Kwa nini mahasimu wa zamani Ethiopia sasa wameungana?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Vikosi vya Tigray na serikali ya shirikisho ya Ethiopia vimeanza tena kupigana, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kwa kuanzisha mashambulizi.

Hali hiyo imeibua hofu ya kurejea kwa vita vikubwa vilivyomalizika kwa makubaliano ya amani mwaka 2022.

Kwa miaka kadhaa, makundi yenye silaha nchini Ethiopia yamekuwa yakipigana katika maeneo tofauti ya nchi. Lakini sasa, baadhi ya makundi hayo ambayo yalikuwa maadui yameamua kuweka tofauti zao pembeni na kuungana dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Makundi hayo saba yameunda muungano wanaouita "Alliance for Survival", wakisema wanataka kushirikiana katika kuikabili serikali na kushinikiza mabadiliko ya kisiasa nchini Ethiopia.

Miongoni mwa makundi yaliyojiunga na muungano huo ni Tigray People's Liberation Front, TPLF, Oromo Liberation Army, pamoja na wapiganaji wa Amhara Fano. Makundi mengine manne yanatoka katika maeneo ya Afar, Somali na Benishangul-Gumuz.

Hii ni hatua kubwa kwa sababu baadhi ya makundi haya si wageni kwenye mapigano dhidi ya kila mmoja. Wakati wa vita vya Tigray, kwa mfano, wapiganaji wa Fano walipigana pamoja na serikali ya Ethiopia dhidi ya TPLF. Kwa hiyo, watu ambao wakati mmoja walikuwa wanakabiliana kwenye uwanja wa vita sasa wamekaa upande mmoja.

Muungano huo unasema Ethiopia inakabiliwa na matatizo makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama. Wanaituhumu serikali ya Abiy Ahmed kwa kushindwa kuleta amani ya kudumu na kuwalinda raia.

Kwa nini wameungana sasa?

Kwa mujibu wa muungano huo, lengo lao ni kuiondoa serikali ya Abiy Ahmed, kuunda serikali ya mpito na kuanza mchakato mpya wa kuandika katiba ya nchi.

Hatua hii imekuja wakati hali ya usalama nchini Ethiopia ikizidi kuwa ya wasiwasi, huku mvutano ukiongezeka tena katika eneo la Tigray. Hali hiyo imeibua hofu kwamba migogoro inaweza kuenea zaidi na kuvuruga maeneo mengine ya nchi.

Kwa makundi haya, kuungana kunaonekana kama njia ya kuwa na nguvu zaidi kuliko kila kundi kupigana kivyake. Pia yameomba uungwaji mkono kutoka kwa Waethiopia, jeshi, nchi jirani na jumuiya ya kimataifa.

Lakini kuna changamoto kubwa mbele yao. Makundi haya yana historia tofauti, yana malengo na vipaumbele tofauti, na baadhi yao yamewahi kupigana yenyewe kwa yenyewe.

Nini kinaendelea?

Jumapili, TPLF, chama tawala Tigray, ilitangaza kuunda muungano na makundi mengine sita yenye silaha kwa lengo la kuipinga serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Siku zilizofuata, mvutano uliongezeka. Mamlaka za Tigray zilisema vikosi vyao vililazimika kujihami baada ya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.

Jumanne, shambulio la anga mjini Alamata liliua watu wasiopungua 14 na kujeruhi 22, kwa mujibu wa mamlaka za Tigray. Meya wa mji huo alidai shule mbili zililengwa, lakini BBC haijaweza kuthibitisha madai hayo kwa kujitegemea.

Wakati huo huo, serikali ya Ethiopia imetuhumu TPLF kuanzisha "mashambulizi makubwa" katika maeneo ya Afar na Amhara.

Wakazi wa Mekelle baadaye waliiambia BBC kuwa vikosi vya Tigray vilichukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa mji huo, hatua iliyofuatwa na Ethiopian Airlines kusitisha safari zote za ndege kwenda Tigray.

Mamlaka za Tigray zinasema vikosi vyao vinapigana kwa kujihami dhidi ya mashambulizi ya serikali ya shirikisho. Kauli hiyo ilitolewa baada ya kuripotiwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani huko Tigray.

Lakini serikali ya Ethiopia inatoa picha tofauti. Getachew Reda, aliyekuwa kiongozi wa Tigray na ambaye sasa ni mshauri wa serikali ya shirikisho, amesema viongozi wa Tigray wameanzisha "mashambulizi makubwa" dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na serikali katika majimbo ya Afar na Amhara.

Rais wa Ethiopia, Taye Atske-Selassie, pia ameitaka dunia kutambua kile alichokiita uvumilivu mkubwa ambao serikali yake imeonyesha licha ya, kwa mujibu wake, kuingiliwa kutoka nje.

Kwa nini mapigano mapya yanatia hofu?

Tigray ilikumbwa na vita vya miaka miwili kati ya 2020 na 2022. Mzozo huo ulisababisha vifo vya watu wengi na mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Mpatanishi wa Umoja wa Afrika alikadiria kuwa karibu watu 600,000 walifariki katika mzozo huo, uliosababisha eneo hilo kuingia katika hali mbaya ya kibinadamu inayokaribia kuwa janga la njaa.

Vita vilimalizika baada ya pande hizo kusaini makubaliano ya amani ya Pretoria mwezi Novemba 2022, yaliyosaidia kusitisha mapigano.

Hata hivyo, tangu wakati huo, serikali ya Ethiopia na viongozi wa Tigray wamekuwa wakituhumiana mara kwa mara kwa kukiuka makubaliano hayo.

Sasa, mapigano mapya yanaibua hofu kwamba amani hiyo inaweza kuvunjika kabisa.

"Jambo hili limeathiri vibaya kisaikolojia mji wetu, na watu wetu wako katika hali ya hofu," Meya wa mji huo, Mogos Shiferaw ameiambia BBC.

Marekani na Umoja wa Afrika wanasema nini?

Marekani imechukua msimamo mkali zaidi kuhusu mzozo huo. Balozi wa Marekani nchini Ethiopia, Ervin Massinga, amewatuhumu viongozi wa Tigray kwa kuanzisha mashambulizi makubwa na kuonya kuwa Washington ina "zana za kuwawekea vikwazo viongozi zaidi" watakaohusika katika kuongeza mzozo.

Hata hivyo, Umoja wa Afrika (AU) umetaka pande zote zionyeshe "uvumilivu wa hali ya juu" na kuchukua hatua za haraka kupunguza mvutano kaskazini mwa Ethiopia.

Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahmoud Ali Youssouf, amemtaka Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, kuingilia kati haraka na kufufua mazungumzo chini ya mfumo wa makubaliano ya Pretoria.

AU pia imezitaka nchi jirani na Ethiopia kutochukua hatua zinazoweza kuongeza mzozo.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya (EU) umesema "una wasiwasi mkubwa" kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya kwa kasi, ikiwemo shughuli za kijeshi na kutwaliwa kwa viwanja vya ndege, na umetaka hatua za haraka za kupunguza mvutano.

Athari zimeanza kuonekana

Baada ya viwanja vya ndege kutwaliwa, shirika la ndege la Ethiopian Airlines imesitisha safari zote za ndege kwenda Tigray.

Nchi kadhaa pia zimetoa tahadhari za usafiri kutokana na hali ya usalama.

Ubalozi wa Marekani mjini Addis Ababa umetoa tahadhari ya kiusalama ukiwataka raia wake walioko maeneo hayo kuwa waangalifu.

Wakati huo huo, Ofisi ya Uingereza ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo imeendelea na tahadhari kali za usafiri kwa baadhi ya maeneo ya Ethiopia,

Kuna pia taarifa za mapigano katika maeneo ya Amhara na Afar, jambo linalozua hofu kwamba mzozo unaweza kuenea zaidi na kuhusisha maeneo na makundi mengi.

Mzozo huo mpya umeibuka wakati uongozi wa Tigray ukitangaza kujiunga na muungano wa makundi mengine sita yenye silaha kwa lengo la kuipindua serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Kwa nini Ethiopia imetofautiana na Eritrea?

Majirani hao wawili kwa muda mrefu wamekuwa na uhusiano tete - kubadilika kutoka kuwa marafiki hadi maadui.

Eritrea ilijitenga rasmi na Ethiopia mwaka 1993 - lakini baadaye ikapigana vita vikali vya mpakani.

Kwa kweli, Abiy alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel mnamo 2019 kwa kumaliza mzozo wa kijeshi wa miaka 20 na Eritrea.

Lakini uhusiano wa kirafiki ulioanzishwa zaidi wakati wa vita vya Tigray umetoa nafasi kwa vita vya maneno juu ya Bahari ya Shamu.

Hii ni kwa sababu Ethiopia, taifa lenye watu wengi zaidi duniani ambalo halina bandari, lilipoteza bandari zake za Bahari Nyekundu wakati Eritrea ilipopata uhuru wake - ikichukua pamoja na ukanda wa pwani wa kilomita 1,350 (maili 840).

Kwa Abiy huu umekuwa mzozo uliopo na amekuwa akishinikiza umiliki wa bandari ya kusini mwa Eritrea ya Assab - takriban kilomita 60 kutoka mpakani - na kuashiria hamu ya kuichukua kwa nguvu.

"Bahari Nyekundu na Ethiopia haziwezi kubaki kutengana milele," Abiy alisema wakati wa hotuba ya bunge hivi majuzi.

Je, mzozo unaweza kuwa mkubwa zaidi?

Hilo ndilo linalotia wasiwasi zaidi kwa sasa.

Eritrea, ambayo inapakana na Tigray kaskazini. Vikosi vyake vilipigana pamoja na jeshi la Ethiopia kwa ajili ya kudhibiti eneo hilo

Amhara, eneo ambalo jirani na Tigray upande wa magharibi na wapiganaji wake pia walipigana upande wa jeshi la Ethiopia. Katika wiki za mwanzo za vita walinyakua ardhi katika eneo lenye utajiri mkubwa wa kilimo la Tigray magharibi, ambalo bado ni chanzo cha mzozo.

Serikali ya Ethiopia imetofautiana tangu wakati huo na mshirika wake wa zamani Eritrea na wanamgambo wenye silaha kutoka Amhara.

Yote yamesababisha kutoaminiana na kumaanisha kuwa makubaliano ya Pretoria yanasambaratika haraka.

Kwa sasa, Uongozi wa Tigray umetangaza kujiunga na muungano wa makundi mengine sita yenye silaha, yanayolenga kuipinga serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Kwa hiyo, muungano huu unaweza kubadilisha kabisa mazingira ya kisiasa na kiusalama nchini Ethiopia, lakini bado haijulikani kama mahasimu hawa wa zamani wataweza kudumu pamoja kwa muda mrefu, au kama kitu pekee kinachowaunganisha kwa sasa ni kuwa na mpinzani mmoja wa pamoja.