Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini Saudia imekusanya nchi 14 kulinda Bahari ya Shamu?
Saudi Arabia na kwa ushirika wa nchi nyingine 13, imetangaza kuundwa kwa muungano wa kimataifa wa ulinzi wa baharini unaoongozwa na Riyadh. Maafisa wa Saudi walisema hatua hiyo inalenga kulinda usafirishaji wa kimataifa, njia za biashara na usafirishaji wa nishati dhidi ya vitisho vinavyoongezeka katika Bahari ya Shamu, Mlango bahari wa Bab al-Mandab na Ghuba ya Aden.
Muungano huo umetangazwa wakati ambapo mashambulizi na vitisho dhidi ya meli za kibiashara, meli za kubeba mafuta na miundombinu ya baharini katika eneo hilo vimeongezeka, hali inayozua wasiwasi kuhusu kuvurugika kwa mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara ya dunia.
Lakini muungano huu mpya utafanya kazi kwa namna gani? Ni nchi zipi zitashiriki? Je, utatofautianaje na vikosi na misheni za kimataifa za kijeshi za majini ambazo tayari zinafanya kazi katika eneo hilo?
Lengo la kuunda muungano huu nin lipi?
Mpango huo unalenga kuanzisha muungano wa kimataifa wa ulinzi wa baharini, ulioanzishwa, unaoongozwa na unaoratibiwa na Saudi Arabia, kwa lengo la kuimarisha usalama wa usafirishaji wa baharini katika Bahari ya Shamu, Mlango wa Bab al-Mandab na Ghuba ya Aden.
Tangazo la kuundwa kwa muungano huo lilitolewa baada ya mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia, uliowakutanisha wawakilishi kutoka nchi 43 pamoja na Umoja wa Ulaya (EU). Mwishoni mwa mkutano huo, nchi 14 zilitoa taarifa ya pamoja zikieleza kuunga mkono mradi huo.
Kwa mujibu wa Riyadh, lengo la muungano huo ni kulinda uhuru wa usafiri wa baharini, kuhakikisha usalama wa njia za biashara za kimataifa na njia za usafirishaji wa nishati, pamoja na kukabiliana na vitisho vinavyolenga meli za kibiashara, meli za kubeba mafuta, miundombinu, na maslahi ya pamoja ya baharini.
Hata hivyo, maelezo ya kiutendaji ya muungano huo bado hayajatangazwa, ikiwemo lini utaanza shughuli zake, idadi ya wanajeshi au meli zitakazoshiriki, mfumo wa uongozi na utoaji wa maamuzi, kanuni za matumizi ya nguvu, pamoja na aina ya ushiriki wa kila nchi.
Nchi zilizoanzisha muungano huo ni zipi?
Mbali na Saudi Arabia, muungano huo unajumuisha nchi nyingine 13 ambazo ni: Uturuki, Pakistan, Misri, Kuwait, Bahrain, Qatar, Jordan, Yemen, Sudan, Djibouti, Somalia, Bangladesh, na Visiwa vya Qam'ar.
Muundo wa wanachama wa muungano huo unaonesha wigo wake mpana wa kijiografia, kwani unazileta pamoja nchi za Kiarabu na za Ghuba zinazopakana na Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, pamoja na nchi za Kiislamu zenye majeshi ya wanamaji au zilizoko karibu na njia za biashara za Bahari ya Hindi.
Wawakilishi wa nchi 43 pamoja na Umoja wa Ulaya walihudhuria mkutano uliotangulia kutangazwa kwa muungano huo, lakini ni nchi 14 pekee zilizotia saini tamko la kuanzishwa kwake. Riyadh ilisema kuwa mlango utaendelea kuwa wazi kwa nchi nyingine kujiunga baada ya kukamilisha taratibu zao za ndani.
Kutokuwapo kwa Falme za Kiarabu (UAE) na Oman katika orodha ya nchi zilizoanzisha muungano huo ni jambo lililovutia. Licha ya kuwa wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) na kuwa na nafasi muhimu katika njia za usafirishaji wa baharini za eneo hilo, nchi hizo mbili bado hazijatangaza sababu zao za kutojiunga na mpango huo.
Kwa nini muungano huu unaanzishwa sasa?
Tangazo la kuundwa kwa muungano huu limekuja wakati ambapo hatari zinazotishia usafiri wa baharini katika Bahari ya Shamu, Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab, na Ghuba ya Aden zimeongezeka kufuatia kuanza tena kwa makabiliano kati ya Saudi Arabia na Wahouthi nchini Yemen.
Mnamo Julai 2026, Wahouthi walirusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea miji na vituo vya mafuta vya Saudi Arabia. Pia walilenga meli zinazohusishwa na Saudi Arabia pamoja na miundombinu ya nishati iliyoko kwenye pwani ya Bahari ya Shamu.
Kundi hilo pia lilitangaza kile lilichokiita "mzingiro wa baharini dhidi ya Saudi Arabia," likionya kuwa linaweza kuvuruga usafiri wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab.
Matukio haya yanatokea katika muktadha wa mvutano mpana wa kikanda unaohusishwa na vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran na washirika wake. Mvutano huo umeweka njia za usafirishaji wa mafuta na biashara katika Bahari ya Shamu, pamoja na maeneo ya karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz na Mfereji wa Suez, katika hatari ya kushambuliwa.
Tishio kwa Saudi Arabia halihusiani tu na usalama wake wa moja kwa moja, bali pia na ulinzi wa mauzo yake ya mafuta, bandari zake, na miradi yake ya pwani, pamoja na kuhakikisha kuwa Bahari ya Shamu inaendelea kuwa njia mbadala ya kusafirisha nishati wakati njia za Ghuba ya Uajemi zinapokumbwa na usumbufu.
Kwa hiyo, muda wa kuzinduliwa kwa mradi huu unaonekana kuhusishwa na juhudi za kuunda mwitikio ulioratibiwa zaidi katika ngazi za kikanda na kimataifa, pamoja na kugawana wajibu wa kulinda njia hizi muhimu za baharini kati ya nchi zinazokabiliwa na hatari hizo, badala ya kuacha jukumu hilo mikononi mwa majeshi ya Magharibi yaliyoko katika eneo hilo pekee.
Hata hivyo, tamko la kuanzishwa kwa muungano huo halikuwataja moja kwa moja Wahouthi wala Iran. Badala yake, lilielezea muungano huo kama mfumo wa kujihami unaolenga kulinda usafiri wa baharini, biashara, na miundombinu ya baharini dhidi ya vitisho mbalimbali.
Je, kuna muungano mwingine wa kijeshi wa wanamaji katika eneo hili?
Ndiyo. Kwa sasa kuna majeshi na misheni kadhaa za kimataifa za wanamaji zinazofanya kazi katika Bahari ya Shamu, Ghuba ya Aden, na Ghuba ya Uajemi, huku maeneo yao ya operesheni na malengo yakifanana kwa kiasi fulani na yale ya muungano mpya.
Mfano mashuhuri zaidi ni Kikosi cha Pamoja cha Usalama wa Baharini (Combined Maritime Forces – CMF), ambacho kinajumuisha nchi 47 na makao yake makuu yako Bahrain. Kikosi hiki kinaongoza vikosi vitano maalumu vya operesheni.
Miongoni mwa vikosi hivyo ni:
Kikosi Kazi cha Pamoja 153 (Combined Task Force 153 – CTF 153), chenye jukumu la kulinda usalama wa Bahari ya Shamu, Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab, na Ghuba ya Aden.
Kikosi Kazi cha Pamoja 151, kinachohusika na operesheni za kupambana na uharamia baharini.
Vikosi vingine ndani ya muungano huo vinaelekeza shughuli zao katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Arabia.
Pia chini ya mfumo huo kuna Operesheni Prosperity Guardian, iliyoanzishwa na Marekani mwezi Desemba 2023 kwa lengo la kulinda meli dhidi ya mashambulizi ya Wahouthi katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.
Aidha, Umoja wa Ulaya unaendesha Operesheni Aspides, ujumbe wa kujihami ulioanzishwa mwezi Februari 2024 kwa ajili ya kusindikiza meli za kibiashara, kutambua vitisho na kuzilinda dhidi ya mashambulizi. Operesheni hiyo imeongezewa muda hadi Februari 2027.
Vilevile, Operesheni Atalanta ya Umoja wa Ulaya inaendelea kutekelezwa kwa lengo la kupambana na uharamia na kulinda usafiri wa baharini katika maji yanayozunguka Somalia na sehemu ya magharibi ya Bahari ya Hindi.
Ni nini kinachoufanya muungano huu mpya kuwa wa kipekee?
Sifa muhimu zaidi ya muungano huu mpya ni kwamba unawasilishwa kama mfumo wa ushirikiano wa usalama wa baharini unaoongozwa na nchi ya kikanda, badala ya kuongozwa na Marekani au nchi za Ulaya. Muungano huu unalenga moja kwa moja kulinda Bahari ya Shamu, Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab, Ghuba ya Aden, pamoja na njia zinazotumika kusafirisha nishati.
Wanachama wake pia wanazijumuisha nchi za Kiarabu zinazopakana na njia hizi muhimu za baharini, kama vile Saudi Arabia, Misri, Sudan, Yemen, Djibouti na Somalia, pamoja na nchi za Kiislamu zenye uwezo mkubwa wa kijeshi baharini, kama Uturuki, Pakistan na Bangladesh.
Mchanganyiko huu unaweza kupanua wigo wa shughuli za muungano kutoka Mashariki mwa Bahari ya Mediterania na Bahari ya Shamu hadi Bahari ya Hindi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotangazwa hadi sasa, ushirikiano kati ya wanachama unatarajiwa kujumuisha kubadilishana taarifa za kiusalama, kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi baharini na operesheni za pamoja, pamoja na kulinda meli, miundombinu na maslahi ya baharini.
Muungano huu unatofautiana na baadhi ya operesheni za sasa zinazoongozwa na mataifa ya Magharibi kwa kuwa operesheni hizo ziliundwa kujibu malengo maalumu, kama vile kukabiliana na mashambulizi ya Wahouthi au kupambana na uharamia. Kwa upande wake, Saudi Arabia inauelezea muungano huu mpya kama mfumo mpana zaidi wa kujihami na wa kudumu kwa ajili ya kuratibu ushirikiano kati ya nchi wanachama.
Hata hivyo, tofauti hiyo bado ni ya kinadharia kwa kiasi kikubwa, kwani Riyadh bado haijatangaza idadi ya vikosi vitakavyotengwa kwa muungano huo, mfumo wa uongozi, kanuni za matumizi ya nguvu, wala jinsi utakavyoshirikiana na majeshi ya kimataifa ya wanamaji yanayofanya kazi katika eneo hilo.
Kwa hiyo, umuhimu halisi wa muungano huu utategemea uwezo wake wa kuvuka hatua ya kuwa tamko la kisiasa tu na kuwa kikosi kinachofanya kazi kwa vitendo, chenye uwezo wa kuratibu ushiriki wa nchi zenye uwezo na maslahi tofauti ya kiusalama.