Wanasayansi waumba panya wenye 'ubongo wa binadamu'

Jiir

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Utafiti huu umeibua maswali kuhusu maana ya kubadili namna wanyama wanavyofikiri na kuhisi.
    • Author, Victoria Gill
    • Nafasi, Weriyaha Sayniska
    • Author, Kate Stephens
    • Nafasi, Weriye sare oo sayniska ah
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Wanasayansi nchini Marekani wamefanikiwa kutengeneza panya ambao wamepandikizwa seli za binadamu kwenye ubongo wao, na seli hizo zinafanya kazi ndani ya ubongo wa panya hao.

Watafiti wanatumaini ugunduzi huo unaweza kusaidia katika kutengeneza tiba za magonjwa ya akili na matatizo ya ukuaji wa mfumo wa neva ambayo hutokea kwa binadamu, lakini hayawezi kuchunguzwa vizuri kwa kutumia panya wa kawaida.

Ingawa wazo la kuwa na panya wenye sehemu ya ubongo wa binadamu linaweza kuonekana kama jaribio la kubuniwa katika filamu za sayansi, wanasayansi wanasema panya hao hawafikiri kama binadamu.

Panya hao walibadilishwa vinasaba na pia kufanyiwa upasuaji ili baadhi ya seli zao za ubongo zibadilishwe na seli za binadamu.

Wanasayansi hao wamesema utafiti huo, uliochapishwa katika jarida la Nature, ulifanyiwa mapitio huru ya kimaadili.

Kwa nini utafiti huu ni muhimu?

Lengo la utafiti huo ni kusaidia kuelewa vizuri jinsi magonjwa ya akili yanavyotokea na kufanya kazi katika ubongo, hasa magonjwa ambayo kwa sasa hayana tiba madhubuti.

Baadhi ya magonjwa haya hayawezi kuchunguzwa kwa kutumia panya wa kawaida kwa sababu panya hawapati baadhi ya matatizo ya akili yanayowapata binadamu.

Profesa Sergiu Pașca wa Chuo Kikuu cha Stanford, ambaye aliongoza utafiti huo, amesema utafiti wa magonjwa ya akili una kiwango cha chini sana cha mafanikio katika majaribio ya dawa.

Amesema hata dawa ambazo zinaonekana kufanya kazi vizuri katika majaribio kwa wanyama mara nyingi hushindwa zinapofanyiwa majaribio kwa binadamu.

Kwa mujibu wa watafiti wa Stanford, utafiti huo unaweza kusaidia kuboresha uelewa na matibabu ya magonjwa kama kifafa, usonji na kupooza kwa ubongo.

Jiir

Chanzo cha picha, S Pasca/Stanford

Maelezo ya picha, Kutokana na picha za uchunguzi wa ubongo wa panya waliopandikizwa seli hizo, watafiti waliweza kuona miunganisho kati ya seli za ubongo wa binadamu na sehemu nyingine za ubongo wa panya.

Jinsi panya hao walivyotengenezwa

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ubongo wa binadamu una mabilioni ya seli zinazounganishwa katika mitandao mingi, jambo linalofanya iwe vigumu kuelewa jinsi unavyokua na kinachotokea katika kiwango cha seli unapokuwa na tatizo.

Watafiti walianza kwa kubadilisha vinasaba vya panya ili karibu wasiwe na sehemu kubwa ya gamba la ubongo, yaani sehemu ya nje ya ubongo inayohusishwa na kufikiri kwa kiwango cha juu, kumbukumbu na hisia.

Kisha walichukua seli za ngozi kutoka kwa binadamu na kuzibadilisha ili zikue na kuwa aina za seli zinazofanana na seli za ubongo.

Seli hizo ziliundwa katika miundo inayojulikana kama organoids. Hizi si akili kamili zilizokuzwa maabara, bali ni makundi ya seli hai yaliyounganishwa.

Watafiti walipopandikiza kwenye ubongo wa panya, seli za binadamu ziligawanyika na kujipanga kulingana na mfumo wa ubongo wa panya. Pia ziliunda miunganisho na sehemu nyingine za ubongo na uti wa mgongo wa panya.

Baada ya miezi kadhaa, seli za binadamu zilianza kuonekana na kufanya kazi kama zile za sehemu ya nje ya ubongo wa panya.

Takriban miezi sita baada ya upasuaji, watafiti waliwafanyisha panya hao majaribio rahisi ya tabia, wakiangalia jinsi walivyokuwa wakisogea katika eneo dogo la majaribio.

Hata hivyo katika hatua za awali, matendo ya panya hayo kwa mujibu wa Profesa Pașca yalikuwa kwa kiasi kikubwa yanafanana na panya wa kawaida na kwamba hawakuwa na uwezo wowote wa ziada.

Jiir

Chanzo cha picha, Luis Alvarez

Maelezo ya picha, Matumaini ni kwamba utafiti huu utatoa njia mpya ya kuchunguza biolojia ya baadhi ya matatizo ya ubongo wa binadamu.

Je, panya hao wanaweza kufikiri kama binadamu?

Wataalamu wa maadili ya sayansi wanasema hakuna ushahidi kwamba utafiti huo umeunda panya anayeweza kufikiri kama binadamu.

Dk Sarah Chan, mtaalamu wa maadili ya utafiti wa Chuo Kikuu cha Edinburgh ambaye hakuhusika katika utafiti huo, amesema hakuna dalili kwamba wanasayansi wametengeneza panya anayeweza kufikiri kama binadamu au ubongo wa binadamu ndani ya mwili wa panya.

Hata hivyo, amesema utafiti huo unaibua swali kuhusu maana ya kuanza kubadilisha uwezo wa kufikiri wa wanyama.

Swali kubwa ni jinsi wanasayansi wanavyoweza kujua uzoefu wa wanyama hao na kuzingatia hilo katika namna wanavyowatunza wakati wa majaribio.

Changamoto za kimaadili

Dk Ilary Allodi, mtaalamu wa sayansi ya ubongo kutoka Chuo Kikuu cha St Andrews ambaye hakuhusika katika utafiti huo, amesema kazi hiyo ni ya kushangaza sana.

Amesema kinachovutia ni kwamba baadhi ya aina za seli zinazopatikana katika ubongo wa binadamu na wanyama wengine, lakini kwa kawaida hazipatikani kwenye ubongo wa panya, ziliweza kujitengeneza zenyewe baada ya seli hizo kupandikizwa.

Panya hao walitengenezwa kwa kubadilishwa vinasaba na kulelewa chini ya masharti makali ya maadili na ustawi wa wanyama.

Watafiti wanaamini panya hao watatumika katika maabara chache kwa ajili ya kuchunguza magonjwa maalum ya ubongo.

Hata hivyo, Profesa James Ainge wa Chuo Kikuu cha St Andrews amesema matumizi ya panya hao yanaweza kuwa machache kutokana na masuala ya kimaadili yanayohusishwa na kukuza seli hai za ubongo wa binadamu ndani ya panya na maana yake kwa uzoefu wa mnyama huyo.

Dk Allodi amesema wanasayansi wanaochunguza ubongo wa binadamu hukutana na changamoto kama hizo kila siku.

Kwa sasa, amesema, watafiti wana njia chache za kuchunguza magonjwa ya binadamu: panya, seli zinazokuzwa maabara na mitandao ya seli za neva inayoendeshwa kwenye kompyuta.

Kwa hiyo, utafiti huu unaweza kuwa njia mpya ya kuchunguza magonjwa ya ubongo wa binadamu.