Kwa nini tunasinzia baada ya kula chakula cha mchana?

Chanzo cha picha, Getty Images
Umemaliza chakula cha mchana na kurejea kwenye dawati lako, ukiwa tayari kuendelea na kazi.
Hata hivyo, saa tisa alasiri zinapowadia, unaanza kuhisi macho yakiwa mazito na ugumu wa kuendelea kujikita kwenye kazi.
Muda si mrefu, jambo pekee unalowaza ni jinsi ambavyo ungependa kupata usingizi wa muda mfupi.
Hali hii, inayojulikana kama "uchovu wa alasiri" au "usingizi wa saa tisa alasiri", ni jambo linalowakumba watu wengi.
Ni kipindi ambacho kiwango cha nguvu mwilini hupungua kwa kiasi kikubwa katikati ya mchana, na kusababisha hisia za uchovu, kusinzia na kupungua kwa umakini.
Ingawa ni rahisi kuhusisha hisia hizi za ghafla za usingizi na chakula cha mchana ulichokula, si chakula pekee kinachosababisha hali hiyo.
Uchovu wa alasiri unasadikiwa kusababishwa na mwingiliano wa sababu mbalimbali za kibaiolojia zinazotokea mwilini kwa wakati mmoja.
Na sehemu ya maelezo ya hali hii huanzia hata kabla ya muda wa chakula cha mchana, kutokana na mzunguko wa asili wa usingizi na uamsho unaodhibiti kiwango cha nguvu na umakini katika vipindi tofauti vya siku.
Shinikizo la usingizi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuanzia tunapoamka asubuhi, hitaji la mwili la kupata usingizi huanza kuongezeka taratibu.
Mchakato huo husababishwa kwa kiasi kikubwa na kujikusanya kwa adenosini, kemikali ya asili inayosaidia kudhibiti hali ya kuwa macho na kulala. Kadiri tunavyokaa macho kwa muda mrefu, ndivyo adenosini inavyoendelea kujilimbikiza kwenye ubongo na kuongeza kile kinachojulikana kama "shinikizo la usingizi."
Hata hivyo, kama hali ingekuwa hivyo pekee, tungeendelea kujisikia usingizi zaidi na zaidi kuanzia baada ya kifungua kinywa. Lakini mwili una mfumo mwingine unaosaidia kutuweka macho na wenye nguvu wakati wa mchana.
Mfumo huo ni saa ya ndani ya mwili (circadian clock), inayodhibiti mzunguko wa kulala na kuamka. Katika kipindi cha mchana, saa hii hutuma ishara zinazosaidia kuongeza umakini na kupunguza hisia za usingizi.
Asubuhi, ishara hizo huwa na nguvu na husaidia kufidia ongezeko la shinikizo la usingizi.
Hata hivyo, mapema alasiri, mfumo huo huingia katika kipindi cha asili ambacho uwezo wake wa kutuweka macho hupungua. Hapo ndipo watu wengi huanza kuhisi uchovu, kupoteza umakini au kutamani kupata usingizi wa muda mfupi.
Wakati huo huo, shinikizo la usingizi linaendelea kuongezeka. Mchanganyiko wa sababu hizi mbili huifanya alasiri kuwa kipindi ambacho wengi huhisi kusinzia zaidi.
Na hapo ndipo chakula cha mchana kinaweza kuongeza mchango wake, kwa kuchochea zaidi hisia za uchovu na usingizi kwa baadhi ya watu.
Ulaji wa chakula huathiri jinsi utumbo, mfumo wa kimetaboliki na ubongo vinavyowasiliana. Tunapokula, ubongo hupokea taarifa kutoka tumboni kuhusu kiwango cha kushiba, virutubisho vilivyopo na homoni zinazotolewa wakati wa mmeng'enyo wa chakula.
Pia, kiasi na aina ya chakula tunachokula kinaweza kuathiri jinsi tunavyojihisi baadaye.
Kwa mfano, kula chakula kingi cha mchana kunaweza kupunguza uwezo wa kuzingatia na kuongeza hisia za usingizi. Hata hivyo, bado haijathibitishwa wazi ikiwa wanga, mafuta au sukari ndiyo husababisha hali hiyo zaidi kuliko makundi mengine ya chakula.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mlo mkubwa wa mchana unaweza kuongeza hisia za uchovu wa alasiri. Hata hivyo, hakuna ushahidi wa wazi unaoonyesha kuwa aina fulani ya chakula, kama wanga, mafuta au protini, ndiyo chanzo kikuu cha usingizi huo kwa kila mtu.
Watafiti bado wanaendelea kuchunguza jinsi chakula kinavyochangia hali hiyo. Moja ya maeneo wanayoyachunguza ni mfumo wa ubongo unaosaidia kudumisha hali ya kuwa macho.
Ndani ya ubongo kuna seli maalumu zinazosaidia mtu kubaki macho na makini. Seli hizi huathiriwa na mabadiliko yanayotokea mwilini baada ya kula, ikiwemo ongezeko la kiwango cha sukari kwenye damu. Hii inaonyesha kuwa chakula kinaweza kuwa na mchango katika kupunguza umakini na kuongeza hisia za usingizi.
Tafiti za hivi karibuni pia zinaonyesha kuwa usingizi unaotokea baada ya kula unatofautiana na ule unaosababishwa na kukosa usingizi wa kutosha usiku.
Katika utafiti mmoja, watafiti walibaini kuwa baada ya kula, shughuli za sehemu za ubongo zinazohusika na umakini na kufikiri hubadilika. Mabadiliko hayo husababisha mtu kuwa na mwitikio wa polepole zaidi na kupungua kwa umakini.
Kwa upande mwingine, kukosa usingizi huathiri ubongo kwa njia tofauti.
Hata hivyo, matokeo yake yanaweza kufanana. Mtu anaweza kuhisi uchovu, kufikiri kwa polepole zaidi na kushindwa kuzingatia kazi vizuri, iwe ni kutokana na usingizi wa baada ya kula au kukosa usingizi.
Kwa kifupi, usingizi wa alasiri hauchangiwi na chakula pekee. Mara nyingi husababishwa na mchanganyiko wa saa ya mwili, ongezeko la hitaji la usingizi kadiri siku inavyoendelea, na athari za chakula baada ya kula.
Mambo ya kufanya na ya kuepuka
Baadhi ya watu huamua kunywa kahawa au chai wanapohisi uchovu wa alasiri. Hata hivyo, njia hiyo haisuluhishi tatizo lenyewe.
Kafeini iliyomo kwenye kahawa na chai husaidia mtu kujisikia macho kwa muda kwa kupunguza hisia za usingizi.
Lakini kafeini haiongezi nguvu mpya mwilini wala ubongoni. Wakati ikikufanya ujisikie macho, hitaji la mwili la usingizi huendelea kuongezeka taratibu.
Ndiyo maana kahawa inaweza kuongeza umakini kwa muda mfupi, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya usingizi wa kutosha.
Kwa kifupi, ikiwa mara kwa mara unahisi uchovu wa alasiri, suluhisho la muda mrefu si kunywa kahawa zaidi, bali kuhakikisha unapata usingizi wa kutosha usiku.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jinsi ya kukabiliana na uchovu wa alasiri
Mbali na kiasi cha kafeini unachotumia, muda unaotumia pia ni muhimu.
Kunywa kahawa au chai mwishoni mwa alasiri kunaweza kukusaidia kujisikia macho kwa muda. Hata hivyo, kafeini ikibaki mwilini hadi wakati wa kulala, inaweza kufanya iwe vigumu kupata usingizi usiku.
Hali hiyo inaweza kusababisha uchovu zaidi siku inayofuata na kuendeleza mzunguko wa kusinzia mchana.
Wataalamu wanasema njia bora zaidi ya kupunguza uchovu wa alasiri ni kutumia mwanga wa asili wa jua.
Mwanga ni moja ya vichocheo muhimu vinavyosaidia mwili kubaki macho na makini. Tafiti zimeonyesha kuwa mwanga wa mchana unaweza kusaidia kuongeza umakini, kuboresha uwezo wa kukumbuka na kupunguza hisia za uchovu.
Athari hii haihusiani na mwanga wa jua pekee. Utafiti mwingine umebaini kuwa matumizi ya taa zinazofanana na mwanga wa mchana yanaweza kuongeza umakini, kupunguza kusinzia na kuboresha ari ya kufanya kazi.
Kwa watu wanaotumia muda mwingi ndani ya majengo, kutoka nje kwa muda mfupi ili kupata mwanga wa jua au kutumia mwanga unaofanana na wa mchana kunaweza kusaidia kuondoa uchovu wa alasiri na kurejesha umakini.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












