Sababu ya vijana wengi wa kiume kufunga mirija ya uzazi

Chanzo cha picha, Alex West
Alex West aliachwa akiwa ameshtushwa sana na uchungu na ugumu wa kujifungua ambao mke wake alipitia wakati wa kujifungua mtoto wao wa kwanza. Ilipofika zamu ya mtoto wao wa pili, alitumaini kuzaliwa huko kungekuwa kwa urahisi zaidi.
Kwa kweli, kujifungua kulikuwa rahisi zaidi kwa mke wake, lakini si kwa Alex.
"Nilipatwa na hofu na nikavunjika moyo kabisa. Sikuwa nimeweza, sikuwa na uwezo wa kuchakata kile kilichotokea," Alex anasema.
Kiwewe ambacho hakikuwa kimetatuliwa kutokana na kujifungua kwa mara ya kwanza kwa mke wake, pamoja na msongo wa mawazo baada ya kujifungua alioupata, kilimfanya Alex asitamani kuendelea na mpango wao wa kupata watoto wanne.
Alex anakumbuka miezi iliyofuata baada ya kuzaliwa kwa wanawe wawili kuwa ilikuwa ya "giza na huzuni", maisha yalionekana hayana furaha wala matumaini, huku watu wakimwambia kila mara kwamba kuwa baba kunapaswa kuwa uzoefu wa ajabu.
"Sikuhisi ule upendo na uhusiano wa karibu ambao kila mtu anasema nilipaswa kuuhisi," Alex anasema.
Kwa kuwa hakutaka kupitia hali hiyo tena, yeye na mke wake walikubaliana kuishia kupata watoto wawili. Kwa kuwa Alex ndiye aliyekuwa msukumo mkuu wa uamuzi huo, alihisi kwamba "haikuwa sawa kumtwika mke wangu jukumu la kutumia njia za uzazi wa mpango."
Hivyo, kama maelfu ya wanaume wengine nchini Uingereza katika miaka ya hivi karibuni, Alex aliamua kufanyiwa vasectomy yaani upasuaji wa kufunga mirija ya mbegu za kiume.
Utaratibu huo unahusisha kukata kisha kufunga au kuziba mirija ya mbegu za kiume, ambayo ipo kwenye kila korodani na husafirisha mbegu za kiume kwenda kwenye mrija wa mkojo. Kwa lugha ya kawaida, utaratibu huu hujulikana kama "the snip", yaani kukatwa kwa mirija ya mbegu ili kuzuia uwezo wa kupata watoto.
Kulingana na takwimu zilizokusanywa na NHS England, jumla ya upasuaji kwa watu 26,385 wa vasectomy ulifanyika katika hospitali na kliniki wakati wa mwaka wa fedha 2024–2025. Hii ilikuwa ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na mwaka wa 2023–2024.
Wanaume wenye umri wa miaka 35 hadi 39 ndio walifanyiwa upasuaji huo kwa idadi kubwa zaidi kuliko kundi lolote la umri, ambapo takribani wanaume 8,400 walifanyiwa upasuaji katika mwaka wa 2024–2025.
Pia kulikuwa na ongezeko dogo la wanaume vijana waliochagua kufanyiwa vasectomy ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Takribani wanaume 950 wenye umri wa chini ya miaka 30 nchini Uingereza walifanyiwa upasuaji huo katika kipindi cha 2024–2025.
Hofu kuhusu ujauzito
Alex, ambaye ni dalali wa mikopo ya nyumba, aliamua akiwa mwishoni mwa miaka yake ya ishirini kufanyiwa upasuaji wa kufunga mrija, lakini daktari wake alimshauri asubiri hadi atakapofikisha umri wa miaka 30, kwa sababu huenda atabadilisha uamuzi wake.
Hatimaye, siku ya miadi ilipowadia mwezi Mei 2024, yeye na mke wake walipanda treni kutoka nyumbani kwao huko Kent kuelekea kliniki moja mjini London.
Alex, ambaye sasa ana umri wa miaka 33, anasema utaratibu huo ulikuwa wa haraka na haukuwa na maumivu.
"Nilivaa vifaa vyangu vya kusikilizia muziki na nikasikiliza takribani nyimbo tatu tu, kabla hawajaniambia kwamba kila kitu kilikuwa kimekwisha."
"Ilikuwa ya kushangaza, haraka kupita kiasi."

Chanzo cha picha, Sam Knight
Sam Knight, ambaye anatoka Marekani, anasema alijua tangu mapema kwamba hakutaka kuwa na watoto.
"Nilikuwa najikuta katika mazingira ambayo kupata watoto kungeweza kuwa jambo linalowezekana, na hilo lilianza kunitisha sana," Sam anasema.
Mpenzi wake wa wakati huo alipopata ujauzito, aliamua kutoa mimba. Sam, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 22, alihisi kwamba alihitaji kufanya mabadiliko.
"Nilitambua kile ambacho nimemsababishia mtu mwingine kupitia, na sikutaka jambo kama hilo litokee tena."
Aliwasiliana na kliniki ya magonjwa ya mfumo wa mkojo huko New York, na kama ilivyokuwa kwa Alex, alilazimika kuwaeleza wataalamu wa afya sababu zilizomfanya atake kufanyiwa vasectomy.
Sam alishauriwa kuuchukulia upasuaji huo kuwa wa kudumu, kwa sababu ingawa kuna uwezekano wa kuurejesha , hilo linawezekana katika mazingira machache tu na halina uhakika wa kufanikiwa.
Masharti makali ya kufanya upasuaji wa kurejesha hali ya awali
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa sababu alikuwa anaomba kufanyiwa vasectomy akiwa bado na umri mdogo, Sam alikuwa amejiandaa kwa maswali ambayo alijua daktari wake angemwuliza:
"Je, huoni kwamba bado wewe ni mdogo sana kuamua hutaki watoto?"
"Inawezekana ukabadilisha mawazo yako baadaye?"
"Unajua kwamba upasuaji wa kurejesha vasectomy ni wa gharama kubwa na si mara zote hufanikiwa?"
"Kwa kweli, daktari aliniambia kwamba alikuwa amebadilisha mtazamo wake hivi karibuni," Sam anasema. "Na kama ningekuwa nimekuja miezi sita mapema, angenikatalia mara moja."
Sam alifanyiwa upasuaji wa vasectomy miezi michache baada ya kuwasiliana na kliniki kwa mara ya kwanza.
Maswali ambayo daktari wa Sam alimwuliza yalikuwa na lengo la kuhakikisha kwamba alikuwa anafanya uamuzi ambao angeweza kuishi nao maisha yake yote. Kulingana na mwongozo wa NHS Scotland, wanaume walio chini ya umri wa miaka 30 wana uwezekano mkubwa zaidi wa kujutia kufanyiwa vasectomy.
Dr Sarah Salkeld, ambaye alikuwa daktari wa familia na sasa ni mkurugenzi wa matibabu katika MSI Reproductive Choices, kundi la kliniki zinazotoa huduma mbalimbali za uzazi wa mpango kwa wagonjwa wa NHS na binafsi, anasema vasectomy ni "salama sana na yenye ufanisi mkubwa."
Hata hivyo, anasisitiza kwamba ni muhimu wanaume "wafikirie kwa makini sana" kabla ya kuamua kama vasectomy ndiyo njia inayowafaa.
"Tunawapa wote ushauri nasaha ikiwa wanahitaji, ili kuwasaidia kuzungumzia uamuzi huo na kuhakikisha wana taarifa zote muhimu kabla ya kuamua."
Anaongeza kuwa upasuaji wa kurejesha vasectomy haupatikani kwa kawaida kupitia NHS, kwa sababu kuna vigezo na masharti makali vinavyopaswa kutimizwa ili mtu afanyiwe huduma hiyo.
Tovuti ya NHS pia inaeleza kuwa kuna njia nyingine za uzazi wa mpango zinazopatikana kwa wanaume, ikiwa ni pamoja na kondomu na mbinu ya kutambua siku za kutunga mimba , ambayo inahusisha kuepuka kufanya ngono au kutumia kondomu katika siku ambazo mwenzi wa kike ana uwezekano mkubwa wa kushika mimba.
Sam alimweleza daktari wake kwamba, ingawa anawapenda watoto na alikuwa na utoto wenye furaha, alitaka kuendelea kuweka mkazo kwenye kazi yake kama mbunifu wa sauti kwa ajili ya michezo ya video.

Chanzo cha picha, Alex West
"Nimejitolea maisha yangu yote kwa kazi hii, na kwa mtazamo wangu, kulea watoto ni jambo ambalo pia linahitaji kujitolea maisha yako yote," Sam anasema. "Sina nafasi ya kiakili, muda, wala hata hamu ya kufanya hivyo."
Sam, ambaye sasa ana umri wa miaka 25, anasema anawaonea wivu wale wanaotamani kuwa wazazi, kwa sababu anaamini uzoefu huo kwa hakika una uzuri na upendo ndani yake. Hata hivyo, anaongeza:
"Mimi hupata hisia hizo kupitia muziki, sanaa, na mambo mengine ninayofanya."
Upasuaji wa vasectomy alioufanyiwa mwaka 2024, pamoja na huduma za uangalizi baada ya upasuaji, ulimgharimu Sam takribani dola za Marekani 1,200. Wakati huo bado alikuwa akitumia bima ya afya ya familia yake.
Kwa mujibu wa National Survey of Family Growth, ambayo ilichambua majibu ya takribani wanaume 4,000 katika kipindi cha 2022–2023, Sam ni miongoni mwa chini ya asilimia 1 ya wanaume nchini Marekani wenye umri wa miaka 18 hadi 29 ambao wamewahi kufanyiwa vasectomy.
Utafiti huo pia ulionesha kuwa wanaume wenye umri wa katikati hadi mwishoni mwa miaka ya arobaini (40–49) ndio waliokuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa wamefanyiwa vasectomy, ambapo asilimia 15 yao walisema walikuwa wamepitia utaratibu huo.
Kujitoa mhanga na kutokuwa na uhakika kunakoambatana na kuwa mzazi
Sam alipata maumivu makali sana mara moja wiki moja baada ya kufanyiwa upasuaji wa vasectomy. Kulingana na Dkt. Sarah Salkeld, hili ni tatizo linalojulikana lakini hutokea kwa nadra baada ya vasectomy. Hata hivyo, maumivu hayo yalipungua na kutoweka baada ya saa chache.
Sam haamini kwamba hali hiyo inapaswa kuwakatisha tamaa wanaume wengine wanaofikiria kufanyiwa vasectomy.
"Kwa ujumla, upasuaji huo unastahili gharama yake na hata maumivu yake," anasema.
Mwanaume mwingine pia alituambia kwamba kujitoa kunakohitajika katika malezi ya watoto, pamoja na kutokuwa na uhakika kuhusu jinsi watoto watakavyokua au watakavyokuwa baadaye, kulimfanya aamue kufanyiwa vasectomy akiwa na umri wa miaka 27.
Huko Kent, Alex na mke wake walihisi kwamba uamuzi wa kufanyiwa vasectomy ulikuwa njia ya haki zaidi na yenye ufanisi zaidi ya uzazi wa mpango iliyowafaa wote wawili.
Walichukua miezi kadhaa kutafakari kwa makini uamuzi huo, wakijua kwamba Alex hakutaka kuongeza idadi ya watoto katika familia yao.
"Ninawapenda sana watoto wangu," Alex anasema, hasa sasa kwa kuwa wamekua kiasi cha kuweza kucheza mpira wa miguu pamoja naye.
"Kama ningekuwa nimeongeza watoto wengine kwenye timu yangu, hilo lisingekuwa jambo sahihi kwangu."















