Muisrael ahukumiwa miaka 13 Jela kwa ujasusi wa Iran
Mahakama nchini Israel imemhukumu kifungo cha miaka 13 jela mwanaume mwenye umri wa miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa niaba ya Iran.
Mwendesha mashtaka alieleza kuwa mtuhumiwa Alexander Granevsky alihusika katika shughuli za kukusanya na kusambaza taarifa kwa mawakala wa Iran, jambo ambalo mahakama ilitaja kuwa lilihatarisha usalama wa taifa la Israel
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, hukumu hiyo ni miongoni mwa adhabu kali zaidi kuwahi kutolewa nchini humo katika kesi zinazohusiana na shughuli za ujasusi kwa niaba ya Iran.
Waendesha mashtaka walisema Granevsky alitekeleza misheni kadhaa baada ya kuwasiliana na mtu aliyedaiwa kuwa wakala wa Iran kupitia programu ya Telegram, akiahidiwa malipo ya fedha kwa kazi alizopewa.
Mahakama ilimpata na hatia ya kuandika kaulimbiu za kupinga serikali katika maeneo mbalimbali kwa kutumia rangi ya dawa ya kupuliza, kuchoma moto magari tisa, pamoja na kufuatilia eneo la makazi la Benny Gantz, aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Israel na Waziri wa Ulinzi.
Pia alihukumiwa kwa kupiga picha za maeneo nyeti, yakiwemo miundombinu ya kuzalisha umeme, na kuwasilisha taarifa hizo kwa mawasiliano yake wa Iran.
Mamlaka za Israel zimekuwa zikitahadharisha kuhusu kile zinachodai ni juhudi za Iran za kuwatumia raia wa Israel kukusanya taarifa za kiintelijensia na kutekeleza vitendo vya hujuma ndani ya nchi.
Hukumu ya Granevsky inaonekana kuashiria msimamo mkali wa Israel dhidi ya vitendo vinavyohusisha ushirikiano na mataifa yanayoonekana kuwa tishio kwa usalama wa taifa.

