Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi taarifa za milipuko ya magonjwa zinavyoathiri afya ya akili na namna tunavyofikiri
- Author, David Robson
- Nafasi, BBC Future
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa kawaida, watu hudhani kwamba ikiwa hawako katika hatari ya moja kwa moja ya kuambukizwa ugonjwa fulani, basi habari kuhusu mlipuko huo haziwahusu sana.
Hata hivyo, utafiti wa saikolojia unaonyesha kuwa taarifa kuhusu magonjwa na vifo zinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa namna tunavyofikiri, kuhisi na kufanya maamuzi, hata pale ambapo hatuko katika hatari ya moja kwa moja ya maambukizi.
Wanasayansi wanaeleza hali hii kupitia dhana inayojulikana kama "mfumo wa kinga wa kitabia" (Behavioral Immune System). Mfumo huu ni mkusanyiko wa michakato ya kisaikolojia iliyobadilika kadiri binadamu walivyoendelea ili kuwasaidia kutambua na kuepuka hatari za maambukizi kabla ya vimelea kuingia mwilini.
Kwa sasa, habari kuhusu magonjwa zimeanza tena kutawala vichwa vya habari duniani.
Mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaendelea kutoa changamoto kwa juhudi za kudhibiti maambukizi, huku kukiwa pia na wasiwasi kuhusu visa vipya vya virusi vya Hanta.
Ingawa watu wengi hawahitaji kuchukua hatua maalumu za kujikinga dhidi ya magonjwa haya, taarifa hizo zinaweza kuwa na athari za kisaikolojia zinazopita mbali zaidi ya afya ya mwili.
Mfumo wa kinga wa kitabia ni nini?
Tofauti na mfumo wa kinga wa mwili ambao hupambana na vimelea baada ya kuingia mwilini, mfumo wa kinga wa kitabia hufanya kazi ya kujaribu kuzuia maambukizi kabla hayajatokea.
Mwanasaikolojia Mark Schaller wa Chuo Kikuu cha British Columbia ni mmoja wa watafiti waliotambulisha dhana hii.
Mfumo huu huchochewa hasa na hisia ya kinyaa Kwa mfano, harufu ya chakula kilichooza au mwonekano wa kitu kinachoonekana kichafu unaweza kusababisha mtu ajisikie kichefuchefu au kutaka kukiepuka.
Haya ni majibu ya asili yanayolenga kupunguza uwezekano wa kuambukizwa magonjwa.
Lakini athari za mfumo huu haziishii kwenye hisia za kinyaa pekee.
Utafiti unaonyesha kuwa hata kukumbushwa tu kuhusu ugonjwa kunaweza kubadili namna tunavyofikiri na kuhusiana na watu wengine.
Kuongezeka kwa utii kwa sheria na kanuni za jamii
Katika historia ya binadamu, jamii nyingi ziliunda mila, desturi na sheria zilizosaidia kupunguza kuenea kwa magonjwa, kama vile taratibu za kuandaa chakula, kutunza usafi na kutupa taka.
Kwa sababu hiyo, mfumo wa kinga wa kitabia unaweza kuwafanya watu wawe tayari zaidi kufuata kanuni za kijamii wanapokumbushwa kuhusu magonjwa.
Katika moja ya tafiti zake, Mark Schaller aligundua kuwa wanafunzi waliokumbushwa kwanza kuhusu kipindi walichowahi kuugua walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupiga kura kulingana na maoni ya wenzao badala ya kufuata mtazamo wao binafsi. Matokeo haya yanaonyesha kuwa hofu ya ugonjwa inaweza kuongeza hamu ya kuendana na msimamo wa kundi.
Matokeo kama hayo yalionekana katika utafiti uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Hong Kong. Washiriki waliotazama picha zinazohusiana na maambukizi, kama vile majeraha yaliyooza au yaliyojaa funza, walionyesha mwelekeo mkubwa zaidi wa kufuata maoni ya wengi walipotathmini kazi za sanaa. Kinyume chake, wale walioonyeshwa picha za ajali za magari au treni hawakuonyesha mabadiliko hayo.
Maamuzi mabaya zaidi ya Kimaadili
Utafiti pia umeonyesha kuwa kukumbushwa kuhusu magonjwa kunaweza kuwafanya watu kuwa wakali zaidi katika kutoa uamuzi wa jambo.
Katika tafiti mbalimbali, washiriki waliokumbushwa uwepo wa ugonjwa walionekana kuwa tayari zaidi kulaani tabia walizoziona kuwa zisizofaa au zinazokiuka maadili ya jamii. Kwa mtazamo wa mfumo wa kinga wa kitabia, mwenendo huu unaweza kuwa ulisaidia jamii za zamani kuhakikisha kila mtu anafuata tahadhari zinazohitajika wakati wa milipuko ya magonjwa.
Kwa maneno mengine, hofu ya maambukizi inaweza kuongeza umuhimu tunaoweka kwenye nidhamu, kufuata sheria na kuheshimu taratibu za kijamii.
Chuki dhidi ya wageni na watu Wanaoonekana tofauti ni miongoni mwa maeneo yanayovutia zaidi katika tafiti za mfumo wa kinga wa kitabia ni uhusiano wake na mitazamo kuhusu watu wa nje ya kundi la kijamii.
Watafiti wamebaini kuwa wakati watu wanahofia magonjwa, wanaweza bila kujua kuwa na mashaka zaidi kuhusu watu wasiowafahamu au wanaoonekana tofauti nao. Line Aarhus na wenzake kutoka Chuo Kikuu cha Aarhus wamependekeza kuwa baadhi ya watu wanaweza, kwa kiwango cha chini cha ufahamu, kuwaona wahamiaji au wageni kama wabebaji wa magonjwa.
Mtazamo huu unaweza kuathiri maoni kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa na wakati mwingine kuchochea chuki dhidi ya wageni (xenophobia) au kupunguza huruma kwa makundi mbalimbali ya wachache.
Mafunzo kutoka Janga la COVID-19
Iwapo mfumo wa kinga wa kitabia unaathiri kweli mitazamo ya kijamii, basi athari zake zinapaswa kuonekana wakati wa milipuko mikubwa ya magonjwa. Janga la COVID-19 lilitoa fursa muhimu ya kuchunguza jambo hili.
Katika utafiti uliofanywa nchini Italia mwaka 2020, watafiti wakiongozwa na Giulia Focchi wa Chuo Kikuu cha Padua walichunguza watu 685 wakati wa wimbi la kwanza la janga hilo. Walibaini kuwa kadiri hofu ya mtu kuhusu virusi ilivyokuwa kubwa, ndivyo alivyokuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na mtazamo hasi zaidi kuhusu makundi mbalimbali ya watu, ikiwa ni pamoja na wahamiaji na makundi mengine yaliyotengwa kijamii.
Washiriki waliokuwa na hofu kubwa waliripoti hisia dhaifu zaidi za utambulisho wa pamoja na mshikamano wa kijamii na makundi hayo.
Athari hizi hazifanani kwa kila mtu
Ni muhimu kutambua kwamba si kila mtu huathiriwa kwa kiwango sawa.
Mitazamo ya watu huundwa na mambo mengi, ikiwemo elimu, mazingira ya familia, marafiki, taaluma, uzoefu wa maisha na tabia za mtu binafsi.
Watu wengine kwa asili huwa na hofu kubwa zaidi ya magonjwa na hivyo huwa nyeti zaidi kwa taarifa zinazohusiana na maambukizi. Wengine huonyesha mwitikio mdogo na hawaathiriki sana na taarifa kama hizo.
Zaidi ya hayo, tafiti zinazofanyika katika mazingira halisi wakati wa milipuko mara nyingi hutoa matokeo yanayochanganyika kutokana na sababu nyingi zinazoathiri tabia za binadamu kwa wakati mmoja.
Habari kuhusu milipuko ya magonjwa haziathiri tu afya ya mwili; zinaweza pia kuathiri afya ya akili na namna tunavyofikiri kuhusu watu na jamii inayotuzunguka. Kukumbushwa kuhusu maambukizi kunaweza kuongeza utii kwa sheria na kanuni za kijamii, kufanya watu wawe waangalifu zaidi katika kuchukua hatari, na wakati mwingine kusababisha hukumu kali za kimaadili au hata mashaka dhidi ya wageni na watu wanaoonekana tofauti.
Hata hivyo, mfumo wa kinga wa kitabia ni sehemu moja tu ya mambo mengi yanayounda maamuzi ya binadamu. Elimu, maadili, uzoefu wa maisha na mazingira ya kijamii vinaendelea kuwa na mchango mkubwa katika namna tunavyotafsiri dunia inayotuzunguka. Kwa hiyo, tunaposoma habari kuhusu mlipuko mpya wa ugonjwa, ni muhimu kutambua kwamba hisia zetu za hofu zinaweza kuathiri maamuzi yetu na mitazamo yetu kwa wengine, na hivyo kutuhimiza kufikiri kwa makini kabla ya kutoa hukumu au kufanya maamuzi muhimu.