Huu ndiyo mji wa mabilionea?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Mwanzilishi wa Facebook, Mark Zuckerberg, alinunua mali ya gharama kubwa zaidi kuwahi kuuzwa mjini Miami mwezi Machi, akilipa dola milioni 170 kwa jumba la kifahari lenye ukubwa wa futi za mraba 2,800 ambalo lilikuwa likijengwa kwenye kisiwa binafsi cha Indian Creek.

Hata hivyo, mali hii si nyumba ya gharama kubwa zaidi inayouzwa kwa sasa katika jiji hili la Kusini mwa Florida.

Rekodi ya sasa ya nyumba ya gharama kubwa zaidi sokoni inashikiliwa na jumba la kifahari la mfanyabiashara wa dhamana (bond trader) John Devaney lililoko Key Biscayne, ambalo linauzwa kwa dola milioni 237. Kwa kweli, kama wewe ni mpenzi wa filamu, huenda ukaitambua nyumba hii.

Jumba hilo lilionyeshwa katika filamu ya mwaka 1983 iitwayo Scarface, iliyoongozwa na Brian De Palma na kuwashirikisha waigizaji kama Al Pacino—likionekana kama makazi ya tajiri wa dawa za kulevya, Frank Lopez.

Hapo ndipo tunapomwona kwa mara ya kwanza Elvira, aliyeigizwa na Michelle Pfeiffer, akishuka kwa kutumia lifti ya kioo maarufu ya jumba hilo.

.

Chanzo cha picha, 1 Oak studios

Maelezo ya picha, Picha ya kisasa ya lifti ambayo Michelle Pfeiffer aliipanda katika filamu ya "Scarface."

Mabilionea wakubwa wa Miami

Kuanzia Jeffrey Preston Bezos, Mark Zuckerberg, Peter Andreas Thiel, David Beckham, Lionel Messi mpaka Ken Griffin. Ni mabilionea baadhi wenye makazi na wengine makazi na biashara Miami.

"Kuna kanuni ya dhahabu katika soko la majengo: kila kitu hutegemea eneo," anasema Mai de la Vega.

Huko Miami, eneo linalotamanika ni lile lenye mtazamo wa bahari au ghuba.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Mali zilizoko kando ya pwani zinauzwa kwa bei ya juu kwa sababu ni adimu," anasema Solomon. "Kwa sasa kuna wanunuzi wengi kuliko nyumba zinazopatikana kando ya maji, na bei zitaendelea kupanda hadi hali hiyo itakapobadilika."

Labda hakuna mahali panapoonyesha hili vizuri zaidi kuliko Indian Creek, kisiwa cha kipekee na cha faragha zaidi jijini Miami. Kulingana na Mai de la Vega, eneo hilo "bado linashikilia rekodi ya bei za juu kupita kiasi katika soko la majengo."

Indian Creek huitwa "makazi ya mabilionea," ambapo watu kama Mark Zuckerberg, Jeff Bezos, na Ivanka Trump wamejenga majumba ya kifahari. Ingawa kisiwa hicho hakizidi sana ukubwa wa bustani ya Central Park ya New York, kina meya na jeshi lake la polisi, na kinafikika kupitia daraja jeupe lisilo na mvuto wa pekee ambalo hulindwa na vituo viwili vya walinzi.

"Ukiuliza kwa nini Indian Creek, jibu ni hili: ni kisiwa cha faragha chenye huduma nyingi na viwanja vikubwa, kilichozungukwa na maji, na ni paradiso kwa wamiliki wa boti. Zaidi ya hayo, kina usalama wa hali ya juu sana," anasema De La Ve

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanzilishi wa Facebook Mark Zuckerberg na mkewe. Mark Zuckerberg amenunua mali ya gharama kubwa zaidi kuwahi kuuzwa mjini Miami.

Ingawa asilimia 99.9 ya watu duniani hawawezi hata kufikiria kulipa kiasi kikubwa namna hiyo kwa ajili ya nyumba, Miami imekuwa kivutio maarufu kwa asilimia 0.1 ya watu wanaoweza kumudu gharama hizo.

"Watu wengi wenye mapato ya juu wamehamia Florida kutokana na faida zinazotokana na kuishi Miami," E. B. Solomon, mwandishi wa habari wa Wall Street Journal anayebobea katika soko la nyumba za makazi, aliambia BBC.

"Kiwango cha uhalifu ni cha chini, hali ya hewa ni nzuri, kuna maeneo mazuri ya makazi, na hakuna kodi za jimbo," anasema Mai De La Vega, mwanzilishi wa One Sotheby's International Realty, mojawapo ya kampuni maarufu zinazoshughulika na nyumba za kifahari Kusini mwa Florida.

Mbali na Zuckerberg, orodha ya mamilionea maarufu waliohamia Miami katika miaka ya hivi karibuni inajumuisha mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos, waanzilishi wenza wa Google Larry Page na Sergey Brin, pamoja na Ivanka Trump, binti wa Rais wa Marekani Donald Trump, na mumewe Jared Kushner

"Wakati watu mashuhuri mmoja, wawili, au watatu katika ulimwengu wa biashara wanapohamia mahali fulani, watu wengine huona faida zake na kufuata mkondo huo," anasema Solomon. "Hawako peke yao tena; wanaunda mtandao wa watu wenye mawazo yanayofanana kuwazunguka."

Mai de la Vega anaamini kuwa soko la majengo na ardhi la Miami limeingia katika "enzi mpya ya mali zisizohamishika za kipekee na zenye hadhi ya juu." "Idadi ya miamala ya nyumba zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 60 inaongezeka, na soko linaendelea kukua," anasema.

"Tukiangalia mwaka wa 2025, ambao ulikuwa mwaka wetu kamili wa mwisho wa utendaji kazi, tulirekodi mauzo ya zaidi ya dola milioni 517, na miamala hiyo yote ilihusu mali zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 60," anaeleza.

Lakini kwa nini Miami? Ni nini kinachofanya jiji hili la Kusini mwa Florida kuwa kivutio kikubwa kwa watu matajiri zaidi duniani?

Jinsi janga la virusi vya korona lilivyokuwa hatua muhimu ya mabadiliko kwa Miami

Kwa muda mrefu, Miami imekuwa kivutio kwa watu wenye utajiri mkubwa—hasa kutoka Amerika ya Kusini, kutokana na hali ya hewa nzuri, fukwe, na urahisi wa usafiri wa anga.

"Lakini wakati wa janga la Covid, watu nchini Marekani waligundua kuwa Florida ilikuwa wazi kwa shughuli za kawaida na haikuwa na vikwazo vilivyokuwepo katika maeneo mengine," anaeleza E.B. Solomon.

Wakati wa janga la Covid, Florida ilizua utata kwa kuwa mojawapo ya majimbo ya kwanza nchini Marekani kuondoa vikwazo vya kutembea katika maeneo ya umma, kuacha sheria ya lazima ya kuvaa barakoa, na kufungua tena shule, baa, na migahawa.

Ingawa maamuzi haya yalikabiliwa na ukosoaji mkubwa, sera hizo hizo zilifanya jimbo hilo likiongozwa na Republican Ron DeSantis kuwa kivutio kwa matajiri walioishi katika majimbo yenye vikwazo vikali zaidi vya kiafya, kama vile New York, California, au Illinois.

"Ukizingatia pia ukweli kwamba Florida ni eneo lenye nafuu kubwa ya kodi na wakazi wake hawalipi kodi ya mapato ya jimbo, tofauti na wakazi wa majimbo mengine, Miami ilipata umaarufu mkubwa si tu kwa sababu ya mazingira na mtindo wa maisha, bali pia kutokana na kivutio hiki kikubwa cha nafuu ya kodi," anaeleza Solomon.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mai de la Vega anasema kuwa kuhama kwa watu mashuhuri wa awali katika nyanja za teknolojia na biashara, kama vile Peter Thiel, mwanzilishi mwenza wa PayPal, na Ken Griffin, mwanzilishi wa mfuko wa uwekezaji wa Citadel, kulizua aina fulani ya mnyororo wa matukio (athari ya domino) na kuvutia watu wengi zaidi wenye utajiri mkubwa kuja Miami.

"Sehemu ya jambo hili inahusiana pia na mwenendo wa watu kufuata mkumbo," anasema Mai de la Vega. "Kuna watu wanaojiambia, 'Fulani, ambaye ana utajiri kama wangu, amenunua nyumba huko; je, nami ninunue nyumba huko?'"

Hali hii imesababisha kuongezeka kwa idadi ya nyumba zinazopatikana sokoni—hasa zile za daraja la juu kabisa la anasa, katika baadhi ya maeneo, pamoja na kupanda kwa bei zake.

Miami ilibadilikaje?

.

Chanzo cha picha, 1 Oak studios

Mfanyabiashara John Dewani anasema kuwa aliponunua eneo ambalo sasa ni jumba lake la kifahari lenye thamani ya dola milioni 237 huko Key Biscayne mnamo mwaka 2003, moja ya sababu kuu ilikuwa ni eneo la kutua helikopta lenye ukubwa wa futi za mraba 1,000 lililojengwa likichomozea juu ya maji, ambalo hapo awali lilitumiwa na Rais wa zamani wa Marekani Richard Nixon.

"Siku moja nilikuwa nikiendesha helikopta nikiwa na umri wa miaka 33," anasema. "Nilipokuwa nikikua huko Key Biscayne, nilipoona eneo hilo la kutua, nilijiambia, 'Ningependa sana kumiliki eneo hilo ili niweze kutua helikopta zangu hapo.'"

Katika makubaliano yaliyovunja rekodi zote wakati huo, alilipa dola milioni 15 kwa ajili ya kipande cha ardhi ambapo nyumba hiyo ilijengwa, na kisha akalipa dola milioni 15 nyingine kwa ajili ya ardhi iliyokuwa karibu na hapo.

De la Vega anaeleza kuwa hizo zilikuwa bei za kawaida huko Miami kabla ya janga la COVID-19.

"Nakumbuka moja ya mali tulizouza wakati huo ilikuwa nyumba ya Shaquille O'Neal iliyoko Star Island, kisiwa kingine cha watu binafsi kilicho kwenye lango la kuingia Miami Beach, ambayo iliuzwa kwa dola milioni 16 au 18," anasema.

Sababu moja inayoelezea kupanda kwa kasi kwa bei za nyumba na ardhi za kifahari sana katika miaka ya hivi karibuni ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho watu matajiri zaidi wanacho na wanaweza kukitumia.

Kulingana na takwimu zilizokusanywa katika ripoti ya "Inequality Index" (Kielezo cha Ukosefu wa Usawa) na wachumi kutoka Chuo Kikuu cha California, Berkeley na Shule ya Uchumi ya Paris, utajiri wa asilimia 0.1 ya watu matajiri zaidi umeongezeka karibu mara 13 katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Katika utafiti huu, watu wenye utajiri wa zaidi ya dola milioni 43 walichukuliwa kuwa ni sehemu ya kundi la asilimia 0.1 ya juu.

Solomon anasema kuwa kiasi hiki cha fedha huongeza kiasi ambacho watu hulipa kwa ajili ya manunuzi: "Wataalamu wa masuala ya nyumba na ardhi husema kuwa thamani ya kitu chochote ni kile ambacho mtu yuko tayari kulipa ili kukipata."

"Kwako na kwangu, kulipa dola milioni 1 kwa ajili ya nyumba au ardhi inaweza kuwa jambo lisilowezekana kufikirika. Kwa wengine, dola milioni 10 ni kiasi kikubwa mno.

Lakini unapokuwa na mabilioni ya dola kwenye akaunti yako, kununua nyumba au ardhi ya dola milioni 60 kunaweza kusiwe jambo la ajabu.

Wengi wao hulipa kiasi hicho kwa pesa taslimu." "Hakika kuna pengo kati ya kiasi ambacho watu wa kawaida wanaweza kumudu kulipia nyumba na majumba haya ya kifahari yenye thamani ya mamilioni ya dola, lakini kiwango cha miamala ya mali zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 60 kinaonyesha kuwa kuna soko linaloendelea kusukuma mipaka ya bei juu zaidi," anasema.

Kulingana na de la Vega, kupanda kwa bei za mali za gharama kubwa zaidi pia kunasababisha kupanda kwa bei za nyumba katika viwango vya chini zaidi.