Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, UN yasema kuna ushahidi Marekani ilifanya uhalifu wa kivita katika mashambulizi dhidi ya Iran

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuna sababu za msingi za kuamini kuwa Marekani ilifanya uhalifu wa kivita katika mashambulizi mawili nchini Iran yaliyosababisha vifo vya raia wasiopungua 177.

Muhtasari

  • Tetesi: Arsenal inamtaka kinda wa Bournemouth Eli Junior Kroupi
  • Polisi wa Nigeria wanachunguza vifo vya watu 37 waliokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za uchimbaji haramu wa madini
  • Axios: Trump kufanya uamuzi mkubwa wa kuingia vitani na Iran
  • Mshauri wa Mojtaba: Mlango-bahari wa Hormuz hautafunguliwa hadi Trump atakapoondolewa madarakani
  • UN yasema kuna ushahidi kuwa Marekani ilifanya uhalifu wa kivita katika mashambulizi dhidi ya Iran

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. Tetesi: Arsenal inamtaka kinda wa Bournemouth Eli Junior Kroupi

    Arsenal ina nia kubwa ya kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth na timu ya taifa ya Ufaransa ya vijana chini ya umri wa miaka 21, Eli Junior Kroupi (20), lakini klabu hiyo ya Bournemouth (inayofahamika kama 'Cherries') inatarajia ada kubwa. (Football London)

    Real Madrid inafikiria uwezekano wa kumsajili beki wa England mwenye umri wa miaka 24 wa Everton, Jarrad Branthwaite, ambaye pia anafuatiliwa na klabu kadhaa za Ligi Kuu ya England. (Goal)

    Chelsea ina nia ya kuchunguza dili la pauni milioni 69 kwa ajili ya winga wa Uhispania na Athletic Bilbao, Nico Williams (24). (Fichajes – In Spanish)

    Arsenal haina mpango wowote wa kumuuza kiungo wa Uhispania mwenye umri wa miaka 27, Martin Zubimendi, mwezi Januari. (Football Insider)

    Real Madrid na Barcelona zimefanya uchunguzi mpya kuhusu kinda wa Marekani Cavan Sullivan (16), ambaye anatarajiwa kujiunga na Manchester City akitokea Philadelphia Union atakapofikisha umri wa miaka 18. (Teamtalk)

    Liverpool italazimika kulipa ada kamili ya kuvunja mkataba ya pauni milioni 130 ili kumsajili mchezaji wa Brazil mwenye umri wa miaka 20, Rayan, kutoka Bournemouth, licha ya uhusiano wa meneja Andoni Iraola na kiungo huyo tangu alipokuwa kocha wa Bournemouth. (ESPN Brazil via Caught Offside)

    Kiungo wa Atletico Madrid na Argentina, Julian Alvarez (26) - ambaye anawaniwa na klabu kama Arsenal na Barcelona - anafikiria kuachana na wakala wake wa muda mrefu kufuatia kipindi cha majira ya joto kilichojaa tetesi za uhamisho. (Mundo Deportivo)

    Everton ina uwezekano mdogo wa kumfuatilia mshambuliaji wa Tottenham na Brazil, Richarlison, licha ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 kuhusishwa na uwezekano wa kurejea Everton wakati wa majira ya joto. (Football Insider)

  2. Polisi wa Nigeria wanachunguza vifo vya watu 37 waliokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za uchimbaji haramu wa madini

    Watu thelathini na saba walioshutumiwa kwa uchimbaji madini haramu kaskazini-magharibi mwa Nigeria wamefariki wakiwa kizuizini, maafisa wa eneo hilo wanasema.

    Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu vifo hivyo, ambavyo Kikosi cha Usalama na Ulinzi wa Raia cha Nigeria (NSCDC) kililaumu mlipuko wa ugonjwa.

    Hata hivyo, ripoti ya kijasusi iliyoshirikiwa na shirika la habari la AFP ilionyesha kuwa kundi hilo lilifariki kutokana na msongamano na uingizaji hewa hafifu ndani ya kituo cha kizuizi katika jimbo la Niger la Nigeria.

    Gavana wa jimbo hilo Mohammed Umaru Bago aliviita vifo hivyo "vya kusikitisha" wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi.

    Kamanda wa NSCDC amekamatwa kufuatia vifo hivyo, Bago pia alisema.

    Alitangaza siku tatu za maombolezo na kuahirisha kuanza kwa kampeni za uchaguzi zilizopangwa kufanyika Januari.

    Maafisa walikuwa wamelikamata kundi hilo la vijana siku ya Jumanne kwa tuhuma za uchimbaji madini haramu karibu na Borgu, katika jimbo lenye utajiri wa madini la Niger. Eneo hilo linajulikana kwa uchimbaji mdogo wa dhahabu.

    Siku mbili baadaye, watu thelathini na saba waliokamatwa kama sehemu ya operesheni inayoshukiwa kuwa haramu walipatikana wamekufa ndani ya kituo cha kizuizi kinachoendeshwa na NSCDC.

  3. Axios: Trump kufanya uamuzi mkubwa wa kuingia vitani na Iran

    Jarida la Axios limemnukuu mwandishi wake, Barack Ravid, akisema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump anasema yuko karibu kufanya uamuzi mzito kuhusu kuanzisha upya mashambulizi makubwa dhidi ya Iran.

    Kulingana na Axios, Donald Trump alisema katika mazungumzo ya simu na Bw. Ravid: "Nina uamuzi mkubwa mbele yangu. Je, nichukue hatua na kuwaangamiza [serikali ya Iran] au la? Ni uamuzi mkubwa. Chaguzi zote zipo mezani."

    Kauli hizi zinakuja wakati Rais wa Marekani akitarajiwa kukutana na viongozi wa Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Bahrain, Kuwait, na Oman siku ya Jumanne, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa jijini New York; mkutano unaotarajiwa kujikita katika mustakabali wa mzozo na Iran.

    Bw. Trump anasema ana mpango wa kutumia mkutano huo kutathmini misimamo ya mataifa ya Ghuba kabla ya kuamua hatua zake zinazofuata.

    Alimwambia Barak Ravid: "Nataka kujua hali yao (nchi za Ghuba) ikoje. Siku zote tumekuwa tukiwaunga mkono na kuwalinda."

    Wakati huo huo, ripoti zinaonyesha kuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, ameviagiza vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati kujiandaa kikamilifu kwa uwezekano wa kurejea kwenye mapigano makali kabla ya mwisho wa mwaka.

    Alipoulizwa ikiwa ana mpango wa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, jijini New York wiki ijayo, Bw. Trump alisema: "Huenda."

  4. Mshauri wa Mojtaba: Mlango-bahari wa Hormuz hautafunguliwa hadi Trump atakapoondolewa madarakani

    Mohammad Baqer Zolghadr, mshauri wa kisiasa wa Mojtaba Khamenei, kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu, amesema kuwa nchi yake haina nia ya kufungua Mlango-bahari wa Hormuz mradi tu Donald Trump aendelee kuwa madarakani.

    Katika taarifa iliyochapishwa na mashirika ya habari nchini Iran siku ya Alhamisi, Bw. Zolqadr alisema: "Taifa hili limeazimia kuvunja pembe ya adui mchokozi na kuvunja migongo ya wenye kiburi."

    Aliendelea kusema kuwa Mlango-bahari wa Hormuz hautafunguliwa hadi pale Donald Trump na Benjamin Netanyahu watakapong'olewa kutoka "kiti cha madaraka," na kwamba hii ni "hatua ya kwanza ya kulipiza kisasi kwa taifa la Iran."

    Sambamba na kauli nyingi na wakati mwingine zinazokinzana za Donald Trump kuhusu vita au mazungumzo na Iran, kuna mgawanyiko mkubwa wa maoni ndani ya nchi hiyo kuhusu iwapo waendelee na makabiliano ya kijeshi au wafanye mazungumzo na Marekani.

    Wakati kundi la maafisa wa ngazi ya juu wa kisiasa nchini humo, kama vile Massoud Pezhikian na Mohammad Bagher Qalibaf, likitaka Marekani irejee kwenye masharti ya Mkataba wa Maelewano wa Islamabad na kuliona hilo kama sharti la kusitisha vita, watu wenye msimamo mkali akiwemo makamanda wa Walinzi wa Mapinduzi wanazungumzia kuendeleza vita na kuuweka Mlango-bahari wa Hormuz ukiwa umefungwa kama suluhisho madhubuti zaidi la kukabiliana na Marekani na Israel.

    Wakati huo huo, kupanda kwa kasi kwa mfumuko wa bei, vikwazo vya kiuchumi, na kuzingirwa kwa bandari za kusini mwa Iran kwa njia ya maji kumeifanya hali ya maisha ya kila siku kwa raia wa nchi hiyo kuwa ngumu zaidi, huku kushuka kwa thamani ya sarafu ya Rial dhidi ya sarafu za kimataifa kukiongeza shinikizo zaidi kwenye hali ya maisha ya kila siku.

  5. UN yasema kuna ushahidi kuwa Marekani ilifanya uhalifu wa kivita katika mashambulizi dhidi ya Iran

    Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuna sababu nzuri za kuamini kwamba Marekani ilitenda uhalifu wa kivita katika mashambulizi mawili nchini Iran yaliyoua raia wasiopungua 177.

    Ripoti mpya ya Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli kuhusu Iran ilisema mashambulizi ya kombora ya Februari kwenye shule ya msingi huko Minab na uwanja wa michezo huko Lamerd yalikuwa mashambulizi yasiyo ya kuchagua na kusababisha vifo vya raia na uharibifu wa miundombinu ya raia.

    Hapo awali Marekani ilikanusha kushambulia Lamerd na kusema ilikuwa ikichunguza kilichotokea Minab. Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema Marekani haikutoa uaminifu kwa matokeo katika ripoti hiyo.

    Wataalamu hao pia waligundua kuwa mamlaka ya Iran ilifanya uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa msako dhidi ya maandamano makubwa ya kupinga serikali mwezi Januari.

    Walisema mauaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama yalitokea kwa "kiwango cha kushangaza na kisicho cha kawaida" katika majimbo yote 31.

    Iran pia haijatoa maoni kuhusu matokeo hayo, lakini hapo awali imekataa madai ya ukiukwaji wa kimfumo wa haki za binadamu.

  6. Natumahi hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja