Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mnyama aliyeishi miaka milioni 240 Iliyopita agunduliwa Tanzania
Wanasayansi wamegundua spishi mpya ya mnyama wa kale aliyeishi takribani miaka milioni 240 iliyopita.
Kiumbe huyo aliyekula mimea, aliyepewa jina la Dinodontosaurus isiyavamanda, aligunduliwa katika eneo ambalo sasa ni Tanzania, Afrika Mashariki.
Kilichowashangaza watafiti ni kwamba hapo awali mabaki ya visukuku vya Dinodontosaurus yalikuwa yamepatikana Amerika Kusini pekee.
Wataalamu wanasema ugunduzi huo unaweza kuwasaidia kuelewa vizuri zaidi ni lini na wapi dinosaria walitokea kwa mara ya kwanza duniani.
End of Unaweza kusoma
Wanasayansi waligundua nini?
Utafiti huo uliongozwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Bristol, ambao walichunguza kwa undani zaidi visukuku vilivyokusanywa nchini Tanzania zaidi ya miaka 60 iliyopita.
Wanasayansi walichunguza mabaki hayo, yaliyohifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Historia ya Asili huko London, na kugundua kwamba yalikuwa ya aina ya kiumbe aliyekula mimea aitwaye dicynodont.
Kwa usahihi zaidi, mabaki hayo yalikuwa ya Dinodontosaurus, aina ya kiumbe wa kabla ya historia ambaye hapo awali alikuwa amepatikana Amerika Kusini pekee.
Uchunguzi zaidi ulionesha kwamba visukuku vya Tanzania vilikuwa vya spishi ambayo haikuwahi kujulikana hapo awali, ambayo watafiti waliipa jina Dinodontosaurus isiyavamanda.
Wataalamu wanasema ugunduzi huo ni muhimu kwa sababu miamba ambako Dinodontosaurus alipatikana pia imetoa baadhi ya visukuku vya kale zaidi vinavyodhaniwa kuwa vya dinosaria.
Kwa kuwa sasa Dinodontosaurus amepatikana Tanzania na Amerika Kusini, wanasayansi waliweza kubaini kwamba miamba yenye visukuku hivyo ina takribani umri sawa.
Mwandishi mkuu wa utafiti huo, Hady George, kutoka Chuo Kikuu cha Bristol, alieleza: "Hili linasaidia kuthibitisha kwamba visukuku vya kale zaidi vinavyodhaniwa kuwa vya dinosaria kutoka Tanzania huenda si vya zamani zaidi kuliko vile vya Amerika Kusini, hivyo kuboresha uelewa wetu wa ratiba ya asili ya dinosaria."
Timu hiyo iliongeza kwamba, kutokana na ugunduzi huo, huenda wanasayansi wakahitaji kutathmini upya ni lini na wapi dinosaria walianza kutokea.