Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Unaijua 'Tsunami ya angani'? Hivi ndivyo inavyotokea
Tunaposikia neno Tsunami, mara nyingi tunafikiria mawimbi makubwa yanayosababishwa na tetemeko la ardhi chini ya bahari.
Lakini kuna aina nyingine ya Tsunami inayoweza kutokea mbali kabisa na bahari, zaidi ni kwenye milimani.
Maporomoko makubwa ya barafu, miamba na udongo yanapoanguka ndani ya ziwa au bahari, yanaweza kusababisha maji kusukumwa kwa nguvu na kutengeneza wimbi kubwa sana.
Baadhi ya wanasayansi huliita tukio kama hili "Tsunami kutoka angani" kwa sababu chanzo chake kinakuwa sio chini ya bahari bali bali kwenye mlima au barafu inayoanguka kutoka.
1. 'Tsunami kutoka angani' inatokeaje?
Fikiria mlima wenye barafu na miamba mingi ukianza kuporomoka ghafla kuelekea chini kwenye maji.
Mamilioni ya tani za barafu, udongo na miamba zinapoanguka ndani ya ziwa au bahari kwa nguvu kubwa, zinasukuma maji kwa kasi.
Maji hayo yanaweza kutengeneza ukuta au wimbi kubwa la maji linaosambaa katika eneo hilo. Linaweza kuwa na athari kubwa kulingana na ukubwa wa udongo ama barafu iliyotua majini na kasi yake.
Hii ndiyo tofauti kubwa kati ya Tsunami inayosababishwa na tetemeko la ardhi chini ya bahari na tsunami inayotokana na maporomoko ya ardhi: katika tukio hili, mlima wenyewe ndio unaosukuma maji.
Hatari inaweza kuwa kubwa zaidi katika maeneo yenye miteremko mikali, maeneo yenye barafu nyingi na yenye maji yaliyo karibu na milima.
Profesa Bill McGuire, mtaalamu wa hali ya hewa na profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha London, anasema kuporomoka kwa barafu kunaweza kuwa tishio linaloongezeka kwa jamii zinazoishi chini ya maeneo ya milimani yenye barafu.
"Tukio hili si ishara tu ya nyakati hizi, bali ni kidokezo cha yatakayotokea siku zijazo," anasema. "Ni tishio ambalo linaweza kuongezeka zaidi kadiri sayari inavyozidi kupata joto."
2. Kilichotokea Alaska na hofu ya kutokea tena
Mfano wa ukubwa wa hatari hiyo ulionekana mwaka 2025 huko Alaska, Marekani.
Maporomoko makubwa ya ardhi, yaliyohusishwa na kuporomoka kwa kasi kwa barafu, yalisababisha wimbi lililofikia takriban mita 481 kwenda juu..karibu viwanja vitano vya mpira ukivisimamisha, urefu unaozidi hata mnara maarufu kule Ufaransa wa Eiffel Tower.
Lilikuwa mojawapo ya mawimbi makubwa zaidi ya aina hiyo kuwahi kurekodiwa duniani.
Watu watatu waliokuwa wamepiga kambi karibu na maeneo ya jirani walinusurika, lakini maji yaliharibu kabisa kambi yao.
Bahati ilikuwa kwamba tukio hilo lilitokea saa chache kabla ya meli za watalii kuingia katika eneo hilo.
Hapo ndipo hofu kubwa ilipo.
Alaska kuna maeneo yenye ghuba ndefu, yenye kina kirefu cha maji, inayozungukwa na miamba mikubwa au milima mirefuambapo hutembelewa na maelfu ya watalii wanaosafiri kwa meli karibu na milima na barafu.
Iwapo maporomoko kama hayo yangetokea wakati meli iko ndani ya ghuba hizi, wataalamu wanaonya kwamba maafa yangekuwa makubwa zaidi.
Baadhi ya kampuni za meli zilibadilisha safari zao za mwaka 2026 ili kuepuka dhahama hiyo.
Dr Tom Robinson, mhadhiri mwandamizi kutoma Chuo Kikuu Canterbury nchini New Zealand na mtaalamu wa hatari za majanga, anasema watalii ndio walio katika hatari kubwa zaidi katika maeneo hayo.
"Tulibahatika mwaka jana kwamba hakukuwa na mtu wakati huo, lakini mambo yangeweza kuwa tofauti kabisa," anasema.
Robinson anaeleza kwamba tatizo ni kasi ambayo tukio kama hili linaweza kutokea. Mara maporomoko yanapoanza na kusababisha wimbi, meli inaweza isiwe na uwezo wa kugeuka au kusogea kwa kasi ya kutosha kulikwepa.
Na Alaska si eneo pekee linalotajwa. Wataalamu wanaona hatari pia katika baadhi ya maeneo ya milima ya Rocky nchini Marekani, safu za milima mirefu (Alps) Ulaya na Himalaya, ambako kuna mchanganyiko wa milima mikali, barafu na maji.
Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuongeza hatari katika baadhi ya maeneo. Barafu inapoyeyuka na kudondoka ama kuporomoka, inaweza kubadilisha uthabiti wa miteremko. Joto linaloongezeka pia linaweza kuyeyusha tababa la ardhi na miamba iliyoganda kwa muda mrefu ambayo husaidia kushikilia miteremko ya milima.
Hata hivyo, wanasayansi wanaonya kwamba si sahihi kuhusisha kila tukio na mabadiliko ya tabianchi. Jiolojia ya eneo, mvuto wa dunia, mienendo ya kijiolojia inayotokea katika tabaka la nje la Dunia na mambo mengine pia yanaweza kuchangia.
3. Funzo kutoka Nepal
Hivi karibuni mwisho wa mwezi Agosti 2026 ukuta mkubwa wa maji, matope na vifusi ulisomba vijiji na maeneo ya uzalishaji umeme karibu na mpaka wa Nepal na China.
Ingawa maporomoko ya ardhi na barafu yanashukiwa kuchangia mafuriko hayo, ingawa wanasayansi bado wanachunguza ni kwa kiwango gani ongezeko la joto na mabadiliko ya tabianchi yalihusika.
Profesa Patrick Lynett, kutoka Chuo kikuu cha Southern California, anasema bado hakuna ushahidi wa kutosha kufikia hitimisho hilo.
"Haiko wazi kwamba ndivyo ilivyokuwa, na itachukua muda kufahamu," anasema.
Watu wasiopungua 1,399 wanaelezwa kupoteza maisha, huku zaidi ya 5,200 wakiwa bado hawajulikana walipo, kwa mujibu wa taarifa za mamlaka.
Kwa mujibu wa Lynett, huenda mabadiliko katika barafu yalifanya eneo hilo liwe tayari kwa maporomoko ya ardhi, au huenda yalikuwa maporomoko makubwa yaliyotokea huku kukiwa na barafu juu yake.
Wanasayansi wanaweza kutumia satelaiti na vifaa vingine chini ya ardhi kufuatilia kama miteremko ya milima inaanza kusogea. Teknolojia hiyo tayari imesaidia katika baadhi ya maeneo kuhamisha watu kabla ya maporomoko makubwa.
Baadhi ya maeneo ya ,ilima yanaweza kuporomoka bila kutoa ishara kubwa mapema. Katika maeneo yenye barafu nyingi kama Alaska, baadhi ya barafu zinaweza kusogea kwa mita kadhaa kwa siku, jambo linaloweza kufanya iwe vigumu kutambua mienendo midogo ya miamba ambayo huenda ikawa ishara ya hatari.
Maneo hayo yana barafu kubwa zilizoganda zambazo zikiporomoka zinaweza kusababisha 'Tshunami' kubwa.
Kwa hiyo, wanasayansi wanaweza kutambua vizuri zaidi maeneo ambayo yanaweza kuwa hatarini, lakini bado ni vigumu kusema ni lini hasa mlima ya mabarafu ama ardhi itaanguka.
Na hapo ndipo "Tsunami kutoka angani" inakuwa tishio lisilo la kawaida, iinaweza kuanza kwa mlima unaoporomoka, lakini ndani ya muda mfupi ikageuka kuwa ukuta mkubwa wa maji ama wimbi kubwa linaloweza kuleta madhara makubwa kwa walio karibu.
Makala hii ina mchango mkubwa kutoka kwa mwandishi Jessica McAllen