Changamoto mpya inayowakabili Democrats: Je, msimamo wao kuhusu Israel ni upi?

Chanzo cha picha, Picha ya video
Zikiwa zimesalia miezi mninne kaba ya uchaguzi wa Marekani wa katikati ya muhula, chama cha Democratickinakabiliwa na changamoto ambazo zinaendelea kuongezeka.
Israel na operesheni zake za kijeshi huko Gaza na eneo zima la Mashariki ya Kati inazidi kuwa suala muhimu na la msingi kwa Chama cha Democratic, huenda ikachangia hoja itakayounda upya uongozi wa chama hicho katika uchaguzi ujao.
Ushahidi kutoka kwa kura za mchujo za Democratic 2026, ambapo wapiga kura watamchagua mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa Novemba, unaonyesha kuwa suala hili linaweza kuwa chanzo cha mapambano kati ya wapiga kura na uongozi wa chama.
Matokeo ya mchujo wa ubunge wa wiki iliyopita katika Jiji la New York yalikuwa mfano wa kile kitakachotokea mbeleni, na mianya ilionekana dhahiri katika kinyang'anyiro cha uwakilishi katika Wilaya ya 10 ya Jiji.
Ingawa wagombea wote wa chama cha Democratic walikuwa Wayahudi, walipinga mipango ya Rais wa Marekani Donald Trump, na kujiona kuwa Wazayuni waliberali, mmoja wao alichukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Israeli kuliko mwingine.
Mkaguzi wa Jiji la New York Brad Lander, ambaye ameitaja operesheni ya kijeshi ya Israeli huko Gaza kuwa mauaji ya halaiki, aliahidi kupiga kura dhidi ya ufadhili wa Marekani kwa jeshi la Israel na kuongeza kuwa hatakubali michango ya kampeni kutoka kwa AIPAC, Kamati ya Masuala ya Umma ya Israel nchini Marekani.
Kwa upande mwingine, Mbunge Dan Goldman, pia ameikosoa serikali ya Israel na kupinga upanuzi wa makazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi, lakini hakutumia neno mauaji ya halaiki kuashiria hali ya Gaza ingawa alawahi kupokea ufadhili kutoka kwa AIPAC.
Bw. Goldman mara kwa mara amezungumzia kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi na kuunga mkono na viongozi kadhaa katika jamii ya Wayahudi wa Orthodox, suala ambalo ni muhimu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Matokeo ya New York 10th District, na chaguzi zingine mbili za mchujo jijini humo zikiwa na wagombea wanaoungwa mkono na Meya wa New York Zahran Mamdani, yalionyesha kwamba wagombea waliopatia kipaumbele ukosoaji wa Israel kuwa katika kampeni zao za kisiasa waliwashinda wagombea ambao wapiga kura waliwachukulia kuwa na misimamo ya wastani.
Matokeo hayo yaliashiria mgawanyiko katika Chama cha Democratic ambao unaweza kuathiri kampeni zijazo msimu huu wa vuli, ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa mchujo wa chama kuamua ni nani atakayegombea kiti ya Seneti cha Michigan katika uchaguzi mkuu wa Marekani mwezi Agosti.
Kwa sababu Jiji la New York kwa kiasi kikubwa ni ngome ya chama cha Democratic, washindi wa uchaguzi wake wa mchujo wana nafasi ya kuingia Bungeni mwaka ujao. Uwepo wao Washington unaweza kuzua majadiliano mazito zaidi kuhusu ufadhili wa Marekani kwa Israelina jeshi lake na kubadilisha msimamo wa chama kuhusu Israel na Gaza.
"Nadhani tunachokiona ni kwamba katika sehemu kubwa ya chama cha Democratic, hasa katika maeneo ya mijini, yaliyo na vijana wanendesha kampeni ya ukosoaji dhidi ya Israel ni ishara kwamba mgombea hatasalia kimya na lengo lakekuu akiingia Bungeni ni kurekebisha mambo," alisema Tali DeGroot, makamu wa rais wa mkakati wa kisiasa na kidijitali katika G-Street, shirika linalounga mkono Israel ingawa limemkosoa Benjamin Netanyahu na mienendo ya vikosi vya jeshi la Israel huko Gaza.
Bi. DeGroote alisema kwamba kadri mitazamo ya Wamarekani unavyobadilika, wapiga kura, hasa vijana wanaojitambulisha kama Wademocrats, "wanataka kuona maafisa waliochaguliwa wakichukua misimamo dhabiti kuhusu suala hili lenye utata."
JStreet ilimuunga mkono Bw. Goldman katika kinyang'anyiro hicho, lakini katika hatua isiyo ya kawaida, pia ilimtaja Bw. Lander kama mgombea "aliyeidhinishwa" ili kuwatia moyo wapiga kura kumfikiria. Bw. Lander pia alipokea uungwaji mkono wa kundi la haki za kijamii la mrengo wa kushoto Jews for Racial and Economic Justice, ambalo limetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na kupinga mauzo ya silaha ya Marekani kwa Israel.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jumanne iliyopita, wale waliompigia kura Bw. Lander mjini Brooklyn, walisema wamevutiwa na msimamo wake dhidi ya Israel na uungwaji mkono wa Mamdani kwa kampeni yake kama sababu iliyochochea uamuzi wao. Meya wa New York pia amekuwa mkosoaji mkubwa wa Israel.
"Nilijifunza mengi kutokana na kumtazama kiongozi wa Kiyahudi akifafanua msimamo wake kuhusu Uzayuni, Israel na kupinga mauaji ya halaiki huko Gaza," alisema Perrin Roosevelt Ireland, ambaye alimpigia kura Bw. Lander Jumanne katika kitongoji cha Park Slope huko Brooklyn. "Imekuwa jambo la kutia moyo sana kwangu kufuata njia hiyo, na napenda uongozi unaobadilika nakutilia maanani maslahi ya umma."
Anaamini kwamba Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti Chuck Schumer na Kiongozi wa Wachache katika Baraza la Wawakilishi Hakeem Jeffries, ambao ni viongozi wawili wakuu Democratic katika Bunge na ambao wanaiwakilisha New York, wamewatenga wapiga kura wao kwa kuunga mkono Israel.
"Nadhani walikosa hoja muhimu sana," anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Israel lilianzisha operesheni yake mjini Gaza kujibu shambulio la Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, ambayo takwimu zake zinachukuliwa kuwa za kuaminika na Umoja wa Mataifa, takriban watu 73,058 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu wakati huo, zaidi ya 21,280 kati yao wakiwa watoto.
Israel imekanusha vikali shtaka la mauaji ya halaiki lililotolewa na mashirika kadhaa ya kimataifa na Israel ya haki za binadamu, wataalam huru wa Umoja wa Mataifa na watafiti.
Wiki iliyopita, ripoti ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa iligundua kuwa mamlaka za Israel na vikosi vya usalama vimewalenga kimakusudi watoto wa Kipalestina huko Gaza, hatua ambayo ni sawa na mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. Jopo la wataalam watatu sio msemaji rasmi wa Umoja wa Mataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilisema "inapinga vikali" ripoti ya tume hiyo, ikiitaja kuwa ni propaganda.
Kura ya maoni ya Kituo cha Utafiti cha Pew mwezi Aprili iligundua kuwa asilimia 60 ya watu wazima wa Marekani wana mtazamo hasi kuhusu Israel, kutoka asilimia 53 mwaka jana.
Asilimia 80 ya wapiga kura wanaoegemea upande wa Democrats walikuwa na maoni sawa, ikiwa ni ongezeko la alama 11 kutoka mwaka jana.
Mabadiliko haya ya maoni ya umma ya Marekani pia yamefikia Chama cha Republican. Kulingana na Pew, zaidi ya nusu ya Warepublican walio chini ya umri wa miaka 50 sasa wana mtazamo hasi kuhusu Israel. Bw. Trump mwenyewe amesema amechoshwa na Netanyahu, na kundi la "America First" la Chama cha Republican linalojitenga limeelezea waziwazi kutoridhika kwake na muungano wa Marekani na Israel.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












