema Margaret.















