Iran ina "mpango mpya wa kumuua Donald Trump"

Chanzo cha picha, Getty Images
Gazeti la The Wall Street Journal linaripoti kuwa Israel imeipatia Washington taarifa zinazoonesha kuwa Iran inazingatia mpango mpya wa kutaka kumuua Donald Trump.
Taarifa hizi zinaonekana kuathiri mtazamo wa Rais wa Marekani zaidi kuliko hapo awali.
Katika siku za hivi karibuni, Trump amezungumzia hadharani vitisho vya kuuawa kwake mara kadhaa, akisema: "Wanataka kumuondoa kiongozi wa Marekani, yaani mimi," na "Jina langu liko kwenye orodha zao zote."
Taarifa hizi ambazo Israel ilimpa Trump, pamoja na jaribio lililoshindwa la kutaka kumuua huko Pennsylvania mnamo Julai 2024, ambalo Donald Trump anadai lilikuwa mpango wa Jamhuri ya Kiislamu, zimemfanya rais huyo wa Marekani kubadilisha suala hilo la jaribio la mauaji kutoka kuwa suala la kiusalama tu na kulifanya kuwa sehemu ya simulizi yake ya kisiasa.
Kundi la wakosoaji wa Trump linasema kuwa hii ni njia ya kujipatia huruma na uungwaji mkono nchini Marekani; hata hivyo, wengi wanachukulia tishio la Jamhuri ya Kiislamu kutaka kumuua Trump kuwa ni jambo zito sana, wakirejelea jaribio la jeshi la Iran la kutaka kumuua John Bolton, aliyekuwa mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, mnamo mwaka 2022.
Lakini hata kama Donald Trump anatumia suala hili kwa ajili ya propaganda za kisiasa, uzoefu wa kihistoria nchini Marekani unaonesha kuwa majaribio ya kuwaua marais hayaleti lazima ongezeko la umaarufu wao wa kisiasa.
Kumekuwa na takribani majaribio sita ya kuwaua marais wa Marekani tangu mwaka 1950, kuanzia mauaji yaliyofanikiwa ya John F. Kennedy hadi majaribio yaliyoshindwa dhidi ya Harry Truman, Gerald Ford, na Ronald Reagan.
Wakati Truman na Ford walishindwa kubadili hali ya kushuka kwa viwango vyao vya kukubalika baada ya mashambulizi hayo, Reagan alikuwa tofauti; ucheshi na utulivu wake baada ya kupigwa risasi mwaka 1981 vilizua wimbi la huruma ya umma na kusababisha ongezeko kubwa la viwango vyake vya kukubalika.
Sasa, wengi wanaamini kuwa Trump, ambaye rais anayempenda zaidi ni Reagan, anajaribu kuonesha taswira kama hiyo ya uthabiti na uongozi kwa kusisitiza mara kwa mara kuhusu tishio dhidi ya maisha yake.
Unaweza kusoma;






















