Je, unasaga meno bila kujua? Tatizo hili linaongezeka miongoni mwa vijana, madaktari waonya

Chanzo cha picha, Getty Images
Ella hakumbuki ni lini hasa alianza kusaga meno yake wakati wa usiku, lakini anakumbuka vyema alivyokabiliwa ba maumivu makali ya taya, maumivu ya kichwa, na kuambiwa kuwa meno yake ya nyumayalikuwa yakipotea.
"Nilikuwa na maumivu makali sana," anasema Ella. "Umbo la uso wangu lilikuwa likibadilika na meno yangu yalikuwa hatarini kuvunjika - nilijua sina budi kushughulikia hali hiyo."
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 31 ana tatizo la *bruxism*—hali inayoweza kusababisha kusaga meno mara kwa mara na mara nyingi kwa nguvu—lakini anasema matibabu aliyopata hivi karibuni yamebadilisha maisha yake.
Tatizo la *bruxism* huathiri mamilioni ya watu kama Ella kote Uingereza. Tafiti kadhaa zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya wanne hukumbwa na hali hiyo, ingawa wengi huenda hawajui hadi pale dalili zinapoanza kujitokeza.
Kulingana na Chama cha Madaktari wa Meno cha Uingereza (British Dental Association), kuna ushahidi usio rasmi unaoonyesha kuwa ''bruxism'' inazidi kuwa ya kawaida, ingawa hakuna takwimu mahususi. Hata hivyo, baadhi ya madaktari wa meno wameiambia BBC kuwa wana wasiwasi kuhusu ongezeko la idadi ya vijana wanaowahudumia wenye matatizo ya meno yanayosababishwa na tabia hiyo ya kusaga meno bila kuacha.
"Hakika tatizo hili linaongezeka," anasema Dkt. Aditi Desai, rais wa Chama cha Uingereza cha Tiba ya Meno Kuhusiana na Matatizo ya Usingizi (BSDSM). "Na si jambo la kushangaza ikizingatiwa kuwa maisha ya sasa yanaweza kuwa na msongo mkubwa wa mawazo."
Dalili za bruxism: Unawezaje kujua kama unasaga meno?
Bruxism ni neno linalotumika kuelezea aina nne za harakati za taya: kukaza meno (clenching), kusaga meno (grinding), kukaza misuli ya taya (bracing) na kusukuma taya mbele (thrusting).
Watu wengine husaga meno usiku pekee, huku wengine wakifanya hivyo mchana bila kutambua. Kwa baadhi ya watu tatizo hilo huwa dogo, lakini kwa wengine linaweza kuwa kubwa kiasi cha kuharibu hata vifaa vya kinga ya meno na kuwaamsha wenzi wao usiku.
Ikiwa hujui kama una bruxism, wataalamu wanasema zipo dalili kadhaa za kuangalia:
- Meno yaliyovaliwa, kupasuka au kusawazika kutokana na msuguano
- Maumivu ya kichwa au ya uso unapoamka asubuhi
- Kukakamaa kwa taya
- Usingizi usiotulia na uchovu mchana
- Kuongezeka kwa hisia za maumivu kwenye meno
- Maumivu ya sikio au sehemu ya mahekalu ya kichwa bila kuwepo maambukizi
Uhusiano kati ya msongo wa mawazo na kusaga meno

Chanzo cha picha, Simon Cove
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa Chama cha Uingereza cha Ushauri Nasaha na Tiba ya Kisaikolojia (BACP), suala la kusaga meno sasa linatajwa mara nyingi zaidi katika vikao vya tiba ya kisaikolojia, huku watu wengi wakizidi kutambua athari za afya ya akili kwa miili yao.
Mtaalamu wa saikolojia Rahi Popat anasema wateja wake wengi, hasa vijana, hueleza kuwa wao au watu wa karibu nao wamegundua tabia ya kusaga meno. Mara nyingi wanaweza kuhusisha tabia hiyo na kipindi cha msongo mkubwa wa mawazo katika maisha yao.
"Wengi hugundua kuwa kusaga meno kuliongezeka au hata kulianza kabisa wakati walipokuwa wakipitia kipindi kigumu na chenye msongo mkubwa," anasema.
'Njia ya kutoa sehemu ya msongo wa mawazo'
Kulingana na Popat, mshtuko wa kihisia, kiwewe au msongo wa mawazo unaweza kuusukuma mwili katika hali inayojulikana kama "fight or flight" (pigana au kimbia).
Katika hali hiyo:
- Mapigo ya moyo huongezeka
- Mwili hutoa homoni ya adrenalin
- Misuli hukaza kujiandaa kukabiliana na tishio
Kwa kuwa taya na mfumo wa fahamu vina uhusiano wa karibu kupitia neva kuu za fuvu la kichwa, misuli ya taya nayo huathiriwa. Matokeo yake ni kukaza au kusaga meno, mara nyingi bila mtu kufahamu.
Kwa baadhi ya wataalamu, hii inaweza kuwa moja ya njia ambazo mwili hujaribu kuachilia mvutano wa kihisia uliojikusanya. Hata hivyo, endapo tabia hiyo itaendelea kwa muda mrefu, inaweza kusababisha maumivu, uharibifu wa meno na matatizo mengine ya afya ya taya.
Jinsi Ella alivyoanza kutafuta msaada
Kwa mujibu wa mtaalamu wa saikolojia Rahi Popat, kusaga meno wakati wa usingizi kunaweza kuwa njia ambayo mwili huachilia sehemu ya msongo na mvutano uliokusanyika mchana.
"Tunapofanya hivyo usiku, inaweza kuwa njia ambayo mwili huachilia baadhi ya msongo na mvutano tuliokumbana nao wakati wa mchana," anasema.
Kwa Ella, kusaga meno akiwa usingizini kuligeuka kuwa njia ya mwili wake kukabiliana na mkazo aliokuwa akibeba akiwa macho.
"Ninajua tatizo hili lina uhusiano na viwango vyangu vya msongo wa mawazo," anaiambia BBC. "Nina wasiwasi wa hali ya juu ambao si rahisi kutambuliwa. Ukikutana nami, huenda usingedhani hivyo."
Anasema mara nyingi hujisitiri nyuma ya ratiba iliyojaa shughuli nyingi.
"Nina shughuli nyingi muda wote na napenda kutoka mara kwa mara. Hiyo ndiyo njia yangu ya kuficha ninachopitia."
Kwa miaka mingi akiwa katika umri wa miaka ya ishirini, Ella alijaribu kuvumilia maumivu yaliyosababishwa na hali hiyo.
"Nilijaribu kuishi nayo tu," anasema.
Lakini hali ilibadilika alipofahamishwa na daktari wake wa meno kwamba meno yake yalikuwa yameanza kuathirika na yalikuwa katika hatari ya kuharibika zaidi ikiwa asingechukua hatua.
Onyo hilo lilimfanya atafakari upya.
Miaka michache baadaye, Ella aliamua kutafuta matibabu, akisema hofu ya kupoteza meno yake ndiyo iliyomsukuma kuchukua hatua baada ya muda mrefu wa kuvumilia maumivu na usumbufu uliosababishwa na kusaga meno usiku.

Chanzo cha picha, Ella
Ingawa matibabu hayo hayapatikani kwa kawaida kupitia Huduma ya Taifa ya Afya ya Uingereza (NHS), Ella aliamua kugharamia mwenyewe sindano za Botox ili kukabiliana na tatizo lake la kusaga meno.
Matibabu hayo yalihusisha kudungwa Botox kwenye misuli ya masseter, misuli inayohusika na harakati za taya na kutafuna. Kwa mujibu wa madaktari, sindano hizo husaidia kulegeza misuli hiyo na kupunguza nguvu ya kukaza na kusaga meno. Athari zake huweza kudumu kwa takriban miezi mitatu hadi minne.
Kwa Ella, matokeo yake yalionekana haraka.
"Kwa miezi michache iliyopita nimeweza kulala vizuri," anasema.
Anasema usingizi wake umeimarika, maumivu aliyokuwa akiyapata yamepungua na hali yake kwa ujumla imebadilika.
"Nina nguvu nyingi zaidi ninapoamka asubuhi, maumivu yamepungua na uso wangu hauonekani wa mraba kama ulivyokuwa awali," anasema.
Kwa watu wengi wanaokabiliwa na bruxism, matibabu huanza kwa matumizi ya kinga ya meno wakati wa usingizi na mbinu za kupunguza msongo wa mawazo. Hata hivyo, baadhi ya wagonjwa kama Ella huamua kutafuta njia mbadala pale ambapo maumivu na athari za kusaga meno zinaendelea kuathiri maisha yao ya kila siku.
Watu wanaosaga meno wanaweza kusaidiwa kupunguza athari za tatizo hilo kwa kutumia kinga maalumu ya meno (mouthguard), lakini wataalamu wanasema ni muhimu zaidi kutafuta chanzo halisi cha tatizo hilo.
Daktari bingwa wa usingizi na afya ya meno, Dkt. Aditi Desai, amesema mara nyingi wagonjwa hupewa kinga za meno bila kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini sababu inayowafanya kusaga meno.
"Mara nyingi sana madaktari wa meno hutoa kinga za meno bila kuangalia kwa nini hali hiyo inatokea," amesema.
Kwa mujibu wa Dkt. Desai, ni muhimu kuzingatia uwezekano wa kuwepo kwa matatizo mengine ya kiafya yanayoweza kusababisha kusaga meno, ikiwemo apnea ya usingizi inayotokana na kuziba kwa njia ya hewa (OSA).
Hali hiyo hutokea wakati njia ya hewa inapoziba mtu akiwa amelala, jambo linaloweza kuathiri upumuaji wake. Katika baadhi ya matukio, mgonjwa anaweza kusaga meno bila kujitambua kama njia ya mwili kujaribu kuondoa au kusogeza kizuizi katika njia ya hewa ili kuruhusu upumuaji kurejea katika hali ya kawaida.
Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa kutambua chanzo kikuu cha kusaga meno kunaweza kusaidia kutoa matibabu sahihi na kuzuia madhara ya muda mrefu kwa afya ya meno na usingizi wa mgonjwa.















