Je, Netanyahu ataivamia tena Iran kabla ya uchaguzi wa Israel?

Chanzo cha picha, Getty Images
Zikiwa zimesalia wiki chache kabla ya uchaguzi wa Israel, kura za maoni bado hazionyeshi idadi ya wabunge inayohitajika kuendelea kwa serikali ya Benjamin Netanyahu, mwanasiasa ambaye amekuwa kileleni mwa siasa za Israel kwa miongo kadhaa na kupitia misukosuko mbalimbali.
Hata hivyo, hali inayojitokeza kuelekea uchaguzi imeibua maswali mapya kuhusu mustakabali wa eneo hilo.
Kauli za hivi karibuni za Netanyahu kuhusu kuendelea kukabiliana na Iran sasa zimeibua maswali kuhusu athari ambazo mzozo mwingine unaweza kuwa nazo kwa mustakabali wake wa kisiasa.
Septemba 3, katika mkutano na makamanda wa jeshi, Benjamin Netanyahu alisema kuipindua serikali ya Iran bado ni "dhamira kuu" ya nchi yake na ni lengo linaloweza kufikiwa. Hii ni licha ya kura ya maoni ya Channel 12 ya Israel ya Septemba 14, iliyoonyesha kuwa kambi ya Netanyahu ilikuwa na viti 50, pungufu ya viti 61 vinavyohitajika kupata wingi bungeni.
Kabla ya uchaguzi wa Oktoba 27, Waziri Mkuu wa Israel bado ana muda wa kujaribu kubadili mazingira ya ushindani wa kisiasa. Lakini je, kuongeza mvutano na Iran kunaweza kuwa moja ya chaguo zake? Na ikiwa ndivyo, msaada wa Marekani na mwitikio wa wapiga kura vitaweka mipaka gani kwake?

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchaguzi una nafasi gani katika uamuzi wa Netanyahu?
Miongoni mwa wapinzani wa Netanyahu, kuna wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutumia vita kama chombo cha kisiasa katika uchaguzi, ingawa wataalamu wanatofautiana kuhusu kiwango ambacho jambo hilo linaeleza mwenendo wake dhidi ya Iran.
Dalia Sheindlin, mwanasayansi wa siasa, mtaalamu wa maoni ya umma na mwandishi wa kitabu The Crooked Stick of Democracy in Israel: Unfulfilled Promises, aliiambia BBC Persian:
"Waungaji mkono wengi wa vyama vya upinzani wanashuku sana kwamba ataongeza mvutano mahali fulani ili kuathiri uchaguzi. Sidhani kama atakuwa na uwezo wa kuongeza mvutano hadi kufikia vita kamili, isipokuwa Marekani, na hasa Trump, imuunge mkono kwa namna fulani."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadhi ya wataalamu wameibua uwezekano kwamba Netanyahu anaweza kurejesha hali ya dharura ya kitaifa katika ushindani wa kisiasa kwa kuongeza mvutano katika upande mmoja. Hali hiyo inaweza kubadili mwelekeo wa kampeni na kuielekeza kwenye namna ya kusimamia vita, huku ikilazimisha upinzani kutumia muda kueleza msimamo wake kuhusu operesheni hiyo. Hata hivyo, uhalali wa shambulio jipya pia unategemea tathmini ya tishio lililobaki kutoka Iran.
Erwin van Veen, mkurugenzi wa mpango wa Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Clingendael ya Uholanzi, anaeleza:
"Kwa maoni yangu, mbali na Hezbollah nchini Lebanon na muundo wa kijeshi ambao Iran ilikuwa ikiunda kusini-mashariki mwa Syria, hakukuwa na wasiwasi mwingine halali wa kiusalama kwa Israel. Vitisho hivyo sasa vimepungua kwa kiasi kikubwa; hatahivyo, mashambulizi yoyote ya ziada dhidi ya Iran kabla ya Oktoba 27 yanaweza kuathiriwa, kwa kiasi fulani, na hesabu za uchaguzi."
Hata hivyo, kwa mujibu wa Netanyahu, lengo la kukabiliana na Iran linakwenda zaidi ya kudhoofisha uwezo wake wa kijeshi hadi kuipindua serikali. Ikiwa lengo hilo litakubaliwa, hata kudhoofisha nguvu za kijeshi za Tehran kunaweza kutoonekana kuwa kumaliza mzozo, kwa mtazamo wa watoa maamuzi wa Israel.
Uchambuzi wa Kituo cha Begin-Sadat cha Mafunzo ya Kimkakati unatathmini mafanikio ya vita dhidi ya Iran kwa kuangalia kiwango ambacho uwezo wa nchi hiyo wa kujenga upya nguvu zake za kijeshi umeathiriwa. Kwa mtazamo huo, kuendelea kuwepo kwa utawala wa Iran hakumaanishi kwamba operesheni hiyo haikufanikiwa. Uchambuzi huo pia unaibua uwezekano wa kuhitajika operesheni ya pili. Kwa mtazamo huu, shinikizo la kijeshi linaloendelea linaweza kuonekana kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu, hata kama linatekelezwa karibu na uchaguzi.
Yagil Levy, profesa wa sosholojia ya kisiasa na sera za umma na mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Mahusiano ya Kiraia na Kijeshi katika Chuo Kikuu Huria cha Israel, aliiambia BBC Persian:
"Tabia ya Netanyahu imejikita katika mtazamo mpana wa kimkakati, ambao vipengele vyake vikuu vinakubalika na siasa za kati za Israel pamoja na jeshi lenyewe. Kwa hiyo, ni vigumu sana kubaini iwapo mtazamo wake kwamba vita na Iran havijaisha na vinapaswa kuendelea unatokana na masuala ya uchaguzi au la, kwa sababu unaendana na misimamo iliyokuwepo muda mrefu kabla ya mazingira ya sasa ya uchaguzi."
Kwa kuwa kuipindua serikali ya Iran sasa kumeibuka kama lengo la vita, kuunga mkono tu kudhoofishwa kwa uwezo wa kijeshi wa Tehran hakutoshi kueleza wazi kile ambacho makamanda wanatarajia kuwa matokeo na mwisho wa operesheni hiyo. Msimamo huo unaweza kuambatana na mashaka kuhusu uwezekano wa kuipindua serikali kupitia vita, tofauti ambayo ni muhimu katika kutathmini kiwango cha uungwaji mkono kwa uamuzi unaoweza kuchukuliwa na Netanyahu.
Dalia Sheindlin, akisisitiza kwamba hana taarifa za moja kwa moja kuhusu misimamo ya sasa ya makamanda wa jeshi na Mossad, anaelekeza kwenye tathmini muhimu zilizofanywa baada ya vita na kusema:
"Tunachosikia sasa ni kwamba maafisa wengi wa sasa au wa zamani wa kijeshi, wanapoitazama nyuma, wanaamini kwamba mpango wa kuanzisha vita kwa lengo la kuipindua serikali ya Iran, au wazo kwamba vita vingewasaidia Wairani kuipindua serikali, au kwamba mwanasiasa wa vibaraka angeweza kuwekwa madarakani nchini Iran, lilikuwa wazo baya sana."

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Je, Trump ataongeza mvutano?
Wakati Washington ikiendelea kuishinikiza Tehran kukubali matakwa yake, kuihusisha Israel kama mshirika kunaweza kuwa moja ya chaguo. Hata hivyo, kuongezeka kwa vita kunaweza kutatiza hesabu za Trump kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani wa Novemba 3, ambao utafanyika wiki moja baada ya uchaguzi wa Israel.
Van Veen, akizungumzia kushindwa kwa Marekani kupata ushindi katika mzozo huo, anasema:
"Kwa kuwa Marekani bado inaonekana kutokuwa tayari kulipa gharama ya kuanzisha vita hivi vibaya na wakati huo huo haiwezi kushinda, mtu angeweza kutarajia kwamba ingekaribisha msaada. Lakini msaada huo haujaonekana wazi hadi sasa, jambo linalonifanya kudhani kuwa Israel ina sababu zake yenyewe."
Hii inajiri wakati vyombo vya habari viliporipoti kwamba mkutano ulifanyika nchini Ujerumani ukihusisha makamanda kutoka Marekani, Israel na nchi kadhaa za Kiarabu. CENTCOM ilisema mada ya mkutano huo ilikuwa kuimarisha ushirikiano wa kiusalama, huku ripoti zikieleza kwamba usalama wa Mlango wa Hormuz na kukabiliana na Wahouthi vilijadiliwa katika mkutano huo.
Reuters pia iliripoti Septemba 15 kwamba utawala wa Trump unapanga kuiuzia Israel kifurushi cha silaha chenye thamani ya dola bilioni 2.8, kikiwemo mabomu 40,000 yenye uzito wa takriban pauni 2,000 kila moja. Mpango huo uliripotiwa kwa njia isiyo rasmi kwa kamati husika za Congress na bado ulikuwa katika hatua ya pendekezo.
Ingawa kuchapishwa kwa ripoti hizi hakuthibitishi kwa kujitegemea kwamba kuna mpango huo, kunaongeza uvumi kwamba mpango wa siri wa kuendesha operesheni mpya dhidi ya Iran unaweza kuwa unaendelea kati ya pande hizo mbili.
Dov Waxman, profesa wa sayansi ya siasa na mkuu wa masomo ya Israel katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, anaona uwezekano wa Trump kujiunga na vita kuwa mdogo, kutokana na masuala yake ya uchaguzi. Alisema:
"Sitazamii Netanyahu kuongeza mvutano na Iran kuelekea uchaguzi wa Israel, kwa sababu jambo hilo linaweza kumkera Trump, ambaye anataka kuepuka kuanzisha tena vita na Iran kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani. Kuichokoza Iran pia kunaweza kuwa hatari kwa Netanyahu ikiwa kutasababisha Iran kuishambulia Israel."
Uzoefu wa awali wa migogoro kati ya Iran, Israel na Marekani umeonyesha kwamba shambulio linaweza kusababisha mzozo mkubwa zaidi unaohusisha maeneo mengi ya Mashariki ya Kati. Mwitikio wa Iran na uwezekano wa mashambulizi kuenea katika nchi nyingine za eneo hilo unaweza kusababisha gharama ambazo hazikukadiriwa ipasavyo kabla ya operesheni kuanza.
Kwa hiyo, kuongeza shinikizo la kijeshi si lazima kuboreshe nafasi ya Marekani katika mazungumzo. Wakati huo huo, wachambuzi wengi wanaamini uwezekano wa Israel kuishambulia Iran bila ushiriki wa Marekani bado ni mdogo.
Jonathan Reinhold, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Bar-Ilan nchini Israel na mtafiti wa mahusiano ya Marekani na Israel, aliiambia BBC Persian:
"Ni vigumu kwangu kufikiria hatua kubwa bila ushiriki wa Marekani. Kinadharia, Israel inaweza kuishambulia Iran bila Marekani, lakini ili hatua hiyo ichukuliwe, kungehitajika uchokozi mkubwa sana kutoka Iran."
Hata katika hali hiyo, haoni kuwa ni jambo la uhakika kwamba Trump angeunga mkono kushambuliwa kwa sekta muhimu za uchumi wa Iran, ikiwemo sekta ya mafuta.
Uchaguzi wa Marekani unapokaribia, uwezekano wa kuvurugika zaidi kwa usambazaji wa nishati pia unaweza kuathiri tathmini ya Washington kuhusu gharama za operesheni hiyo, hasa ikiwa mwitikio wa Tehran utalenga usafirishaji wa mafuta au meli katika eneo hilo na mzigo wa kiuchumi wa vita ukahamishiwa kwa wapiga kura wa Marekani.
Akizungumzia gharama hizo, Sheindlin anasema:
"Trump amejaribu mara nyingi kupata ushindi wa mwisho wa Marekani na kumaliza kabisa vita, lakini hajafanikiwa. Hajafanikiwa kuboresha nafasi ya Marekani katika mazungumzo ili kufikia makubaliano kuhusu suala la nyuklia. Vita hivi vinamgharimu sana, na sidhani kama anataka kuanzisha tena vita kamili kabla ya uchaguzi wa Marekani, kwa sababu vita dhidi ya Iran vimekuwa visivyopendwa sana nchini Marekani."

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Vita vinaathirije wapiga kura?
Katika kutathmini faida za uchaguzi zinazoweza kutokana na operesheni hiyo, mwitikio wa wapiga kura ambao wanaweza kukubaliana na serikali kuhusu umuhimu wa kukabiliana na Iran lakini bado wakapendelea vyama vingine kuongoza nchi ni muhimu.
Erwin van Veen, akirejea kura za maoni, anasema vita dhidi ya Iran vinaungwa mkono na viongozi wa kisiasa pamoja na umma, lakini anaona uwezekano mkubwa wa mwitikio hasi iwapo kutakuwa na vifo vingi vya raia.
Hata hivyo, ripoti ya Reuters ya Machi ilionyesha kwamba licha ya uungwaji mkono mkubwa kwa vita, nafasi ya Netanyahu katika uchaguzi haikubadilika kwa kiasi kikubwa. Hivyo, kuridhika na operesheni pekee hakumaanishi kwamba wapiga kura wamebadili mtazamo wao kuhusu serikali.
Kwa kuzingatia uzoefu huo, Sheindlin anaona uwezekano wa wapinzani kubadili msimamo wao kuwa mdogo, akisema:
"Vita vya awali viliboresha nafasi yake ya kisiasa kwa kiwango kidogo tu, na athari hiyo haikudumu kwa muda mrefu. Ni vigumu kwangu kufikiria kwamba vita na Iran vitasababisha wengi, au hata baadhi, ya wale wanaounga mkono upinzani sasa kurejea kwa Netanyahu; kwa sababu hawakumrejea baada ya vita vilivyopita."
Katika uchaguzi ambao uundwaji wa serikali unategemea makubaliano ya vyama vingi, kuendelea kwa wapinzani wa Netanyahu kuongoza katika kura za maoni hakuhakikishi kwamba wataweza kukubaliana kuhusu serikali mbadala.
"Idadi kubwa ya watu mara kwa mara inasema itapigia kura vyama ambavyo havimuungi mkono Netanyahu," Scheindlin anasema. "Lakini hilo halimaanishi kwamba wanaweza kushinda uchaguzi ujao, kwa sababu wanapaswa kuunda muungano wa vyama."
Hali hii imefanya maoni ya umma nchini Israel kuwa magumu zaidi. Kwa upande mmoja, huenda bado wanaona Iran kuwa tishio kwa mustakabali wa nchi yao, lakini kwa upande mwingine wameshuhudia kwamba vita viwili vilivyopita havikufanikiwa kuondoa tishio hilo, na huenda hali imekuwa mbaya zaidi.
Sasa kuna mazungumzo machache kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, huku juhudi zote zikielekezwa katika kufungua njia ya maji katika Ghuba ya Uajemi ambayo ilikuwa wazi kabla ya vita vya majira ya baridi mwaka uliopita.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wapinzani na jeshi wataitikiaje?
Sehemu nyingine yenye ushawishi katika mchakato wa kufanya maamuzi na kuendesha operesheni nchini Israel ni mitandao mbalimbali ya kijeshi, kijasusi na kiusalama.
Wakati huo huo, suala la kukabiliana na Iran huenda likawa miongoni mwa masuala machache ambayo hakuna tofauti kubwa kati ya makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Israel, ingawa kunaweza kuwa na mitazamo tofauti kuhusu mbinu za kutekeleza hilo.
Van Veen anaeleza kwamba anaamini wapinzani wa Netanyahu pia wanakubaliana na kanuni ya vita hivyo, ingawa wanatofautiana na waziri mkuu kuhusu namna ya kuendesha vita. Anaongeza kwamba baadhi ya wapinzani wa Netanyahu wanamkosoa kwa kutokwenda mbali vya kutosha dhidi ya Iran.
Reinhold analitazama suala hilo kwa mtazamo tofauti na anaamini kwamba ikiwa Iran itafanya uchokozi na taasisi za ulinzi za Israel zikaunga mkono shambulio dhidi ya Iran, uwezekano mkubwa ni kwamba wapinzani wa Netanyahu watajiunga na hatua hiyo.
Ikiwa baadhi ya vyombo vya usalama havitaona ulazima wa operesheni hiyo, serikali inaweza kukabiliwa na tathmini kutoka ndani ya taasisi hizo hizo zinazopaswa kuitekeleza, katika kueleza sababu za shambulio hilo.
"Ikiwa idadi kubwa ya watu katika taasisi za usalama watafikiri kwamba operesheni hiyo haina uhalali, jambo hilo litajulikana haraka sana, na katika hali hiyo, nadhani kutakuwa na mwitikio mkubwa sana wa umma," Reinhold alisema.
"Lakini hilo lina uwezekano mdogo sana, kwa sababu huenda Netanyahu angeongeza mvutano kwa sababu za kisiasa tu ikiwa tayari kungekuwa na sababu za kutosha za kiusalama za kuchukua hatua hiyo, ili isionekane wazi kuwa ni hatua ya kisiasa."
Wachambuzi wanaamini kwamba ikiwa kutokubaliana kuhusu umuhimu wa operesheni hiyo kutafikia ndani ya jeshi, uwezekano wa kupinga uamuzi wa serikali utaongezeka. Katika hali hiyo, upinzani unaweza kurejea tathmini za kijeshi bila ukosoaji wao kuonekana kama sehemu tu ya ushindani wa uchaguzi.
Akisisitiza kuendelea kwa upinzani kutoka upande wa jeshi, Levy anasema:
"Upinzani huo unaweza kuashiria uwezekano, lakini si uhakika, kwamba masuala ya kijeshi si sababu kuu. Hili huwa wazi zaidi pale ambapo jeshi linasema kuna njia mbadala au kwamba hatua inayopendekezwa ina hatari kubwa na huenda hata ikashindwa."
Levy pia anabainisha kwamba jeshi, kutokana na uwezekano wa kubadilika kwa serikali baada ya uchaguzi, linataka kuwa makini lisije likatuhumiwa kutumikia maslahi ya kisiasa ya Netanyahu. Kwa maana hiyo, mwenendo wa makamanda pia unaweza kuathiriwa na mazingira ya kisiasa kabla ya kura.
Reinhold anaibua uwezekano mwingine kuhusu matumizi ya kisiasa ya mgogoro halisi, akisema:
"Wasiwasi ni kwamba kuna suala halali la kiusalama, kisha anataka kulitumia kuchelewesha uchaguzi. Sidhani kwamba wazo la yeye mwenyewe kuunda hali kama hiyo linaaminika."
Uwezekano huo, bila shaka, haumaanishi kwamba Waziri Mkuu ana mamlaka ya kuahirisha uchaguzi kwa uamuzi wake mwenyewe. Kuongeza muda wa Bunge zaidi ya muda uliowekwa kisheria kunahitaji kuwepo kwa mazingira maalum na kupitishwa kwa sheria kwa kuungwa mkono na angalau wabunge 80.
Kwa kuzingatia vikwazo vya kuchukua hatua dhidi ya Iran, Waxman anaona uwezekano mkubwa zaidi wa kuongezeka kwa mvutano na Hezbollah na Hamas, huku Scheindlin pia akitaja uwezekano wa kuongezeka kwa mvutano katika Ukingo wa Magharibi na maeneo mengine.
Kwa tathmini yao, jaribio linalowezekana la Netanyahu kubadilisha mazingira ya uchaguzi linaweza kufanyika katika eneo ambalo anategemea kidogo zaidi msaada wa Washington.
Ikiwa Netanyahu anategemea mzozo mpya na Iran kubadilisha mazingira ya uchaguzi, atalazimika kuzingatia athari za mwitikio wa Tehran. Wapiga kura ambao watakuwa wakitathmini rekodi yake ya kiusalama wanaweza tena kutumia wiki zinazoelekea uchaguzi wakiwa wamejificha kutokana na mashambulizi.
Hata hivyo, Netanyahu ameonyesha mara kadhaa, hasa kuhusu Iran, kuwa yuko tayari kufanya maamuzi ambayo wengi hawakuyatarajia, iwe kutoka kwa umma au wachambuzi.















