Watu 12 Wafariki kwa moto Hispania huku kiwango cha joto kikiongezeka kusini mwa Ulaya

Chanzo cha picha, EPA
Takriban watu 12 wamefariki dunia kutokana na moto mkubwa wa porini uliozuka katika eneo la Los Gallardos, Almería kusini mashariki mwa Hispania, kwa mujibu wa serikali ya eneo la Andalusia. Watu wengine sita wamejeruhiwa.
Baadhi ya miili ya waliofariki ilipatikana ndani ya magari yaliyoteketezwa na moto huo.
Mashuhuda wamesema moto huo ulianza baada ya waya wa umeme kuanguka na kusababisha moto ulioenea haraka hadi kwenye eneo la msitu. Hata hivyo, mamlaka bado hazijathibitisha chanzo rasmi cha moto huo.
Joto kali lenye viwango vya takribani nyuzi joto 40 limechochea milipuko ya moto wa porini katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Ulaya.
Mamia ya maafisa zimamoto wanaendelea kupambana na moto mkubwa nchini Hispania, Ufaransa na Ureno, huku maelfu ya wakazi wakilazimika kuhama makazi yao kwa usalama.
Serikali ya Andalusia ilisema idadi ya vifo imeongezeka hadi 12 baada ya kuthibitishwa kwa vifo sita zaidi.
Rais wa serikali ya Andalusia, Juanma Moreno, alielezea tukio hilo kuwa ni janga kubwa. Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, alisema: "Mioyo yetu imejaa huzuni na tumegubikwa na majonzi."
Takribani maafisa zima moto 150 walikuwa wakifanya juhudi za kuuzima moto katika kijiji cha Bedar.
Miongoni mwa waliojeruhiwa, mmoja alipelekwa hospitalini baada ya kuvuta moshi mwingi, huku mwingine akipata majeraha ya moto.
Watu wengine wanne walipatiwa matibabu katika eneo la tukio kutokana na majeraha madogo ya moto na matatizo ya kupumua yaliyosababishwa na moshi mzito.
Moto huo pia ulisababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara, huku wakazi wapatao 1,000 wakihamishwa kutoka makazi yao kwa tahadhari, kwa mujibu wa huduma za dharura.





















