Hizi ndizo silaha ambazo Marekani imezituma anga za juu

q

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Robert Granwell
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Tangazo la Marekani kwamba imetuma silaha katika anga ya juu limeibua maswali kuhusu silaha zinazoweza kutumika angani na namna zinavyoweza kutumika katika migogoro ya kijeshi.

Marekani haijatoa maelezo mengi kuhusu silaha hiyo.

Waziri wa Jeshi la Anga la Marekani, Troy Mink, amesema silaha hiyo iliyoko katika mzingo wa dunia (obiti) ni muhimu kwa ajili ya kulinda wanajeshi wa Marekani dhidi ya vitendo vya maadui.

Hata hivyo, hakueleza silaha hiyo ina uwezo gani wala ni lini itaanza kutumika katika obiti.

Kwa hiyo, silaha hiyo inaweza kuwa ya aina gani?

Silaha angani si jambo jipya

Anga ya juu limekuwa eneo la kijeshi tangu mwanzo wa enzi ya safari za anga.

Mwishoni mwa miaka ya 1960, Umoja wa Kisovieti ulipeleka angani silaha zilizoundwa kushambulia satelaiti nyingine.

Mpango huo, uliojulikana kama "Satellite Destroyer", ulihusisha satelaiti zilizoweza kutoa makombora au vipande vya chuma katika njia ya satelaiti nyingine ili kuiharibu.

Leo, mataifa yenye teknolojia kubwa za kijeshi hutumia satelaiti kwa shughuli mbalimbali.

Satelaiti hutumika kukusanya taarifa za kijasusi, kuwezesha mawasiliano salama, kugundua kurushwa kwa makombora na kusaidia kubaini kwa usahihi maeneo yanayolengwa katika mashambulizi.

Wataalamu wanaamini matumizi ya teknolojia za kijeshi angani yataongezeka kadiri teknolojia za vita zinavyoendelea.

Silaha hiyo ya Marekani ikoje?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa sasa hakuna taarifa rasmi inayoonyesha silaha hiyo ni ya aina gani.

Dk Baldin Bowen, mtafiti wa masuala ya kijeshi katika Royal United Services Institute na mhadhiri wa sera za anga katika Chuo Kikuu cha Durham, amesema kuna dhana kadhaa.

Ameambia BBC kwamba huenda Marekani imetuma mfumo wa vita vya kielektroniki unaoweza kuvuruga mawasiliano ya redio.

Pia huenda ikawa ni silaha ya kukabiliana na satelaiti ambayo haihitaji kuiharibu moja kwa moja.

Silaha za aina hii tayari zinatumika duniani na zinaweza kuvuruga mawasiliano ya satelaiti.

Bowen amesema satelaiti ikinyimwa mawasiliano ya redio, inaweza kushindwa kutekeleza kazi zake.

Hata hivyo, hajaondoa uwezekano wa kuwa Marekani imetuma silaha yenye uwezo wa kusababisha uharibifu mkubwa zaidi.

Amesema kuna uwezekano mdogo kwamba silaha hiyo ni kifaa kinachorusha kitu kugonga na kuharibu satelaiti nyingine.

Pia kuna uwezekano kwamba ni satelaiti inayoweza kuikaribia satelaiti nyingine kwa ajili ya kuichunguza au kuingiliana nayo moja kwa moja.

Dk Rod Thornton, profesa wa masuala ya ulinzi na usalama wa Urusi katika King's College London, amesema kinadharia satelaiti hizo zinaweza kutumika kama "hunter-killer satellites".

Hizi ni satelaiti zinazoweza kugonga satelaiti nyingine au kuiondoa kwenye obiti yake.

Aina fulani za silaha za anga zinaweza kuzalisha kiasi kikubwa cha takataka za angani na kusababisha uharibifu mkubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aina fulani za silaha za anga zinaweza kuzalisha kiasi kikubwa cha takataka za angani na kusababisha uharibifu mkubwa.

Tishio la silaha za nyuklia

Urusi pia ina uwezo wa kutumia makombora yanayoweza kulenga satelaiti.

Thornton amesema Urusi ina makombora yanayoweza kurushwa kutoka ardhini kuelekea satelaiti zinazozunguka katika obiti ya chini ya dunia.

Pia ina makombora ya kukabiliana na satelaiti yanayoweza kurushwa kutoka kwenye ndege.

Kwa mujibu wa Thornton, NATO ina satelaiti nyingi zaidi na zenye uwezo mkubwa zaidi wa kutumika kijeshi kuliko Urusi.

Hivyo, anasema Urusi imewekeza katika silaha za kukabiliana na satelaiti ili kupunguza pengo hilo.

Thornton pia ameonya kuhusu uwezekano wa matumizi ya silaha za nyuklia angani katika hali ya mwisho kabisa.

Mlipuko wa nyuklia unaweza kutoa nguvu kubwa ya sumakuumeme ambayo inaweza kuzima satelaiti katika eneo kubwa, ikiwa hazijalindwa dhidi ya athari hiyo.

Hata hivyo, Bowen amesema tukio kama hilo haliwezi kutenganishwa na vita vinavyoweza kuwa vinaendelea duniani.

Kwa nini Marekani imetangaza sasa?

Kwa kuwa silaha za kijeshi angani zimekuwepo kwa muda mrefu, swali ni kwa nini Marekani imeamua kutoa tangazo hili sasa.

Wataalamu waliozungumza na BBC wanasema tangazo hilo si lazima limaanishe kwamba kumetokea maendeleo makubwa mapya ya kiteknolojia, bali linaweza pia kuwa na ujumbe wa kisiasa.

Bowen anaamini huenda hatua hiyo inahusiana na maendeleo ya kijeshi ya China.

Amesema China imekuwa ikiimarisha jeshi lake kwa takribani miaka 30 na imeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya satelaiti za kijeshi ilizonazo angani.

Kadiri Marekani na China zinavyotegemea zaidi mifumo ya anga kwa shughuli zao za kijeshi, ndivyo mifumo hiyo inavyoweza pia kuwa sehemu ya mashindano yao ya kijeshi.

Hali hiyo imeongeza msukumo wa Marekani kuendeleza uwezo wake wa kijeshi angani.

Katika tukio la vita angani, wataalamu wanasema kuna uwezekano wa kutumika aina mbalimbali za silaha na teknolojia, zikiwemo makombora, satelaiti zinazoweza kuzuia au kuharibu satelaiti nyingine.