Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
AFCON 2027: Kenya yakimbizana na muda huku shinikizo likiongezeka
- Author, Celestine Karoney
- Nafasi, BBC Sport Africa, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Rais wa Shirikisho la soka barani Afrika, Patrice Motsepe, amezitaka Kenya, Tanzania na Uganda, ambazo ni wenyeji wenza wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) la mwaka ujao, kuongeza "hali ya uharaka" katika maandalizi yao.
Mashindano hayo yanatarajiwa kurejea Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza baada ya miaka 51, huku mechi ya ufunguzi ikipigwa tarehe 19 Juni na fainali ikipangwa kufanyika tarehe 17 Julai.
Viwanja vinatarajiwa kuwa tayari kwa ajili ya kufanyiwa majaribio ndani ya takriban miezi mitatu ijayo, na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Motsepe, amesema hakuna nafasi kubwa ya kuchelewa.
"Ingawa tuna miezi tisa, tunahitaji kuanza kutumia viwanja hivyo mwezi Januari mwakani ili kuvifanyia majaribio na kuona maboresho zaidi yanayohitajika," aliiambia BBC Sport Africa baada ya kukagua maandalizi nchini Kenya siku ya Ijumaa.
Motsepe amesema kumekuwa na "maendeleo mazuri sana", huku akikiri kuwa baadhi ya miundombinu bado haijafikia kiwango kinachohitajika.
"Tuna viwango vya juu sana kuhusu matarajio yetu ya miundombinu, huduma na viwanja, hoteli, barabara, pamoja na viwanja vya mpira ambako mazoezi yatafanyika," aliongeza raia huyo wa Afrika Kusini.
"Tunataka huduma hizo ziwe za kiwango cha kimataifa."
Licha ya kuchelewa katika baadhi ya maeneo, Motsepe amesisitiza kuwa "hakuna hata wazo dogo la kuahirisha mashindano hayo."
"Hakuna sababu ya kufanya hivyo kwa sababu kuna dhamira kubwa ya kuhakikisha mashindano yanafanyika."
Kenya kuharakisha maandalizi
Motsepe alianza ziara yake ya kukagua maandalizi ya Afcon 2027 nchini Tanzania kabla ya kuelekea Kenya, ambako alikagua viwanja viwili jijini Nairobi: Uwanja wa Kasarani na Uwanja mpya wa Talanta wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000.
BBC Sport Africa inaelewa kuwa moja ya maeneo makuu yanayotia wasiwasi nchini Kenya ni Uwanja wa Kasarani pamoja na kituo chake cha mazoezi.
Uwanja huo pia unatarajiwa kutumika kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha ya mwaka 2029, ambayo Nairobi ilipewa nafasi ya kuwa mwenyeji siku ya Jumanne, ikiishinda London na Roma.
Wakati Caf ilipofanya ukaguzi wake wa awali katikati ya Februari, waandaaji wa ndani waliambiwa kuwa viwanja pamoja na vituo vyake vya mazoezi vinapaswa kuwa vimekamilika kwa takriban asilimia 80 kufikia Agosti.
Hata hivyo, kumekuwa na maendeleo machache katika Uwanja wa Kasarani katika kipindi cha miezi saba iliyopita, huku maeneo kadhaa bado yakihitaji kufanyiwa kazi.
Moja ya changamoto kubwa ni sehemu ya kuchezea, ambayo bado haijawekwa. Kazi pia inahitajika kwenye mifumo ya nyaya kwa ajili ya shughuli za utangazaji na televisheni, taa za uwanjani pamoja na maeneo maalum ya wageni waalikwa katika uwanja huo.
Motsepe pia alizungumzia mahitaji yanayotokana na kuwakaribisha mamia ya wageni mashuhuri na wakuu wa nchi, akisema baadhi ya miundo ya viwanja italazimika kufanyiwa marekebisho.
"Masuala ya usalama yanayohusiana na mahali ambapo wageni maalum, hasa wakuu wa nchi, watakaa yanahitaji marekebisho ya mipango ya awali," alieleza Motsepe mwenye umri wa miaka 64.
Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Kenya anayesimamia michezo, Salim Mvurya, alisisitiza kuwa maandalizi yatakamilika kwa wakati.
"Naahidi Caf na Wakenya kwamba tutaharakisha maandalizi ya Afcon 2027," alisema Mvurya.
"Tunakamilisha kila kitu ifikapo Desemba ili kuhakikisha tunaweza kuandaa mechi za majaribio katika vituo mbalimbali."
Desemba ni mwezi muhimu kwa sababu Motsepe anatarajiwa kurejea katika eneo hilo mwezi Januari kwa ziara ya mwisho ya kutathmini maandalizi.
Mashindano ya hivi karibuni ya Caf yamekuwa yakiahirishwa mara kwa mara kutoka katika tarehe zake za awali.
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake la mwaka huu lilichezwa mwezi Julai, baada ya kuanza kwake kupangwa mwezi Machi lakini likaahirishwa siku 12 tu kabla ya kuanza.
Mashindano ya African Nations Championship ya mwaka 2024 yaliyofanyika Kenya, Tanzania na Uganda yaliahirishwa kutoka tarehe zake zilizopangwa za Februari 2025 hadi Agosti 2025, ili kuhakikisha miundombinu na huduma "zinafikia viwango vinavyohitajika". Uamuzi huo ulitangazwa siku 18 tu kabla ya mashindano kuanza.
Wakati huohuo, Afcon 2023 nchini Ivory Coast ilihamishwa hadi mwanzoni mwa mwaka 2024 kutokana na wasiwasi kuhusu msimu wa mvua.
Miaka miwili iliyopita, aliyekuwa naibu wa Motsepe, Veron Mosengo-Omba, alikiri kuwa Caf ilikuwa inakabiliwa na "changamoto kubwa ya upangaji wa ratiba" ili kuingiza mashindano yake yanayofanyika kila baada ya miaka miwili katika kalenda yenye msongamano wa soka.
Baadhi ya wachambuzi wanadai kuwa hilo ni miongoni mwa sababu zilizo nyuma ya uamuzi wa kuandaa Afcon ya wanaume kila baada ya miaka minne kuanzia baada ya mwaka 2028.
Urathi katika Michezo
Licha ya mashindano ya awali kuahirishwa na kuwepo kwa wasiwasi kuhusu maandalizi ya Afrika Mashariki, Motsepe ameweka wazi kuwa ratiba ya Afcon 2027 haitafanyiwa marekebisho.
"Hakuna mpango B, wala mpango C," alisema.
Kwa Kenya, kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa wakati huu ni muhimu zaidi kwa sababu Afcon imekuwa sehemu ya mpango mpana wa michezo nchini humo.
"Moja ya sababu zilizofanya Kenya ishinde zabuni ya kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Dunia ya Riadha ya 2029 ni kwa sababu tunaandaa Afcon. Kwa hiyo, hili ni suala la urithi," alisema Mvurya.
"Michezo si burudani tu, bali ni chanzo cha kipato na kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi.
"Kwa hiyo, tunatambua kuwa fursa ya kuwa mwenyeji wa Afcon itakuwa muhimu katika kuchochea uchumi wetu. Sekta yetu ya utalii itanufaika kwa kiasi kikubwa.
"Kama serikali, tuna imani kwamba tutaandaa Afcon yenye mafanikio."
Miezi mitatu ijayo huenda ikawa muhimu sana katika kuhakikisha ahadi hiyo inatimia.