Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kukoroma kwa mwenza wako kunaweza kuathiri afya yako bila wewe kujua?
- Author, Ella Kipling
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Umewahi kulala karibu na mwenza anayekoroma na kuamka siku inayofuata ukiwa na msongo wa mawazo, ukikosa umakini au kusahau mambo?
Kwa kuwa kukoroma ni jambo linalotokea kwa watu wengi, mara nyingi huachwa bila kutibiwa na kuchukuliwa kuwa ni usumbufu usio na madhara. Lakini kwa mujibu wa wataalamu, kulala karibu na mtu anayekoroma kunaweza kuathiri afya yako.
Kukoroma husababishwa na mtetemo wa tishu laini zilizopo kwenye njia ya juu ya hewa wakati wa usingizi, anaeleza Dkt. Clare Simon, daktari wa meno anayebobea katika tiba ya usingizi inayohusiana na afya ya meno.
Takribani asilimia 40 ya watu wazima nchini Uingereza hukoroma, huku tatizo hilo likiwaathiri wanaume zaidi kuliko wanawake, kwa mujibu wa British Snoring and Sleep Apnoea Association (BSSAA).
Asilimia 75 ya watu wenye wenza wanaokoroma wanasema usingizi wao umeathirika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa Marekani na Sleep Foundation.
Haya ndiyo unayopaswa kujua kuhusu madhara kwa wenza wa watu wanaokoroma - na mambo unayoweza kufanya.
Umakini na kumbukumbu
Prof. Ama Johal, daktari bingwa wa meno aliyebobea katika kurekebisha mpangilio wa meno na mtaalamu wa usingizi katika, anaeleza kuwa mwenza wa mtu anayekoroma anaweza kuathirika kiasi cha kufikia hatua ya kulazimika kuamka na kwenda kulala katika chumba kingine ili aweze kupata usingizi.
Anaongeza: "Kama binadamu, kimwili hatuwezi kufanya kazi bila usingizi huo muhimu."
Wakati wa usiku, tunapitia hatua mbalimbali za usingizi kwa mizunguko inayojirudia, kwa kawaida kila baada ya dakika 90.
Hatua za usingizi mzito ni muhimu kwa mwili kujirekebisha na kupata nafuu.
Ikiwa usingizi wako unasumbuliwa mara kwa mara, unaweza kutumia muda mchache katika hatua hizi za kurejesha nguvu. Hii inaweza kukufanya uamke ukiwa umechoka, hata kama umetumia muda mrefu kitandani, inaeleza BSSAA.
Ubongo wako huchakata na kuhifadhi taarifa ulizokutana nazo wakati wa mchana unapolala. Usingizi uliokatizwa - ambao unaweza kutokea unapokumbushwa kuamka kutokana na mwenza anayekoroma - unaweza kuvuruga mchakato huu na kuathiri umakini pamoja na kumbukumbu.
Usingizi uliokatizwa pia unaweza kuathiri udhibiti wa homoni, jambo linaloweza kuathiri kiwango cha nguvu na hamasa yako.
Usingizi pia una jukumu katika kudhibiti mifumo ya ubongo inayohusika na msongo wa mawazo na hisia. Unapokatizwa, mifumo hii inaweza kukosa uwiano, hali ambayo inaweza kukufanya uwe mwenye hasira au ukose uvumilivu wa kukabiliana na msongo wa mawazo.
Hili ni jambo ambalo Meg Warren, mwenye umri wa miaka 29, alikumbana nalo wakati kukoroma kwa mwenza wake wa zamani kulipomzuia kulala.
Anasema: "Kila mara nilipoamka kutokana na kukoroma, nilijikuta nikiwa katika hali ya tahadhari kubwa sana."
Meg, ambaye ni afisa wa mawasiliano katika shirika la hisani, alikuwa akimsukuma mwenza wake mara kwa mara usiku na kujaribu kumshawishi ageuke kutoka kulala chali na kulala ubavu.
Anasema alikuwa akiamka "akiwa amechanganyikiwa na mzito wa kichwa, wakati mwingine kiasi kwamba nilihisi kama nina hangover."
Kukoroma kulianza kuathiri uhusiano wao, huku Meg akieleza: "Siku zote nilisema kwamba kama tungeishi pamoja, tungelazimika kuwa na chumba cha ziada kwa usiku ambao kukoroma kungekuwa hakuvumiliki kabisa."
Simon anasema usingizi uliokatizwa kutokana na mwenza kukoroma unaweza kusababisha hasira, mabishano na - iwapo itaamuliwa kulala katika vyumba tofauti - kupungua kwa ukaribu wa kimapenzi.
Anna-Louise Dearden, mwandishi wa habari mwenye umri wa miaka 52, anasema wakati mwingine hulala katika chumba tofauti na mwenza wake kutokana na kukoroma kwake.
Kuwa na chaguo hilo humwezesha kuhakikisha anapata usingizi wa kutosha wakati kukoroma kunapokuwa kumezidi.
Anna-Louise alisema: "Ukiamka na hujapata usingizi mzuri usiku, unakula zaidi na unakuwa mwenye hasira zaidi."
Awali alikuwa akiamka mara kwa mara usiku kutokana na kukoroma, lakini amegundua kuwa kutumia vizibo vya masikioni (ear plugs) ni "msaada mkubwa" kwa sababu vinamwezesha kulala bila kusumbuliwa sana na kelele anaposhirikiana kitanda na mwenza wake.
Ni wakati gani wa kutafuta msaada?
Kuna mambo yanayoweza kufanyika, wanasema Simon na Johal. Lakini kwanza, ni muhimu kutambua ikiwa mwenza wako anakoroma tu au ana tatizo la apnea ya usingizi (sleep apnoea).
"Kitu usichotaka kufanya ni kumfanya mtu akorome kwa sauti ndogo tu usiku huku ukikosa kugundua tatizo la msingi la upumuaji linalohusiana na usingizi," Simon anasema.
Dalili za apnea ya usingizi, hali inayosababisha mtu kuacha kupumua na kuanza tena mara kwa mara akiwa amelala, ni pamoja na kusimama kwa pumzi, kukabwa au kushtuka usiku, kuamka mara kwa mara na kuumwa na kichwa asubuhi.
Ikiwa hivi ndivyo unavyokabiliana navyo, unaweza kupendekezwa kutumia mashine ya Continuous Positive Airway Pressure (CPAP), au hata kufanyiwa upasuaji katika baadhi ya hali, Simon anaeleza.
Kwa kukoroma kwa kawaida, Simon anasema mabadiliko ya mtindo wa maisha yanaweza kusaidia, kama vile kupunguza uzito, kuacha kuvuta sigara, kupunguza unywaji wa pombe kabla ya kulala au kubadilisha mkao wa kulala - kwa mfano, kulala ubavu badala ya chali.
Unaweza pia kumshauri mwenza wako amuone daktari, ambaye anaweza kutoa ushauri zaidi au kumpeleka kwa mtaalamu.
Mtaalamu anaweza kupendekeza kutibu kuziba kwa pua au mzio ikiwa hayo ndiyo yanayosababisha kukoroma, au kutumia kifaa maalumu cha mdomoni kinachosogeza taya ya chini mbele taratibu na kusaidia kuweka njia ya hewa wazi.
Johal anasema wanandoa wengi huvumilia kukoroma "kwa muda mrefu sana", jambo linaloathiri uhusiano wao na ustawi wao.
"Jambo muhimu ni kwamba kuna msaada unaopatikana; kinachohitajika ni kuutafuta na kuutumia."