Kwa nini China inawawinda waandishi vijana wa taarifa za Mapenzi ya jinsia moja?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Mwanamke aliyekamatwa nchini China kwa kuchapisha taarifa za mapenzi ya watu wa jinsia moja anasema, "Nilionywa nisizungumzie suala hilo," kabla ya kuelezea kilichojiri siku aliyokamatwa.

Anaandika kuwa hatasahau kamwe siku aliyokamatwa, siku aliyopelekwa kwenye gari la polisi mbele ya watu, kulazimishwa kuvua nguo zote ili kukaguliwa mbele ya watu asiowajua, na kulazimishwa kukaa kwenye kiti huku akitetemeka kwa hofu ili kupigwa picha ya kukamtwa kwake.

Akaunti ya mitandao ya kijamii iitwayo "Pingping An'an Yongfu" ni mojawapo ya takriban akaunti nane ambazo wamiliki wake wameripoti kukamatwa, kupitia Weibo, jukwaa la mitandao ya kijamii la China, katika miezi ya hivi karibuni kwa kuchapisha hadithi za mapenzi ya watu wa jinsia moja.

Baada ya simulizi za waandishi hawa kuhusu uzoefu wao kuchapishwa, mawakili kadhaa wamejitokeza na kueleza utayari wao wa kuwapa huduma za kisheria bila malipo.

Kwa mujibu wa wakili anayemwakilisha mmoja wa waandishi hao, takriban waandishi 30, karibu wote wakiwa wanawake wenye umri wa miaka ya ishirini, wamekamatwa kote nchini.

Wengi wao wameachiwa kwa dhamana huku wengine wakisubiri kesi zao kusikilizwa, lakini baadhi wakizuiliwa kizuizini. Wakili mmoja aliambia BBC kuwa watumiaji wengine wengi pia wameitwa ili kuhojiwa.

Waandishi hao walikuwa wamechapisha kazi zao katika Haitang Literature City, mtandao wa Taiwan unaojulikana kwa kuchapisha "danmei"aina ya fasihi ya kubuni inayolenga mahusiano ya kimapenzi na ya karibu kati ya wanaume, na ambayo kwa kawaida huwekwa katika mazingira ya kihistoria, njozi, au hadithi za kisayansi. Aina hiyo ya fasihi imejijengea kundi la mashabiki waaminifu kwa miaka mingi, hasa miongoni mwa wanawake vijana wa China.

.

Chanzo cha picha, X / errslance

Waandishi hao wanashutumiwa kwa kukiuka Sheria ya Kupinga Ponografia ya China kwa "kutengeneza na kuchapisha maudhui machafu."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Chini ya sheria hiyo, waandishi wanaopata pesa kutokana na kuchapisha kazi zao wanaweza kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 10 jela.

Sheria hiyo inalenga hasa "maelezo dhahiri ya mahusiano ya kingono ya jinsia moja au tabia zingine zinazochukuliwa kuwa ni tofauti za kingono chini ya sheria ya China."

Kwa upande mwingine, kazi zinazoangazia mahusiano ya jinsia moja kwa ujumla hazina vikwazo vingi.

Kwa mfano, kazi za baadhi ya waandishi mashuhuri wa China, akiwemo mshindi wa Tuzo ya Nobel Mo Yan, zina maudhui ya kingono waziwazi, lakini bado zinapatikana kwa wasomaji wengi.

Ingawa waandishi wa kazi za fasihi ya ngono zinazohusu mahusiano ya jinsia tofauti, pia wamewahi kuhukumiwa kifungo gerezani nchini China, wachunguzi wanasema aina hiyo ya fasihi inakabiliwa na vikwazo na udhibiti mdogo zaidi.

Wale walioripoti kukamatwa kwao walikataa kuzungumza na vyombo vya habari, wakihofia madhara. Polisi katika mji wa kaskazini magharibi wa Lanzhou,mji unaotuhumiwa kuhusika na wimbi hilo la ukamataji, hawakujibu ombi la BBC la kutaka maoni yao.

Wimbi hili la hatua kali limeibua mjadala mpana na, wakati huo huo, limesababisha mojawapo ya maandamano adimu dhidi ya sheria hiyo.

Mtumiaji mmoja wa mtandao wa Weibo aliuliza, "Je, tunapaswa kuona aibu kuhusu ngono?" Alisema kuwa sheria za China kuhusu ponografia haziendani na uhalisia wa sasa.

Mtumiaji mwingine aliandika kuwa wanawake hawana nafasi ya kuamua wenyewe ni nini kinachochukuliwa kuwa ponografia, kwa sababu ufafanuzi wa kawaida na ule unaotawala huamuliwa na watu wengine.

Baadhi ya wanasheria wameelezea wasiwasi wao kwamba ikiwa maudhui yataonekana kuwa "machafu", hata watu 5,000 kuyatazama tu kunaweza kuchukuliwa kuwa uhalifu wa "kusambaza" maudhui hayo; jambo ambalo wanasema limepunguza kwa kiasi kikubwa kigezo kinachotumika kuwakamata watayarishaji wa maudhui.

Hali hiyo imeitia wasiwasi serikali ya China, kiasi kwamba mijadala hiyo imetoweka ghafla kwenye mitandao ya kijamii. Hashtag ya "Wakamateni waandishi wa Haitang" kwenye Weibo ilikuwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 30 kabla ya kudhibitiwa.

Machapisho yaliyokuwa na ushauri wa kisheria pamoja na ripoti kutoka tovuti maarufu ya habari ya China yalifutwa, na akaunti za waandishi hao, pamoja na akaunti nyingine kadhaa, zilifungwa pia.

Baada ya chapisho la "Pingping An Yongfu" kusambaa kwa kasi, alilifuta na kuwashukuru wale waliomuunga mkono kupitia chapisho jingine.

Pia alikiri kuwa machapisho yake yalikiuka sheria za China. Muda mfupi baadaye, alifuta akaunti yake.

Kabla ya chapisho hilo la mwisho, akaunti hiyo ilikuwa imeandika,"Siku zote nilikuwa binti mwema machoni pa wazazi wangu. Lakini siku hiyo, niliwafanya waone aibu. Hawataweza tena kutembea wakiwa wameinua vichwa vyao kwa fahari."

Na kipengele hiki kimekuwa sehemu ya utambulisho wa mtandao wa Haitang, jina ambalo katika lugha ya Kichina ya Mandarin linamaanisha "ua linalochanua katika vivuli vyote vya rangi ya waridi."

Haitang na *danmei* zimekuwa nafasi zinazotawaliwa zaidi na wanawake, ingawa taarifa zake hujikita kwa wahusika wa kiume.

Katika utamaduni ambapo namna wanawake wanavyoonyesha hisia zao za kimapenzi mara nyingi hufuatiliwa kwa karibu na kudhibitiwa, *danmei* imekuwa njia ya ubunifu na isiyo ya moja kwa moja ya kuonyesha hisia hizo, ni nafasi ambapo wanawake wanaweza kuandika kuhusu matamanio na hisia zao kwa wanawake wengine.

Liang Ge, profesa wa sosholojia ya kidijitali katika Chuo Kikuu cha London (UCL), anasema hili ndilo linalofanya *danmei* kuvunja kanuni zilizopo.

Aina hii ya fasihi, anasema, inawawezesha wanawake "kujitenga na uhalisia wa majukumu ya kijinsia" ambayo wengi wao huyahusisha na matarajio kama vile ndoa na uzazi.

Kwa mfano, katika taarifa za mtindo wa *danmei*, wanaume wanaweza kupata mimba na kukabiliana vyema na hali ya udhaifu, jambo linalotofautiana sana na mahusiano yasiyo na usawa ambayo wanawake wengi wa China hukabiliana nayo katika maisha halisi.

"Danmei inanikomboa kutoka katika mawazo ya hatari yote yanayoweza kuwepo katika mahusiano ya kimapenzi ya kawaida kati ya wanaume na wanawake," anaeleza Li Shen, mwandishi ambaye amekuwa akishiriki kikamilifu katika ulimwengu wa *danmei* kwa zaidi ya muongo mmoja.

Hata hivyo, riwaya za *danmei* zina wakosoaji wake, kwani baadhi yake huwa na matukio ya vurugu kali au yaliyopitiliza. "Kama wazazi, ni wangapi kati yetu wanaoweza kukubali watoto wao kusoma taarifa kama hizo, achilia mbali sisi wenyewe kuziandika?" aliandika mtumiaji mmoja wa mtandao wa Weibo.

Umri wa waandishi pia umekuwa suala la wasiwasi. Watu kadhaa waliozungumza na BBC walisema walianza kusoma na kuandika taarifa za ngono zinazohusu mahusiano ya watu wa jinsia moja, kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, baadhi wakiwa na umri mdogo wa miaka 11.

"Ma," mwandishi wa *danmei* ambaye alitaja jina lake la ukoo pekee, anasema jamii ya waandishi wa aina hii, anasema wanahitaji kulikubali suala hili na kutafuta suluhisho. Anaongeza kuwa hii ni changamoto isiyoishia kwenye *danmei* pekee, bali inawakabili waundaji wa aina zote za maudhui ya watu wazima, kwani hakuna vikwazo maalum vya umri au mifumo ya uainishaji wa maudhui nchini China.

Hata hivyo, *danmei* imekabiliwa na shinikizo kubwa katika muongo uliopita, huku China ikianzisha mfululizo wa kampeni za "kusafisha" mtandao.

Mnamo mwaka wa 2018, mwandishi wa *Danmei* alihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kuuza nakala 7,000 za riwaya yake, "Conquest."

Mapato yaliyokuwa ushahidi wa uhalifu wangu

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kulingana na Liang Ge, wakati viwango vya ndoa na uzazi nchini China vikishuka na Xi Jinping akijaribu kuendeleza mpango wa "ufufuaji wa taifa," serikali imeongeza ukali wa hatua zake dhidi ya *Danmei*.

"Serikali ya China inataka kukuza maadili ya jadi ya familia, na hamu ya kusoma riwaya za *danmei* inaonekana kuwa sababu inayopunguza nia ya wanawake kupata watoto," alieleza.

Hii ni wimbi la pili la ukamataji wa watu wengi ndani ya kipindi cha chini ya miezi 12. Mwishoni mwa mwaka jana, waandishi 50 walifikishwa mahakamani. Mwandishi mmoja maarufu, ambaye alikuwa amejipatia takriban yuan milioni 1.85, alihukumiwa kifungo cha karibu miaka mitano gerezani.

"Lakini safari hii, hata wale waliohusika kwa kiasi kidogo hawakuachwa salama," alisema wakili mmoja.

"Ndani ya siku mbili tu, zaidi ya watu 150 waliomba ushauri," alisema wakili anayetoa ushauri bure.

Wengi wao walikuwa bado hawajafunguliwa mashtaka rasmi, lakini waliingiwa na hofu kubwa kutokana na uwezekano huo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

"Hii ni hali halisi ya 'kuvua samaki katika maji ya mbali,'" anasema wakili ambaye ameandaa "mwongozo wa kivitendo" kuwasaidia waandishi wa aina ya *Danmei*.

Nchini China, msemo wa "kuvua samaki katika maji ya mbali" hutumika kuelezea matukio ambapo polisi wa eneo fulani hufanya kazi nje ya mamlaka yao ya kisheria. Wakosoaji wanasema polisi wa jiji la Lanzhou waliwaita waandishi wanaoishi sehemu mbalimbali za nchi, hatua ambayo wanaamini huenda ilikuwa nje ya mamlaka ya kisheria ya chombo hicho.

Waandishi wa *Danmei* wanafahamu vyema kwamba nafasi ya kuvumiliwa kwa kazi zao inaweza kupungua wakati wowote. Kwa sababu hiyo, wameamua kutumia sitiari na lugha ya mafumbo ili kukwepa udhibiti wa maudhui.

Hata hivyo, ukali wa hatua hizo uliwashangaza wengi. Mwandishi mmoja alielezea wito huo wa polisi kama "simu iliyovunja ndoto zangu."

Wanawashutumu polisi kwa kupekua simu zao za mkononi bila kibali cha mahakama. Pia wanasema kuwa mamlaka zilijumlisha idadi ya mara ambazo kila sura ya kazi zao ilitazamwa ili kupima ukubwa wa "uhalifu" huo; mbinu ambayo wanasema inapotosha kwa sababu inaelekea kuonyesha idadi kubwa zaidi ya wasomaji kuliko uhalisia.

Mwandishi mwingine wa *Danmei* aliandika,"Niliandika kwa miaka mingi kwenye jukwaa la Haitang, na ni watu wachache tu waliosoma kazi zangu. Lakini hadithi ambazo hakuna aliyezijali zilitazamwa zaidi ya mara 300,000 kwa jumla, na kiasi cha yuan 4,000 kilichokuwa kwenye akaunti yangu kama malipo ya hakimiliki kikageuka kuwa ushahidi wa uhalifu wangu."

Haijulikani iwapo huu utakuwa mwisho wa kazi zao kwenye jukwaa la Haitang.

Mwandishi mmoja wa *Danmei* anayetumia jina la mtandaoni "Sijin De Sijin" aliandika, "Kama ningeweza kurudisha nyuma muda, bado ningechagua kuandika. Na nitaendelea kuandika."

"Matumaini yangu pekee ni kwamba sheria itaweza kuona zaidi ya maneno yaliyoandikwa,kuona msichana aliyeacha kula ili kuweka akiba, msichana aliyeuza nywele zake ili aweze kununua kalamu, msichana aliyeamini kuwa kupitia uandishi angeweza kupata njia ya kubadili hatima yake. Natumai sote tutapewa fursa" aliandika.