Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump asema ameshangazwa na Wairani kulia katika mazishi ya Khamenei

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Trump ameiambia Axios kwamba pande zote mbili zimekubaliana kusitisha mazungumzo kwa muda wa wiki moja hadi shughuli za mazishi zitakapokamilika.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Serikali ya Tanzania yapinga mijadala ya mapema kuhusu uchaguzi wa 2030

    Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kuwafuatilia na kuwabaini watu wanaoendeleza mijadala kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 badala ya kujikita katika shughuli za maendeleo.

    ''Mkuu wa mkoa fuatilia wale wote ambao wanaendelea kuzungumzia uchaguzi uliopita tunataka tuwajue'', Waziri Mkuu wa Tanzania amuagiza Kanali Mtambi.

    Vile vile amesema: ''Tuna wananchi kiu yao ni kuona barabara.Sisi viongozi tunapata wapi muda?, Kila wakati kwa makundi ya whatsapp ni kujadili uchaguzi wa 2030,'' anasema Mwigulu.

    Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Bunda, mkoani Mara, Dkt. Nchemba amesema serikali haitaki kuona au kusikia mijadala ya kisiasa kuhusu uchaguzi wa mwaka 2030 kwa wakati huu, akisisitiza kuwa mjadala huo hauchangii juhudi za kuwahudumia wananchi na kuharakisha maendeleo.

    ''Kama sio ubinafsi ninini?Tuachane na mambo ya ubinafsi, tuelekeze huku kwenye mambo ya maendeleo'',anaendelea kusisitiza agizo hilo.

    Kauli hiyo inakuja wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza ajenda yake ya maendeleo na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

    Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, uchaguzi mkuu hufanyika kila baada ya miaka mitano, huku mjadala kuhusu uchaguzi wa mwaka 2030 ukiibuka mapema katika baadhi ya mijadala ya kisiasa na kwenye mitandao ya kijamii.

    Taasisi za kimataifa, zikiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, zimekuwa zikisisitiza umuhimu wa mazingira ya kisiasa yanayoruhusu ushiriki wa wananchi katika mijadala ya umma sambamba na kuendeleza juhudi za maendeleo na utawala bora.

    Haya yanajiri baada ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema kuwa litachukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu watakaojihusisha na vitendo vinavyohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani kwa maandamano yanayodaiwa kufanyika siku ya saba ya mwezi wa saba wiki ijayo.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Urusi yapendekeza usitishaji wa mapigano karibu na eneo la Kostiantynivka

    Urusi imependekeza kusitishwa kwa mapigano katika eneo la Kostiantynivka ili kuruhusu kukusanywa na kukabidhiwa kwa miili ya wanajeshi wa Ukraine waliouawa wakitetea mji huo.

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema iko tayari kutekeleza hatua hiyo Jumatatu kati ya saa sita mchana na saa kumi na mbili jioni kwa saa za Moscow na Kyiv.

    Moscow imesema inatarajia kupata jibu kutoka Ukraine ifikapo Jumapili mchana.

    Urusi inaendelea kudai kuwa imeuteka mji wa Kostiantynivka, kitovu muhimu cha ulinzi wa maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Donetsk ambayo bado yanadhibitiwa na Ukraine.

    Aidha, haijawasilisha ushahidi wa kuthibitisha madai hayo. Kwa upande wake, uongozi wa kijeshi wa Ukraine umekanusha madai hayo, ukisema makamanda wa Urusi mara nyingi hutangaza ushindi ambao haujapatikana.

    Hata hivyo, Jeshi la Ukraine limekiri kuwa hali katika Kostiantynivka ni ngumu na kwamba wanajeshi wa Urusi wanaendelea kuingia mjini humo katika makundi madogo.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Sala ya mazishi yafanyika kwa kiongozi wa zamani wa Iran Ali Khamenei na familia yake

    Sala ya mazishi imefanyika mjini Tehran kwa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, na baadhi ya wanafamilia wake waliouawa katika shambulizi la Marekani na Israel mapema mwaka huu.

    Sala hiyo iliongozwa na Ayatollah Jafar Sobhani katika Msikiti wa Imam Khomeini, ambao ni moja ya vituo vikuu vya kidini na kitamaduni nchini Iran.

    Ibada hiyo ilifanyika katika hatua tatu. Hatua ya kwanza ilihusisha sala ya mazishi ya Ali Khamenei. Hatua ya pili ilihusisha sala za mazishi za binti yake Bushra Khamenei, mkwe wake Misbah al Huda Baqeri, na shemeji yake Zahra Haddad Adel.

    Hatua ya tatu ilihusisha sala ya mazishi ya mjukuu wake mdogo, Zahra Mohammadi.

    Soma zaidi:

  4. Iran yasema itatoza ada za huduma kwa meli zinazopita mlango bahari wa Hormuz

    Iran imesema itaanza kutoza ada za huduma kwa meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz, hatua ambayo Marekani imeipinga.

    Balozi wa Iran nchini China, Abdolreza Rahmani Fazli, amesema katika Kongamano la Amani Duniani mjini Beijing kwamba Iran, kwa ushirikiano na Oman, inaandaa utaratibu mpya wa kusimamia njia hiyo muhimu ya majini.

    “Kama nchi ambayo sehemu ya Mlango wa Hormuz iko ndani ya maji yake ya eneo, bila shaka tutatoza ada za huduma,” alisema, huku akisisitiza kuwa ada hizo si ada za kupita.

    Kwa mujibu wake, utaratibu huo unalenga kuimarisha usalama wa meli zinazopita katika mlango huo, kufuatilia usafiri wa majini na kushughulikia athari za kimazingira zinazotokana na msongamano wa meli.

    Aidha, amesema nchi zilizoiunga mkono Iran katika nyakati ngumu zitapatiwa upendeleo maalum.

    Kwa mujibu wa makubaliano ya awali kati ya Iran na Marekani ya kusitisha vita, meli za kibiashara zinaruhusiwa kupita katika Mlango wa Hormuz bila kulipa ada kwa siku 60.

    Hata hivyo, bado haijabainika utaratibu utakaotumika baada ya kipindi hicho kumalizika.

    Kwa kawaida, karibu asilimia 20 ya mafuta ghafi na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani hupitia katika Mlango wa Hormuz.

    Wakati wa vita vya Mashariki ya Kati, Iran ilizuia kwa kiasi kikubwa njia hiyo, hali iliyosababisha bei za nishati duniani kupanda kwa kasi.

    Soma zaidi:

  5. Morocco yatinga robo fainali za Kombe la Dunia kwa kuichapa Canada

    Morocco imekuwa timu ya kwanza kufuzu robo fainali za Kombe la Dunia la Wanaume baada ya kuifunga Canada mabao 3 kwa 0 katika mchezo wa hatua ya 16 bora.

    Kwa matokeo hayo, Canada imekuwa mwenyeji wa kwanza wa mashindano hayo kuaga michuano.

    Ezzedine Ounahi aliifungia Morocco mabao mawili ya kwanza, kabla ya Sofyan Rahimi kufunga bao la tatu katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza.

    Morocco, mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika, sasa itasubiri mshindi wa mechi kati ya Ufaransa na Paraguay ili kujua mpinzani wake katika robo fainali.

    Soma zaidi:

  6. Trump asema ameshangazwa na Wairani kulia katika mazishi ya Khamenei

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema alikuwa akifuatilia mazishi ya kiongozi wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, na kushangazwa na kuona baadhi ya Wairani wakilia wakati wa mazishi.

    Akizungumza na tovuti ya habari ya Axios, Trump alisema alikuwa na dhana kwamba watu wengi nchini Iran walimchukia Ali Khamenei.

    Hata hivyo, baada ya kutafakari kwa muda, alinukuliwa akisema: “Huenda machozi hayo si ya kweli.”

    Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Trump alirudia madai yake kwamba Wairani walikuwa “wakisihi kufikiwa kwa makubaliano”.

    Aidha, alisema pande zote mbili zimekubaliana kusitisha mazungumzo kwa muda wa wiki moja hadi shughuli za mazishi zitakapokamilika.

    Trump aliongeza kuwa katika kipindi hicho, hakuna upande utakaofyatulia mwenzake risasi. Alisema: “Wote wako hapo. Risasi moja tu ingeweza kuwaondoa wote, lakini hatutafanya hivyo, kwa sababu hapo hatutakuwa na mtu wa kufanya naye mazungumzo.”

    Rais huyo wa Marekani pia aliiambia Axios kwamba Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameomba kukutana naye katika Ikulu ya White House, na kwamba mkutano huo unaweza kufanyika baada ya kurejea kutoka mkutano wa NATO wiki ijayo.

    Akizungumzia uhusiano wake na Netanyahu, Trump alisema: “Tuna uhusiano mzuri sana. Anajua nani mwenye mamlaka.”

    Axios ilieleza kuwa huo utakuwa mkutano wao wa kwanza tangu Februari, wakati Benjamin Netanyahu alipowasilisha mpango wake wa vita dhidi ya Iran.

    Tangu wakati huo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wa karibu na Trump wamekuwa wakizidi kukata tamaa kuhusu Netanyahu.

    Afisa mmoja wa Marekani alinukuliwa akisema: “Washauri wengi wa karibu wa Trump wanaamini kwamba Benjamin Netanyahu alikuwa na makosa kuhusu kila jambo.”

    Soma zaidi:

  7. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 05/07/2026.