Shirika la ndege la Kenya Airways latangaza ucheleweshaji wa safari kwa zaidi ya saa sita
Shirika la ndege la Kenya Airways limesema mgomo unaoendelea wa wafanyakazi wa sekta ya anga nchini Kenya umesababisha usumbufu wa safari katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA, huku baadhi ya safari zikichelewa kwa zaidi ya saa sita.
Katika taarifa yake Jumatatu, Kenya Airways imesema baadhi ya safari zimelazimika kupangwa upya kutokana na mrundikano wa safari uliosababishwa na mgomo huo.
Abiria wanaosafiri na shirika hilo wameelekezwa kwenda uwanja wa ndege baada ya kuthibitisha safari zao pamoja na hali ya ndege zao.
Wale wanaotaka kubadili muda wa safari wameelezwa kuwa wanaweza kufanya hivyo bila kutozwa ada ya ziada.
Kenya Airways imesema timu zake zinaendelea kushughulikia mrundikano wa safari ili kupunguza athari za mgomo huo kwa abiria.
Hatua hiyo ya wafanyakazi wa anga ilianza Jumapili, baada ya wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Anga Kenya, KAWU, kuanza mgomo wa kupunguza kasi ya kazi katika viwanja vya ndege nchini.
Wafanyakazi hao wanadai kuboreshwa kwa maslahi yao, mazingira bora ya kazi na kutekelezwa kwa makubaliano ya awali kuhusu mafao ya ajira.
Iran yasema imeshambulia vituo vya Marekani vilivyoko Jordan na UAE baada ya shambulio la Larak
Chanzo cha picha, Getty Images
Iran imesema imeshambulia vituo vya Marekani nchini Jordan pamoja na maeneo ya kijeshi ya Marekani katika kambi ya anga ya Al Minhad nchini Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, baada ya vikosi vya Marekani kushambulia kurunzi mbili za roketi katika Kisiwa cha Larak nchini Iran.
Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, wamesema shambulio hilo la Marekani dhidi ya Kisiwa cha Larak liliwaua na kuwajeruhi wanajeshi kadhaa wa Iran pamoja na raia, kwa mujibu wa shirika la utangazaji la serikali, IRIB.
Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ya UAE imekanusha madai ya Iran kwamba Kambi ya Anga ya Al Minhad ililengwa.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Tehran haitafuti vita, lakini haiwezi kukaa kimya inaposhambuliwa.
Wakati huo huo, vikosi vya Israel vimefanya operesheni kubwa katika mji wa Nablus, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, ambapo Wapalestina wawili wameripotiwa kuuawa.
Abiria walala katika uwanja wa ndege wa JKIA nchini Kenya huku mgomo wa wafanyakazi wa sekta ya anga ukiendelea
Maelezo kuhusu taarifa
Author, Laillah Mohammed
Nafasi, BBC Swahili
Chanzo cha picha, Getty Images
Shughuli za
usafiri zimeendelea kutatizika katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jommo
Kenyatta nchini Kenya kwa siku ya pili Jumatatu hii, maelfu ya wasafiri
wakilalamikia kuahirishwa kwa safari zao au nyingine kukwama wasijuwe
watasafiri lini.
Uwanja huu
ndio wenye shughuli nyingi kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki na maziwa
makuu, ukiwa na wasafiri 13,000 kila siku, huku watu milioni 8.6 wakisafiri
kupitia uwanja huo kila mwaka huku ndege 200 zikitua uwanjani humo na nyingine
195 zikiondoka.
Baadhi ya
wasafiri wameelezea mahangaiko ya kusubiri hadi saa 10 katika uwanja wa ndege
ili kusafiri.
Hapo jana
mamlaka ya kusimamia viwanja vye ndege KAA ilitoa taarifa kusema kuwa
inashughulikia suala hilo kupunguza mahangaiko ya wasafiri katika viwanja vya
ndege lakini hali hiyo imeendelea kukumba viwanja vyote vya ndege vya umma
nchini Kenya kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa viwanja vye ndege.
Akizungumza
na BBC mapema Jumatatu, Bwana Moss Ndiema amesema kwamba wana mengi ya
kulalamikia ila masuala makuu matatu yamewalzaimu kurejelea mgomo miezi michache
tu baada ya KAWU kuafikiana na serikali ya Kenya kusitisha mgomo mwingine.
Kulingana na
KAWU, Mamlaka ya kudhibiti mishahara ya watumishi wa umma nchini Kenya SRC
iliiamrisha Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya KCAA kutumia moja kati ya mikataba
mitatu ya makubaliano yaliyotiwa Saini kati ya 2015 na 2025.
Mpango huu
ungeangazia suala la nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi wa viwanja wa ndege
ambao wamelalamikia kutopata nyongeza hiyo tangu 2015.
Hatua ya
Mkurugenzi wa Mamlaka ya kusimamia viwanja vya ndege KAA Moses Wekesa kuwatumia
maafisa wa huduma ya vijana NYS kutekeleza majukumu ya Ulinzi wa viwanja ambao
KAWU imesema ni jukumu la maafisa wa KAA limewakera mno wakimtaka kuondolewa
kazini kwa ajili ya kile wamekitaja kama kiburi na dharau kwao.
Suala la
tatu ambalo wamesema ni muhimu kwao ni wafanyakazi wa kampuni ya ndege ya Jambo Jet ambayo inamilikiwa na shirika la ndege nchini Kenya – Kenya Airways. Jambo
Jet imedaiwa kutowaruhusu wafanyakazi wake kujiunga na vyama vya wafanyakazi
kama vile KAWU , hali ambayo wamedai inawanyimanafasi ya kutetea haki zao
ambazo KAWU inasema inadhulumiwa kazini.
Na japo
Katibu Mkuu Ndiema amesema wasafiri wanaendelea kuhangaika uwanjani kwa kuwa
safari zao zimeahirishwa au kukwama, inawabidi kufanya hivyo kwa ajili ya
kupata haki yao ya kikatiba.
‘Ni
masikitiko makubwa lakini hatuna budi ila kuilazimu serikali kuketi nasi chini
mezani na kutatua mzozo huu ambao sasa tunahisi umekuwa mbaya zaidi kwetu,’
alisema Bwana Ndiema kwenye mahojiano ya simu n BBC.
Katika
uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta,
wasafiri waliendelea kulalmikia kukwama kwa siku ya pili Jumatatu.
Siku ya
Jumapili wengi waliwaeleza wanahabari kuhusu hali ya kukata tamaa. Kulingana na badhi ya wasafiri, hali hiyo
iliwapata kwa mshtuko mkubwa.
Nicole
Jepkorir, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 24 anayesoma katika chuo kikuu nje ya
Kenya amesema; "Tulitakiwa kuondoka
saa kumi jioni leo, lakini kutokana na usumbufu na maandamano yaliyokuwepo hapa
asubuhi ya leo, tutaondoka saa sita usiku. Hali hii inaleta usumbufu mkubwa kwa
sababu tulifika hapa mapema sana asubuhi.
Tulitakiwa kuwa tumekamilisha
taratibu za kuingia kwenye ndege (check-in) kufikia sasa, lakini hatuwezi
kufanya hivyo. Hatuna la kufanya kwa sababu KAA [Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Kenya] inapaswa kupokea ndege ili ziweze kuja kutuchukua na kuondoka; kwa hivyo
hakuna kinachoendelea. Tunapata taarifa kwa kuchelewa; kama tungeambiwa mapema,
tusingekuja hapa. Labda tungekuja wakati ambao tulitakiwa kuondoka."
Naye William
Obino, ambaye ni mwanafunzi pia amesema,"Tulitakiwa kukamilisha taratibu za kuingia kwenye ndege (check-in)
majira ya saa sita mchana na kuondoka saa kumi jioni, lakini safari yetu ya
ndege sasa imecheleweshwa hadi saa sita usiku. Kuna watu wengi waliokwama hapa,
ikiwemo sisi wenyewe, kwa hivyo ni jambo la kusikitisha sana."
William
Obino, mwenye umri wa miaka 22 amesema kwamba ;"Imetuathiri sana kwa sababu inavuruga ratiba yetu; tulikuwa na
ratiba iliyopangwa kwa ajili ya siku zote za safari yetu, na sasa kutokana na
kuchelewa huku, huenda tukalazimika kuondoa baadhi ya mambo kwenye ratiba
hiyo."
Hazikizimana
Lolewi Spoil, mfanyabiashara kutoka Rwanda amesema ; "Nilipaswa kusafiri
saa 11 jioni, lakini nilipofika hapa, nilipokea barua pepe ikisema kuwa kuna
ucheleweshaji na kwamba safari yangu ya ndege imeahirishwa hadi saa 5 usiku.
Nilipomuuliza mmoja wa wafanyakazi, aliniambia ni kweli, na kwamba tunapaswa
kuwa na subira na kusubiri hadi wakati huo."
KAWU imesema
inatarajiwa kukutana na Waziri wa uchukuzi wa umma nchini Kenya davis Chirchir,
Katibu wake Teresiah Mbaika, Maafisa kutoka wizara ya Leba, Maafisa wa Mamlaka
za KCAA na KAA na Katibu Mkuu wa vyama vya wafanyakazi nchini kenye, COTU
Francis Atwoli kujaribu kutatua mzozo uliopo..
Trump atoa video ya shambulio dhidi ya kisiwa cha Kharg iliyotengenezwa kwa akili mnemba (AI)
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kisiwa cha Iran cha Kharg
Rais wa
Marekani Donald Trump amechapisha video iliyotengenezwa kwa teknolojia ya akili
mnemba (AI) kwenye mtandao wa Truth Social, ikionyesha kituo kikubwa cha mafuta
kikilipuka na kuungua.
Bw. Trump
aliandika katika maelezo ya video hiyo: "Kisiwa cha Kharg kinaharibiwa
kabisa na kusawazishwa na ardhi!!!"
Video hiyo
imetoka wakati ambapo mivutano ya kijeshi kati ya Iran na Marekani imepamba
moto kwa wakati mwengine.
Hapo awali,
vikosi vya Marekani vililenga mifumo miwili ya kurushia makombora ya Iran
kwenye Kisiwa cha Larak, na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi lilitangaza kuwa
lilijibu mashambulizi hayo kwa kulenga kambi mbili za Marekani nchini Jordan
kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani (drones).
Kisiwa cha
Kharg ni mojawapo ya vituo muhimu zaidi vya Iran vya kusafirisha mafuta nje ya
nchi katika Ghuba ya Uajemi, na sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya mafuta ghafi ya
nchi hiyo hufanyika kupitia vituo vilivyoko kisiwani humo.
Familia 32 za Kenya kugawanya fidia ya ndege ya Ethiopian Airlines iliopata ajali
Karibu miaka saba baada ya ndege ya Ethiopian Airlines Nambari 302 kuanguka ikiwa safarini kuelekea Nairobi, familia 32 za Kenya zinatarajiwa kupokea malipo mapya ya fidia kufuatia kesi ndefu dhidi ya kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing katika mahakama za Marekani.
Kila familia itapokea dola milioni 2.73, sawa na takriban Shilingi milioni 353, chini ya mpango wa hivi karibuni wa fidia kutokana na ajali hiyo ya Machi 2019. Malipo hayo mapya yanafikia jumla ya dola milioni 87.36, au takriban Shilingi bilioni 11.3, kwa kaya hizo 32 za Kenya zilizoathirika.
Ikijumuishwa na fidia iliyolipwa katika hatua za awali za mchakato wa kisheria, jumla ya fedha ambazo familia hizo zitapokea inakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 17.3.
Ndege hiyo nambari 302 ilianguka tarehe 10 Machi 2019, dakika sita baada ya kupaa kutoka Addis Ababa, Ethiopia, ikiwa safarini kuelekea Nairobi.
Abiria na wahudumu wote 157 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walipoteza maisha katika ajali hiyo. Kenya ilirekodi idadi kubwa zaidi ya vifo miongoni mwa raia wa mataifa zaidi ya 30 waliokuwemo kwenye ndege hiyo.
Makubaliano hayo ya hivi karibuni ya fidia yanakuja kufuatia kesi zilizofunguliwa nchini Marekani, ambapo familia hizo zilidai fidia kutoka kwa Boeing kuhusiana na ajali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, familia hizo zilipata hadhi ya kisheria kama waathiriwa wa uhalifu ndani ya mfumo wa haki ya jinai wa Marekani baada ya Boeing kushutumiwa kwa kuwapotosha wadhibiti wa sekta hiyo.
IRGC: Meli kubwa ya mafuta yashika moto katika Mlango-Bahari wa Hormuz baada ya kushambuliwa
Chanzo cha picha, Dutch Coastguard
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) linasema kuwa
"meli ya mafuta iliyokuwa ikijaribu kupita katika njia isiyo halali
kusini mwa Mlango-Bahari wa Hormuz ilishika moto na kusimama baada ya
kushambuliwa na makombora miwili ya baharini"
Katika taarifa iliyochapishwa na vyombo vya habari vya Iran,
IRGC ilionya: "Hatima ya meli zinazokiuka kanuni za usalama za
Mlango-Bahari wa Hormuz haitakuwa tofauti na hii."
Haijulikani wazi jina la meli hiyo au nchi inayomiliki meli
hiyo.
IRGC imezitaka meli zinazopita katika Mlango-Bahari wa
Hormuz "kuzingatia kikamilifu kanuni zilizotolewa na Jeshi la Wanamaji la
IRGC kuhusu upitaji na usafiri wa baharini," na kuzishauri zisiruhusu
"kudanganywa" na Marekani kupita njia nyingine, wala kuziweka mali na
maisha ya wafanyakazi wa meli hizo katika hatari ya uharibifu usio wa lazima.
Mamia ya raia wa kigeni bado hawajulikani walipo katika eneo la mpaka Nepal
Chanzo cha picha, RSS
Watalii
kutoka kote duniani huja Nepal kwa ajili ya milima na maeneo yake matakatifu.
Taarifa
kuhusu watu hao waliopotea ni kama ifuatavyo:
India - Takriban
raia 320 wa India hawajulikani walipo, kulingana na wizara ya mambo ya nje
mjini Delhi
China -
Wizara ya mambo ya nje ya China inasema karibu raia 100 wa China hawajulikani
walipo nchini Nepal
Marekani -
Wamarekani 90 bado hawajulikani walipo, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya
Marekani
Ukraine - Raia
62 wa Ukraine hawajulikani walipo, polisi wa Nepal wanasema
Malaysia - Raia
51 wa Malaysia waliokuwa wakisafiri na kampuni ya Fishtail Tours and Travels
hawajulikani walipo kufuatia mafuriko, maafisa wanasema
Australia - Hakuna taarifa kuhusu walipo raia 41 wa Australia, kulingana na naibu waziri wa
uhamiaji wa nchi hiyo
Uingereza - Polisi
wa Nepal wanasema raia 33 wa Uingereza hawajulikani walipo; shirika la
utangazaji la serikali ya China, CCTV, pia linaripoti kuwa raia 15 wa Uingereza
ni miongoni mwa waliopotea huko Tibet - haijulikani ni wangapi kati yao ambao
tayari wamejumuishwa katika takwimu zilizotolewa na Nepal
Canada -
raia 30 wa Canada hawajulikani walipo, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo
inasema
Idadi ndogo
ya wasafiri kutoka Korea Kusini, Afrika Kusini, Ureno, Uholanzi na New Zealand
pia ni miongoni mwa waliopotea.
Nepal yaimarisha juhudi za kuwanusuru mamia ya watu waliokwama katika mahandaki ya umeme
Chanzo cha picha, Reuters
Ofisi ya
Waziri Mkuu wa Nepal imesema kuwa juhudi za uokoaji katika handaki kwenye mradi
wa umeme wa maji wa Trishuli-3A zimeongezewa nguvu, zikijumuisha shughuli za
ulipuaji.
Katika
ujumbe kwenye mtandao wa X, ofisi hiyo imesema kuwa timu ya pamoja ya watu 90
imetumwa eneo la tukio, ikijumuisha vikosi vya usalama, polisi, na waokoaji
wanaoambatana na mbwa waliofunzwa.
Awali, shimo
lenye ukubwa wa futi 2 kwa 3 (mita 0.6 kwa 0.9) lilitengenezwa kwenye sehemu ya
juu ya handaki, na waokoaji wakashuka chini kwa kutumia kamba. Hawakupata
majibu yoyote kutoka ndani walipopiga kelele kuita.
Shughuli za
uokoaji zinaendelea, huku timu hiyo ikifanya kazi bila kuchoka usiku na mchana
licha ya kuwepo kwa mazingira magumu na hatari, ofisi ya Waziri Mkuu imesema.
Miongoni mwa
watu zaidi ya 2,500 waliopotea, mamia wanadhaniwa kuwa ni wafanyakazi katika
miradi ya umeme wa maji nchini Nepal.
Marekani yashambulia mitambo ya kurushia makombora ya Iran kwenye Kisiwa cha Larak
Chanzo cha picha, Reuters
Vikosi vya
Marekani vimeshambulia mitambo miwili ya kurusha makombora ya Iran, afisa mmoja
wa Marekani amesema, akiashiria mashambulizi ya kwanza yanayojulikana ya
Marekani dhidi ya Iran tangu mwishoni mwa Julai.
"Vikosi
vya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) vilionekana vikijiandaa kurusha
makombora yenye mabomu ya baharini kwenye Mlango wa Hormuz," mshirika wa
BBC wa Marekani CBS News alimnukuu msemaji wa Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom)
Cdr Tim Hawkins akisema.
IRGC ilisema
shambulio la Jumapili liliua na kujeruhi watu kadhaa, na kuapa "kulipiza
kisasi".
Baadaye
ilisema ilizindua shambulio dhidi ya malengo ya kijeshi ya Marekani huko
Jordan, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Iran.