Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwaheri Cape Verde - timu 'kibonde' ambayo Kombe la Dunia halitaisahau
- Author, Charlotte Coates
- Nafasi, BBC Sport
- Author, Elizabeth Conway
- Nafasi, BBC Sport Miami
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Ingawa Cape Verde inaweza kuwa ilikuwa nchi ya pili kwa udogo kushiriki Kombe la Dunia, lakini bila shaka yoyote iliacha alama kubwa katika mashindano hayo ya mwaka 2026.
Sahau kuhusu Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Erling Haaland na Harry Kane – ni timu hiyo inayoshiriki kwa mara ya kwanza ndiyo iliyovutia hisia za wengi.
Kulikuwa na uchezaji wa kishujaa wa kipa Vozinha ambalo jina maarufu wakati jina halisi ni Josmar, Jose Evora Dias walipopata pointi yao ya kwanza katika Kombe la Dunia dhidi ya Hispania.
Kulikuwa na msisimko walipofunga mabao yao ya kwanza katika Kombe la Dunia dhidi ya Uruguay.
Na kulikuwa na bao la ajabu la Sidny Lopes Cabral walipokaribia kusababisha mshangao mkubwa zaidi wa mashindano hayo dhidi ya mabingwa watetezi Argentina.
'Hakuna anayeuliza tena ilipo Cape Verde kwenye ramani'
Safari ya Cape Verde katika Kombe la Dunia ilikuwa na kila aina ya matukio.
Wakati kipenga kilipopulizwa kuashiria mwisho wa muda wa ziada mjini Miami usiku wa Ijumaa, wachezaji wa 'Blue Sharks' walianguka chini kwa uchungu baada ya kupoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya mabingwa watetezi Argentina katika hatua ya timu 32 bora – lakini wanaweza kuondoka Marekani wakijua kuwa wamekonga nyoyo za watu wengi.
"Cape Verde imepoteza, lakini imeshinda," alisema mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Scotland, James McFadden, kupitia BBC Radio 5 Live.
"Wameonyesha ujasiri, ushirikiano, umoja na imani thabiti katika utambulisho wao na uwezo wao.
"Hadithi kuu ya mashindano haya ni Cape Verde. Hicho ndicho unachotaka kuona katika timu ya soka."
Waliingia kwenye mashindano hayo wakiwa katika nafasi ya 67 duniani, lakini sare tatu katika hatua ya makundi – ikiwemo kuwazuia mabingwa wa Ulaya, Hispania, kwa sare tasa ya 0-0 katika mchezo wao wa ufunguzi – iliweka mazingira ya jaribio kubwa la kusababisha moja ya matokeo ya kushangaza zaidi kuwahi kushuhudiwa katika Kombe la Dunia.
Dhidi ya Argentina, waliruhusu bao la Messi, lakini walirudi mchezoni na kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 1-1, jambo lililosababisha mchezo kwenda muda wa ziada. Kisha waliruhusu bao jingine – kabla ya shuti kali la Cabral kusawazisha tena. Hata hivyo, haikuwa bahati yao, kwani mpira ulibadilisha mwelekeo baada ya kugonga mwili wa Diney Borges kufuatia mpira wa kichwa wa Cristian Romero, jambo lililoiwezesha Argentina kusonga mbele.
Beki wa zamani wa kulia wa England, Gary Neville, alikiambia kituo cha runinag cha ITV kuwa huo ulikuwa "moja ya maonesho bora zaidi" kuwahi kuyaona kutoka kwa timu isiyopewa nafasi kubwa ya kushinda.
"Wanalia kwa sababu wanaelekea nyumbani," aliongeza. "Hawataki kurudi nyumbani. Wanataka kubaki hapa kwa maisha yao yote." Wanataka kubaki hapa milele. Huu ni wakati ambao huenda usijirudie tena kwa baadhi ya wachezaji hawa. Ni jambo la kustaajabisha na la kuvutia, lakini pia la kuhuzunisha.
Licha ya kupoteza mchezo, kocha wa Cape Verde, Bubista, alijawa na fahari baada ya timu yake kusalia na dakika 10 pekee kabla ya kuilazimisha Argentina kuingia katika hatua ya mikwaju ya penalti.
"Tulionyesha kuwa ingawa sisi ni nchi ndogo, tunaweza kucheza dhidi ya timu bora zaidi duniani," alisema. "Hiyo ni sababu ya kujivunia.
"Tuliweka historia kwa ajili ya nchi yetu. Wanaweza kujivunia kuiwakilisha nchi yetu.
"Kuweza kucheza vile tulivyocheza dhidi ya mabingwa wa dunia, na kusawazisha bao mara mbili, ni jambo la ajabu sana."
Mlinzi wa kati wa Shamrock Rovers, Roberto 'Pico' Lopes, ambaye alicheza mechi zote nne za Cape Verde katika Kombe la Dunia, aliiambia BBC: "Moja ya mambo mazuri yaliyotokana na Kombe hili la Dunia ni kwamba hakuna anayeuliza tena Cape Verde iko wapi kwenye ramani - hii yenyewe ni historia kwetu. Tumejiweka kwenye ramani ya dunia.
"Sisi ni taifa dogo lakini lenye mioyo mikubwa na tulionesha kile kinachowezekana - na ukiamini, unaweza kufanikiwa."
Wazo la kupanua Kombe la Dunia ili kushirikisha timu 48 lilikuwa gumzo kubwa kabla ya mashindano kuanza, lakini Neville alisema "hatakuwa na shaka tena" kuhusu jambo hilo.
Aliyekuwa mshambuliaji wa England, Ian Wright, akizungumza pia kupitia kituo cha ITV, aliitaka FIFA kusaidia kuibua matukio mengine kama lile la Cape Verde.
"Hicho ndicho unachotamani kionekane kote duniani, na ndiyo maana FIFA inapaswa kufanya juhudi kubwa kuhakikisha fedha wanazopata zinawafikia wahusika wote," alisema Wright.
"Hili linawaonesha watu kwamba ukweli ukitoa fursa, timu zinaweza kufika kwenye jukwaa kubwa zaidi bila kujali udogo wake, na zinaweza kushindana na mabingwa wa dunia au wachezaji bora zaidi duniani.
"Kwa hakika, ilikuwa ni juhudi kubwa na ya kipekee kutoka kwao."
'Vozinha alikuwa wapi?'
Picha ya Vozinha akitokwa na machozi na kisha kuinua bendera ya Cape Verde juu kwa fahari baada ya kuzuia mashambulizi ya Hispania katika mechi ya ufunguzi wa kundi ilisambaa duniani kote – na kumfanya kuwa shujaa wa mashabiki kwa muda mfupi.
Lakini sababu ya umaarufu wake si picha hiyo au hisia zake pekee; kiwango chake cha uchezaji kimemfanya kuwa nyota mkubwa. Kipa huyo mwenye umri wa miaka 40 kwa sasa hana klabu, baada ya mkataba wake na timu ya daraja la pili nchini Ureno, Chaves, kumalizika.
Hata hivyo, Neville haamini kuwa kipa huyo atakosa klabu kwa muda mrefu.
Neville alisema kupitia ITV: "Vozinha atapata klabu nzuri kutokana na mafanikio haya.
"Kombe la Dunia la aina yake. Kila anachofanya anakifanya kwa utulivu na umakini mkubwa. Alikuwa wapi huyu? Tunapaswa kuwa tumemjua mapema zaidi."
Wright aliongeza kuwa Vozinha ana "haiba ya kishujaa" kutokana na kiwango chake alichoonesha akiichezea Cape Verde dhidi ya Argentina.
Baada ya kuokoa michomo minane jijini Miami, Vozinha alifikisha jumla ya michomo 18 iliyookolewa katika Kombe la Dunia la mwaka huu, idadi inayomfanya kushika nafasi ya tatu nyuma ya Eloy Room wa Curacao (20) na Orlando Gill wa Paraguay (19) kufikia hatua ya sasa.
Imetafsiriwa na Florian Kaijage