Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi uamuzi wa Dangote wa kuuza mafuta kwa kutumia dola utakavyokuathiri
Uamuzi wa kampuni ya mafuta ya tajiri Aliko Dangote kuanza kuuza mafuta kwa dola za Marekani badala ya naira ya Nigeria umezua mjadala mkubwa miongoni mwa Wanigeria na wanauchumi, hasa kuhusu athari zake kwa wananchi wa kawaida.
Kampuni hiyo imesema mabadiliko hayo yamesababishwa na mahitaji ya kibiashara na hali ya soko la ubadilishanaji wa fedha za kigeni.
Hata hivyo, hatua hiyo imeibua maswali kuhusu jinsi itakavyoathiri bei ya mafuta, thamani ya naira, na uwezo wa wananchi wa kawaida kumudu gharama za maisha, hasa wakati ambapo wengi tayari wanakabiliwa na kupanda kwa gharama ya maisha.
Baadhi ya watu wanaamini kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia sekta ya mafuta kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, wengine wana hofu kwamba kuuza mafuta kwa dola kunaweza kuongeza ugumu wa maisha unaowakabili Wanigeria.
Kwa nini Dangote amechukua hatua hii, na ina athari gani kwa wananchi wa Nigeria?
Mchumi na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Philomath, Profesa Ahmad Adamu, alijibu maswali ya BBC kuhusu mabadiliko haya na athari zinazoweza kujitokeza kwa uchumi wa taifa la Nigeria na mataifa mengine yanayotegemea mafuta kutoka nchi hiyo.
Nini kimesababisha mabadiliko haya?
Profesa Ahmad Adamu, anasema kuwa hali hii imetokana na kupungua kwa uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi, jambo ambalo limekifanya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote kuwa na nafasi kubwa zaidi katika uzalishaji wa mafuta nchini Nigeria.
"Wakati vita vya Iran vilipoanza, uagizaji wa mafuta wa Nigeria ulipungua kwa kiwango kikubwa, na kiwanda cha Dangote kilikuwa kikizalisha takriban asilimia 80 ya mafuta yanayotumiwa nchini Nigeria."
Kulingana na Adamu, mabadiliko hayo yamesababisha kampuni hiyo kupata kiasi kikubwa zaidi cha fedha ya naira kutoka kwenye soko la ndani, huku kikiwa kinahitaji dola za Marekani kwa ajili ya kutekeleza baadhi ya shughuli zake muhimu.
"Kwa sasa anapokea naira nyingi zaidi kuliko alivyokuwa akipokea awali. Kwa hiyo ana naira nyingi zaidi, lakini anahitaji dola zaidi kwa sababu kuna aina fulani za mafuta ghafi zinazonunuliwa kwa dola," anaelezea Ahmad Adamu.
Mtaalamu huyo aliongeza kuwa hata ndani ya Nigeria kuna baadhi ya miamala ambayo haiwezi kuepuka matumizi ya dola, hasa katika ununuzi wa aina fulani za mafuta ghafi na bidhaa nyingine zinazohitajika katika mchakato wa kusafisha mafuta.
"Kuna sehemu za mafuta ghafi ambazo lazima zinunuliwe kwa dola, kwa sababu hata mamlaka ya nishati ya Nigeria yenyewe haitataka kulaumiwa kwa kutokuwa na dola za kutosha,"
Utegemezi mkubwa wa kiwanda cha Dangote katika uzalishaji wa mafuta nchini Nigeria umeifanya kampuni yake ya kusafisha mafuta kutafuta njia mbadala za kupata dola ili kukidhi baadhi ya mahitaji yake muhimu ya kibiashara.
Athari za mabadiliko haya kwa Wanigeria
Mtaalamu huyo anaelezea kuwa athari za mabadiliko haya yanaweza kuongeza shinikizo zaidi kwa uchumi wa Nigeria, kwa kuwa mahitaji makubwa ya dola ni mojawapo ya changamoto kuu zinazoikabili nchi hiyo.
Kulingana na Adamu, kila mara thamani ya dola inapopanda dhidi ya naira, hali ya kiuchumi ya wananchi wa kawada huwa ngumu zaidi kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa na kupungua kwa uwezo wao wa kununua.
"Tatizo kubwa la uchumi wa Nigeria ni dola. Kila wakati dola inapopanda thamani, uchumi wa Nigeria huathirika, na hudhoofika zaidi, na Wanigeria huwa maskini zaidi kutokana na mfumuko wa bei," anaelezea.
Profesa huyo anasema kuwa iwapo itafikia hatua ambapo ununuzi na uuzaji wote wa mafuta utategemea dola, hali hiyo itaongeza mahitaji ya fedha za kigeni katika soko la Nigeria, jambo ambalo linaweza kuendelea kudhoofisha sarafu ya naira.
"Ikiwa mahitaji yote ya bidhaa za mafuta yaliyosafishwa yatalipiwa kwa dola, hilo litaongeza mahitaji ya dola. Hii itasababisha naira kushuka zaidi thamani, na bei za bidhaa za mafuta zitaendelea kupanda kila mara dola inapopata nguvu."
Pia alifafanua kuwa athari za hali hii hazitaishia kwa wafanyabiashara wakubwa wa mafuta pekee, bali gharama kubwa ya kupata dola hatimaye itahamishwa kwa watumiaji.
Profesa Ahmad Adamu anasema kuwa iwapo hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu bila kuchukuliwa hatua za kuzuia, inaweza kusababisha bei za mafuta na bidhaa nyingine kupanda zaidi, na kuongeza mzigo wa maisha kwa wananchi wa kawaida wa Nigeria.
"Hili ni tatizo kubwa, kwa sababu ongezeko lolote la mahitaji ya dola lina athari ya moja kwa moja kwa bei na maisha ya jamii."
Suluhisho ni ipi?
Profesa huyo alieleza kuwa kwa sasa, kutokana na bei ya mafuta yanayouzwa sokoni na thamani ya dola, kuna uwezekano kwamba baada ya kufanya hesabu na ubadilishanaji wa fedha, lita moja ya mafuta inaweza kuwa karibu sawa na dola moja.
"Kwa sasa lita moja ya petroli inauzwa kwa takriban naira 1,300, na dola moja ina thamani ya karibu naira 1,300 au 1,400. Kwa hiyo inaweza kusemwa kuwa kila lita inaweza kuwa karibu sawa na dola moja."
Hata hivyo, alisema hali hiyo haimaanishi kuwa bei zitabakia katika kiwango hicho, kwani ongezeko lolote zaidi la thamani ya dola linaweza kusababisha bei ya mafuta kupanda zaidi.
"Lakini siku zijazo, ikiwa dola itaendelea kupanda thamani, bei ya mafuta pia inaweza kuongezeka, kwa sababu gharama ya kununua au kuzalisha mafuta inapoongezeka, bila shaka itaathiri bei anayolipa mtumiaji wa bidhaa hiyo."
Profesa Adamu anashauri kuwa, kuna haja ya kufuatilia kwa karibu matumizi ya dola katika sekta ya mafuta, kwa kuwa mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni yanaweza kuathiri moja kwa moja maisha ya Wanigeria.
Profesa huyo anaongezea kuwa serikali ina jukumu muhimu katika kushughulikia matatizo yanayoweza kujitokeza baadaye kutokana na uamuzi wa Dangote kuanza kuuza mafuta kwa dola badala ya naira.
Mtaalamu huyo alisema hatua ya kwanza ni serikali kufanya mazungumzo na kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote ili kuhakikisha kuwa mafuta yanaendelea kuuzwa kwa naira katika soko la ndani.
Alieleza kuwa iwapo kampuni hiyo inahitaji dola kwa ajili ya kuendesha shughuli zake, serikali inaweza kuisaidia kwa kuipatia fedha za kigeni, huku kampuni ikiendelea kuuza mafuta kwa Wanigeria kwa kutumia naira.
Mtaalamu huyo alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza shinikizo kwa watumiaji wa mafuta, hasa wakati thamani ya naira inakabiliwa na changamoto katika soko la fedha za kigeni.
Aliongeza kuwa serikali ina uwezo wa kutumia akiba yake ya dola kupunguza kiwango cha ununuzi wa mafuta unaofanywa kwa fedha za kigeni.
"Kwa kuwa serikali ina dola mikononi mwake, inaweza kuzitumia kupunguza ununuzi wa mafuta nchini unaofanywa kwa dola, kwa kununua kwa naira kiasi chote ambacho kingeuziwa kwa dola."
Pia alisema hatua nyingine ambayo serikali inaweza kuchukua ni kutoa ruzuku ya muda kwa wauzaji wa mafuta ili kupunguza uwezekano wa kupanda kwa bei ya mafuta sokoni.
Mtaalamu huyo anasema kuwa serikali inapaswa kutumia njia zote zinazowezekana kusaidia kuwalinda watumiaji wa mafuta dhidi ya ongezeko la gharama ya maisha linaloweza kusababishwa na mabadiliko katika mfumo wa uuzaji wa mafuta.