Uhandisi mgumu unaotumika kutengeneza vioo vya ndege

    • Author, Chris Baraniuk
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Janga la viwandani lilikuwa likiendelea kusini mwa Los Angeles, California.

Mwishoni mwa mwezi Mei, tanki la kuhifadhia kemikali lililokuwa na zaidi ya lita 26,000 za kemikali yenye sumu lilianza kupata joto kwa kasi.

Tanki hilo lilikuwa mali ya GKN Aerospace, kampuni inayosambaza vipuri kwa sekta ya anga, ikiwemo vioo vya ndege.

Joto ndani ya tanki hilo la chuma lilipokuwa likiongezeka, wafanyakazi waligundua kuwa walikuwa wanakabiliwa na tatizo kubwa.

Tanki hilo lilikuwa katika hatari ya kulipuka, jambo ambalo lingeweza kusababisha methyl methacrylate (MMA), kemikali inayoweza kuwasha ngozi na mapafu na inayotumika katika utengenezaji wa plastiki, kusambaa katika maeneo ya makazi yaliyo karibu.

Zaidi ya wakazi 50,000 wa Garden Grove walihamishwa, huku wazima moto wakianza kulimwagia maji tanki hilo ili kulipoza.

Wakati mmoja, tanki hilo "lilivimba", kwa mujibu wa mkuu wa kikosi cha zimamoto eneo hilo.

Kwa bahati nzuri, mlipuko haukutokea.

Miezi kadhaa baadaye, mwezi Agosti, GKN na mamlaka za eneo hilo zilitangaza mpango wa dola milioni 100 wa kuwafidia wakazi waliohamishwa wakati wa tukio hilo.

Hata hivyo, tukio hilo lilivuruga uzalishaji wa vioo vya ndege katika kiwanda hicho, na uzalishaji bado haujarejea kikamilifu.

Athari kwa sekta

Tukio hilo limezua wasiwasi katika sekta ya utengenezaji wa ndege, kwa sababu GKN ni miongoni mwa kampuni chache duniani zinazotengeneza vioo vya ndege — bidhaa zinazohitaji uhandisi wa hali ya juu na ambazo ni muhimu kwa usalama wa ndege.

Uzalishaji katika kiwanda cha GKN kilichopo Garden Grove kwa sasa uko katika kiwango cha takriban asilimia 50 ya uwezo wake wa kawaida, kwa mujibu wa taarifa za kampuni yake mama ya Uingereza, Melrose Industries.

Lengo ni kurejesha uzalishaji kikamilifu kufikia Septemba 28.

GKN ilikataa kufanya mahojiano na BBC.

"Wao ni miongoni mwa wasambazaji wachache sana wa vioo muhimu," anasema Marisa García, mchambuzi wa sekta ya anga.

"Moja ya udhaifu wa mnyororo wa usambazaji wa sekta ya anga ni kwamba kuna kampuni chache sana zilizoidhinishwa kufanya kazi fulani, na tatizo linapotokea, mfumo mzima unaweza kuyumba."

Boeing imeiambia BBC kwamba "inachukua hatua kupunguza athari zozote zinazoweza kujitokeza", na imeeleza uhaba huo wa uzalishaji kuwa hali inayoathiri "sekta nzima."

"Tunamuunga mkono msambazaji wetu," msemaji wa kampuni hiyo aliongeza.

Msemaji wa Airbus alisema:

"Tunafuatilia kwa karibu hali hiyo na tunaona maendeleo mazuri kuelekea kurejea katika hali ya kawaida."

Haya yanatokea wakati ambapo mashirika ya ndege "hayawezi kupata ndege mpya kwa kasi inayohitajika," anasema Mike Stengel wa kampuni ya ushauri ya AeroDynamic Advisory.

"Wanalazimika kutumia ndege zao kwa muda mrefu zaidi."

Ingawa kuna kampuni chache tu zinazotengeneza vioo vya ndege, ni vigumu kwa washindani wapya kuingia katika soko hilo kutokana na kanuni kali zinazosimamia sekta hiyo, kwa mujibu wa Stengel.

"Kubadilisha wasambazaji kunaweza kuchukua muda."

Mtaalamu huyo anasema hali hii inalazimisha kuwepo kwa "uwiano wa maslahi" kati ya watengenezaji wa ndege na kampuni wanazozitegemea kwa ajili ya usambazaji wa vipuri mbalimbali.

Vioo vinazidi kuwa vikubwa

Ili kufahamu zaidi kinachohusika katika utengenezaji wa kioo cha ndege, nilizungumza na Jean-Eric Vermont, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Ufaransa ya Saint-Gobain Aerospace.

"Tunajikita zaidi katika ndege za abiria, ndege za safari za kikanda na helikopta," anasema.

Hata hivyo, Vermont alikataa kufichua sehemu ya soko ambayo kampuni yake inamiliki katika biashara ya vioo vya ndege, ambavyo katika sekta hiyo hujulikana kama transparencies.

Vioo vya mviringo vilivyo kwenye sehemu ya abiria, pembeni mwa viti, kwa kawaida hutengenezwa kwa vifaa vya plastiki, anaeleza Vermont.

"Huanzia kwenye karatasi ya akriliki," anasema. "Kisha hukatwa kulingana na ukubwa unaohitajika ili kupata umbo lake."

Msemaji wa Saint-Gobain alithibitishia BBC kwamba kampuni hiyo haihifadhi wala kuchakata MMA kama GKN, bali hununua karatasi za MMA iliyokwishaunganishwa kikemikali, au akriliki.

Kwa mujibu wa Vermont, watengenezaji wa ndege wanaagiza vioo vikubwa zaidi vya abiria ili kuwapa wasafiri mwonekano mpana zaidi wa nje.

Ingawa hili ni jambo linaloweza kuvutia abiria, vipimo zaidi vinahitajika ili kuhakikisha kuwa vioo vikubwa vina nguvu sawa na vile vidogo.

Saint-Gobain hujaribu vioo vyake kwa kuvipa shinikizo mara nyingi zaidi ya lile ambalo kwa kawaida ndege hukabili inapokuwa ikiruka katika mwinuko mkubwa.

Vioo hivyo vya abiria, vinavyotengenezwa kwa akriliki, kwa kawaida huwa na tabaka mbili za nyenzo hiyo.

Saint-Gobain pia hufanya vipimo kuhakikisha kuwa kioo kitaendelea kustahimili shinikizo hata ikiwa moja ya tabaka hizo itaharibika.

Vioo tofauti kwenye chumba cha marubani

Kwa mujibu wa Vermont, vioo vya chumba cha marubani "ni tofauti kabisa."

Kwa kawaida hutengenezwa kwa kioo ambacho huimarishwa kikemikali kwa kuongezwa potasiamu.

Mchakato huo unahusisha kubadilisha ioni ndogo za sodiamu na ioni kubwa zaidi za potasiamu. Hii husaidia kukamilisha muundo wa molekuli za kioo.

Mchakato huo hukifanya kioo kujibana wakati kinapopoa katika hatua ya utengenezaji, na hivyo kuunda muundo wenye nguvu na mshikamano mkubwa zaidi.

Baadhi ya ndege za kisasa zaidi hutumia vioo vya chumba cha marubani vilivyopinda ili kuboresha aerodynamics, hali inayosaidia kupunguza matumizi ya mafuta.

Hata hivyo, kutengeneza vioo vilivyopinda ni changamoto, kwa sababu hata upotoshaji au kasoro ndogo kabisa inaweza kuonekana wazi kwa rubani.

Udhibiti mkali wa ubora hutumika kuhakikisha kuwa hakuna kasoro kama hizo katika bidhaa ya mwisho.

Kwa mujibu wa Vermont, vioo vyote vya ndege lazima viwe na uwezo wa kustahimili kugongwa na vitu, lakini vioo vya chumba cha marubani vilivyo mbele ya ndege viko katika hatari kubwa zaidi ya kugongwa na ndege au ndege wa porini. "Tatizo si kasi ya ndege huyo, bali ni kasi ya ndege," anasema.

Saint-Gobain hutumia uigaji wa kihisabati na "vipimo halisi vinavyowakilisha mgongano na ndege mkubwa" ili kujaribu uwezo wa vioo vyake kustahimili tishio hilo.

"Kwa kawaida, ukikumbwa na dhoruba ya mvua ya mawe au ukigonga ndege mkubwa vya kutosha, kioo cha nje kitapasuka," anasema Vermont.

"Kioo cha chumba cha marubani kimeundwa kukabiliana na hilo."

Hivi karibuni, ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka London kwenda Londonderry ilikumbwa na tatizo la kupasuka kwa kioo cha chumba cha marubani.

Ingawa hali hiyo ilisababisha kutangazwa kwa dharura wakati ndege ikiwa angani, ndege hiyo ilifanikiwa kutua salama.

"Matukio kama hayo yanaweza kutokea," anasema Vermont, ingawa anaongeza kuwa vioo vya Saint-Gobain havijahusishwa na matukio yoyote ya hivi karibuni.

"Ni wazi kwamba hii ni sehemu inayokutana na mazingira mawili tofauti kabisa," anasema Stengel.

"Ndiyo maana bidhaa hizi zinahitaji uhandisi wa hali ya juu zaidi."