Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump afungua mlango wa mazungumzo na Iran

Iran bado haijatoa jibu kwa matamshi ya Trump. Trump amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba mwisho wa vita kupitia mazungumzo uko karibu kufikiwa, lakini mashambulizi ya kulipizana yamekuwa yakirejea tena na tena.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Wafanyakazi wawili wafariki baada ya helikopta za kuzima moto kugongana nchini Ugiriki.

    Wafanyakazi wawili wamefariki dunia baada ya helikopta mbili kugongana angani nchini Ugiriki wakati zikishiriki kuzima moto wa nyika.

    Waliofariki ni rubani wa Denmark na afisa wa mawasiliano wa idara ya zimamoto ya Ugiriki. Rubani raia wa Uingereza na mratibu mwingine raia wa Ugiriki waliokuwa kwenye helikopta ya pili walinusurika.

    Video ya tukio hilo, lililotokea takribani umbali 65 (mail42) magharibi mwa mji mkuu wa Athens, inaonesha helikopta aina ya Bell ikigonga mbawa za helikopta nyingine, ambayo ilishika moto. Helikopta nyingine ilitua kwa dharura.

    Moto wa nchi umezuka nchini Ugiriki wiki hii na kusababisha uhamishaji wa watu kwa wingi. Nchi nyingine za Ulaya pia zimekumbwa na moto mkubwa na hatari wakati wa vipindi virefu vya joto kali.

    Kwa mujibu wa Idara ya Zimamoto ya Ugiriki, helikopta hizo aina mbili za Bell—ambazo zimekodishwa kutoka kampuni ya Australia ya McDermott Aviation—ziligongana Jumapili wakati zikishiriki juhudi za kuzima moto mkubwa uliokuwa ukiwaka katika mpaka wa Attica na Boeotia.

    Wafanyakazi wa helikopta moja waliokolewa wakiwa hai, huku wa helikopta ya pili wakipatikana wakiwa hawajitambui na baadaye kuthibitishwa kufariki dunia.

    Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, alielezea "masikitiko yake makubwa" kufuatia ajali hiyo.

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, alisema kupotea kwa mratibu huyo raia wa Ugiriki na rubani raia wa Denmark "kunatujaza sote huzuni." Pia alitoa rambirambi kwa familia zao.

  2. WAFCON 2026: Mali yaibuka na ushindi wa kwanza, Cameroon yakaribia kutinga hatua ya mtoano

    Mali Yaibuka na Ushindi wa Kwanza, Cameroon Yakaribia Kutinga Hatua ya Mtoano AFCON ya Wanawake

    Katika mashindano ya soka kuwania kombe la taifa bingwa barani Afrika kwa kina dada yanayoendelea nchini Morocco, Mali ilijinyakulia alama tatu muhimu pale ilipoilaza Cape Verde magoli matatu kwa mawili.

    Ushindi huo ndio uliokuwa wa kwanza kwa mali katika mashindano hayo.

    Katika mechi nyingine Cameroon, iliilaza Ghana bao moja kwa bila.

    Cameeron sasa ina alama sita baada ya kushinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Mali.

    Cameroon sasa inahitaji sare au ushindi katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Cape Verde ili kufuzu kwa hatua ya muondoano.

    Hii leo wenyeji Morocco wanatoa na jasho na Senegal huku Kenya ikipepetana na Algeria.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Mahakama yaamuru kusitishwa kwa mpango wa kutumia mamba kuzunguka gereza la Wapalestina nchini Israel

    Mahakama ya Israeli imetoa amri ya muda ya kusimamisha mpango tata wa kutumia mamba wa mto Nile kuzunguka gereza linalowashikilia wafungwa wa Kipalestina hadi taarifa zaidi itakapotolewa, baada ya kundi la haki za wanyama kuwasilisha ombi la dharura la kuzuia mpango huo.

    Kulingana na mpango huo, ambao unaungwa mkono na Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israeli Itamar Ben-Giver, mtaro ulipaswa kuchimbwa kuzunguka moja ya malango ya usalama ya gereza la Katziut katika Jangwa la Negev na mamba wa Nile wangewekwa hapo.

    Maafisa wa Israeli wanasema lengo la hatua hii ni kuongeza hatua za usalama na kuzuia majaribio yoyote ya wafungwa kutoroka.

    Uchimbaji wa mtaro ulianza kama mwezi mmoja uliopita, lakini ripoti zinaonyesha kuwa hakuna mamba ambaye amehamishwa hadi eneo hilo. Kulingana na hati zilizochapishwa, mtaro huo utakuwa na urefu wa takriban mita 170 na unakusudiwa kuzunguka sehemu ya gereza ambalo wafungwa wa Kipalestina wanazuiliwa.

    Mpango huo umekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa makundi ya haki za binadamu na haki za wanyama tangu kutangazwa kwake.

    Mashirika ya haki za wanyama yamesema katika kesi yao kwamba kuwatumia wanyama wa porini kama walinzi wa usalama kunakiuka sheria za ustawi wa wanyama na ulinzi wa wanyamapori na kuwaweka katika hali zisizofaa.

  4. Watu wenye silaha waua 12, wateka wanawake na watoto kaskazini mwa Nigeria

    Watu waliojihami kwa silaha wamewaua takribani watu 12 na kuwateka wanawake na watoto wakati waliposhambulia kijiji kimoja katika jimbo la Sokoto kaskazini magharibi mwa Nigeria, walioshuhudia tukio hilo wanasema.

    Jamaa sita wa familia moja walifariki baada ya washambuliaji kuchoma nyumba yao. Mmoja wa wakaazi aliiambia shirika la Habari la Reuters.

    Washambuliaji waliokuwa na silaha waliingia katika kijiji cha Lajinge mwendo wa saa tano usiku siku ya Jumamosi na kuwashambulia wakazi hadi saa tisa usiku kuamkia Jumapili, wakazi walisema.

    Eneo hilo limeshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa magenge yenye silaha kali, wanaojulikana kama majambazi, ambao huvamia vijiji, kuwateka nyara wakaazi kwa lengo la kulipwa kikombozi na kuiba mifugo.

    "Waliua takriban watu 12, wakajeruhi wengine wanne, waliwateka nyara wanawake na watoto baada ya kuiba mifugo mingi," mkazi Auwal Hassan aliambia Reuters kwa njia ya simu.

    Polisi walikuwa wakichunguza na watatoa taarifa baadaye, msemaji wa kikosi cha Sokoto Ahmed Rufai alisema.

    Shambulio hilo linakuja wiki moja baada ya majambazi kuwaua wakulima wasiopungua 24 katika jimbo jirani la Zamfara.

    Soma Zaidi Hapa:

  5. Trump afungua mlango wa mazungumzo na Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema mazungumzo mapya na Iran yataanza leo Jumatatu, baada ya kusitisha kile alichosema kingekuwa mashambulizi "makubwa" dhidi ya taifa hilo.

    "Walijua ukubwa wa shambulio hilo kwa sababu walilikisia jinsi litakavyokuwa," aliwaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya Air Force One siku ya Jumapili. "Tunazungumza nao kupitia majadiliano. Mazungumzo hayo yataanza kesho alasiri," yaani leo.

    Katika mtandao wa Truth Social, rais wa Marekani alisema ameombwa na Iran na nchi nyingine za Mashariki ya Kati "kusitisha kwa muda," shambulio lolote akidai kuwa misingi ya makubaliano ilikuwa tayari imeafikiwa.

    Iran bado haijatoa jibu kwa matamshi ya Trump. Rais huyo wa Marekani amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba mwisho wa vita kupitia mazungumzo uko karibu kufikiwa, lakini mashambulizi ya kulipizana yameendelea kurejelewa.

    Akizungumza akiwa ndani ya ndege ya Air Force One, Trump alikataa kuweka muda maalum wa kufikiwa kwa makubaliano na Tehran, akisema: “Tutaona tu hali itakavyokuwa. Tuko tayari kuchukua hatua wakati wowote tutakapotaka... Sitafuti kuua watu.”

    Soma Zaidi:

  6. Hujambo na Karibu katika matangazo yetu mubashara, 03//08/2026.