Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Polisi, jeshi watanda kuzuia maandamano 7/7 Tanzania
- Author, Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC News Swahili
- Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Usalama unaendelea kuimarishwa kwenye miji mikubwa nchini Tanzania ambapo kumeshuhudiwa maafisa wa polisi na jeshi wenye silaa wakifanya doria, huku Serikali ikionya kuwa itachukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakayehamasisha vurugu siku hiyo.
Maafisa hao wameonekana kwa wingi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye mizunguko ya barabara na mitaa katika jiji kuu la kibiashara la Dar es Salaam na miji mingine, hali ambayo wengi wanadaiwa kutokuwa ya kawaida, baadhi yao wakisema ni njia ya kudhibiti maandamano yanayopangwa kufanyika siku ya Jumanne.
Hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii, wanaharakati wamekuwa wakihamasisha kufanyika maandamano siku ya Jumanne, kushinikiza kuwepo kwa uhuru wa kisiasa na uwajibikaji kufuatia matukio ya mauaji yaliyotokea kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Maandamano hayo yanayodaiwa kupangwa yanakuja wakati ambapo serikali ikidai kuwa na taarifa za kiintelijensia kuwa kuna watu wanapanga kudhuru baadhi ya viongozi, wananchi pamoja na kuharibu mali.
Wakati hayo yakiedelea, Jumanne ni siku ambayo ni ya kitaifa ya Maonesho ya Biashara ya Dar es Salaam , maarufu kama Saba Saba, ambayo ni miongoni mwa maonesho makubwa zaidi ya kibiashara nchini Tanzania.
Mitandao ya kijamii sababu ya maandamano?
Serikali imedai kuwa kuna raia ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano au vurugu hivyo imejipanga kuchukua hatua kudhibiti hali yoyote ile itakayojitokeza.
Kwa mujibu wa viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania, uhamasishwa mkunbwa umekuwa ukifanyika kupitia mitandao ya kijamii na wanaharakati ambao wenye lengo la kuleta vurugu.
Japokuwa wanaharakati hao mitandaoni wamekuwa wakisema lengo lao ni kudai mageuzi ya kidemokrasia, haki kwa watu waliouawa wakati wa machafuko yaliyofuatia uchaguzi pamoja na uwajibikaji kwa viongozi wa Serikali na vyombo vya dola.
Polisi yadai watu wapanga mauji, kuharibu mali
Polisi wanasema wanaendelea kufuatilia kwa karibu viashiria vya baadhi ya watu wanaodaiwa kuhamasisha vurugu na kupanga kufanya maandamano yasiyofuata taratibu za kisheria na kiusalama.
Ili kukomesha suala hilo, tayari limekamata baadhi ya watu kwa ajili ya uchunguzi, bila kuweka bayana idadi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumapili, Msemaji wa Polisi, David Misime alisema, "Ufuatiliaji unaoendelea kufanyika umeendelea kubaini kuwa hao watu wanaendelea kuhamasisha vurugu kwa kuhamasishana kuwa safari hii hawaji kinyonge…
" …hivyo watahakikisha wanaua baadhi ya viongozi, wananchi watachoma shule, moto wataharibu na kupora mali za umma na binafsi na kwamba wataua askari wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kupora silaha wazitumie kwenye mipango waliyopanga ya kuhakikisha amani inatoweka nchini."
Misime alisema hali ya usalama nchini Tanzania inaendelea kuwa tulivu na kwamba mamlaka hazitarajii kutokea kwa matukio yoyote yasiyotarajiwa.
'Jeshi ladai ni upotoshaji kuwa litalinda waandamanaji'
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) nalo lilitoa onyo Jumamosi kwa watu na makundi yanayodaiwa kuchochea kile lilichokitaja kuwa ni vurugu nchini, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua stahiki za kisheria.
Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Sylvester Mangure, alisema," Kumekuwa na uhamasishaji na upotoshaji, unaofanywa na wasiolitakia mem anchi yetu, kwa kuwataka wananchi kuushiriki kwenye vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi…"
"…Watu hao wanafanya uhamasisshaji na upotoshaji huo kwa kulichafua jeshi kwamba litahusika kuwalinda wafanya vurugu na ghasiza hizo.Vitendo hivyo vinaweza kusababisha madhara kwa washiriki na wananchi wengine, uharibifu wa mali, kuvuruga shughuli za wananchi za kila siku na hatimaye kuharibu uchumi wa nchi," alisema Mangure.
Jeshi hilo pia lilieleza kuwa hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari na mipaka ya taifa ipo salama, likiwataka wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu.
Kundi la 'chui' laibuka likidai kukabiliana na waandamanaji
Wakati hayo yakiendelea, kundi lililoibuka likidaiwa kuongozwa na mtu anayejitambulisha kama kiongozi wa dini, Sheikh Saidi Mwaipopo, likizua mjadala mtandaoni kuhusu iwapo kundi lake linalojiita "Mbwamwitu" au "kundi la chui" linafadhiliwa na serikali kwa malengo ya kisiasa.
BBC haijaweza kudhibitisha uhusiano wa kundi hilo na Serikali ya Tanzania.
Katika siku za karibuni, Mwaipopo ameonekana kwenye mitandao ya kijamii akizungumza na vyombo vya habari akisema kuwa kundi hilo linakusudia kukabiliana na waandamanaji siku ya Jumanne.
Katika video ameonekana, kiongozi huyo akiwa na watu walioziba nyuso zao huk akitangaza kuwa atasambaza maelfu ya vijana wa aina hiyo katika mikoa mbalimbali nchini ili kukabiliana na waandamanaji.
"Makundi yetu yatamkabili mtu yeyote atakayejaribu kuandamana. 'Chui' mmoja hapa anaweza kukabiliana na watu 15 wenye silaha ndogo ndogo kwa wakati mmoja," alisema
Jeshi la Polisi halijajinu ombi la BBC la kutaka ufafanuzi kuhusu kundi hilo na iwapo linafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria na kwa makubaliano na Serikali.
Mikutano ya kisiasa yasitishwa kwa muda usiojulikana
Mnamo Juni 26, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi iliisimamisha mikutano yote ya hadhara ya kisiasa, ikisema uamuzi huo ulikuwa muhimu kutokana na vitisho vya kiusalama.
Hata hivyo, makundi ya upinzani yalipinga hatua hiyo, yakisema ni kinyume sheria na inakiuka uhuru wa kikatiba.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, alisema kusimamishwa kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa ni hatua ya muda inayolenga kusaidia vyombo vya dola kuwabaini watu wanaoshukiwa kupanga vitendo vya vurugu.
Alisema shughuli za kawaida za kisiasa zinaweza kurejea mara baada ya changamoto za kiusalama kushughulikiwa.
Katambi alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya serikali kubaini kuwa baadhi ya mvutano wa kisiasa umechangia hali ya taharuki, huku kukiwa na taarifa za miito ya maandamano kuelekea kilele cha Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
"Hatua hii inalenga kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi katika mazingira ya amani na utulivu, huku vyombo vya dola vikifanya kazi ya kuwabaini wahalifu bila changamoto zinazoweza kusababishwa na mikusanyiko mikubwa ya watu," alisema Katambi.
Vyama vya siasa vimepinga hatua hiyo wakisema kuwa ni hatua ya kudhoofisha demokrasia nchini Tanzania na kwamba zuio hilo halipo kikatiba.
Chama cha ACT Wazalendo kimesema kinakusudia kupinga agizo hilo la serikali mahakamani.
Chama kikuu cha upinzani, Chadema pia kimepinga hatua hiyo kikisema kuwa ni hatua ya uminyaji haki na kinalenga kudhoofisha upinzani huku wakidai kuwa serikali imeshindwa kujibu hoja muhimu zenye maslahi ya taifa.
Hata hivyo Serikali imesisitiza kuwa imesitisha kwa sababu za kiusalama.
Je, Tanzania ina changamoto za kiusalama?
Mnamo Juni 27, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, alitetea hatua hizo za serikali kuwa zinalenga kuimarisha usalama.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi mkoani Singida, Waziri Mkuu alisema kuwa zuio la muda la mikutano ya hadhara ya kisiasa lilitokana na taarifa za kiintelijensia zilizoashiria kuwepo kwa mipango ya kufanya mashambulizi ya vurugu.
Alisema polisi walikamata watu kadhaa wanaotuhumiwa kuwalipa vijana wa Kitanzania kushiriki katika maandamano, akiwemo mtu mmoja ambaye alidaiwa kukiri kuwa alikuwa akilipwa shilingi milioni tano za Kitanzania (zaidi ya dola 1,800 za Marekani) kwa mwezi.
Julai Mosi, akiwa mkoani Mara, Waziri Mkuu akiwa mkoani Mara alisema linapokuja suala la nchi na usalama wa wananchi wake, hawatapuuza jambo lolote hata likiwa ni dogo.
"Nimekuwa nikisisitiza kwamba amani ya nchi ikivurugwa, muathirika wa kwanza ni mwananchi mwenyewe. Pasiwepo mtu ama kwa makusudi ama kwa kudaganywa wa kukubali kuiwasha moto nchi yako," alisema na kuongeza kuwa Watanzania wasikubali kufuata uhamasishaji unaoendelea mitandaoni kwa lengo la kuanzisha vurugu,
Mijadala iko vipi?
Wengi wanajadili vizuizi vya sasa, lakini pia wengine wamefufua mjadala wa muda mrefu kuhusu mikutano ya kisiasa na uhuru wa kuandamana nchini Tanzania.
Raia mmoja wa Dar es Salaam, (jina tunalo) aliiambia BBC, "Sioni haja ya maandamano maana ndugu zetu wataishia kuumia lakini wananchi wanapaswa kusikilizwa na serikali kutatua matatizo yao."
Raia mwingine katika jiji la Mwanza alisema kuwa ni haki ya kikatiba kuandamana na kwamba kuzuia hakutajenga kitu zaidi ya kuongeza chuki kati ya raia na Serikali.
Hivi karibu kupitia mtandao wake wa Instagram, msanii nguli wa mziki wa Bongo Flava nchini Tanzania,Selemani Msindi maarufu Afande Sele alisema yanayoendelea ni kwasababu sababu zilizosababisha maandamano wakati wa uchaguzi hayajashughulikiwa.
Sele alisema, "Baada ya maandamano ya oktoba, nchi inakuwa kwenye sintofaahamu, yote ni kwasababu hatujashughulikia mzizi wa matatizo…
"…kwamba zile sababu zinazosababisha watu kuandamana hazijashughulikiwa," alisema Msanii huyo huku akisema kuwa haungi mkono maandamano yoyote kwani tayari Rais Samia alishakwisha toa ahadi ya kupatikana kwa katiba mpya.
Oktoba 2025 imechangia haya?
Mvutano wa sasa wa kisiasa unadaiwa kuchangiwa na matukio ya awali na yaliyofuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Katika, uchaguzi huo Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa kupata takriban asilimia 98 ya kura, baada ya wagombea wawili wakuu wa urais kutoka upinzani kushindwa kushiriki uchaguzi huo.
Hatua hiyo ilizua ukosoaji kutoka kwa vyama vya upinzani, wanaharakati na kuchangia kuzuka kwa maandamano makubwa siku ya uchaguzi na siku zilizofuata.
Baadaye, Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na serikali ilibaini kuwa watu 518 walifariki kutokana na kile ilichokiita 'vifo visivyo vya kawaida' wakati wa machafuko hayo, wakiwemo watu 197 waliouawa kwa risasi.
Hata hivyo, vyama vya upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu vilipinga matokeo hayo, vikidai kuwa idadi halisi ya waliofariki ilikuwa kubwa zaidi na vikilishutumu jeshi la polisi kwa kuhusika na vifo vya watu wengi.
Serikali imekanusha tuhuma kwamba polisi na vyombo vya usalama vilitumia nguvu kupita kiasi na hapo awali ilieleza kuwa machafuko hayo yalikuwa jaribio la kuipindua serikali iliyoingia madarakani kupitia uchaguzi.
Je, jaribio la maandamano lilitokea tena hivi karibuni?
Mvutano wa kisiasa ulioendelea katika miezi iliyofuata baada ya uchaguzi huo, ikiwemo kuwepo maandamano yaliyopangwa Desemba 9, mwaka jana lakini yalidhibitiwa na vyombo vya usalama.
Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema wanaharakati wamekuwa wakikabiliwa na kukamatwa, kushambuliwa na kutekwa, huku viongozi wa upinzani wakidai kuwa nafasi ya shughuli za kiraia imeendelea kubanwa kwa kiasi kikubwa.
Mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa upinzani nchini, Tundu Lissu, alikamatwa mwezi Aprili 2025 na kushtakiwa kwa uhaini. Mpaka sasa ni zaidi ya mwaka mmoja kesi yake bado inaendelea mahakamani, jambo ambalo limekuwa kitovu cha mjadala kwa wafuasi wa upinzani na wanaharakati wa haki za binadamu wanaodai kuwa kucheleweshwa kwa mwenendo wa kesi hiyo kumeongeza mgawanyiko wa kisiasa.
Wachambuzi wa siasa, wamekuwa wakieleza kuwa kwa miongo kadhaa, Tanzania ilikuwa ikijijengea sifa ya kuwa miongoni mwa nchi zenye utulivu wa kisiasa ikilinganishwa na mataifa mengine ya ukanda wa Afrika Mashariki. Hata hivyo, matukio yaliyofuatia uchaguzi huo yameibua maswali mapya kuhusu utawala wa kidemokrasia, uhuru wa kisiasa na uhusiano kati ya dola na vyama vya upinzani.