Jinsi Mecca na maeneo mengine matakatifu yanavyolindwa

Chanzo cha picha, ABDEL GHANI BASHIR/AFP via Getty Images
Muungano wa vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya Yemen na unaotambuliwa na Umoja wa Mataifa, umesema vikosi vya ulinzi wa anga vya Saudi Arabia vilitungua ndege isiyo na rubani (drone) iliyokuwa ikirushwa na Wahouthi, kabla haijaingia katika anga ya mji wa Makka.
Ingawa Wahouthi wa Yemen wamekanusha madai hayo, tangu taarifa hizo kuchapishwa kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu uwezo na ufanisi wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Saudi Arabia, pamoja na mfumo wa ulinzi wa anga unaotumiwa na Riyadh kulinda Makka na miji mingine dhidi ya tishio la mashambulizi.
Saudi Arabia haijaweka wazi ni mfumo gani wa ulinzi ilitumia kuidungua drone hiyo inayodaiwa, lakini Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ilitoa video mwezi Mei 2026 iliyoonyesha mifumo kadhaa ya kurusha makombora, mfumo wa rada na mizinga mikubwa ya kukinga mashambulizi ya anga.
Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia ilisema kikosi cha ulinzi wa anga kinachotumia silaha hizo kina jukumu la "kulinda maeneo matakatifu na kuzuia tishio la mashambulizi ya anga dhidi yake."
BBC Urdu ilizungumza na Hamad Walid, mtafiti wa masuala ya kijeshi na silaha, ili kufahamu ni silaha gani zinazotumiwa na Saudi Arabia kulinda anga yake, hususan katika kulinda maeneo matakatifu ya Kiislamu.
Ni mifumo gani ya ulinzi wa anga ambayo Saudi Arabia inayo?

Chanzo cha picha, Saudi Ministry of Defense
Hammad Walid, mtafiti katika Taasisi ya Strategic Vision Institute, kituo kinachojikita katika utafiti wa silaha, aliiambia BBC Urdu kwamba video iliyotolewa na Saudi Arabia mwezi Mei mwaka huu ilionyesha mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot, pamoja na mifumo ya kurusha makombora na rada zilizotengenezwa nchini Marekani.
Kwa mujibu wake, taarifa rasmi ya Saudi Arabia ilisema mfumo wa Patriot ulipelekwa katika miji hiyo kwa ajili ya kulinda maeneo matakatifu kama Makka na Madina.
Hammad Walid pia aliongeza kuwa mfumo wa bunduki ya kukinga mashambulizi ya anga ulioonekana kwenye video hiyo ni Oerlikon 35mm, uliotengenezwa na kampuni kutoka Uswisi.
Aidha, Saudi Arabia ilinunua mfumo wa ulinzi wa anga wa THAAD kutoka Marekani mwezi Mei 2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ulinzi wake wa anga.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya Saudi Arabia, hafla ya kuzindua mfumo huo wa ulinzi ilifanyika katika Kituo cha Kikosi cha Ulinzi wa Anga za Juu jijini Jeddah.
Mfumo wa makombora wa Patriot ni nini?

Chanzo cha picha, Saudi Ministry of Defense
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa Hammad Walid, mtafiti katika Kituo cha SVI, Saudi Arabia hutumia mfumo wa makombora wa Patriot kuangusha ndege zisizo na rubani (drones) na ndege za kawaida za usafirishaji, pamoja na makombora ya cruise na makombora ya cruise ya masafa marefu.
Mfumo huu wa ulinzi wa makombora na anga ulitengenezwa na kampuni ya Marekani ya Lockheed Martin.
Kwa mujibu wa Lockheed Martin, Saudi Arabia pia ina mfumo wa ulinzi wa Patriot Advanced Capability 3 (PAC-3), ambao una uwezo wa kukabiliana na makombora ya masafa marefu, makombora ya cruise na ndege za kivita.
Mfumo huo unajulikana kwa kutumia rada ya kisasa inayoweza kufuatilia na kuangamiza mashambulizi kadhaa kwa wakati mmoja.
Mbali na kuwa tayari kutumika ndani ya muda mfupi, mfumo huo wa makombora una uwezo wa kustahimili hujuma za kielektroniki.
Hata hivyo, Hammad Walid alisema silaha zinazotumiwa katika mifumo ya PAC-2 na PAC-3 hugharimu mamilioni ya dola.
Kwa sababu hiyo, Saudi Arabia pia hutumia mizinga ya Oerlikon ya kukinga mashambulizi ya anga, mfumo ambao pia unaonekana katika video iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa mtafiti huyo, risasi za milimita 35 zinazotumiwa na mizinga hiyo ya kukinga mashambulizi ya anga ni nafuu zaidi ikilinganishwa na makombora ya mfumo wa Patriot.
"Hii ina maana kwamba mfumo wa ulinzi wa Patriot hutumika kukabiliana na vitisho vikubwa zaidi, kama vile makombora au drones kubwa, wakati mizinga ya Oerlikon ya milimita 35 hutumiwa kuangusha drones ndogo."
Hammad Walid pia alisema mizinga ya Oerlikon ya milimita 35 hutumiwa nchini Pakistan, na ilitumika kwa mafanikio kukabiliana na drones za India mwezi Mei mwaka jana.
Changamoto za usalama za Saudi Arabia
Andrew Davidson, mchambuzi wa jarida la Geopolitical Affairs na aliyekuwa afisa wa Marekani aliyewahi kuhudumu Mashariki ya Kati, anaamini kuwa Saudi Arabia ina uwezo wa kukabiliana na vitisho vinavyoweza kujitokeza, lakini inaweza kupata hasara kubwa iwapo mashambulizi yataendelea kwa muda mrefu au kuwa ya kiwango kikubwa.
Akinukuu takwimu zilizochapishwa na Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati (IISS) mwaka 2025, alisema Saudi Arabia ina makombora 108 ya Patriot, lakini "vita na Iran vinaonyesha kwamba bado inawezekana kushambulia maeneo muhimu."
Kwa mujibu wake, wakati wa mzozo wa hivi karibuni, Saudi Arabia ililazimika kuelekeza rasilimali zake za usalama katika kulinda maeneo matakatifu ya kidini pamoja na miji mingine, vituo vya kijeshi na miundombinu ya nishati.
Andrew Davidson alisema kulenga ulinzi katika maeneo fulani kunamaanisha kuwa rasilimali zinazoweza kutumika kulinda maeneo mengine huwa chache.
"Drones zinazoruka katika mwinuko wa chini hufanya iwe vigumu zaidi kugunduliwa. Wakati huohuo, mashambulizi ya mara kwa mara huweka shinikizo kwenye akiba ya makombora ya ulinzi."
Ingawa hali halisi ya sasa ya akiba ya risasi na silaha za Saudi Arabia haijulikani, hali hiyo inazua wasiwasi kwamba nchi hiyo ya Mashariki ya Kati inaweza pia kukumbwa na athari za uhaba wa kimataifa wa mifumo ya ulinzi wa makombora.



































