Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mauaji ya kutisha ya wanawake yalivyoitikisa Afrika Kusini
- Author, Puma Fihlani
- Nafasi, Mwandishi
- Akiripoti kutoka, Ekurhuleni
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kwa sauti iliyojaa majonzi, Nokwanda Matshikiza anasema familia yake imeachwa katika hali ya sintofahamu baada ya kuuawa kwa mpwa wake, Dineo Motapane.
"Sijui tutafanya nini, lakini lazima kuwe na mabadiliko," amesema Nokwanda akizungumza na BBC. "Kwa ajili yetu na kwa ajili ya wanawake wengine wote. Je, ni miili mingapi zaidi itakayopatikana kabla ya hatua kuchukuliwa?"
Nokwanda alizungumza akiwa nyumbani kwa familia karibu na Johannesburg, siku mbili baada ya ndugu kuutambua mwili wa Dineo.
Dineo, mama wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 38, alionekana mara ya mwisho akiwa hai Jumapili iliyopita. Baadaye, mwili wake uliokuwa na majeraha mabaya na ulioungua kwa sehemu ulipatikana katika eneo la Ekurhuleni.
Kwa mujibu wa Nokwanda, familia sasa inakabiliwa na kibarua kigumu cha kumweleza binti ya Dineo kuhusu kifo chake.
"Unaelezaje kwamba mzazi wako aliuawa kikatili, kutupwa kama takataka?" anauliza huku akilia.
Amesema maumivu ya kumpoteza Dineo ni jambo ambalo familia haiwezi kulikubali wala kulisahau kwa urahisi.
Kifo cha Dineo kinakuja wakati kukiwa na ongezeko la matukio ya aina hiyo katika eneo la Ekurhuleni. Mwili wake ni miongoni mwa miili mitatu iliyopatikana katika eneo hilo wiki hii, huku jumla ya miili tisa ya wanawake waliouawa ikipatikana katika mazingira yanayofanana tangu mwezi Julai. Hali hiyo imezua hofu na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa wanawake nchini Afrika Kusini.
Themba Kekana pia anaendelea kuishi katika hali ya mshtuko kufuatia kifo cha mpendwa wake.
Dada yake, Itumeleng Kekana, alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kutoweka katika eneo la Ekurhuleni.
Mwili wa mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 32 ulipatikana mwezi Julai, siku 17 baada ya kuonekana akiwa hai kwa mara ya mwisho. Mwili wake ulikuwa na majeraha mabaya, ukiwa umevalishwa nguo chache na kutupwa chini ya daraja.
"Tumevunjika moyo kwa huzuni," anasema Themba huku akibubujikwa na machozi.
"Ninapomtazama binti mdogo wa dada yangu, macho yangu hujaa machozi. Najua hakuna namna yoyote ninayoweza kumuondolea maumivu haya.
"Hakuna familia inayopaswa kukabiliana na hali kama hii tunayopitia sisi."
Mpaka sasa, ni mtu mmoja tu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo, hatua iliyochukuliwa siku mbili baada ya mwili wa kwanza kupatikana tarehe 15 Julai.
Hata hivyo, hakuna mtu aliyetiwa mbaroni kuhusiana na mauaji ya Itumeleng, Dineo au wanawake wengine sita waliouawa katika eneo la Ekurhuleni.
Waathiriwa wengi walikuwa wanawake vijana wenye umri wa kati ya miaka 20 na 30, na karibu wote walikuwa wamefanyiwa ukatili mkubwa kabla ya kuuawa.
Polisi wa Afrika Kusini hutoa takwimu za uhalifu kila baada ya miezi mitatu. Takwimu za karibuni zinaonyesha kuwa watu 5,427 waliuawa nchini humo kati ya Aprili na Juni mwaka huu.
Ingawa takwimu za serikali hazionyeshi idadi ya wanawake waliouawa pekee, Tume ya kutetea Haki za binadamu ya Afrika Kusini ilisema wanawake 569 waliuawa katika kipindi hicho, sawa na wastani wa wanawake sita kila siku. Pia, wanawake 1,052 walinusurika majaribio ya mauaji.
Matukio haya ya hivi punde yamezidisha hofu miongoni mwa wanawake nchini, ambao tayari walikuwa wakiihofia usalama wao.
Aidha, hali hiyo imeongeza shinikizo kwa serikali kuchukua hatua zaidi, chini ya mwaka mmoja tangu viongozi wa nchi hiyo watangaze ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kuwa janga la kitaifa.
Mnamo Novemba mwaka jana, Waziri wa Maendeleo ya Jamii wa Afrika Kusini, Nokuzola Sisisi Tolashe, alitangaza kuwa ukatili wa kijinsia utashughulikiwa kama janga la kitaifa, akisema hatua hiyo ingeisaidia serikali kukabiliana kwa ufanisi zaidi na tatizo hilo.
Tangazo hilo lilifuatia wiki kadhaa za maandamano, yaliyofikia kilele kwa maandamano ya "Women's Shut Down", wakati Afrika Kusini ikiandaa mkutano wa G20.
Wiki hii, wito wa kutaka hatua zaidi zichukuliwe zimeongezeka.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema hatua muhimu katika kuwalinda wanawake nchini Afrika Kusini ni kuitambua femicide (mauaji ya wanawake kutokana na jinsia yao) kama kosa la jinai linalojitegemea.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa Amnesty International nchini humo, Shenilla Mohamed, alisema: "Kila siku ambayo femicide haitambuliwi kama kosa la jinai ni kushindwa kukabiliana na mauaji yanayowalenga wanawake. Ni wakati wa kulitaja tatizo hili kwa jina lake halisi: femicide."
Aliongeza kuwa femicide ni uhalifu unaochochewa na jinsia, ambapo mwanamke huuawa kwa sababu tu ya kuwa mwanamke.
Kwa mujibu wa Amnesty International, nchi 33 duniani zimeainisha mauaji ya kikatili ya wanawake (femicide) kama kosa maalum la jinai, zikiwemo Gabon na Morocco barani Afrika.
Shirika hilo linaamini kuwa kuifanya femicide kuwa kosa la jinai nchini Afrika Kusini kutasaidia kuonyesha ukubwa halisi wa tatizo hilo na kulipa uzito unaostahili.
"Hatua hiyo itailazimisha serikali kukabiliana na mapungufu yake katika kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya ukatili. Huwezi kutatua tatizo usilolifuatilia kwa karibu," alisema Mohamed.
Wengi nchini Afrika Kusini wanakubaliana kuwa hatua zaidi zinahitajika ili kukomesha mauaji na ukatili dhidi ya wanawake.
Wiki hii, Rais Cyril Ramaphosa aliahidi kwamba uchunguzi wa mauaji yaliyotokea Ekurhuleni utafanyika kikamilifu, akisisitiza kuwa hakuna jambo litakaloachwa bila kuchunguzwa.
"Kama taifa, lazima tusimame kidete kutetea haki, usalama na hadhi ya wanawake na wasichana," alisema rais huyo.
Lebogang Ramofoko, mtetezi wa usawa wa kijinsia na haki za kijamii, amesema kuwa viwango vya ukatili dhidi ya wanawake nchini Afrika Kusini vinaakisi tatizo kubwa zaidi la kutothamini utu wa binadamu.
"Kwa muda mrefu, kuanzia enzi za ukoloni hadi zama za ubaguzi wa rangi, vifo vya wanawake weusi nchini Afrika Kusini havijapewa umuhimu unaostahili," aliiambia BBC.
"Kinachowakumba wanawake leo ni matokeo ya athari za muda mrefu za mifumo hiyo ya ukatili, huku makovu yake ya kisaikolojia yakisalia bila kushughulikiwa kikamilifu," alisema.
"Hii haimaanishi kwamba wanaume wa Kiafrika ni wakatili, lakini katika jamii ambazo zilishuhudia ukatili kwa miongo mingi, wanawake weusi kihistoria ndio walioendelea kubeba mzigo mkubwa wa ukatili huo, na mzunguko huo bado haujavunjwa," alisema Ramofoko.
Katika eneo la Kempton Park, Ekurhuleni, ambako miili mitano kati ya tisa iliyopatikana hivi karibuni iligunduliwa, wanaharakati wa kutetea haki za wanawake wameendelea kushinikiza hatua zaidi zichukuliwe kukabiliana na wimbi la mauaji.
Lumka Maqhubela, mwanachama wa shirika la Girl2Woman Foundation, ambalo limeandaa maandamano ya kuhamasisha umma kuhusu uhalifu huo, amesema jamii imegubikwa na hofu na majonzi.
"Tumejawana huzuni na hofu. Ikiwa polisi hawawezi tena kutulinda, basi serikali inapaswa kuingilia kati na kuchukua hatua," amesema.
Kwa mujibu wa Maqhubela, mamlaka kuwataka wanawake wawe waangalifu zaidi pekee haitoshi.
"Ni wazi kwamba hatupo salama. Polisi hawawezi kutuambia tuwe macho zaidi. Wanapaswa kuongeza juhudi za kuimarisha usalama. Tunatarajiwa kufanya nini kingine? Hatuko salama mahali popote, si majumbani mwetu wala mitaani. Hali hii lazima ikome."
Hofu hiyo inaonekana pia miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
"Sijihisi nikiwa salama. Ninapokwenda dukani, lazima niwe mwangalifu. Hali hii imeniletea msongo mkubwa wa mawazo," amesema Thulisile Sibande, mwenye umri wa miaka 32.
Naye Thembi Mabena, mwenye umri wa miaka 60, amesema alikuwa akiishi katika mtaa mmoja na Dineo Motapane.
"Alikuwa mchangamfu na kupenzi cha wote," alisema akimkumbuka.
"Sasa nina wasiwasi. Ninawajua wasichana wengi wanaosema wanaogopa kwenda dukani peke yao. Hakuna usalama, hata kwangu mimi. Mimi ni mzee, lakini bado sijihisi nikiwa salama."
Kwa upande wake, Lerato Mzizi mwenye umri wa miaka 20 ameelezea hali hiyo kwa maneno machache lakini yenye uzito mkubwa:
"Wanawake nchini Afrika Kusini, hawako salama tena."