Jeshi Tanzania: Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaohusika na uvunjifu wa amani
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema kuwa litachua hatua kali za kisheria dhidi ya watu watakaojihusisha na vitendo vinavyohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani.
Katika taarifa yake kwa umma, JWTZ imesema kuwa ina jukumu la kulinda usalama wa nchi na wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Ulinzi wa Taifa Sura ya 192.
Jeshi hilo limeeleza kuwa litaendelea kushirikiana na vyombo vya dola kukabiliana na matukio yoyote ya vurugu, ghasia na uvunjifu wa amani.
Aidha, wananchi wamehimizwa kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji, mitaa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu viashiria vya uchochezi ili kudumisha utulivu nchini.JWTZ pia limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda mipaka, Katiba na mamlaka ya nchi sambamba na kushirikiana na wananchi katika kuimarisha amani, umoja na maendeleo ya taifa.