Je, TikTok na Reels zinaharibu umakini na kumbukumbu za vijana?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Huenda ukachukua simu yako na kuanza kutazama video fupi kabla ya kulala au wakati wa mapumziko mafupi. Dakika chache za kwanza hupita unapokuwa ukitazama mfululizo wa video zinazoonekana kutokuwa na mwisho, na hatimaye unapoinua macho kutoka kwenye skrini yako, unagundua kuwa saa kadhaa zimepita bila wewe kutambua.

Tabia hii ya kila siku imekuwa sehemu ya namna watu wengi wanavyotizama video fupi kwenye mitandao kama TikTok, Instagram Reels, YouTube Shorts na Facebook.

Swali si tu ni muda gani vijana hutumia mbele ya skrini, bali pia ikiwa kasi ya kubadilisha video moja hadi nyingine, pamoja na namna vifaa hivi vilivyoundwa, inaweza kuathiri uwezo wao wa kuzingatia, kukazia fikira na kuhifadhi taarifa.

Nini hutokea wakati picha hazikomi?

Tathmini ya hivi karibuni ya kisayansi ya tafiti 42, iliyohusisha takriban watu 46,900 wenye wastani wa umri wa miaka 16.8, iliyochapishwa na Springer Nature mwezi Juni chini ya kichwa "Can endless browsing be controlled?" (Je, kuangalia vitu mtandaoni bila kikomo kunaweza kudhibitiwa?), ilibaini mara kwa mara uhusiano kati ya matumizi makubwa ya video fupi, mara nyingi kwa saa kadhaa kwa siku, na mambo yafuatayo:

  • Kuongezeka kidogo hadi kwa wastani kwa matatizo ya umakini.
  • Kupungua kwa wastani kwa uwezo wa kumbukumbu ya kufanya kazi na uwezo wa kujidhibiti.
  • Viwango vya juu kwa wastani vya wasiwasi, msongo wa mawazo na huzuni.
  • Kuongezeka kwa wastani kwa dalili zinazoashiria uraibu.

Hata hivyo, tathmini hiyo haisemi kuwa matokeo haya yanathibitisha kwamba video fupi husababisha moja kwa moja kuharibika kwa kumbukumbu au kupungua kwa uwezo wa kuzingatia.

Hii ni kwa sababu tafiti nyingi zilizochambuliwa zilikuwa za kulinganisha hali kwa wakati mmoja (cross-sectional), zilizofanyika kwa kipindi kifupi, na tafiti za muda mrefu na zenye nguvu zaidi bado zinahitajika ili kubaini uhusiano huo ukoje.

Kasi na kutazama bila kikomo

Tafiti zimeonyesha kuwa matumizi kupita kiasi ya maudhui ya sauti na video katika miaka ya awali ya maisha yanaweza kuathiri tabia na muundo wa ubongo. Matokeo haya yanaonyesha uwezekano wa athari za kibaolojia katika hatua mbili muhimu za ukuaji: utoto na ujana.

Watafiti wa utafiti huo pia walizingatia mambo matatu ambayo wabunifu wa mitandao ya kijamii hutumia kuifanya mifumo yao iwe tofauti:

  • Algoriti huchagua maudhui kwa ajili ya mtumiaji.
  • Video huendelea moja baada ya nyingine bila ishara ya wazi ya mwisho wa asili.
  • Kasi ambayo mtumiaji huhama kutoka video moja kwenda nyingine.

Algoriti huchagua video kwa ajili ya mtu mmoja baada ya nyingine, jambo ambalo linaweza kuongeza muda ambao mtu hutumia kwenye jukwaa bila kukusudia.

Je, wazazi wanapaswa kuwa na wasiwasi?

Ushahidi uliopo sasa haujathibitisha wazi kwamba kutazama video fupi kwa muda mrefu husababisha uharibifu wa kudumu wa ubongo au kuharibika kwa kumbukumbu.

Hata hivyo, unaonyesha jambo muhimu: matumizi makubwa yanahusishwa na matatizo mbalimbali ya kiakili na kihisia, ingawa suala hili bado linahitaji utafiti wa kina zaidi.

Mhadhiri Mwandamizi Van Bavel anaamini kuwa matokeo haya yanaangazia suala zito ambalo wazazi wanapaswa kulichukulia kwa uzito, hasa matumizi yanapogeuka kuwa kuvinjari bila kikomo kwa saa kadhaa.

Badala yake, tathmini hiyo inabainisha mambo yanayoweza kusaidia kupunguza hatari, ikiwa ni pamoja na kuwa na mazingira yenye msaada, mfumo wa matumizi ya kidijitali wenye mpangilio na kiwango cha juu cha uelewa na utamaduni wa kidijitali.

Hatimaye, huenda swali muhimu zaidi si ikiwa video fupi ni mbaya zenyewe, bali namna zinavyotumiwa, mara ngapi vijana huzitazama, huzitazama wakati gani, zinachukua nafasi ya shughuli zipi, na ikiwa muundo wake unamlazimisha mtumiaji kuendelea kutazama bila kuwa na sehemu ya wazi ya kusitisha.

Swali kubwa ni: Je, kutazama video kwa kasi kubwa kunaweza kubadilisha namna umakini na kumbukumbu zinavyofanya kazi?

Jibu bado linafanyiwa utafiti.