Dangote: Wataalamu kuamua kiwanda kijengwe Tanzania au Kenya

    • Author, Abdalla Seif Dzungu na Laila Mohammed
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Bilionea na mfanyabiashara wa Afrika Aliko Dangote amekutana na rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na kuahidi kwamba kiwanda cha kusafishia mafuta kitajengwa mwaka huu.

Dangote amesema kwamba kamati ya Wataalamu itatoa ushauri wao kuhusu ni eneo gani kiwanda hicho kitajengwa katika eneo la Afrika mashariki.

Awali rais wa Kenya William Samoei Ruto alikuwa amependekeza ujenzi wa kiwanda hicho kufanyika katika mji wa Tanga, lakini Dangote akasema angependelea ujenzi huo kufanyika mjini Mombasa.

Hatahivyo akizungumza hii leo baada ya kukutana na rais Samia , bwana Dangote amesema kwamba kuna masuala mengi ya kuzingatiwa kabla ya uamuzi kuhusu ni wapi ujenzi wa kiwanda hicho utafanyika.

Tajiri huyo amesema kwamba kiwanda anachotaka kujenga kitakuwa na ukubwa wa kusafisha mapipa 650,000 ya mafuta kwa siku.

''Kama kule Nigeria, hatukujenga kiwanda cha mafuta katika eneo lenye mafuta , tunajenga pale ambapo tunaweza kupata aina tofauti ya mafuta ghafi na kwamba kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyafanyia utafiti'', alisema bilionea huyo.

Dangote amesema kwamba mataifa ya Afrika Mashariki yatamiliki kiwanda hicho bila kujali eneo kitakapojengwa.

Mkutano wa viongozi hao wawili unajiri kufuatia madai ya pendekezo la kujenga kiwanda cha kusafishia mafuta mjini Tanga Tanzania.

Mpango huo kwa mara ya kwanza ulitangazwa na Rais William Ruto wa Kenya aliyependekeza ujenzi wa kiwanda hicho mjini Tanga.

Akizungumza nchini Tanzania, Rais Ruto alisema kuwa ukaribu wa Tanga na Mombasa, takriban kilomita 190, unatoa faida za vifaa ambazo zinaweza kusaidia kuunganisha miundombinu ya mafuta na usambazaji bora wa bidhaa zilizosafishwa katika kanda yote.

Hatahivyo akizungumza katika mkutano huo Rais Samia alishangazwa na tangazo hilo na kumtaka Ruto kumuelezea kwa kina kuhusu mpango huo.

Rais Samia Suluhu Hassan, alieleza kutoridhishwa kwake akiongezea kwamba hakushirikishwa ipasavyo kabla ya tangazo la mradi huo katika mkutano wa miundombinu uliopita.

Lakini akizungumza katika mkutano wa kibiashara uliowaleta pamoja viongozi wa Afrika na Ufaransa, bilionea Aliko Dangote alitaka kiwanda hicho kujengwa mjini Mombasa akidai ni chaguo lenye mantiki kutokana na ukubwa wa uchumi wa Kenya na kiwango kikubwa cha matumizi ya mafuta.

Bwana Dangote pia alikadiria gharama ya ujenzi wa kiwanda hicho kuwa kati ya dola bilioni 15 na 17 za Marekani.

Je, Dangote amebadili msimamo wake?

Hilo ndilo swali ambalo wengi wanalitafakari wakati huu ambapo mfanyabiashara huyo tajiri kutoka Nigeria anakutana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nishati wa Tanzania Deogratius Ndejembi.

Ikiwa Tanga ni mojawapo ya sababu kuu za Dangote kuzuru Tanzania wakati huu ambapo anaripotiwa kutafuta eneo bora la kuwekeza Afrika Mashariki, basi wachambuzi wa kibiashara huenda wakasema kwamba Rais Ruto alifanikiwa kumshawishi kukubaliana na pendekezo lake la Tanzania kuwa kitovu cha usafishaji wa mafuta yanayozalishwa papa hapa.

Kenya ina mradi wa kuchimba mafuta katika kaunti ya Turkana huku Uganda ikichimba mafuta katika mji wa kaskazini magharibi wa Hoima. Awali Uganda ilikubaliana na na Tanzania kuhusu mpango wa kujenga bomba la kusafirisha mafuta hayo hadi bandarini, kwa ajili ya mauzo ya kimataifa.

Je, ndoto hii inawezekana kweli?

Pamoja na faida zake, ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ni miongoni mwa miradi migumu zaidi ya viwanda duniani.

Inahitaji uwekezaji wa mabilioni ya dola, teknolojia ya hali ya juu na mipango ya muda mrefu ya usimamizi.

Mchumi Dk. Hildebrand Shayo anaeleza ukubwa wa changamoto hiyo: "Kiwanda cha aina hii kinahitaji muda mrefu kujenga na uwekezaji wa muda mrefu. Mfano wa Dangote kule Nigeria umechukua zaidi ya miaka 12 kukamilika."

Lakini, changamoto nyingine ni rasilimali fedha. Japo kiwanda cha Tanga kinaonekana kitakuwa na uungwaji mkono kifedha kutoka nchi kadhaa kama Kenya, Uganda zilizoonyesha utayari, miradi hii inagharimu fedha nyingi sana. Kwa mfano kiwanda cha Dangote, Nigeria ujenzi wake umegharimu karibu dola $20 billion. Hizi ni fedha nyingi ni bajeti ya serikali kwa nchi kama Tanzania.

Changamoto nyingine ni uhakika wa malighafi. Kiwanda kinahitaji mafuta ghafi ya kutosha kwa muda mrefu ili kifanye kazi kwa ufanisi. Bila mikataba thabiti ya usambazaji, kiwanda kinaweza kufanya kazi chini ya uwezo wake na kupoteza faida.

Pia kuna suala la siasa na uratibu wa kikanda. Kila nchi zinaendelea na mipango yake ya viwanda vya mafuta, kwa tija tofauti, jambo linaloweza kuleta ushindani badala ya ushirikiano ikiwa mipango haitaratibiwa vyema.

Hata hivyo, fursa bado ni kubwa. Dk. Shayo anaongeza: "Kama kitajengwa, kitaikomboa Afrika Mashariki… tutapunguza utegemezi, bei zitashuka na ajira zitaongezeka." Hapa ndipo mvutano ulipo, kati ya ugumu wa utekelezaji na ukubwa wa faida zinazoweza kupatikana.

Umuhimu wa Tanga kumiliki kituo hicho

Kulingana na Ruto, ukaribu wa Tanga na Mombasa, takriban kilomita 190, unatoa faida za vifaa ambazo zinaweza kusaidia kuunganisha miundombinu ya mafuta na usambazaji bora wa bidhaa zilizosafishwa kote kanda.

Ruto amesema mpango huo unaenda zaidi ya usafishaji wa mafuta, akionyesha nia pana ya kuanzisha uwezo wa kikanda wa usindikaji wa madini.

"Tunapojadili Tanga kama kitovu cha kituo hicho cha mafuta ni lazima pia tufikirie kukiweka kituo cha kusafisha madini, akiongezea kwamba sio vyema kwa sisi kuuza malighafi nje ya nchi, kama eneo ni lazima tuepuke kwa makusudi kusafirisha thamani, ajira na fursa nje ya nchi, badala yake tuzihifadhi na kuzitumia ndani ya nchi, huo ndio mustakabali wa maendeleo yetu," alisema.