Kwa nini mpango wa Marekani kuiuzia Saudi Arabia ndege ya kivita ya F-35 unazua utata?

Rais Donald Trump (kulia) akikutana na Mrithi wa Kiti cha Enzi na Waziri Mkuu wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, wakati wa mazungumzo ya pande mbili katika Ofisi ya Oval, Ikulu ya White House, Washington DC, tarehe 18 Novemba 2025.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Trump na Mwanamfalme mtawala Mohammed bin Salman katika Ikulu ya Marekani
    • Author, Tom Bateman
    • Nafasi, Mwandishi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Utawala wa Rais Donald Trump umesema umeidhinisha uuzaji wa takriban ndege za kivita aina ya F-35 kwa Saudi Arabia, hatua inayotajwa kuashiria mabadiliko ya sera ya Marekani na ambayo imeibua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wabunge wa nchi hiyo.

Kwa miaka mingi, Saudi Arabia imekuwa ikishinikiza kununua ndege hizo za kisasa, zinazotambulika kwa uwezo wake wa kutogundulika kirahisi na mifumo ya rada ya adui.

Hata hivyo, kwa muda mrefu Washington imekuwa ikisita kuidhinisha mauzo hayo. Moja ya sababu kuu ni kwamba tayari huiuzia mshirika wake wa karibu, Israel, ndege za F-35. Chini ya sheria za Marekani, Israel inapaswa kuendelea kuwa na upendeleo wa kupata silaha za kiwango cha juu zaidi kuliko zile zinazoweza kupatikana na mataifa jirani katika Mashariki ya Kati.

Bunge la Marekani lina siku 30 za kupitia na kuchunguza mpango huo, au kujaribu kuuzuia. Mauzo hayo yanakadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 24 (pauni bilioni 17.8) kwa Riyadh, ambayo ni mnunuzi mkubwa wa silaha za Marekani.

Ndege ya kivita aina ya F-35 ya Jeshi la Anga la Marekani ikiruka juu ya eneo la National Mall mjini Washington, DC, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru ya “Salute to America”, tarehe 4 Julai 2026.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Ndege ya F-35 ya Jeshi la Anga la Marekani

Mwakilishi wa jimbo la Illinois kutoka Chama cha Democratic, Raja Krishnamoorthi, alipinga mpango huo siku ya Alhamisi, akionya kuwa unaweza kuhatarisha usalama wa baadhi ya teknolojia nyeti zaidi za kijeshi za Marekani.

Wabunge wengine wa Democratic na baadhi ya maafisa wa ulinzi wa Marekani pia wameeleza wasiwasi kuhusu uamuzi wa kuiuzia Saudi Arabia ndege za F-35. Wanaonya kuwa teknolojia ya hali ya juu inayotumiwa katika ndege hizo inaweza kuishia mikononi mwa China kutokana na ushirikiano wa kiusalama unaoendelea kati ya Riyadh na Beijing.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetetea mpango huo, ikisema unalingana na malengo ya sera ya nje na maslahi ya usalama wa taifa ya Marekani.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, mauzo hayo yataimarisha uwezo wa ulinzi wa Saudi Arabia, mshirika muhimu wa Marekani ambaye si mwanachama wa NATO, na kuchangia uthabiti wa kisiasa pamoja na maendeleo ya kiuchumi katika eneo la Ghuba.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wizara hiyo pia ilisisitiza kuwa uuzaji wa ndege hizo na huduma zinazohusiana nazo hautabadilisha mizani ya nguvu za kijeshi katika Mashariki ya Kati.

Rais Donald Trump ana uhusiano wa karibu na Mrithi wa Utawala wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ambaye alitembelea White House mwezi Novemba mwaka jana.

Viongozi hao wawili pia walikutana Riyadh mwezi Mei mwaka jana, ambako walishuhudia kutiwa saini kwa makubaliano ya mauzo ya silaha yenye thamani ya dola bilioni 142. White House ilieleza makubaliano hayo kuwa makubwa zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya sekta ya ulinzi.

Pendekezo jipya linahusisha mauzo ya ndege 48 za kivita aina ya F-35 zinazotengenezwa na kampuni ya Lockheed Martin.

Iwapo yatatekelezwa, mauzo hayo yataifanya Saudi Arabia kuwa miongoni mwa waendeshaji wakubwa wa ndege hizo katika eneo la Mashariki ya Kati, ikiwa na idadi inayokaribia ile ya Israel, ambayo kwa sasa ina ndege 50 za F-35.

Hata hivyo, Israel tayari imeidhinisha ununuzi wa safu nyingine ya F-35, hatua itakayoiongezea idadi ya ndege hizo hadi 100.

Kwa sasa, ndege moja aina ya F-35A inakadiriwa kugharimu takriban dola milioni 82.5.

Bunge la Marekani limewahi kuonyesha wasiwasi kuhusu mikataba ya silaha na Saudi Arabia, hasa baada ya mauaji ya mwandishi wa habari wa Saudi, Jamal Khashoggi, mwaka 2018.

Utawala wa aliyekuwa Rais Joe Biden pia uliwahi kuzingatia uwezekano wa kuiuzia Saudi Arabia ndege za F-35 iwapo Riyadh ingekubali kuhalalisha uhusiano wake na Israel, lakini juhudi hizo za kidiplomasia hazikufanikiwa.

Pendekezo la mauzo hayo linakuja wakati Saudi Arabia inaendelea kupambana na waasi wa Houthi, kundi linaloungwa mkono na Iran ambalo linadhibiti sehemu kubwa ya magharibi mwa Yemen.

Katika miezi ya hivi karibuni, waasi hao wamefanikiwa kuteka maeneo kadhaa ya pwani ya Bahari ya Shamu nchini Yemen kutoka kwa vikosi vinavyoiunga mkono serikali na vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa vyanzo viwili vinavyofahamu mazungumzo hayo, ambavyo vilinukuliwa na CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, Mwanamfalme na Mtawala wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, amekuwa akimshinikiza Rais Donald Trump kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya waasi wa Houthi.

Hata hivyo, vyanzo hivyo vinasema Trump amekataa kuhusisha moja kwa moja jeshi la Marekani katika mzozo huo.

Ripoti ya ziada imeandaliwa na Sareen Habeshian.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi