CHADEMA yakanusha kufanya mazungumzo ya siri na serikali

.

Chanzo cha picha, CHADEMA

Maelezo ya picha, John Mnyika
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Chama Kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kimesema hakijafanya mazungumzo yoyote na Serikali ama mamlaka nyingine yoyote kuhusu masuala ya kisiasa na maridhiano ya kisiasa nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, amesema chama hicho pamoja na Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, hakijafanya mazungumzo ya aina hiyo akikanusha kuhusu kuwepo kwa mawasiliano yanayoendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 3, 2026, Mnyika alisema kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa Julai 30, 2026 wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya siasa haikuhusu CHADEMA.

"Sisi kama chama tunasisitiza kwamba Mwenyekiti Lissu wala CHADEMA hatujawahi kuwa na makubaliano ya siri wala ya kificho. Msimamo wetu umekuwa wazi kwa umma muda wote," alisema Mnyika.

Julai 30, 2026, Rais Samia alikutana na viongozi wa vyama 18 kati ya 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu. CHADEMA hakikushiriki mkutano huo. Katika hotuba yake, Rais alisema; "Kuna mwenzetu mmoja bado anaendelea kutafakari. Bado tunaendelea kupokea misukumo yake, conditions zake na matakwa yake".

Japo Rais Samia hakutaja mtu wala chama, kauli hiyo ilitafsiriwa na wengi kama inailenga CHADEMA ama na Kiongozi wake Tundu Lissu. Kwa kuwa ndiye kiongozi pekee na chama pekee kati ya ambacho hakikushiriki mkutano huo.

Kuhusu hilo Mnyika aliongeza kuwa baada ya kusikia kauli hiyo ya Rais, viongozi wa chama walimtafuta Tundu Lissu ili kujiridhisha kama kulikuwa na mazungumzo yoyote na serikali, lakini Lissu aliwaeleza kuwa tangu alipokutana na Rais Mstaafu wa Malawi, Lazarus Chakwera, hajazungumza na mamlaka yeyote kuhusu masuala ya maridhiano ya kisiasa au katiba

Kutokana na hali hiyo, Mnyika amesema viongozi na wanachama wa CHADEMA wanapaswa kuendelea kushikilia msimamo wa chama kama ulivyotangazwa hadharani, kwamba hawatashiriki mazungumzo ya maridhiano ya kisiasa mpaka Lissu anayeshiukiliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa kesi ya uhaini, aachiwe huru na mazungumzo yashirikishe mpatanishi kutoka nje.