Nani humlinda Putin? Siri ya ulinzi mkali wa rais wa Urusi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alitembelea India kuhudhuria Mkutano wa 18 wa BRICS uliofanyika katika kituo cha Bharat Mandapam mjini New Delhi, Septemba 12 na 13.

Ziara hiyo ilikuwa ya pili kwa Putin nchini India tangu Desemba mwaka uliopita, alipokwenda kwa ziara ya pande mbili baada ya kutofika nchini humo kwa miaka minne.

Akiwa India, Putin alifanya mazungumzo ya pande mbili na Waziri Mkuu Narendra Modi, ambapo walijadili masuala mbalimbali kuhusu uhusiano kati ya Urusi na India.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alisema kabla ya ziara hiyo kwamba baadhi ya masuala kati ya viongozi hao yalijadiliwa kwa siri kutokana na kile alichodai kuwa ni juhudi za baadhi ya nchi kuzuia ushirikiano kati ya Urusi na India.

"Baadhi ya masuala hayawezi kujadiliwa hadharani kwa sababu kuna nchi zinazojaribu kuzuia maendeleo ya ushirikiano kati ya Urusi na India. Kwa hiyo, masuala hayo hujadiliwa kwa njia ya siri, lakini yenye ufanisi na matokeo," alisema Peskov.

Mamia ya walinzi hufuatilia kila hatua ya Putin

Putin, ambaye sasa ana umri wa miaka 73, amekuwa madarakani tangu mwaka 2000, na hivyo kuwa kiongozi wa Kremlin aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi tangu Joseph Stalin. Kwa sasa yuko katika muhula wake wa tano kama rais.

Upinzani nchini Urusi hauna nguvu kubwa ya kumzuia, na iwapo ataamua kuendelea madarakani, huenda akabaki hadi mwaka 2036.

Kuhusu usalama wake, mamia ya walinzi hufuatilia kwa karibu kila hatua yake na kuwa naye saa 24 kwa siku.

Kwa mujibu wa ripoti ya BBC News, chakula cha Putin huandaliwa kwa usiri mkubwa, huku kila kinywaji anachokunywa kikichunguzwa na washauri wake wa karibu.

Putin, ambaye zamani alikuwa afisa wa KGB, anafahamu vyema hatari zinazomzunguka.

Nani humlinda Putin?

Miongoni mwa taasisi za usalama za Urusi, kuna chombo maalumu kinachohusika na kumlinda rais na familia yake, kinachojulikana kama Huduma ya Usalama ya Rais wa Urusi, SBP.

Chombo hicho kiko chini ya Huduma ya Ulinzi ya Shirikisho la Urusi, FSO, ambayo ilianzishwa kutokana na taasisi ya ujasusi ya KGB.

Walinzi wa SBP, waliovalia suti nyeusi na wakiwa na vifaa vya mawasiliano, huwa pamoja na Putin mchana na usiku kama kivuli chake.

Kwa mujibu wa chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali ya Urusi, Russia Beyond, walinzi wanaoambatana na Putin katika ziara za nje hugawanywa katika makundi manne ya ulinzi.

''Safu ya kwanza ya ulinzi ni walinzi wake binafsi.''

''Safu ya pili ni walinzi ambao kwa kawaida watu hawawezi kuwatambua kwa urahisi.''

''Safu ya tatu huwekwa kuzunguka umati wa watu ili kuzuia watu wanaotia shaka kumsogelea.''

''Safu ya nne, iliyo mbali zaidi, inahusisha wapiga risasi wanaowekwa juu ya paa za majengo yanayozunguka eneo analokuwapo.''

Mark Galeotti, mtaalamu wa mfumo wa usalama wa Urusi na mkurugenzi wa Mayak Intelligence, kampuni inayochambua masuala ya usalama nchini humo, amesema Putin hapendi kusafiri kwa helikopta.

Kwa kawaida husafiri katika msafara mkubwa unaojumuisha pikipiki, magari mengi makubwa meusi na magari mengine yenye ulinzi mkali. Wakati wa safari zake, mara nyingi ndege zisizo na rubani hupigwa marufuku kuruka katika anga hilo na usafiri mwingine husimamishwa.

Jeshi 'maalumu' la rais

Huduma ya Usalama ya Rais wa Urusi, SBP, huungwa mkono na Walinzi wa Kitaifa wa Urusi, Rosgvardia. Baadhi ya watu hulitaja jeshi hilo kama kikosi maalumu cha rais.

Kikosi hicho ni tofauti na Majeshi ya Urusi. Kazi zake rasmi ni kulinda mipaka ya nchi, kupambana na ugaidi na kudumisha sheria na utulivu wa umma.

Hata hivyo, kwa uhalisia, moja ya majukumu yake muhimu zaidi yanatajwa kuwa kumlinda Putin dhidi ya vitisho mbalimbali.

Stephen Hall, mtaalamu wa Urusi katika Chuo Kikuu cha Bath nchini Uingereza, amesema inafahamika kuwa Walinzi wa Kitaifa wa Urusi kwa kiasi kikubwa ni walinzi binafsi wa Putin, na rais huyo yuko katika mazingira yenye ulinzi mkali pamoja na taasisi nyingine za usalama.

Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya wanajeshi katika kikosi hicho imeongezwa hadi 400,000.

Hall amesema hiyo ni idadi kubwa sana, akibainisha kuwa hata idadi ya walinzi katika mfumo wa usalama wa rais wa Marekani haifikii kiwango hicho.

Usalama wa Putin unasimamiwaje?

Ni vigumu kufahamu kwa undani jinsi hatua za usalama za Putin zinavyotekelezwa na kwa kiwango gani. Hata hivyo, Kremlin na wataalamu wa usalama nchini Urusi wametoa baadhi ya taarifa.

Katika mfumo wa usalama wa Putin, tahadhari kubwa zaidi huchukuliwa kuhusu chakula na vinywaji vyake.

Galeotti amesema kwa sababu ya hofu ya kupewa sumu, Putin ana mtu maalumu anayekionja chakula chake kwanza ili kuhakikisha kuwa ni salama.

Aliambia BBC Mundo, ''mfumo huo unafanana zaidi na ule wa mfalme wa zama za kale kuliko rais wa kisasa''.

Aidha, Putin anaposafiri nje ya Urusi, timu yake ya usalama hukagua kila kitu anachotumia.

Galeotti amesema ''kila kitu anachokula au kunywa huletwa na timu yake. Kwa mfano, katika hafla rasmi ambako divai inatolewa, Putin hunywa tu kutoka kwenye chupa iliyoletwa na timu yake, na si kwenye chupa nyingine.''

Matumizi ya simu janja hayapo

Hatua nyingine muhimu katika usalama wa Putin ni kuzuia matumizi ya simu janja ndani ya Kremlin.

Putin mwenyewe aliwahi kusema kuwa hatumii simu janja. Alisema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Urusi, TASS, mwaka 2020.

Alisema ana laini maalumu ya simu ya kikazi ambayo inaweza kupigiwa iwapo mtu anahitaji kuwasiliana naye.

Washauri wake wamethibitisha hilo. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amekuwa akisema mara kwa mara kuwa Putin hatumii simu ya mkononi kwa sababu hana muda wa kufanya hivyo.

Hata hivyo, sababu nyingine inayotajwa ni kwamba Putin haamini intaneti.

Aliwahi kumtaja kwa njia isiyo ya moja kwa moja mtandao kama CIA, shirika la ujasusi la Marekani.

Pia amewahi kuwahimiza raia wa Urusi kutotumia Google Search, akiamini kuwa taarifa zote hukusanywa na Marekani.

Galeotti amesema Putin hutumia intaneti mara chache. Anafahamika kwa kutopenda simu na ni mtu anayezingatia sana usalama, kwa kuwa simu janja si salama vya kutosha.

Kwa mujibu wa wataalamu, Putin hupokea taarifa katika mafaili ya karatasi na kuyawasilisha kwa washauri wake.

Hall amesema Putin huanza siku yake kwa taarifa tatu za kiusalama. Ya kwanza inahusu hali ya dunia, ya pili mambo yanayoendelea ndani ya Urusi, na ya tatu inahusu mambo yanayoendelea katika ngazi ya juu kabisa ya uongozi wa nchi.

Amesema taarifa hizo ndizo muhimu zaidi kwake na huamua hatua atakazochukua siku hiyo.

Hall ameongeza kuwa ''aliwahi kuzungumza na wanadiplomasia na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ambao walimweleza kuwa wanapokuwa na taarifa ambazo mashirika yao ya ujasusi yanaona si sahihi, Putin huamini taarifa kutoka kwa wapelelezi wake na kuwaona wanadiplomasia kuwa ndio wenye makosa.''