Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Nilitibiwa saratani kwa miaka 11, kumbe sikuwa nayo'
- Author, David Lumb
- Nafasi, in Coventry
- Author, Vanessa Pearce
- Nafasi, West Midlands
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Becky Jones alikuwa na umri wa miaka 21 tu alipoambiwa kuwa alikuwa na uvimbe wa saratani kwenye ubongo ambao ungekuwa hatari kwa maisha yake, na kwamba alikuwa na miezi michache tu ya kuishi.
Alikuwa amemfahamu hivi karibuni mwenza wake na alikuwa na ndoto ya kufanya kazi katika jeshi la polisi, lakini ghafla mustakabali wake ukawa wa kusikitisha.
Uchunguzi huo, uliofanywa na daktari bingwa mwenye uzoefu wa saratani, ulimpelekea kutumia matibabu ya chemotherapy kwa miaka 11, jambo lililobadilisha maisha yake.
Mara kwa mara alihisi kichefuchefu, hakuweza kushiriki katika hafla za kifamilia, ndoto yake ya kazi ikakatizwa na aliishi katika hali ya hofu na wasiwasi kila mara.
Sasa akiwa na umri wa miaka 34, amegundua hivi karibuni kwamba hakuwahi kuwa na saratani hata kidogo, bali alikuwa na tatizo la kuvimba kwa ubongo ambalo lingeweza kutibiwa kwa dawa za steroid.
Mama huyo wa watoto wawili ni miongoni mwa wagonjwa zaidi ya 40 wanaochukua hatua za kisheria dhidi ya University Hospitals Coventry and Warwickshire (UHCW) NHS Trust, kutokana na matibabu ya saratani yaliyodumu kwa muda mrefu au kutokuwa ya lazima.
"Niliambiwa mara kwa mara kwamba bila chemotherapyningekufa," alisema.
Akiwa mwanamke kijana, Jones anasema Profesa Ian Brown, daktari bingwa katika University Hospital, Coventry, alimwambia kwamba angehitaji kutumia dawa ya chemotherapy iitwayo temozolomide (TMZ) kwa maisha yake yote.
Hii ni licha ya miongozo kupendekeza mizunguko sita ya matibabu kwa kipindi cha miezi sita.
Alipouliza kuhusu vipimo kadhaa vya picha vya ubongo ambavyo havikuonekana kuonyesha dalili za uvimbe, anasema daktari huyo alimwambia kwamba uvimbe huo usingeonekana "kwa macho".
Ilikuwa mwaka 2025 tu, wakati kesi za wagonjwa wa saratani katika hospitali hiyo waliokuwa wamehusishwa na Prof Brown zilipoanza kuchunguzwa, ndipo alipogundua ukweli.
"Sikuwahi kuwa na uvimbe wa ubongo. Niligunduliwa kimakosa na nimepitia matibabu haya yote kwa sehemu kubwa ya maisha yangu ya utu uzima, bila sababu yoyote," alisema.
"Kwa kweli, ameharibu maisha yangu," aliongeza.
Wagonjwa wengine wengi waliowahi kutibiwa na Prof Brown wameiambia BBC kwamba walipewa TMZ kwa miaka kadhaa, hali iliyowasababishia matatizo mbalimbali makubwa ya kiafya.
Mgonjwa mmoja alisema anaamini dawa hiyo ilimfanya ashindwe kupata watoto, huku mwingine akipatwa na saratani ya damu baada ya kutumia mizunguko 100 ya matibabu ambayo haikuwa ya lazima.
Matokeo ya awali ya uchunguzi uliofanywa na Royal College of Physicians (RCP) yalibaini kuwa wagonjwa katika hospitali hiyo walipewa dawa hiyo kwa muda mrefu, huku kukiwa na "ushahidi mdogo sana au kutokuwepo kabisa kwa ushahidi wa manufaa yake".
Uchunguzi huo ulibaini kuwa mapungufu ya wafanyakazi katika hospitali hiyo yalifikia kiwango cha "kuisaliti imani ya wagonjwa", na pia ulihoji kwa nini timu za madaktari wa dawa za saratani hazikupinga wagonjwa kutumia chemotherapy ya kumeza kwa mfululizo kwa miaka 10 hadi 15.
UHCW ilisema haitatoa maoni kuhusu kesi binafsi, lakini ikasema hatua zimechukuliwa ili kuhakikisha kuna "usimamizi madhubuti zaidi wa uagizaji na matumizi ya TMZ".
Mwaka 2012, maisha ya Jones yalikuwa ndiyo yanaanza. Alikuwa akifanya kazi kama mwendeshaji wa kamera za CCTV katika uwanja wa Coventry City.
Huko alikutana na mwenza wake Pete, ambaye alikuwa akifanya kazi ya ulinzi, lakini muda mfupi baadaye alianza kupata maumivu makali ya kichwa na kutafuta matibabu.
Alifanyiwa uchunguzi wa kuchukua sampuli ya tishu za ubongo, uliofanywa na daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo kutoka sekta binafsi.
Lakini Fiona Tinsley, mshirika katika kampuni ya sheria ya Brabners, alisema Prof Brown aligundua kuwa alikuwa na glioblastoma ya daraja la nne, aina mojawapo ya saratani hatari zaidi ya ubongo, kabla ya majibu ya vipimo hivyo kurejea.
BBC imejaribu mara kadhaa kuwasiliana na Profesa huyo aliyestaafu.
Jones alielezea miaka yake ya kutumia dawa za chemotherapy kuwa "ya kutisha".
"Nilikuwa na kichefuchefu kila mara, maumivu ya tumbo, vidonda mdomoni, uchovu wa kila siku; ilikuwa hali mbaya sana," alisema.
Dawa hiyo iliathiri kila sehemu ya maisha yake, huku hofu ya kupata maambukizi ikimfanya aepuke hafla za kijamii na mikusanyiko ya kifamilia.
Leseni yake ya kuendesha gari pia ilichukuliwa mwanzoni, na baadaye ikawekewa vikwazo.
"Kabla ya matibabu nilikuwa nikifanya mazoezi kwenye gym kila mara, nilikuwa nikikimbia, na mimi na Pete tulikuwa tukienda kula pamoja mara kwa mara, jambo ambalo baadaye sikuweza tena kufanya," alieleza.
Wenzi hao pia waliambiwa kwamba hangeweza kupata ujauzito.
"Baadaye nilipata watoto wawili, jambo ambalo aliniambia wote walikuwa watoto waliokuja kimiujiza," alisema.
Matibabu yake yaliendelea kwa zaidi ya muongo mmoja, hadi ghafla mwaka 2024 alipokea simu kutoka kwa daktari aliyemwambia kwamba chemotherapy yake itasitishwa.
"Hakuwa na sababu yoyote ya kueleza kwa nini. Aliniambia Ian Brown amestaafu - hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kusikia kuhusu hilo," alisema Jones.
Aliambiwa kwamba maswali yake yote yangejibiwa na daktari wake mpya wa saratani, lakini hakutajwa jina la daktari huyo.
"Sikujua nifanye nini, niende wapi wala nizungumze na nani kwa sababu sikupewa msaada wowote na hospitali wakati huo," alisema.
Mwezi Mei 2025, baada ya madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na wataalamu wa radiolojia kufanya uchambuzi huru kwa niaba ya mawakili wake, aliambiwa kwamba hakuwahi kuwa na saratani ya ubongo.
Kwa kweli, alikuwa akisumbuliwa na hali iitwayo tumefactive demyelination - kuvimba kwa ubongo ambako kwa kawaida hutibiwa na madaktari bingwa wa mfumo wa fahamu kwa kumpa mgonjwa dawa kali za steroid.
Jones alipokea taarifa hizo kupitia mazungumzo ya video akiwa na mawakili wake na wataalamu hao.
"Tulipogundua ukweli, kulikuwa na machozi machoni mwa kila mtu," alisema Tinsley, anayewawakilisha baadhi ya wagonjwa hao.
Uchunguzi wa RCP, ambao haukumtaja Profesa Ian Brown kwa jina bali ulimrejelea kama "Daktari Y", ulibaini kuwa kati ya kesi 20 zilizochunguzwa, 15 zilikuwa "zisizoridhisha kwa ujumla".
Daktari huyo bingwa hakushiriki katika uchunguzi huo.
Timu ya uchunguzi ilibaini kuwa kulikuwa na "ushahidi mdogo sana" unaoonyesha uelewa na uwekaji wa kumbukumbu kuhusu hatari za kutumia dawa hiyo.
Matokeo ya awali yalisema kulikuwa na "udadisi mdogo wa kitabibu" katika baadhi ya kesi, pamoja na ukosefu wa ushirikiano na wataalamu wengine katika timu za matibabu, hali iliyoruhusu makosa ya utambuzi kuendelea.
Jones alielezea matokeo hayo kuwa "ya kutisha".
"Sio tu kuhusu alichofanya, bali pia ni kuhusu jinsi walivyomruhusu kufanya hivyo peke yake kwa muda mrefu," aliongeza.
"Ni kana kwamba alikuwa akiendesha mambo yake mwenyewe na hakukuwa na mtu wa kumfuatilia."
Uchunguzi zaidi
Msemaji wa UHCW alisema wagonjwa wote walioathirika wamefanyiwa uchunguzi na madaktari bingwa, na "mipango mwafaka ya matibabu imewekwa".
"Pia tunafanya uchunguzi huru kuhusu mifumo yetu ya kuripoti na kuibua wasiwasi, unaoongozwa na mtu huru, ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata msaada kamili na wanajiamini katika kutoa taarifa kuhusu wasiwasi wowote.
"Trust itapitia kwa kina ripoti kamili ya RCP itakapochapishwa na itachukua hatua zaidi zinazofaa kulingana na matokeo yake.
"Tunataka kuuhakikishia umma wetu kwamba usalama wa wagonjwa, uzoefu wao na ustawi wao vinaendelea kuwa vipaumbele vyetu," iliongeza trust hiyo.