Zifahamu tawala 10 za kimabavu Afrika

    • Author, Abdou Aziz Diédhiou
    • Nafasi, BBC News Africa
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 9

Katika baadhi ya nchi za Kiafrika, kuzungumzia hadharani masuala ya kisiasa au kuwakosoa walio madarakani kunaweza kukufanya kuzuiliwa jela, au hata kukugharimu maisha yako.

Katika miongo michache iliyopita, tawala nyingi zimechukua mkondo wa kiimla, zikiminya uhuru wa kujieleza, kukandamiza sauti yoyote pinzani, na kudhibiti mchakato wowote wa uchaguzi, kama upo, na kufanya demokrasia kuwa suala tu linaloangaziwa kwenye vitabu.

Kudorora kwa demokrasia

Takribani nchi 10 kati ya 55 za Afrika, zimegeuka kuwa tawala za kiimla huku 26 zikiwa tawala za kiimla zinazofanya uchaguzi, kulingana na ripoti ya Taasisi ya Varieties of Democracy (V-Dem).

"Demokrasia imerejea katika kiwango chake cha mwaka 1978 kwa raia wa kawaida duniani kote," imesema taasisi hiyo yenye makao yake katika Chuo Kikuu cha Gothenburg nchini Uswidi, katika ripoti yake.

"Hatua zilizopigwa katika 'wimbi la tatu la kuleta demokrasia'—ambalo lilianza mwaka 1974 nchini Ureno kupitia Mapinduzi ya Carnation yaliyoondoa madarakani utawala wa Salazar na kuenea katika maeneo mengi ya dunia—'yanakaribia kufutika kariba'."

Kulingana na Taasisi ya V-Dem, kiwango cha demokrasia kwa raia wa kawaida Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini kiko katika kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha zaidi ya miaka 50, hasa kutokana na mwenendo wa utawala wa kiimla nchini Marekani.

Kwingineko barani Afrika, tunashuhudia hali hiyo hiyo licha mafanikio yaliyofikiwa katika masuala ya kidemokrasia miaka 25 iliyopita na ambayo yalileta matumaini makubwa barani humo.

Idadi kubwa ya watu wanaishi chini ya tawala za kimabavu

Kufikia mwisho wa mwaka 2025, "dunia ilikuwa na tawala za kiimla 92, ikilinganishwa na demokrasia 87. Hivyo, asilimia 74 ya watu duniani (bilioni 6) sasa wanaishi chini ya tawala za kiimla, huku ni asilimia 7 tu ya watu duniani (bilioni 0.6) wakiishi katika demokrasia huria."

Kumekuwa na mabadiliko makubwa ya mwelekeo katika miongo michache iliyopita, hali inayokinzana na matumaini yaliyokuwepo mwanzoni mwa karne ya 21.

"Karibu kila nyanja ya demokrasia imepata pigo kubwa katika muongo uliopita. Kufikia mwaka 2025, uhuru wa kujieleza ulikuwa umepungua katika nchi 44, huku mateso yakiendelea kutumika kukandamiza upinzani wa kisiasa. Aidha, demokrasia imedorora katika nchi 33."

"Mielekeo mitatu tofauti inadhihirika wazi kutokana na wimbi hili: kupungua kwa demokrasia katika baadhi ya nchi ambazo kijadi zilikuwa na demokrasia imara; kurudi nyuma kwa kiasi kikubwa, au hata kuanguka kwa demokrasia, katika nchi ambazo zilikuwa zimefanikiwa kuanzisha demokrasia mwishoni mwa karne ya 20 na mwanzoni mwa karne ya 21; na hatimaye, kuimarika kwa utawala wa kiimla katika nchi ambazo tayari zilikuwa na mifumo hiyo," linaandika Taasisi ya V-Dem.

Kusini mwa Jangwa la Sahara, eneo lisilopendelea demokrasia

Barani Afrika hasa katika eneo la kusini kwa jangwa la Sahara, kiwango cha demokrasia sasa kimerejea katika hali iliyokuwepo mwanzoni mwa miaka ya 2000, kulingana na viashirio viwili: kurejea kwa mapinduzi ya kijeshi katika eneo la Sahel na kuimarika kwa tawala za kiimla.

"Kuimarika kwa tawala za kidikteta katika nchi kama Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji na Togo kunachangia mwelekeo huu mbaya," inabainisha Taasisi ya V-Dem.

Katika eneo hilo, idadi kubwa - 66% ya ya watu - wanaishi chini ya tawala za kidikteta.

Utawala wa kidikteta unaofanya ''uchaguzi'', kama vile Ethiopia, Tanzania na Uganda, ni nyumbani kwa 48% ya idadi ya watu.

Takriban 14% ya idadi ya watu wanaishi katika tawala za kidikteta.

Ni 10% tu wanaoishi katika zinazokumbatia demokrasia za uchaguzi kama vile Botswana, Ghana, Afrika Kusini n.k. na 24% katika nchi zilizo na demokrasia "isiyoeleweka", kama vile Kenya na Nigeria.

Ifuatayo ni orodha ya tawala 10 za kidikteta Afrika - katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

1- Eritrea

Kuanzia katikati ya miaka ya 1990 na kuendelea, Waeritrea walipitia kipindi cha uwazi, kilichoashiriwa na kuibuka kwa magazeti huru yakipaza sauti kwa sauti za ukosoaji, ikiwa ni pamoja na ndani ya chama tawala, Popular Front for Democracy and Justice (PFDJ).

Bunge la Mpito lilikuwa limepanga tarehe ya uchaguzi, tume ya uchaguzi ilikuwa inaundwa, na rasimu ya sheria kuhusu vyama vya siasa ilikuwa ikijadiliwa. Baada ya vita vyake vya muda mrefu vya uhuru dhidi ya Ethiopia, nchi hiyo ilionekana kuanza hatua kwa hatua kuelekea kwenye njia ya demokrasia.

Hata hivyo, kinyume na matarajio, serikali ilibadili mwelekeo mnamo Septemba 2001. Ingawa tahadhari ya ulimwengu ilielekezwa kwenye mashambulizi ya Septemba 11 huko Marekani, wenye mamlaka walifunga magazeti yote huru kwa siku moja, na kunyamazisha sauti kuu za kukosoa nchini humo. Waandishi wengi wa habari walikamatwa na wengine kutoweka katika njia za kutatanisha.

Wakati huo huo, serikali iliwakamata wanachama 11 wa kundi lililojulikana kama G-15, wakiwemo mawaziri watatu wa zamani wa mambo ya nje, mkuu wa zamani wa majeshi na wajumbe kadhaa wa Bunge la Kitaifa. Tangu kukamatwa kwao, hakuna taarifa rasmi za kuaminika zilizotolewa kuhusiana na hatima yao.

Matumaini ya demokrasia yaliyothaminiwa na Waeritrea wengi yalitoweka, na kutoa nafasi kwa mojawapo ya tawala kali za kimabavu katika bara la Afrika.

Kwa zaidi ya miongo mitatu ya utawala wa Rais Isaias Afwerki, hakuna uchaguzi wa urais ambao umewahi kufanyika nchini Eritrea.

2- Burkina Faso

Tangu aingie madarakani Septemba 2022, mkuu a kijeshi nchini Burkina Faso hajaficha chuki yake dhidi ya demokrasia.

Mamlaka za kijeshi zimesitisha utangazaji wa vyombo vingi vya habari vya kimataifa na kuwafukuza baadhi ya wanahabari wao.

Mwezi Oktoba mwaka jana, alivunja Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI), kufuta vyama vyote vya siasa miezi mitano baadaye Februari 2026.

Katika mahojiano yaliyotangazwa kwenye televisheni ya taifa tarehe 2 Aprili, Kapteni Traoré alitoa wito kwa raia wa Burkina Faso "kusahau suala la demokrasia," wakati vyama vya kisiasa vimevunjwa.

"Hatuangazii masuala ya uchaguzi kwanza (...), watu wanapaswa kusahau kuhusu demokrasia. Demokrasia sio yetu," alitangaza.

Ikishiriki katika vita dhidi ya harakati za kigaidi, serikali ya kijeshi wakati mwingine huwateka nyara wapinzani na wakosoaji. Baadhi ya watu wanaothubutu kuukosoa utawala wake wakati mwingine wanapelekwa vitani sambamba na jeshi, hata kama ni raia.

3- Mali

Mnamo Machi 26, 1991, uasi wa umma uliangusha utawala wa kidikteta wa Jenerali Moussa Traoré nchini Mali.

Afisa kijana wa jeshi, Amadou Toumani Touré, akachukua madaraka akiwa na nia ya kuiongoza nchi kwenye njia ya demokrasia.

Baada ya kipindi cha mpito, Mali ilifanya uchaguzi wa vyama vingi uliomfanya Alpha Oumar Konaré kuwa rais. Hii ilikuwa mwanzo wa jaribio la kidemokrasia ambalo lingetumika kama mfano kwa muda mrefu Afrika Magharibi.

Lakini miongo mitatu baadaye, nchi hiyo inaonekana kurudi mahali ilipoanzia.

Tangu 2020, jeshi, ambalo lilichukua madaraka kufuatia mapinduzi mawili mfululizo, limeendelea kusitisha mchakato wa kidemokrasia hatua kwa hatua.

Nafasi ya kiraia na kisiasa imeminywa kwa kiwango kikubwa. Vyama vya siasa vimevunjwa na shughuli za mashirika mengi ya kiraia zimedhibitiwa vikali.

Wnasiasa mashuhuri wa wamekamatwa au kufungwa, huku waandishi wa habari, wanaharakati na baadhi ya wapinzani wakilazimika kutoroka nchini.

Licha ya kuendesha vita dhidi ya makundi yenye misimamo mikali ya kidini, utawala wa kijeshi, ambao hapo awali ulikuwa umejitolea kuingoza nchi katika kipindi cha mpito cha miaka minne, umeendelea kusalia madarakani na haujatoa tena ratiba sahihi ya kurejesha nchi kwenye utaratibu wa kikatiba.

4- Niger

Niger pia sawa na chi zingine katika kanda ya Afrika Magharibi, inakabiliwa na kushuka kwa demokrasia.

Nchi hiyo, hata hivyo, ilipata fursa ya kujiimarisha kisiasa miaka ya 1990, kwa kubadili mfumo wa utawala wa chama kimoja kati ya 1991 na 1993 na kukumbatia utawala wa siasa za vyama vingi.

Tangu wakati huo, tawala za kiraia zimefanikiwa kupokezana madaraka katika miaka ya 2000, ikiwa ni pamoja na ile ya Mahamadou Issoufou, aliyechaguliwa mwaka 2011 kwa muhula wa miaka mitano, na kuchaguliwa tena mwaka 2016.

Kupinduliwa kwa mrithi wake Mohamed Bazoum na kundi la maafisa wa kijeshi mnamo 2023 kuliashiria kurejea kwa utawala wa kijeshi uliokandamiza vyama vya siasa, kuahirisha uchaguzi na mpito wa utawala wa kiraia kwa muda usiojulikana, na kuimarisha udhibiti wake wa mifumo ya kisiasa, na kukandamiza uhuru wa kujieleza nchini.

5- Sudan Kusini

Baada ya miaka mingi ya kupigania uhuru, wa Sudan Kusini mamlaka ya nchi imeshikiliwa na chama kikuu cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM), kinachoongozwa na Rais Salva Kiir.

Tangu ijinyakulia uhuru wake Julai 2011, vyombo vyote vya serikali vimekuwa vikidhibitiwa na SPLM, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa nafasi ya kidemokrasia.

Tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, mamlaka imekuwa ikihusishwa na mzozo kati ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake, Makamu wa Rais Riek Machar.

Suala la demokrasia, kwa raia wa taifa huru la mwisho la Kiafrika halijapata ufumbuzi .

6- Sudan

Ni utawala wa kijeshi unaoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mwenyekiti wa Baraza la Uhuru linalotawala Sudan.

Kwa miaka kadhaa, Sudan imekuwa ikikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vyenye katika mzozo ambao vikosi vya serikali vimekuwa vikipambana na vikosi vya waasi wa Rapid Support Forces (RSF).

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanalaani mauaji makubwa na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu unaofanywa na pande hizo mbili zinazozozana.

7- Somalia

Tangu mapinduzi ya Siad Barre mwaka 1969, raia wa Somalia hawajawahi kupata fursa ya kuwachagua viongozi wao.

Siad Barre alikuwa amemaliza siasa za vyama vingi, kusimamisha katiba na kuanzisha utawala wa kiimla ambao uliiingiza nchi katika mgoro mkubwa wenyewe kwa wenyewe katika miaka ya 1990.

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi imekuwa ikitafuta njia ya kumaliza zaidi ya nusu karne ya kuminywa kwa mchakato wa kidemokrasia kwa kuanzisha mfumo wa upigaji kura unaowajumuisha watu wote na kuandaa chaguzi za vyama vingi.

8- Guinea

Nchini Guinea, licha ya kuandaliwa kwa uchaguzi mnamo Desemba 2025 na Mei 2026, serikali imechukua mkondo unaozidi kuwa wa kimabavu, unaoadhimishwa na kukamatwa, kutoweka na vifo vya kutatanisha vya raia na watu walio kizuizini.

Katika uchaguzi wa urais wa Desemba 2025, Jenerali Mamadi Doumbouya, aliyeingia madarakani kufuatia mapinduzi ya mwaka wa 2021, alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 86.72 ya kura.

Viongozi wakuu wa upinzani hapo awali walikuwa wametengwa kwenye kinyang'anyiro cha urais, jambo ambalo lilitia dosari mchakato mzima wa uchaguzi.

Mashirika kadhaa ya kiraia yameshutumu mwenendo wa serikali kudhibiti nafasi ya kiraia na kisiasa. Yanasema hatua ya serikali kufungia vyama kadhaa vya kisiasa, kupiga marufuku maandamano ya umma, na kudhibiti uhuru wa vyombo inaashiria jinsi demokrasia ulivyokandamizwa.

9- Eswatini

Eswatini ndiyo nchi ya mwisho barani Afrika inayongozwa kupitia mfumo wa utawala wa kifalme wenye mamlaka kamili.

Mfalme Mswati III anashikilia mamlaka yote (ya utendaji, kutunga sheria na mahakama), na anasimamia jeshi la polisi, jeshi la taifa pamoja na mfumo wa mahakama wa ufalme huo.

Tangu kutolewa kwa amri ya kifalme mwaka 1973, vyama vya siasa vimepigwa marufuku nchini humo. Bunge la taifa la ufalme huo lina jumla ya wabunge 69, ambao 10 kati yao huteuliwa moja kwa moja na mfalme.

"Uchaguzi ni kinyang'nyiro kati ya vyama vya siasa. Lakini wachambuzi wa siasa wanasema hauo sio uchaguzi, bali ni mfumo wa uteuzi unaofanywa na wafuasi wa ufalme. Ukishiriki, huwezi kutetea mawazo yako ya kisiasa," alieleza Alvit Dlamini, rais wa NNLG—chama cha zamani zaidi nchini humo—mnamo mwaka 2018.

10- Guinea-Bissau

Guinea-Bissau imekubwa na migogoro ya kisiasa na kitaasisi ambayo, kwa miaka mingi, imeiweka mbali na viwango vya kidemokrasia vinavyozingatiwa katika nchi kadhaa za Afrika.

Mnamo Novemba 2025, wakati nchi hiyo ikishiriki katika mchakato wa uchaguzi ulioadhimishwa na uchaguzi wa rais uliokuwa na ushindani mkubwa na wakati shughuli ya kuhesabu kura ilipokuwa ikiendelea, jeshi liliondoka kwenye kambi yake na kumpindua rais anayeondoka.

Katika hali isiyo ya kawaida, ni rais aliyeondolewa madarakani, Umaro Sissoco Embaló, ambaye mwenyewe alitangaza kwa jumuiya ya kimataifa kwamba amepinduliwa na jeshi.

Kufuatia mapinduzi hayo, wapinzani wa kisiasa wamewekewa vikwazo mbalimbali, huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu kuheshimiwa kwa uhuru wa kimsingi na mustakabali wa vyama vingi vya kisiasa nchini.

Muda mrefu kabla ya kuvunjika huku kwa utaratibu wa kikatiba, utawala wa Umaro Sissoco Embaló ulikuwa tayari ukosoaji.

Mtindo wake wa utawala mara nyingi ulielezewa kuwa wa kimabavu na wapinzani wake wa kisiasa na mashirika kadhaa ya kiraia.

Mvutano ulionekana hasa wakati wa mchakato wa uchaguzi, hadi kufikia hatua ya kutatiza juhudi za upatanishi za Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), ambayo ilitaka kuleta maridhiano kati ya wahusika wakuu wa kisiasa ili kulinda utulivu wa nchi.