Viza ya kiongozi wa kijeshi wa Sudan yakataliwa na Marekani, akitarajiwa kuhutubia mkutano wa UN
Marekani imezuia viza ya mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, kabla ya ziara yake iliyopangwa ya Umoja wa Mataifa (UN), katika hatua ambayo vyanzo vya Sudan na vingine vinasema inahusishwa na pendekezo la kusitisha mapigano linaloungwa mkono na Marekani ambalo Khartoum imekataa.
Kulingana na shirika la habari la Reuters, hatua hiyo inatishia kuongeza mvutano kati ya Washington na jeshi la Sudan wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea, vita ambavyo Umoja wa Mataifa unavitaja kuwa miongoni mwa migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani.
Chanzo kimoja cha ngazi ya juu nchini Sudan kimesema Burhan ameahirisha safari yake kwenda New York, lakini bado hajapokea taarifa rasmi kwamba viza yake imekataliwa.
“Serikali ya Sudan inaelezea masikitiko yake makubwa, kwa sababu hii ni ukiukaji wa Mkataba wa UN na sheria za kimataifa,serikali ya Sudan iko tayari kwa amani” chanzo hicho kilisema
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, amemwomba Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, kuingilia kati, akisema kupitia barua kwamba kumzuia Burhan kuhudhuria mkutano mkuu wa UN kutakiuka wajibu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi wanachama.
Kwa mujibu wa chanzo cha kidiplomasia cha Sudan ameiambia Reuters kuwa, maafisa wa Marekani wameweka sharti la Burhan kuhudhuria mkutano huo, ni lazima akubali kusitisha mapigano kwa siku 90, kama ilivyopendekezwa na Mshauri Mkuu wa Marekani anayehusika na Masuala ya Waarabu na Afrika, Massad Boulos.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilikataa kutoa maoni kuhusu viza ya Burhan.
Msemaji wa Wizara hiyo, Tommy Pigott, alisema katika taarifa baadaye kuwa Jeshi la Sudan (SAF), kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF), na viongozi wao “hawawakilishi utawala halali wa kikatiba nchini Sudan.”
“Serikali ya Marekani na Rais Trump wako tayari kufanya kazi na yeyote aliye mshirika wa dhati katika juhudi za kuleta amani nchini Sudan.”
Mvutano huo unaashiria kudorora kwa uhusiano kati ya sudan na Marekani, tangu kuzuka kwa vita nchini humo mwezi Aprili 2023.
Burhan alikuwa anatarajiwa kuhutubia Mkutano Mkuu wa UN hii leo, ila hotuba hiyo itatolewa na Waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan, Mohieldin Salem.
Soma pia: