Kwa nini udi unaochomwa majumbani ni hatari?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Koteru Sravani
    • Nafasi, BBC correspondent
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakati wa sikukuu na matukio ya baraka, watu wengi huchoma vijiti vya udi ili kutoa harufu nzuri na kuleta hali ya utulivu nyumbani.

Hasa kwa wanawake kutoka maeneo ya pwani Afrika Mashariki, hupendelea sana kutokana na mila na desturi zao.

Hata hivyo, tafiti mbalimbali za kisayansi zinaonya kwamba moshi na harufu ya udi vinaweza kusababisha matatizo ya kiafya kwa watu wengi.

Katika video ya hivi karibuni aliyoichapisha kwenye Instagram, daktari wa magonjwa ya mapafu, Sonia Goyal, alieleza madhara ya kuvuta moshi wa udi kila siku.

Aliufananisha udi na sumu inayoingia polepole kwa mapafu, akisema kuwa vichafuzi vinavyojitokeza kutokana na udi hutokana na mchakato wa kufukiza na vina madhara yanayofanana na yale ya kuvuta sigara.

Chuo cha Marekani cha Mzio, Pumu na Kinga (ACAAI) kilionya katika mkutano wake wa kisayansi uliofanyika Boston mwaka jana kwamba kuvuta moshi wa udi kunaweza kuwa hatari kwa watu wenye mzio na pumu, na pia kwa watoto na wazee. Chuo hicho kina makao yake Illinois na kina zaidi ya wataalamu 6,000 wa afya.

Kwa mujibu wa ripoti yao, kuvuta moshi wa udi kunaweza kusababisha maumivu ya kichwa, kupungua kwa ufanisi wa mfumo wa upumuaji, matatizo ya ngozi na mwitikio wa mzio.

Pia ilibainika kuwa kila gramu ya udi unaowaka hutoa takriban miligramu 45 za chembechembe (PM), ilhali sigara hutoa miligramu 10 tu. Hivyo, udi huzalisha chembechembe karibu mara nne zaidi ya sigara.

Pia, utafiti uliotajwa na Maktaba ya Kitaifa ya Tiba uligundua kuwa moshi wa vijiti vya udi unaweza kuongeza vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo na kiharusi kwa takriban asilimia 12.

''Watu wengi hawatambui kuwa udi unaweza kusababisha madhara, hasa kwa watoto'', anasema Mary Lee-Wang, mtaalamu wa mzio na mwandishi mkuu wa utafiti huo.

Shirika la ACAAI pia linatahadharisha kuwa vijiti vya udi vinaweza kuchafua hewa na hata kusababisha ajali za moto.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Vichafuzi vinavyotokana na kuchoma udi

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mujibu wa maelezo yaliyofunuliwa na Maktaba ya Kitaifa ya Dawa, hebu tuangalie uchafuzi unaotolewa na vijiti vya uvumba hapa chini.

1. Chembechembe (PM2.5)

Hizi ni chembe ndogo sana zinazoweza kupenya hadi sehemu za mwisho za mfumo wa upumuaji. Vijiti vya udi, sigara, na mishumaa ndio sababu kuu zinazohusika na kuzagaa kwa chembe majumbani.Mfiduo wake mkubwa unaweza kusababisha:

  • magonjwa sugu ya upumuaji,
  • magonjwa ya moyo,
  • uharibifu wa tishu za mapafu,
  • vifo vya mapema,
  • na kuongeza hatari ya saratani.

2. Monoksidi ya kaboni (CO)

Hutolewa wakati misombo ya kikaboni haijachomwa vizuri.Misombo hii huunda carboxyhemoglobin, kupunguza uwezo wa kubeba oksijeni ya damu.Wakati haya yanapoingia kwenye miili yetu kwa dozi ndogo, dalili kama vile, maumivu ya kichwa, kichefuchefu na uchovu, huku dozi kubwa zikiwa hatarishi kwa maisha.

3. Dioksidi ya sulfuri na dioksidi ya nitrojeni

Gesijoto hizi huweza kuzidisha magonjwa ya moyo na mapafu na kudhoofisha ulinzi wa asili wa mapafu.

4. Misombo tete ya kikaboni (VOCs)

Ni gesi zinazoachiliwa na kemikali mbalimbali kutoka kwa vifaa vya kioevu na kigumu. Huleta muwasho wa macho, pua na koo, pamoja na maumivu ya kichwa, kichefuchefu na kutapika. Mfiduo wa muda mrefu unaweza:

  • kuongeza hatari ya saratani,
  • kuathiri ini,
  • na kudhuru mfumo wa neva.

5. Aldehidi

Ni aina nyingine ya VOC inayokera sana. Husababisha muwasho mkali wa pua na koo, na kikohozi. Mfiduo mwingi wa formaldehyde pia ni wasiwasi. Inaainishwa kama kansajeni.

6. Hidrokaboni zenye pete nyingi za kunukia (PAHs)

Kemikali hizi huongeza hatari ya ugonjwa wa mishipa ya pembeni (PAD).

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Watu walio katika hatari zaidi

Watoto, wazee, watu wenye pumu na wale walio na mapafu dhaifu wako katika hatari kubwa ya kuvuta moshi wa uvumba.

Mfiduo wa muda mrefu unaweza kuongeza hatari ya kupata pumu, COPD (ugonjwa sugu wa kuziba kwa njia za hewa) na saratani ya mapafu. Hatari huongezeka zaidi ikiwa vyumba havina hewa ya kutosha.

Moshi huu unaweza pia kuathiri msimbojeni (DNA) wa binadamu.

"Hatari ya COPD ni kubwa kutokana na moshi wa udi. Ni kawaida zaidi kwa wale wanaochoma sana na kuvuta moshi. Watu ambao tayari wana pumu hupata COPD haraka. Watu wasio na pumu wana uwezekano mkubwa wa kuendeleza ugonjwa huo ndani ya miaka kumi hadi kumi na tano," alisema Dk Anudeep Pothina, mtaalamu wa mapafu katika Hospitali ya NIMS.

"Pumu ya mara kwa mara imeongezeka kwa watoto. Watoto wanapokuwa na ugonjwa huu, wanakohoa mara kwa mara. Kwa wakati huu, watoto wanapaswa kupata ushauri wa kitaalam mara moja kwa daktari wa mapafu. Watoto wanapaswa kuwekwa mbali na vitu kama moshi wa udi, vumbi na vifuniko vya mbu ambavyo vinaweza kusababisha usumbufu. Moshi kutoka kwa vijiti vya udi unaweza kusababisha usumbufu zaidi kwa watu wenye pumu. Watoto na wale walio na matatizo wanapaswa kuchukuliwa kwa uangalifu kwa sababu wanapaswa kuepushwa kwa haraka wasivute moshi wa vijiti vya udi," alipendekeza Dkt Anudeep Potina.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Ni tahadhari gani zichukuliwe?

  • Epuka kukaa kwenye moshi wa uvumba kwa muda mrefu.
  • Hakikisha madirisha yako wazi unapowasha uvumba.
  • Usichome uvumba ikiwa una watoto wadogo nyumbani.
  • Ikiwa ni lazima kuwasha, waweke watoto mbali na moshi.

Kuna vijiti vya udi vinavyodaiwa kuwa rafiki kwa mazingira, lakini madaktari wanaonya kuwa aina yoyote ya moshi inaweza kuwa na madhara.

BBC haijathibitisha kwa uhuru iwapo udi unaotangazwa kuwa wa asili au rafiki kwa mazingira hauna madhara kwa mazingira au afya.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid