Kwa nini kuna hofu kwamba Kanisa Katoliki linaweza kugawanyika?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Maelfu ya watu walikusanyika katika kijiji kimoja nchini Uswizi kushuhudia ibada ya kuwateua maaskofu wapya wanne wa Kanisa Katoliki, licha ya Papa Leo wa XIV kuwaomba wasiendelee na tukio hilo.

Wanne hao, akiwemo askofu mmoja kutoka Marekani, mmoja kutoka Uswizi na wengine wawili kutoka Ufaransa, ni wanachama wa chama cha mapadre chenye utata kinachojulikana kama Society of Saint Pius X (SSPX), ambacho wakati mwingine huitwa Lefebvrists, jina linalotokana na Marcel Lefebvre, mwanzilishi wa kundi hilo.

Kundi hilo linapinga baadhi ya mageuzi makubwa yaliyofanywa na Vatican katika miaka ya 1960 na 1970, ikiwemo uamuzi wa kuruhusu Misa isomwe katika lugha za wenyeji wa waumini badala ya Kilatini pekee kama ilivyokuwa awali.

Mapema wiki hii, Papa Leo alitoa wito wa mwisho, akiwataka viongozi wa SSPX wasiendelee na tukio hilo, akilielezea kama kitendo cha "kugawanya Kanisa" na "kuvuruga umoja wa Kanisa"

Hata hivyo, Jumatano asubuhi, chini ya anga baridi la milima ya Alps, kundi hilo lilikaidi ombi la Papa.

Angalau watu elfu 15,000 walikusanyika Écône kuwaangalia mapadri hao waliovaa makanzu, wakiwa wamebeba mishumaa na misalaba, na wakitumia ubani walipokuwa wakipita kijijini katika msafara wa kuelekea kwenye eneo la tukio la kuapishwa kwa mapadre hao walioasi itikadi za kanisa katoliki.

Katika sherehe hiyo, muziki ulichezwa, huku viapo vya kupokea majukumu ya uaskofu vikifanywa, kama ilivyotarajiwa, kwa lugha ya Kilatini.

Lakini kwa wanaume hao wanne, muda wao wa kuwa maaskofu unaweza kuwa mfupi sana.

Mara ya mwisho SSPX kuwateua maaskofu wapya ilikuwa mwaka 1988, na walioapishwa wakati huo walitengwa mara moja kutoka Kanisa katoliki.

Ingawa Papa Benedikto wa XVI aliondoa adhabu hiyo mwaka 2009 katika jaribio ambalo halikufanikiwa kikamilifu la kurekebisha uhusiano kati ya Vatikani na SSPX, inatarajiwa kwamba Papa Leo XIV pia anaweza kutowatambua maaskofu hao wapya ndani ya Kanisa Katoliki.

Kwa baadhi ya watu, sababu za kanisa la Vatican kukataa SSPX zinaweza kuonekana kuwa kinzani, hasa ikizingatiwa kuwa dini nyingi zina matawi tofauti, mengine yakifuata mila za zamani zaidi kuliko mengine.

Ndani ya Kanisa Katoliki, kumuweka mtu kuwa askofu bila idhini ya Papa huonekana kama kosa kubwa linalo enda kinyume na umoja wa Kanisa.

Sababu ya mtengano huu wa SSPX si tu wa kuendelea kusoma Misa kwa lugha Kilatini pekee.

Chama hiki kilianzishwa mwaka 1970 na Askofu mkuu Mfaransa mwenye utata Marcel Lefebvre, ambaye tangu mwanzo alitetea uhifadhi wa mitindo ya zamani ya Kanisa ambapo mapadri, maaskofu, makardinali na Misa yenyewe vilionekana kuwa karibu zaidi na Mungu kuliko waumini wa kawaida, hivyo kutengeneza mgawanyiko mkubwa kati ya viongozi wa Kanisa na waumini wa kawaida.

SSPX imekuwa na migongano ya muda mrefu na Vatikani kuhusu masuala mengi yaliyolenga kulifanya Kanisa kuwa wazi zaidi kwa waumini wote na kukuza usawa ndani ya muundo wake. Miongoni mwa masuala hayo ni kuboresha uhusiano na dini nyingine, kutambua uhuru wa kuabudu, na kushiriki katika majadiliano kuhusu masuala makubwa ya kijamii na kisiasa.

Kiongozi wa SSPX, Davide Pagliarani, alikanusha kuwa kundi hilo linataka kuendeleza migogoro, akiuambia umati uliokusanyika Écône kwamba ibada hiyo ya kuwateua maaskofu ilifanyika "hasa kwa sababu tunampenda Papa kama mkuu wa Kanisa hatutaki kumuona Papa akidhalilishwa na wachungaji wa uongo wanaowakilisha dini za uongo."

Kitendo hiki cha kukaidi kanisa na kuwaapisha maaskofu hao kinaweka shinikizo kwa Papa Leo XIV, ambaye bado ni mgeni katika wadhifa wake.

Ingawa SSPX ni kundi dogo lenye wafuasi takriban 600,000 ukilinganisha na Kanisa Katoliki lenye zaidi ya waumini bilioni 1.4 duniani, lina uwepo katika nchi nyingi, zikiwemo Marekani, ambako lina wafuasi wengi hasa katika jimbo la Kansas.

Kundi hilo pia linaonekana kuwa na uwezo wa kifedha. Sherehe ya kuwekwa wakfu kwa maaskofu ilionyeshwa moja kwa moja kupitia mtandao wa YouTube kwa lugha saba tofauti.

Maelfu ya watu waliokuwepo waligawiwa kofia zilizoandikwa "Écône 2026." Pia kulikuwa na zawadi maalum kama chupa za divai ya Uswizi zilizouzwa kwa dola 92 kila moja, zikiwa na picha ya kilemba cha askofu.

Ingawa Papa Leo hajawatambua maaskofu hao wapya anaichukulia sherehe hiyo kama shambulio dhidi ya Kanisa Katoliki,na huenda akachukua hatua kali zaidi kuepuka mgawinyiko mkubwa kutokea katika kanisa hilo.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula