Kingai, CDF, IGP kutotoa ushahidi, Lissu afunga ushahidi wake

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, hatatoa ushahidi kwa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kwa mujibu wa Lissu.
Lissu ameliambia Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, leo Septemba 18, 2026, kwamba amekutana na DCI Kingai na kuzungumza naye kuhusu maeneo aliyotarajia ayatolee ushahidi.
Kwa mujibu wa Lissu, Kingai amemweleza kuwa hayuko tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi.
Lissu amesema amemwelewa Kingai na hawezi kumlazimisha kutoa ushahidi ambao hataki kuutoa.
Lissu pia amesema Kingai amemweleza kuwa mashahidi wengine wawili ambao mahakama imeagiza wapewe wito, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Nkunda, na Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillius Wambura, nao hawatakuwa tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi watakaporejea nchini na kupokea wito wa mahakama.
Kwa hali hiyo, Lissu amesema hana mashahidi wengine na ameomba kufunga ushahidi wa upande wa utetezi.
Jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, limekubali kufungwa kwa ushahidi wa pande zote mbili za kesi hiyo.
Lissu ameomba mahakama ipange siku ya kuwasilisha hoja za mwisho za pande zote mbili, akisema muda wa sesheni ya mahakama unaisha Septemba 25 na mwenendo wa kesi una zaidi ya kurasa 1,000.
Amesema yuko tayari kuwasilisha hoja za mwisho kuanzia Jumatano, Septemba 23.
Upande wa mashtaka, Nassoro Katuga ni Wakili Mkuu wa Serikali nchini Tanzania anayeongoza upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, umeunga mkono pendekezo hilo na kusema uko tayari kwa ajili ya hoja za mwisho siku hiyo.
Jaji Ndunguru amesema majumuisho ya pande zote yatafanywa kwa njia ya mdomo Jumatano, Septemba 23.
Tundu Lissu anakabiliwa na kesi hiyo ya uhaini namba 19605/2025, akiwa ndani tangu April, 2025.















