Kwa nini baadhi ya 'wabeba vyuma' hufa mapema?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mapema mwezi uliopita, Mileson Araujo alichapisha picha yake akiwa kwenye ukumbi wa mazoezi, kama ilivyokuwa kawaida yake. Picha hiyo ilionyesha umbo lake la mwili, ambalo lilimwezesha kuwa mtaalamu wa kujenga misuli au bodybuilder na mshawishi wa masuala ya mazoezi ya mwili mwenye makumi ya maelfu ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii.

Akiwa amevalia T-shirt nyekundu, Araujo alionyesha mikono yake mikubwa na yenye nguvu, akionekana kama 'shujaa wa vita.'

Masaa machache baadaye, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 35 kutoka Brazil alifariki baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake katika jimbo la Bahia, kaskazini mashariki mwa Brazil.

Ingawa chanzo rasmi cha kifo cha Araujo bado hakijathibitishwa, yeye ni miongoni mwa wabeba 'vyuma' na vitu vizito wengi maarufu wanaojenga misuli waliofariki ghafla.

Mwishoni mwa Mei, Gabriel Ganli, mmoja wa wajenzi wa misuli maarufu zaidi nchini Brazil, alifariki kutokana na mshtuko wa ghafla wa moyo akiwa na umri wa miaka 22.

Mwaka uliopita, wanamichezo wengine wawili wa Brazil, wenye umri wa miaka 30 na 40, walifariki kutokana na matatizo yanayohusiana na moyo. Mmoja wao alifariki akiwa katika mashindano ya kubeba vyuma.

Vifo vya aina hii pia vimeripotiwa katika nchi nyingine duniani, akiwemo mjenzi wa misuli wa Marekani Dallas McCarver, aliyefariki mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 26, na mtaalamu wa mazoezi na afya kutoka Ujerumani Joe Lindner, aliyefariki mwaka 2023 akiwa na umri wa miaka 30.

Kwa nini basi baadhi ya wajenga wa misuli kupitia kubeba vyuma na vitu vizito, ambao kwa nje huonekana kuwa na nguvu na afya njema, hufariki ghafla wakiwa bado vijana?

.

Chanzo cha picha, Maddie Meyer/Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hatari zinazohusishwa na michezo ya kujenga misuli kwa ushindani ziliangaziwa katika utafiti uliofanywa mwaka 2025. Utafiti huo ulihusisha karibu wanamichezo 20,000, wakiwemo washiriki wa ngazi ya wasio wataalamu na wataalamu, ambao walishiriki katika mashindano yaliyoandaliwa na shirikisho la kimataifa linalosimamia mchezo huo kati ya mwaka 2005 na 2020.

Utafiti huo, uliochapishwa katika jarida la European Journal of Cardiology, ulibaini kuwa wajenzi wa misuli wa kitaalamu wana uwezekano mara tano zaidi wa kufariki ghafla, hasa kutokana na hali ya moyo kusimama ghafla, ikilinganishwa na wale wanaoshiriki kwa kiwango cha wasio wataalamu.

Kifo cha ghafla kinachotokana na tatizo la moyo huwapata pia vijana wanaoonekana kuwa na afya njema, na mara nyingi huhusishwa na magonjwa ya moyo na mishipa ambayo huenda hayajagunduliwa.

Utafiti huo ulirekodi vifo 121, ambapo 46 vilikuwa vifo vya ghafla vinavyohusiana na moyo.

Umri wa wastani wa waliofariki ulikuwa miaka 45, lakini kwa wajenzi wa misuli wa kitaalamu, umri huo ulikuwa miaka 34.7 pekee.

Mwandishi mkuu wa utafiti huo, Dkt Marco Vecchio wa Chuo Kikuu cha Padua nchini Italia, alisema kuna sababu kadhaa zilizochangia vifo vya wajenzi wa misuli, zikiwemo "matumizi yaliyoenea" ya dawa za kuongeza uwezo wa mwili kufanya mazoezi, kupunguza uzito kwa haraka kabla ya mashindano na "mazoezi endelevu, makali na ya kiwango cha juu."

Utafiti mwingine uliofanywa na watafiti nchini Denmark na kuchapishwa katika jarida la Circulation mwaka 2025, uliwafuatilia wanaume 1,189 waliotumia dawa za steroid na kuwalinganisha na karibu wanaume 60,000 kutoka kwa jamii kwa ujumla, kwa kipindi cha miaka 11.

Utafiti huo ulibaini kuwa watumiaji wa steroid walikuwa na uwezekano wa karibu mara tisa zaidi wa kupata ugonjwa wa moyo unaodhoofisha misuli ya moyo. Hatari yao ya kupata ugonjwa wa moyo ilikuwa mara tatu zaidi ikilinganishwa na watu wengine.

Mbali na matatizo mengine ya kiafya kwa wanaume, kama vile kupungua kwa idadi ya mbegu za kiume na tatizo la nguvu za kiume, matumizi ya steroid za anabolic yanaweza kuongeza shinikizo la damu, kuharakisha mrundikano wa mafuta na utando wa mafuta kwenye mishipa ya damu, na kusababisha mabadiliko katika muundo wa moyo wenyewe.

Kwa hakika, katika utafiti uliochapishwa katika jarida la European Heart Journal, watafiti walifanya uchunguzi wa miili ya waliofariki ili kubaini mabadiliko yaliyotokea katika mioyo yao.

Katika visa vingi, uchunguzi huo ulionyesha kuwa moyo ulikuwa umeongezeka ukubwa. Sehemu ya kushoto ya moyo ambayo ndiyo chemba kubwa inayosukuma damu kwenda mwilini, ilikuwa imepanuka. Hali hii inaweza kuongeza hatari ya mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida na kushindwa kwa moyo kufanya kazi ipasavyo.

Matokeo ya uchunguzi wa miili ya vijana waliofariki pia mara nyingi yalionyesha kuwa walikuwa na mioyo iliyopanuka.

Miongoni mwa visa vilivyojulikana zaidi ni cha mjenzi wa misuli wa Marekani Dallas McCarver, mmoja wa nyota wakubwa katika ulimwengu wa kujenga misuli, aliyefariki mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 26.

Uchunguzi wa mwili wake baada ya kifo ulionyesha kuwa moyo wake ulikuwa na uzito wa gramu 833, sawa na takriban pauni 1.8 zaidi ya mara mbili ya uzito wa kawaida wa moyo wa mwanaume.

.

Chanzo cha picha, Bispo & Zago, 2024, Arquivos Brasileiros de Cardiologia (CC BY)

Utafiti wa mwaka 2022 uliotumia takwimu kutoka kwa uchunguzi wa miili ya wajenzi wa misuli nchini Marekani ulibaini kuwa, kwa wastani, mioyo yao ilikuwa na uzito mkubwa kwa asilimia 74 ikilinganishwa na watu wa kawaida. Pia, unene wa kuta za sehemu ya kushoto ya moyo (left ventricle) ulikuwa mkubwa kwa asilimia 125 zaidi ya watu wa kawaida.

Katika visa kadhaa, wanamichezo waliokuwa na umri wa miaka 20 walibainika kuwa na mioyo iliyopanuka, kuongezeka sana kwa ukubwa wa misuli ya moyo na ugonjwa wa mishipa ya moyo.

Mjenzi mmoja wa misuli mwenye umri wa miaka 24 alikuwa na mishipa mikuu ya moyo iliyoziba kwa zaidi ya asilimia 75, licha ya kutokuwa na historia ya ugonjwa wa moyo katika familia yake.

Mtaalamu wa homoni na tiba ya michezo, Clayton Macedo, anasema:

"Moyo ni misuli kama misuli nyingine yoyote mwilini. Huwa nasema kwamba ninapomtazama mgonjwa na kuona ukubwa wa misuli yake ya biceps, ninaweza kupata picha ya ukubwa wa moyo wake, kwa sababu moyo pia hukua sambamba na misuli mingine mwilini."

Hakuna njia salama ya kutumia steroid za anabolic.

.

Chanzo cha picha, Rodrigo Goes

Mjenzi wa misuli wa zamani, Rodrigo Gois, aliiambia BBC News Brazil kwamba alishiriki mashindano bila kutumia dawa za kuongeza misuli hadi alipofikisha umri wa miaka 30. Hata hivyo, baadaye aliamua kuanza kutumia steroid baada ya kumtembelea daktari.

"Cycle" ni kipindi maalum, kwa kawaida cha wiki kadhaa, ambapo mtumiaji hutumia steroid za anabolic kisha huacha kwa muda ili kuupa mwili nafasi ya kurejea katika hali yake ya kawaida.

"Athari zake mwilini ni za kushangaza. Unakua haraka kuliko ambavyo ungekuwa kawaida. Mwili wako unaonekana kuwa na misuli iliyojitenga zaidi, na misuli yako hupona haraka. Ndiyo maana inasisimua sana," alisema Gois.

Ingawa Gois anasema alichukua tahadhari na kutumia steroid hizo kwa ushauri wa daktari, alikumbana na madhara mbalimbali ya kiafya, ikiwemo kupoteza nywele, wasiwasi, kukosa usingizi na kutokwa na jasho jingi usiku.

Lakini anasema madhara makubwa zaidi aliyokumbana nayo yalikuwa ya kisaikolojia.

"Sikuwahi kujisikia vizuri kuhusu wazo la kujidunga sindano. Kihisia, nilijihisi kama mraibu wa dawa za kulevya. Ni vigumu kusema hivyo, lakini nilihisi kwamba nilikuwa nikifanya jambo lisilo sahihi."

Kwa sasa, Gois anaendesha kampeni dhidi ya matumizi kupita kiasi ya steroid.

"Hakuna njia salama ya kutumia steroid za anabolic. Madaktari wanaweza kutibu tu madhara ambayo tayari yametokea, lakini madhara hayo yatabaki."