Kwanini kondo la nyuma linauzwa katika soko haramu?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Onyo: Taarifa hii ina picha zinazoshtua za tishu za binadamu.

Mamlaka nchini Pakistan zinachunguza mtandao unaoshukiwa kujihusisha na biashara haramu ya kondo la nyuma la binadamu (placenta), ambalo linadaiwa kuchakatwa na kusafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya kutengeneza sindano zinazodaiwa kusaidia kupunguza dalili za uzee.

Shirika la Upelelezi la Shirikisho (FIA) limeshutumu genge hilo kwa kununua takriban kilo 200 za kondo la nyuma kutoka hospitali mbalimbali kila mwezi.

Kisha huzikausha na kuzichakata kabla ya kuzisafirisha kwenda nje ya nchi, Shirika la FIA liliiambia BBC News Urdu.

Katika msako uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita, mamlaka zilikamata kilo 500 za kile walichoamini kuwa ni kondo la nyuma la binadamu katika kituo haramu cha kuchakata bidhaa hizo mjini Islamabad, na kuwakamata watu watano.

Picha zilizotolewa na FIA zinaonyesha trei zenye kondo za nyuma zilizokaushwa zikiwa zimewekwa ndani ya nyumba ambayo ilikuwa imegeuzwa kuwa kituo cha kuhifadhi na kuchakata kondo la nyuma.

Hina Kanwal, afisa kutoka mamlaka ya upandikizaji wa viungo vya binadamu ya Pakistan aliiambia BBC News Urdu kwamba washukiwa hao watano walilipa takriban dola za Marekani 2.90 kwa kila kondo la nyuma kwa hospitali zilizoko Islamabad na Rawalpindi. Alisema jambo hilo lisingewezekana bila ushirikiano wa wasimamizi wa hospitali hizo.

Ka mujibu wa FIA, kondo hizo zilipaswa kusafirishwa nje ya nchi na kubadilishwa kuwa sindano za kupunguza dalili za kuzeeka, huku kila sindano ikiuzwa kwa takriban dola 2,530.

Kanwal anasema kuna mahitaji makubwa ya placenta ya binadamu katika upasuaji wa urembo, lakini nchini Pakistan ni kinyume cha sheria kununua au kuuza placenta hiyo.

Watu watakaopatikana na hatia ya kuchukua viungo vya binadamu kwa madhumuni ya kibiashara wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 10 jela na kutozwa faini ya hadi dola 3,600.

FIA imesema shughuli za mtandao huo zimeenea hadi miji mingine mikubwa, ikiwemo Lahore na Peshawar.

Aidha, maafisa wa uhamiaji, kampuni za usimamizi wa taka na hospitali vinafanyiwa uchunguzi kutokana na tuhuma za kushirikiana katika shughuli hizo.

Afisa mmoja aliyezungumza na BBC News Urdu alisema kuwa FIA hapo awali ilikuwa imechukua hatua dhidi ya biashara haramu ya usafirishaji wa viungo vya binadamu, lakini hii ilikuwa kesi ya kwanza iliyohusisha "mtandao wa kimataifa wa kusafirisha kondo la nyuma la binadamu."

Mamlaka zilisema washukiwa hao watano awali walidai kuwa bidhaa hiyo ilikuwa kondo la nyuma la kondoo, lakini baadaye walikiri wakati wa mahojiano kuwa ilikuwa kondo la nyuma la binadamu.

Wakati huo huo, maafisa wa FIA walioko katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Islamabad walikamata kilo 100 za kondo la nyuma la binadamu zilizokuwa zikisafirishwa kwenda Vietnam. Ingawa matumizi ya kondo la nyuma la wanyama yanaruhusiwa nchini Vietnam, matumizi ya kondo la nyuma la binadamu yamepigwa marufuku.

Idadi ya watu waliokamatwa na FIA kwa tuhuma za kujihusisha na usafirishaji haramu wa kondo la nyuma la binadamu imefikia tisa.

Sadaf Tariq, daktari wa magonjwa ya wanawake nchini Pakistan, anasisitiza kuwa kuna kanuni kali kuhusu utupaji wa kondo la nyuma, ambalo linachukuliwa kuwa "taka hatarishi za kitabibu zenye uwezekano mkubwa wa kuambukiza."

Akizungumza na BBC News Urdu, Tariq alisema kuwa kondo la nyuma hutenganishwa mara tu baada ya mama kujifungua na kuwekwa katika mfuko wa njano wa "taka hatarishi " wenye alama inayoonyesha kuwa kuna kondo la nyuma, kisha hufungwa kwa nguvu, ili kuzuia kondo la nyuma kuoza na kutoa harufu mbaya, na husafirishwa kutoka chumba cha kujifungulia au chumba cha upasuaji kwenda kwenye eneo kuu la kuhifadhia taka baridi la hospitali."

Tariq aliongeza kuwa kondo la nyuma linaweza kuhifadhiwa kwa muda usiozidi saa 24.

"Baada ya hapo, taka zote za kitabibu, kama vile kondo la nyuma, hutupwa kwa kuchomwa moto ambao ndiyo utaratibu wa kawaida wa kitabibu. Iwe ni hospitali ya serikali au ya binafsi, njia hiyo hiyo hutumika," alisema.

Matumizi yake katika tiba

Watu wanaamini kuwa kondo la nyuma, ambalo lina wingi wa protini, madini ya chuma na mafuta, linaweza pia kuwa na virutubisho kwa watu wazima.

Kwa mujibu wa Polaris, kampuni ya utafiti wa masoko yenye makao yake nchini Marekani, thamani ya biashara halali ya kondo la nyuma duniani kwa sasa inazidi dola milioni 700 kwa mwaka, na inatarajiwa kuvuka dola bilioni 1.4 ifikapo mwaka 2034.

Polaris inasema ukuaji huo unatokana na ongezeko la mahitaji ya kondo la nyuma kutoka kwa nguruwe, kondoo, farasi na binadamu.

"Kondo la nyuma limekuwa kiungo kinachozingatiwa sana si tu katika ujauzito, bali pia katika tiba na sayansi," alisema Nitin Tambe, mchambuzi wa Polaris.

"Kuanzia kumlisha mtoto akiwa tumboni hadi matumizi ya kitabibu na kuchochea ubunifu katika sekta ya urembo, uwezekano wa matumizi yake unaendelea kuongezeka," aliongeza.

Bidhaa nyingi zinazotokana na kondo la nyuma hutumiwa katika bidhaa zinazohusishwa na kuzeeka.

Baadhi ya matumizi ya bidhaa hizo ni pamoja na kupunguza au kuzuia mikunjo ya ngozi, kupoteza nywele, kukoma kwa hedhi, ugumba

Hata hivyo, kondo la nyuma, ambalo lina kiwango kikubwa cha homoni za kike kama estrojeni na projesteroni, hutumika katika baadhi ya dawa, ikiwa ni pamoja na zile zinazotumika kutibu msongo wa mawazo baada ya kujifungua.

Pia linaweza kutumika katika matibabu ya magonjwa ya kingamwili na matatizo ya mfumo wa neva kama vile kiharusi, uchovu sugu, ugonjwa wa Parkinson, ugonjwa wa sclerosis, na kudhoofika kwa misuli (muscular dystrophy).

Matumizi mengine ni katika matibabu ya magonjwa ya ini, ugonjwa wa Crohn, na hata saratani, ambako matibabu ya kawaida yameonyesha mafanikio madogo.

Aidha, baadhi ya watu wanaamini kuwa vidonge na sindano zinazotokana na tembe za kondo la nyuma husaidia katika urejeshaji wa tishu za mwili.

Kampuni ya Japan Bio Products (JBP) husafirisha vidonge vya kondo la nyuma vilivyokaushwa kuwa unga, kama virutubisho vya lishe katika maeneo mbalimbali ya bara Asia. Baadhi ya bidhaa hizo hutokana na kondo la nyuma la binadamu, huku nyingine zikitokana na kondo la nyuma la nguruwe au farasi, kulingana na soko husika.

Biashara haramu nchini China

Nchini China, licha ya kupigwa marufuku kwa biashara hii, kondo la nyuma la binadamu bado linaendelea kuuzwa kwa siri au kufichwa kwa majina tofauti kwenye majukwaa mbalimbali ya mtandaoni.

Muuzaji mmoja mtandaoni aliiambia Global Times kwamba kondo moja la nyuma la binadamu linaweza kuuzwa kwa zaidi ya dola 50.

"Ikiwa utanunua zaidi, naweza kupunguza bei hadi dola 40. Tunanunua malighafi hiyo kwa dola 30 kwa kila kilo," alisema.

Mwanasheria Zhang Bo pia aliiambia gazeti hilo kuwa watu wanaokamatwa kwa kawaida hutozwa faini isiyozidi mara tano ya kiasi walichopata kutokana na biashara hiyo haramu.

Hata hivyo, Dk. Huang Chengsheng, daktari wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Shanghai, aliiambia Global Times kwamba mtu anaweza kuambukizwa kwa kula "kondo la nyuma lisilo salama kiafya" ambalo linaweza kuwa na virusi kama vile vya HIV, homa ya ini aina hepatitis B, na kaswende.

Dk. Huang alielezea, kuwa akina mama wengi wapya hupendelea kuchukua kondo lao la nyuma na kulila badala ya kulitupa.